IlipoishiaHizi ni risasi zilezile, chukueni maiti hizi na wengine  fanyeni msako hapa haraka sana” Ilikuwa ni sauti ya mmoja wa  Askari waliokuja pale kanisani, bado Mtaalam Sande, Mzee  Dawson na vijana wake wakiwa ndani ya Andaki bila kuwa na  taarifa kuwa Jesca alikuwa ameuawa na Six, lilipofunguliwa lango kuu la Kanisa ndipo mshituko na Mshangao mkubwa  ulipowashika polisi hao, walikuta Miili ya watu ikiwa  inatokwa na mvuke kama vile nyama inayochomwa, harufu ya  nyama ilitapakaa kanisa zima wakaagiza zima moto kumwaga Maji  katika kanisa hilo, muda mchache polisi walifanikiwa kuingia  ndani ya kanisa na kukuta Miili mingi ikiwa imeharibika  vibaya sana. 

Taarifa ilizagaa kwa haraka sana juu ya shambulio hilo la  kutisha ambalo lilitumia silaha ya sumu na risasi, Sande  akawashauri akina Mzee Dawson kuwa hawapaswi kutoka kwa  wakati huo hadi polisi watakapo maliza msako wao. Endelea 

SEHEMU YA TISA

“Nina mashaka juu ya uhai wa Jesca, yeye ni mmoja wa walinzi  wa hapa kanisani, sijasikia majibizano ya risasi, huwenda  amekufa kifo Baridi” Alisema Mzee Dawson akionekana kushindwa  kuzuia chozi lake 

“Una maanisha nini kusema Kifo Baridi?” Alihoji Mtaalam Sande  Olise huku akimtazama Dawson kwa jicho lililo kaza 

“Kufa bila kujibu mapigo, Walengwa tunaotafutwa katika vita  hii ni sisi. Sitaki makubwa yawakute wasio na hatia” Alinena  Dawson 

“Una maaana gani?” 

“Ni bora nijitokeze kupambana nao ili kunusuru Maisha ya  wengi yanayowekwa rehani, ikiwa kufa Mimi au kupona wao  ninachotaka ni usawa” Aliongeza Dawson 

“Kumbuka Polisi watakuangalia kama muarifu kuanzia hivi sasa,  hautokuwa huru kufanya chochote kama Mkuu wa Kitengo, vita  hii ni ngumu Mkuu! Vipi kama Rais ataamuwa kukupaka tope?  Utakuwa salama?” Aliuliza Sande Olise, Mzee Dawson akameza  funda zito la mate kisha akasema 

“Tusipopambana sasa hivi tutakuja kupambana nje ya muda,  tunapaswa kuwa macho zaidi” 

“Unashauri tufanye Nini Mkuu tupo tayari kukusaidia katika  vita hii” Alisema Kisko kwa utii Mkubwa, Dawson alikuwa kama  Mzazi kwao, ndiye aliyewachukua kutoka katika kituo cha  Watoto yatima na kuwaonesha Mwanga wa Maisha, Dawson  akawageukia na kuwaambia 

“Natamani hii vita msipigane sababu mna kila sababu ya kuwa  hai ili mje mpigane hapo baadaye sisi tukiwa tumetundika  daruga au tukiwa tumekufa. Niliwaandaa mje kuwa hazina muhimu baadaye” Alisema Dawson kwa sauti ya Baba kwa Watoto wake,  nyuso za Kisko na Chande zilisinyaa huku macho yao yakitazama  chini. 

“Babaa!! ” Aliita Chande, Dawson akageuza macho yake  kumtazama 

“Tupo tayari kwa sasa kufa kwa ajili ya Taifa letu, turuhusu  tukusaidie hii vita” Dawson alipomaliza kumsikiliza Chande  akarudisha macho yake kwa Sande Olise, Wakajikuta  wanatazamana huku sura zao zikizungumza Kijasusi 

“Tuangalie tunatokaje hapa Shimoni, haribuni kila kitu ili  kupoteza ushahidi wa kazi za hapa ndani, kila mmoja avae sura  bandia haraka sana” Aliagiza Mzee Dawson kwa sauti iliyojaa  mamlaka ya Kijeshi, kazi ikaanza rasmi. 

MSAKO 

“Shit!” Ilikuwa ni sauti ya John Brain baada ya kupokea  taarifa usiku huo, hakutegemea kusikia kuwa Dawson na Sande  Olise bado wanaendelea kupumua, aliona ni makosa makubwa ni  sawa na kumjeruhi mnyama Mkali. 

“Inawezekanaje wasiwepo kanisani wakati mtoa taarifa  amehakikisha kuwa Sande aliingia hapo? Endapo Sande na Dawson  wakapata muda wa kupanga mipango yao kazi hii itakuwa ngumu  kwetu” Alisema tena John Brain huku akizitazama sura za Six  na Malaika ambao walikuwa wamenywea. 

“Nimefanya msako kanisa zima lakini sikupata kuhisi hata  harufu zao, huenda walicheza mchezo wa sarafu baada ya  kugundua kuwa tunawafuatilia” Alijibu Malaika 

“Watakuwa wapi?” Aliuliza John Brain akionesha kutafakari  jambo peke yake, kisha akawaambia 

“Nendeni lakini Mjiandae kwa msako maalum” Malaika na Six  wakaondoka, John Brain akampigia simu Rais na kumjulisha  taarifa ile ambayo ilionekana kumchanganya sana Rais 

“Hivi mnajua mnafanya masihara kwa Watu gani? Hao jamaa wana  medali za ushindi kwenye kila jambo, Dawson ana fahamu siri  yetu hivyo hapaswi kuendelea kuishi” Alisema Rais kama Mtu  aliyeingia kwenye mshituko ni wazi kuwa alitarajia kusikia  kuwa Dawson na Sande wameuawa

“Tunalijuwa hilo na vijana wangu wanalifanyia kazi jambo la  muhimu ni kuhakikisha unatupatia Mtu wetu baada ya siku  chache, tutakuwa tumeimaliza kazi hii na kuondoka hapa  Nchini” 

“Msifanye Makosa mengine John , mtajikuta mnawajibishwa!  Ngoja nijisafishe haraka sana” Rais alikata simu, alionekana  kuwa mwenye msongo wa mawazo huku akionekana kuwa na hofu juu  ya mpango wake wa siri juu ya Mauwaji ya Makam wa Rais  kujulikana na kuwekwa hadharani, akanyanyua simu na kumpigia  Mkuu wa Idara ya polisi na kumueleza kuwa Dawson ni mharifu  anapaswa kusakwa kwa kila njia ili apatikane, Rais aliamuwa  kucheza karata mbili. 

Moja ni kuwatumia Mafia Gang kumfyeka Dawson na nyingine ni  kutumia Jeshi la polisi kumsaka popote alipo, agizo la Rais  lilianza kutekelezwa, Polisi wakaagizwa kuelekea nyumbani kwa  Dawson usiku huo huo. 

Rais alikaa katika kiti chake huku akizidi kujiingiza  mawazoni, Nchi ilikuwa imeingia katika Msako, Polisi  walivunja nyumba ya Dawson na kufanya msako mkubwa bila  mafanikio, wakati huo Dawson na timu yake wakiwa wanatoka  katika shimo kule kanisani, Polisi wachache walikuwepo eneo  la tukio kule kanisani usiku huo, Walifanikiwa kuchomoka pale  kanisani kimya kimya kisha wakaruka ukuta wa kanisa na  kutokomea. 

Dawson alishajua kuwa polisi wataenda nyumbani kwake hivyo  akawaambia wasiende huko badala yake waelekee kwenye makazi  ya siri ambayo alikuwa akiishi Inspekta Zola, ilikuwa ni  safari ya Kilomita kadhaa kutoka pale kanisani hadi kufika  huko, walilazimika kutembea kwa mguu sababu polisi walikuwa  wakikagua magari yanayoingia na kutoka kila kona ya jiji  hilo, haikuwa salama kwao kutumia usafiri wa gari licha ya  kuvaa sura bandia, mwendo wa masaa mawili Walifika kwenye  makazi hayo, Dawson alifahamu namba za siri za kufungulia  milango hiyo ikawa rahisi wao kuingia ndani. 

Kumbukumbu ya Zola iliendelea kuwatesa baada ya kuingia humo,  Sande aliiona picha aliyopiga na Zola wakiwa mafunzoni hadi  chozi lilimbubujika aligundua kuwa Rafiki yake huyo alikuwa  akimpenda na kumkumbuka sana, walikuwa na ndoto ya kuonana  siku moja lakini ndiyo hivyo Sande alichelewa kurudi hadi  Zola akauawa, Dawson aliifahamu nyumba hii vizuri sana sababu  mpango wa nyumba hii aliusuka mwenyewe ili Zola aitumie  nyumba hii kwa kazi zake maalum, akawaonesha chumba ambacho  kilikuwa na silaha akawataka kujiandaa kwa ajili ya kazi hiyo  kubwa iliyo mbele yao.

“Baada ya kupambazuka tutakuwa katika hekaheka nzito yenye  maamuzi ya kuondoa uhai wetu au kuturuhusu kuendelea kupumua,  kama tuna muda wa kufurahi basi huu Usiku uliobaki unaweza  kuwa ndio muda pekee wa kufanya hivyo” Alisema Dawson akiwa  ana mimina mvinyo kwenye glasi, kila mmoja akanyanyua na  kuanza kunywa 

“Kwa ajili ya Zola, tusherehekee Maisha yake sababu  ameimaliza kazi aliyokula kiapo kuifanya ili kulinda Taifa  lake” Yalikuwa ni maneno ya Sande Olise ambaye naye aliungana  na Mzee Dawson wakanywa Glasi moja moja, Chande na Kisko  wakaungana pale wote wakapata Mvinyo kama Ishara ya kuyaenzi  Maisha ya Inspekta Zola ambaye ameuawa ndani ya Ikulu, hadi  kufikia muda huo hakukuwa na taarifa iliyotolewa popote kuwa  Inspekta Zola alikuwa amekufa, si akina Dawson wala upande wa  Rais ambao ndio walitekeleza Mauwaji hayo. 

Asubuhi ya siku iliyofuata iliwakuta Dawson na vijana wake  wakiwa ndani ya jumba la siri hilo alilokuwa akiishi Mtaalam  Zola, taarifa kuwa Dawson amelisaliti Taifa ilianza kuzagaa,  akatajwa Dawson kama ndiye Mhusika namba moja wa Mauwaji ya  Waumini kule kanisani, taarifa ikafika mbali na kusema ana  viashiria kuwa alitaka kuipindua Nchi hiyo kwa kusababisha  taharuki ikiwemo Mauwaji ya kutisha yaliyokuwa yakifanyika  pia Mauwaji ya Makam wa Rais, gunzo lilikuwa limetanda, ni  kama Bundi mweusi alikuwa ameyazunguka Maisha ya Dawson,  ikatolewa taarifa kuwa Dawson anashirikiana na Askari mmoja  wa Usalama wa Taifa aliyeitwa Sande Olise ambaye alikuwa  akiishi Botswana. 

“Huyu Mjinga anajaribu kuharibu taswira niliyoijenga Miaka  mingi katika Taifa hili” Alisema Dawson kwa hasira huku  akitafuta rimoti ya TV ili aizime, Sande alimzuia 

“Huna haja ya kupaniki, anachokifanya Rais ni kujaribu  kujisafisha na kuyatia doa Maisha yetu. Kwakuwa anajua una  siri zake basi anaitumia hii nafasi kukudidimiza ili  usiaminike na yeyote yule” Alisema Sande kisha Dawson  akamuuliza 

“Mimi ni mzalendo kwa Taifa hili, nimekuwa kwenye nafasi hii  kwa Marais zaidi ya tano, iweje huyu aje kuharibu kila jema  nililopanda kwenye Taifa hili, baada ya kuniulia Rafiki yangu  anadiriki kuniita Msaliti wa Taifa hili” Dawson alionekana  kuchukizwa sana na kitendo kile, akapapasa kiuno chake akatoa  bastola 

“Unaenda wapi?” Alihoji Sande

“Ikulu kuondoa uhai wa hayawani yule, hastahili kuishi pale,  anastahili kuwa Kaburini au Jela kwa yote aliyoyafanya” 

“Hebu tulia, kumbuka John Brain ni Mtu mwenye akili sana. Huu  ni mtego na lengo ni kukufanya uchukie, Rais anakujua vizuri  hupendi mchezo na uzushi, ukitoka hapa hata hufiki mbali  wanakuuwa” Alisema Sande huku akimsistiza Dawson atulie,  chozi lilikuwa likimbubujika Mzee Dawson, akajitupa kitini  kama Mtu aliyekata tamaa. 

“Huna haja ya kukurupuka, Tumetajwa kuwa Wauwaji na wasaliti,  tukikamatwa huko nje hatutokaa kuonekana tena, tutaliacha  Taifa hili katika giza kama ambavyo Zola ameliacha. Nimekuja  hapa kwa ajili ya kazi hii, nitazame Mimi kwa sasa kama  ambavyo ulikuwa ukimtazama Zola na kumuamini, hamisha kila  kitu kutoka kwake kisha kiweke kwangu, Mimi ni Zola niliye  katika Umbo la Sande, hakuna kitakacho haribika” Yalikuwa ni  maneno ya Kikomandoo kutoka kwa Sande Olise, alisema akiwa  amefanikiwa kumpokonya Bastola Dawson. 

Akampatia ile Bastola Kisko akamwmbia 

“Ukiitumia vibaya itakupeleka pabaya, tuliza akili ndipo  uitume ifanye kazi yake” Alimkabidhi kisha Akasema 

“Baada ya miaka mingi narudi kazini kupambana na John Brain,  kivuli chake kitaendelea kuitesa hii Nchi, huyu Rais Mpumbavu  siku zake za kuwa madarkani zinahesabika” Alisema kisha  akaelekea kwenye moja ya vyumba vya siri vya jengo hilo  ambavyo vilikuwa vimeshafunguliwa na Mzee Dawon. 

Akakuta Ramani ya mpango wa Zola ikiwa ukutani, akaangalia  namna Zola alivyopanga mambo yake pale akajikuta akitabasamu  kwani kila jambo alikuwa ameliandika katika Ramani hiyo. 

Nyuma ya Sande alikuja kusimama Mzee Dawson huku akimtazama  Sande namna alivyokuwa makini kutazama Ramani ya Zola 

“Ulikuwa na askari shujaa sana ambaye hasahau mbinu zako”  Alisema Sande Olise kisha aligeuka na kumtazama Mzee Dawson  aliyekuwa akifuta chozi lake, kifo cha Zola kilimuumiza sana. 

“Nina uhakika kama utawatunza vijana hawa wawili wanaweza  kuwa Sande na Zola wa baadaye, kwasasa Mzee Dawson pumzika.  Afya yako haikuruhusu kuendelea na vita hii, nitapambana Mimi  na hawa vijana, utabakia hapa” Aliongeza Sande, ni kweli afya  ya Dawson haikuwa nzuri kutokana na pombe na sigara.

Wakapanga mipango ya kumuondoa Rais Madarakani kisha kuanika  uchafu na madudu yake yote, Dawson alitakiwa kubakia pale  kwenye jumba la siri wakati ambao Sande na vijana wawili wa  Dawson watakapokuwa wanaondoka, wakapewa sura bandia ili  watakapotoka nje wasijulikane. 

Muda huo Magari mawili meusi yalikuwa yakiingia Ikulu,  alikuwa ni John Brain, Six na Malaika, utatu ambao  ulilisumbua Taifa kwa muda mrefu, waliitwa na Rais huyo  Mshenzi. Waliingia wakiwa kama wageni wakiwa ndani ya sura  bandia ili wasitambulike sababu Vyombo vingi vya habari hasa  vya nje vilikuwa vikiripoti taarifa zao za Mauwaji na jinsi  ambavyo walikuwa wakitafutwa, Waliongoza hadi ofisini kwa  Rais huyo bila Ulinzi wowote kutokana na maagizo ya Rais. 

Rais alipowaona alinyanyuka na kusogea karibu na John Brain  kisha akamuuliza 

“Mnataka niwape nini ili Dawson na Sande wauawe? Mnapaswa  kujuwa kuwa Dawson ni nyati aliyejeruhiwa akitoka huko  mafichoni hatutokuwa salama” Alisema huku akionekana  kuchanganikiwa, jasho lilikuwa likimvuja 

“Tatizo umechanganya vitu viwili kwa wakati mmoja, Polisi  wanahangaika kuwatafuta na sisi tunahangaika kuwapata. Kila  tunapopiga hatua polisi wanakuwa eneo la tukio, au unataka  tusamabratishe na polisi wako?” 

“Kama hilo ni tatizo nitawaingiza katika mfumo wa usalama wa  Taifa mkiwa katika sura hizo, John utakaa pembeni sababu ya  rangi yako ila Malaika na Six wataingia na kufanya kazi mara  moja, watakuwa na amri kwa askari pindi wanapokutana katika  jukumu la kuwawinda Sande na Dawson,watapewa vitambulisho  maalum” 

Rais akawaingiza Six na Malaika katika mfumo wa idara ya  Usalama wa Taifa, wakapewa na Vitambulisho  

vilivyowatambulisha kama Watu wa Usalama, ikawa rahisi kwao  kuwa huru kufanya kazi ya kuwasaka Dawson na Sande Olise  ambao walikuwa kizingiti kikubwa kwa Rais na John Brain  kumpata kijana wake aliyekuwa akishikiliwa na Rais. 

Polisi wakatawanywa kila kona ya Jiji kuhakikisha Dawson na  Sande hawapigi hata hatua moja, kazi ya polisi ilikuwa  kuwakamata lakini kazi ya Six na Malaika ni kuwauwa, wakiwa  ndani ya Sura bandia walirudi pale Kanisani ambako  walisababisha Mauwaji ya kutisha ya Waumini na Askari mmoja  wa siri wa Mzee Dawson, walirudi kama Watu wa Usalama,  wakahitaji kuchunguza eneo hilo huku akili zao zikiwaambia kuwa pengine Dawson na Sande bado wapp eneo hilo, walimjua  vizuri Dawson jinsi alivyo na akili nyingi. 

Walitumia vyema macho yao ya Kijasusi na mafunzo waliyoyapata  kutoka kwa John Brain wakagundua kuwa kuna andaki eneo la  maegesho ya Magari 

Six na Malaika wakapeana ishara, haraka bastola zao zikawa  zinatazmaa eneo hilo ili kama kuna Mtu atatokea basi  wamdhibiti haraka sana. 

Wakalisukuma gari na kuona mlango wa kuingia ndani, haraka  wakiwa makini sana wakafungua na kuanza kuingia humo taratibu  huku masikio yao yakiwa makini kusikiliza ndani ya andaki  hilo lenye giza sana. 

Walipofika chini wakawasha tochi ya simu kisha wakaona mahali  ambapo wangewasha taa, walipowasha wakaona vitu vikiwa  vimeharibiwa pale, wakakagua kila kona lakini hakukuwa na  Watu, tayari Mzee Dawson na vijana wake walishaondoka pale  muda mrefu sana kisha wakaharibu vitu ndani ya andaki hilo,  elimu yao ya kijasusi haikuwafanya wao kukata tamaa ya kutaka  kujuwa andaki hilo lilihusiana na nini 

“Kwa vyovyote haya yalikuwa makazi ya siri ya Dawson! Huenda  ameishi hapa kwa kitambo sana” Alisema Six 

“Hata awe makini vipi ni lazima ataacha alama humu, tutajua  kama ni yeye na ameenda wapi” Alisema Malaika, msako  uliendelea ndani ya andaki hilo lililoonekana kuwa makazi ya  kutulia sana, katika upekuzi wao waliona Makaburi manne  ambayo yalikuwa ndani ya chumba kimoja. 

Walipoangalia vizuri waliona namba za siri ambazo Mzee Dawson  aliwapa vijana wake kama majina na alama zao, namba hizi  zilikuwa za siri sana, ilikuwa ngumu kugundua chochote lakini  alizitambua kisha akampigia simu John Brain na kumueleza  kuhusu Makaburi hayo manne yenye namba za siri, John Brain  alikuwa na mtandao mkubwa sana na alizijua siri nyingi za  Mataifa mbalimbali 

“Hayo ni majina ya Watu wa siri wa Mzee Dawson, Sande yupo  hai, moja ya kaburi hapo linaweza kuwa kaburi la Zola,  fukueni haraka sana.” Ilisikika sauti ya John Brain, aliamini  Dawson ni Mtu mwenye akili sana kwenye mambo yake. 

Mengine yalionekana kuwa ya zamani sana lakini moja lilikuwa  bado jipya, wakalifukua hilo kwa kutumia chepe iliyo kwenye  kona ya chumba hicho chenye makaburi. Kazi hii ilifanywa na Six aliyekuwa amebana rasta zake kwa nyuma. Jasho lilikuwa  likimtoka, harufu kidogo ilianza kutapakaa pale, haikuwazuia  kufanya kazi yao,

Comments ziwe nyingi apa wikiendi itoke EPISODE NDEFU YA 10 

Nini Kitaendelea? USIKOSE SEHEMU YA SABA  USISAHAU PIA Kununua Kitabu Cha KOTI JEUSI Kupiga Namba+255760871896 Ufikishiwe Mpaka Ulipo

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

SOMA RIWAYA YA MSALA HAPA

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa 

  Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx   Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx   Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx   Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx 

  

21 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version