Ilipoishia  “Fuata maelekezo yangu, kuwa makini hao Watu wana akili ya  ziada sana wakati mwingine Watu hawaamini kama Huyo Mzungu ni  Binadamu, wana akili iliyozidi…unaweza kuwa umetegwa, kabla  ya kutoka Msibani hakuna ishara tata?” Alimpa wakati wa  kufikria, Zola akasema 

“Nilikuwa makini kuliko kawaida, hakuna aliyeniona ila wakati  natoka…” Ukimya ukatawala, Mzee Dawson akamuuliza Zola 

“Enhee ilikuwaje?” Zola akafikiria alipokuwa akitoka pale  aliparamiana na Mwanamke mmoja mzuri sana, hakutaka kulisema  hilo akiamini sio ishara ya kumueleza Mzee Dawson 

“Sio ishara!”  Endelea  

“Sawa endelea kuwa makini na gari hilo” Gari hiyo ndogo  nyeusi iligota katika moja ya hoteli maarufu sana Mjini hapo  iliyoitwa Sarafina Hotel, Muda huu jamaa mwenye upara alikuwa  akishuka bila kuonesha wasiwasi wowote huku Zola akiwa  anatafuta sehemu rahisi ya kupaki Gari yake, Jamaa wa upara  akaingia kwenye lifti wakati Zola akiwa amejibanza mahali  anamchungulia, haraka akapandisha ngazi kuelekea juu kwa  spidi ambayo kila mmoja alishangaa kwa Mzee kama Zola  kupandisha zile ngazi kwa spidi kubwa kama umeme, Naam  ilikuwa ni kawaida kwake kutokana na mafunzo aliyoyapata  zamani nchini Mexico na Cuba. 

Alipofika Floo ya pili alipokelewa na ukimya, akili yake  ikamwambia kuwa Jamaa wa upara atakuwa Floo ya juu yake yaani  ya tatu, basi Zola kwa spidi ile ile alizidi kupandisha ngazi  na kuendelea kustaajabisha Watu aliopishana nao, mwisho wa  Floo ya pili alimuona jamaa wa Upara akikata kona upande wa  kushoto, Zola hakutaka kupoteza muda alizidi kumfuatilia ili  ajuwe Jamaa yule alikuwa akienda wapi, huku akili yake  ikimwambia kuwa ni miongoni mwa wale waliousuka ule mpango wa  vifo vya Robert na Bosco na hatimae kumtumia Anastanzia kama  mchezo wa kuigiza ili kuficha jambo ambalo kwa asilimia kubwa  lilifanikiwa. Alipokata kushoto alianza kuhisi hali ya  tofauti, achilia mbali ukimya bali kulikuwa na milango miwili  ambayo ilikuwa wazi tena ikiwa inacheza kuashilia kuwa  ilikuwa imeguswa sekunde chache zilizopita. 

Zola akakunja mkono wake wa kushoto ambao alipendelea kuuita  Mkono Wa Mungu, kisha akachomoka na Bastola yake yenye  kiwambo maalum cha kuzuia mlio wa risasi kutoka, tayari  alikuwa na hisia kuwa alikuwa ameingizwa mtegoni, akachomoa  Ear phone masikioni baada ya kuhisi mawasiliano kati yake na  Mzee Dawson yalikuwa yanasuasua na hakutaka kuzungumza kwa  sauti kubwa, Kitendo cha Zola kuchomoa zile Ear Phone  masikioni kilimpa ishara Mzee Dawson, akahisi pengine Zola  yupo kwenye mtego wa kifo, haraka akachukua gari kuitafuta  Sarafina Hoteli ilipo, Naam! Zola alikuwa akinyata kama paka  aliyekuwa akimvizia panya ili aweze kumla, alipiganisha akili  yake huku macho akiwa anayaelekeza kwenye ile milango miwili  iliyo wazi 

Akauchagua mlango mmoja akaingia taratibu kisha akafunga  mlango bila kuruhusu sauti ya kufungwa kwa mlango huo  kusikika, mbele aliona kuna korido iliyo kimya sana, akawa  anaifuata. Alikuwa amejikunja kama duma vile huku akijuwa  kuwa kosa lolote atakalo lifanya linaweza kuondoa uhai wake,  akaupita mlango wa kwanza na wa pili, akili ikamwambia  aufungue mlango wa tatu, alikuwa ni mwenye hisia kali kama  Mbwa wa polisi vile, alihema taratibu sana, alifundishwa kuwa kuhema kwa nguvu kunaweza kusababisha shabaha kwenda tofauti  jambo ambalo hakutaka litokee pale, akiwa ameshikilia kitasa  hicho huku akivuta taratibu Zola alikutana na teke kali  lililomnyumbisha na kusababisha bastola yake kuanguka chini,  akiwa anataka kuiokota Bastola hiyo ilipigwa teke na  kuburuzika mita kadhaa, Ndipo Zola akajuwa sasa yupo katika  hatari mno, kwa umakini akageuka taratibu kumtazama  aliyempiga teke. 

Alikutana na sura ya Malaika, ambaye yeye alimtambua kama  Judith tena alikuwa katika sura bandia ambayo Zola alikuwa  akiijuwa. Mzee Zola akayakumbuka maneno ya polisi aliyempigia  simu na kumtaarifu juu ya mauwaji ya polisi katika kituo cha  polisi, akautumia muda huo kuyatazama maungio ya Msichana  huyo mwembamba lakini hatari sana akagundua ana ujuzi mkubwa  wa kareti. 

Zola hakutaka kupoteza muda wake japo alijuwa Msichana huyo  ni hatari sana kwake, akakunja mguu na kutupa teke lililofika  hadi kwenye mbavu za msichana huyo ambaye aliudaka mguu wa  zola kisha akaukunja na kumsababishia Zola maumivu mkali,  akapigwa kwenye ngoko ndipo Zola alipotoa sauti ya maumivu,  akauvuta mguu haraka ili usivunjwe, akawa na maswali mengi  kichwani aliyotaka kumuuliza Msichana huyo lakini aligundua  kuwa hana muda wa kupoteza hapo. 

Akaweka mikono yake vizuri ili aweze kutupa shambulio,  Malaika akajirusha na kutua kwenye mikono ya Mzee Zola ambayo  ilikuwa imekazwa, kisha akavingirika na kumpa teke la uso  Mzee Zola akaangukia pembeni, akamfuata na kuanza kumpiga  sehemu ya tumbo huku akimwambia 

“Wewe ni mahiri sana kwa upelelezi lakini mwisho wa kuifanya  kazi hiyo ni leo, nakuuwa Hapa ili kupeleka ujumbe kwa  aliyekutuma” Zola alikuwa akigugumia kwa maumivu, haraka  akauvuta mguu wa Malaika na kumuangusha akapata muda wa  kujipanga upya,,, safari hii Zola hakuwa na bahati kabisa,  Malaika aliutumia ujuzi wake wa mapigano na kumpiga kisawa  sawa Zola hadi akatema Damu, akamuinua na kumkaba shingoni  huku akiwa amemgandamiza ukutani, Zola akaitumia nguvu chache  iliyobakia akampiga teke sehemu nyeti ikawa auheni kwake,  Malaika akaanguka chini haraka akajiokota, ni kama vile  alikuwa amemchokoza basi Zola alikutana na Ngumi za uso  mfululizo hadi akachanganikiwa 

Akajikuta muda mchache ameanguka chini na kushindwa kuinuka,  Malaika alipoona Zola hawezi tena kurudisha majibu ya  mpambano huo uliopigwa kisiri ndani ya Hoteli hiyo, akavua  sura ya Bandia ndipo Zola akapata kuiona sura halisi ya  Mwanamke huyo.

“Naitwa Malaika! Najua huna uwezo wa kufanya chochote hapo  Zola sababu zimebakia sekunde chache nikupoteze, kama  ulifikiria kuwa mtaweza kupambana na Mafia Gang basi huu uwe  ujumbe kwa wajinga wenzako, Mtakufa wote endapo mtaendelea  kutufuatilia” Malaika akachomoa kisu chake kutoka katika  mfuko wa koti alilovaa, akamsogelea Mzee Zola akamwambia 

“Kwakuwa umefanikiwa kunijuwa basi huna haki ya kuendelea  kuishi” Malaika akanyanyua kisu ili amchome Zola sehemu ya  moyo, Ghafla alisikia mlango ukifunguliwa huku risasi  zikimiminwa mfululizo, akajirusha na kuanza kukimbia kwa  kuzikwepa hadi akazama kwenye korido, alikuwa ni Mzee Dawson  ndiye aliyemsaidia Zola pale vinginevyo Zola angeuawa pale. 

“Pole Zola” alisema huku akiwa amempa mkono Zola aweze  kusimama, akamsaidia akasimama kisha Dawson akaiendea Bastola  ya Zola ambayo ilikuwa sakafuni akampatia 

“Mshenzi yule alikuwa anaondoa uhai wangu na kama sio wewe  basi mgekuja kuchukua maiti yangu hapa” 

“Bado siamini kama msichana yule amekukalisha chini Zola!” 

“Dawson! Niliposikia hadithi ya yule Msichana ya kuuwa polisi  zaidi ya 15 katika kituo cha polisi nilifikiria ni utani  lakini leo nimeamini kwanini aliwashinda polisi, ana ujuzi wa  Kareti kitu ambacho ni hatari zaidi kwetu” 

“Oooh!! Mungu wangu, hatuna muda wa kupoteza hapa, tuondoke”  Alisema Mzee Dawson, mara moja wakashuka hadi chini kila  mmoja akaingia kwenye gari yake na kuelekea alipopafahamu. 

Zola alikuwa na hasira sana akiwa ndani ya gari, kupigwa na  Malaika kulimuumiza sana lakini alifanikiwa kuijua sura  halisi na jina la huyo Mwanamke ambalo ni Malaika, akili yake  ikamtuma aelekee kituo cha polisi, Mkono mmoja ulikuwa na  maumivu makali sana lakini alijikaza, alichotaka kujuwa ni  mafaili gani yule Malaika aliyaiba ndani ya kituo cha polisi,  akaambiwa kuwa mafaili hayo yalikuwa ya kesi moja  iliyoshikiliwa na kitengo cha Ikulu. 

Kesi hiyo ilimuhusu jamaa mmoja aliyeitwa Jamaal, ambaye  alikamatwa siku moja baada ya tukio la kuuawa kwa Makam wa  Rais kutokea, Historia ya jamaa huyo ilimuelezea kuwa ni Mtu  aliyepitia mafunzo maalum ya kijeshi ya ulengaji wa shabaha  ya masafa marefu na upiganaji, alikamatwa katika uwanja wa  ndege baada ya msako mkali uliokuwa ukiendelea.

Baada ya kumnasa walikuta Bunduki na risasi ambayo ilitumika  kumuuwa makam wa Rais, moja kwa moja alishtakiwa kwa kosa  hilo na kufungwa kwa siri katika gereza moja la siri sana,  Jamaal alikutwa na vitambulisho vilivyomuonesha kuwa ana  Uraia wa Nchi nane ikiwemo Marekani na Ukraine jambo ambalo  liliwashangaza sana lakini Jamaal alizungumza lugha nyingi  vizuri sana japo alikuwa na asili ya Somalia. Pia taarifa  ilienda mbali zaidi na kusema kuwa Jamaal alikutwa na  vitambulisho vya kijeshi vilivyoonesha kuwa aliwahi  kulitumikia jeshi la Israel na Palestina ndani ya miaka  miwili, 

Zola alikaa chini na kujishika kichwa chake kisha akauliza 

“Kwasasa Jamaal anashikiliwa gereza gani?” Swali hili  lilimfanya polisi aliyekuwa akimueleza Zola akae kimya kidogo  kisha akasema 

“Gereza lipo Ikulu ya Nchi, sisi hatuhusiki tena na kesi hiyo  Zola” Zola akauliza tena 

“Kwanini mafaili ya kesi bado yalikuwa hapa?” 

“Kwasababu kesi ilianzia hapa lakini cha kushangaza baada ya  kukamatwa tuliondolewa katika kesi hiyo” 

“Nani alitoa oda ya Nyie kuacha hii kesi na ikaenda sehemu  nyingine wakati nyie ndio mnakazi hiyo?” 

“Aliyetoa oda ni Rais wa Nchi” Zola aliondoka baada ya kupata  majibu yaliyochanganya akili yake kisha akawasiliana na Mzee  Dawson wakapanga kukutana katika makazi ya siri ya Zola,  Usiku Dawson alienda kuonana na Zola, kama kawaida yao  waligida pombe ili maongezi yaanze 

“Enhee umegundua nini Zola?” Aliuliza Dawson 

“Mafaili yaliyobiwa katika kituo cha polisi yalikuwa ya kesi  ya Mtu anayedaiwa kuwa alihusika kumuuwa Makam wa Rais”  Alisema Zola 

“Unasemaje? Ina maana polisi wanajuwa ni nani alihusika?” 

“Sio polisi pekee hata Mkuu wako wa Nchi ambaye anakupa kazi  ya kulisaka kundi la Mafia Gang anajuwa na kibaya zaidi  ametoa amri ya jeshi la polisi kuiacha kazi hiyo” Mzee Dawson  alionekana kushangaa sana 

“Inawezekanaje Zola?”

“Hiyo ndio hali halisi ndio maana nimekuita hapa ili  tuzungumze, nahisia mbaya juu ya Mkuu wa Nchi lakini sitaki  kujiaminisha chochote” 

“Unataka kusema Mkuu wa Nchi kuna kitu anakificha hapa?” Wote  waliacha kunywa pombe wakazama katika maongezi yao 

Nini Kitaendelea? USIKOSE SEHEMU YA SITA  USISAHAU PIA Kununua Kitabu Cha KOTI JEUSI Kupiga Namba+255760871896 Ufikishiwe Mpaka Ulipo

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

SOMA RIWAYA YA MSALA HAPA

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa 

  Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx   Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx   Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx   Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx

8 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version