Ilipoishia “Inawezekanaje Zola?”

“Hiyo ndio hali halisi ndio maana nimekuita hapa ili  tuzungumze, nahisia mbaya juu ya Mkuu wa Nchi lakini sitaki  kujiaminisha chochote” 

“Unataka kusema Mkuu wa Nchi kuna kitu anakificha hapa?” Wote  waliacha kunywa pombe wakazama katika maongezi yao  Endelea 

SEHEMU YA SITA

“Kama hausiki kwanini atoe amri kwa jeshi la polisi? Kwanini  Mtuhumiwa afungwe katika Gereza lililopo Ikulu?” Alihoji Zola  huku Dawson akionesha kuanza kuvuta picha ya maelezo ya Zola. 

“Mimi nafikiria kwasasa tujikite zaidi na upelelezi kuhusu  Mafia Gang, hili jambo tuliweke kiporo Zola” Alisema Mzee  Dawson, ni wazi kilichomfanya akae kimya kwa muda mrefu  kilikuwa ni hicho. 

“Wewe ni mwalimu mzuri sana Dawson, kuliacha hili jambo ni  sawa na kumega Mkate alafu ukajiaminisha kuwa hakuna  kilichotoka, umefundisha vijana wengi masuala ya upelelezi na  Ujasusi, sidhani hata hicho unachokizungumza kinatoka katika  akili yako, sitaki kuamini pia kuwa pombe imekuingia kiasi  hicho. Ili tuukate huu mti ni lazima tukubali kung’oa mizizi  ya Mti wenyewe ili usichipue tena” 

“Zola tunaanzia wapi kumpeleleza Mkuu wa Nchi ambaye ndiye  ametupa kazi hii, kama hili kundi lina maslahi kwake kwanini  ameagiza tulifyeke? Nachelea kusema anaweza kuwa hausiki  hapa” Alisema Dawson huku macho yake madogo kama ya paka  yaking’aza huku na kule, pombe ilikuwa ikishuka kwenye koo  lake lenye koromeo kubwa, kisha alibakua 

“Ni bora kuachana na kazi hii Dawson kuliko kuruhusu dosali  kwenye upelelezi huu, nimeweka Maisha yangu rehani, mwenyewe  umeona nilitaka kuuawa kama sio wewe kuwahi kuniokoa,  tukubaliane hapa kuwa Rais apelelezwe kuhusu Mfungwa  aliyefungwa magereza ya Ikulu” Ulikuwa ndio msimamo wa Zola,  Dawson alimuamini sana Zola akamwambia 

“Kama ni hivyo basi uwanja ni wako Zola, siku ukithibitisha  kuwa Rais anahusika na Mauwaji haya utanijulisha,” Ilikuwa  ndio kauli ya mwisho ya Dawson, umri wake ulionesha ni jinsi  gani alikuwa akipambana na akili za uzee alizonazo licha ya  kuwa ni Mtu aliyeaminiwa sana na Idara ya Usalama wa Taifa,  akamuaga Zola huku akimuachia ujumbe kuwa 

“Wakati unawatafuta wao wapo macho wanakutafuta” Alisema  kisha alijizoa na kuondoka pale kwa kutumia gari yake ya  kifahari, licha ya uzee lakini alimudu kuliendesha mwenyewe.  Muda huo mvua ilikuwa ikinyesha, Zola akawa anamtazama Dawson kupitia dirisha la kioo, Mzee Dawson alikuwa fundi wa  kuendesha gari jambo lililomchekesha Zola akajikuta akisema 

“Ng’ombe huyu amegoma kuzee Maini yake” Akarudi kuketi huku  akizidi kutafakari, akamkubuka rafiki yake Mmoja aliyeitwa  Sande Olise aliyekuwa uhamishoni Nchini Botswana,  alipomkumbuka alijikuta akitabasamu kisha akaenda ukutani  ambapo kulikuwa na picha waliyopiga pamoja. 

Sande Olise alikuwa ni miongoni mwa Wanafunzi waliopelekwa  Nchini Mexico kujifunza masuala ya upelelezi, Sande  alipishana umri wa miaka saba na Zola, tabia zao za kupenda  wanawake ndizo zilizowafanya wakafahamiana, akakumbuka Jinsi  walivyopigana vita vya kukiokoa kisiwa kimoja kilichopo Nje  kidogo ya Mji Mkuu, kisiwa hicho kilivamiwa na Waasi kutoka  Nchi jirani na kukiweka chini ya Ulinzi kwa zaidi ya siku  saba. 

Zola alikaa chini akafikiria kumpigia simu Sande Olise,  alipekuwa baadhi ya nyaraka fulani akakuta namba ya Sande  kisha akampigia huku akitabasamu. Simu ilipokelewa huku sauti  nzito ilisikika upande wa pili 

“P045 Olise! Kuna mpango maalum?” Alichofanya Zola alipiga  simu ya Sande kwa kutumia namba maalum za siri, Wapelelezi  wote walikuwa na simu za siri hivyo Sande alipoona simu hiyo  alijuwa kulikuwa na shida mahali, japo sauti yake ilionesha  kuwa alikuwa ameamshwa na simu ya Zola lakini alikaza sauti  yake 

“P102 Zola! Over..” Alisema Zola 

“Over!! Zola, za miaka mingi rafiki yangu” Alisema Sande  Olise huku ile sauti ya ukakamavu ikiwa imetoweka baada ya  kugundua aliyekuwa akimpigia alikuwa ni rafiki yake kipenzi,  Mafunzo waliyoyapokea huko Mexico waliambiwa kitu pekee  wanachotakiwa kukiepuka ni urafiki sababu usaliti wa Nchi  huanza kirafiki hatimaye kuwa janga la Taifa, hivyo  waliheshimu misingi hiyo, ndiyo sababu ya kukaa Miaka mingi  bila kuwasiliana. 

“Nzuri ndugu yangu Sande, upo wapi siku hizi?” Alihoji Zola “Nipo Botswana uhamishoni, nina kitengo cha siri huku” 

“Pole kwa majukumu! Ulisikia juu ya kifo cha Makam wa Rais na  Matukio yanayoendelea huku?”

“Nimesikia Zola, najua Mtaalam wa kazi utakuwa upo mzigoni,  lakini hao mnaopambana nao sijui kama ni saizi yenu, walikuja  huku Miaka mitatu iliyopita lakini balaa lake ni kubwa sana,  wameuwa makomando 50, na taarifa nyingine zimefichwa”  Yalikuwa ni maelezo ya Sande Olise 

“Sande hali ni tete sana, hili jambo ni zito na hawa jamaa  wana mtandao Mkubwa sana Duniani, kupambana nao ni sawa na  kutupa jiwe gizani, wanauwa kama hawana akili nzuri” 

“Ha!ha!ha!” Alicheka Sande 

“Mbona unacheka Sande” 

“Hao jamaa wanamafunzo maalum nasikia Mkuu wao anaitwa John  Brain, huyo Brain ndiyo mwalimu wa Osama Bin Laden,  anajihusisha pia na Alqaeda…Ni ngumu kumtambua kwa sura ila  alama kubwa ni vidole viwili wanavyoviacha wakiwa wamefanya  mauwaji, Mimi nipo Uhamishoni, majukumu yamepungua nakula  bata tuu sababu Mimi huku ni Bosi” Alisema Sande, lengo kuu  la Zola lilikuwa ni kumshawishi Sande arudi Nchini ili  washirikiane kupambana na Mafia Gang sababu Sande ni Mtu  pekee anayeweza kumuamini 

“Sande lengo langu la kukupigia na kuhitaji msaada wako  katika kazi hii ngumu niliyonayo, kuna uhusiano Mkubwa sana  kati ya Rais wa Nchi na hawa Mafia Gang, ni hatari kwa sasa,  siwezi kuinusa kwa pua zangu” 

“Unataka nije kufa huko? CCP ina Wanafunzi wengi tulioenda  Mexico kipindi kile, ni Mimi tu Zola?” 

“Hadi nakupigia wewe nina uhakika kazi hii tutaiweza kabla  mambo hayajaharibika zaidi, ujio wako utakuwa wa siri sana  ili tupeleleze kwa kina ni jambo gani lipo nyuma ya kapeti” 

“Ooh! Zola unajuwa siwezi kukukatalia, nitakujulisha nipe  siku tatu” 

“Over!” 

“Over!” Simu ilikatika mara moja, Zola akawa na tumaini la  Ujio wa Sande Olise ambaye waliwahi kumuita Duma wakimaanisha  ni Mtu mwenye kufanya mambo kwa haraka sana. 

Zola akaelekea kitandani na kujipumzisha huku picha ya Rais  ikiwa katika macho na akili yake, alimuwazia Rais huyo. Akiwa  bado hajapata Usingizi Zola alipokea ujumbe wa simu kuwa  Askari aliyezungumza naye na kumpa taarifa juu ya Mfungwa aliyefungwa katika Gereza la Ikulu ameuawa kwa kupigwa Risasi  akiwa ndani ya Kituo hicho, alishtuka kisha aliamka na  kuwasha taa, muda huo huo simu kutoka kwa Dawson iliingia 

“Zola umeisikia hiyo taarifa?” Aliuliza Dawson 

“Ndio nimeipata muda huu” Alijibu Zola kisha simu ilikatika 

“Uuups!” Zola alivuta pumzi zake, taswira mbili zilimjia kwa  haraka haraka kuhusu mauwaji yale, upande mmoja ulimwambia  kuwa Rais ndiye aliyekuwa akihusika na mauwaji yale lakini  upande mwingine ulishindwa kumpa majibu ya kwanini Mafia Gang  wanafanya matukio yale, Kichwa chake kiliwaka moto. 

Asubuhi mapema aliamka na kueleka kituo cha polisi, akakuta  hali ya huzunii ikiwa imetanda miongoni mwa polisi, Zola  akauliza ni Nani aliyefanya Mauwaji yale, cha ajabu alikuwa  ni mmoja wa polisi ndiye aliyemuuwa yule polisi, Zola  akashika kiuno chake kwa mshangao, akapelekwa alipohifadhiwa  Askari Muuwaji, hakutaka kuzungumza na Askari huyo akamwambia  polisi mmoja amletee Mafaili ya kesi iliyowahusu Robert,  Sandra na Bosco sababu ndio chanzo cha kuingizwa yeye katika  majukumu yale mazito, akaondoka kituoni na kurudi katika  Makazi yake ya siri, akayachoma moto mafaili hayo huku  akiamini kuwa matukio yote yale yalifanywa kwa lengo la  kupumbaza jeshi la polisi ili wasijikite zaidi, walifanikiwa  kuwapoteza lakini Zola aliinusa hatari hiyo huku akijiuliza  Mafia Gang wanataka nini katika Nchi yao. 

Muda huo huo Hekeheka ndani ya Kichwa Cha Zola iliongezeka,  alijikuta akiwa katika hali ambayo ilihitaji matumizi makubwa  ya akili kuliko chochote kile. Kijasho chembamba kilikuwa  kikimtoka kwenye paji lake la uso, picha ya askari aliyeuawa  ilizunguka katika akili yake huku akijiuliza ni nani alitoa  maagizo ya Askari yule kuuawa, alijuwa fika kuwa askari  aliyemuuwa Askari mwenzake alishinikizwa kufanya hivyo, bado  aliamini Rais alikuwa mhusika namba moja wa mauwaji yale,  akatoka nje huku akiwa anatazama taswira ya jua lilivyokuwa  likichangamsha bustani yake ndogo katika Makazi yake,  pembezoni kulikuwa na njiwa waliokuwa wakiruka na kulia kwa  kupokezana. 

Zola akaingia kwenye gari yake, akaelekea kituo cha polisi,  safari hii alihitaji kumbana askari yule aliyemuuwa mwenzake,  akaelekea chumba ambacho alihifadhiwa askari huyo kisha  akaomba polisi wote waondoke, wakabakia wawili tuu. 

Zola alimtazama askari aliyekuwa akimtazama Zola kwa sura  kavu iliyojaa umakini, hakuonekana kujuta kwa kitendo kile  hata kidogo, Zola akamshika kichwa Askari huyo akamuuliza

“Nani amekuagiza umuuwe Askari mwenzako?” Aliuliza Zola huku  akizidi kuvuta nywele za Askari huyo aliyefungwa pingu  mikononi kwa nyuma 

“Nani yupo nyuma ya tukio hili? Sababu najuwa huwezi kufanya  hivi pasipo agizo maalum, huyu Askari alinieleza siri  aliyoijuwa….Nina imani hata wewe unaijuwa hiyo na ndiyo  sababu ya kumuuwa Askari mwenzako!!” Aliuliza tena Zola baada  ya kuona swali la kwanza halikujibiwa 

“Fanya uliwezalo Zola, fanya tuu lakini siwezi kukwambia  chochote zaidi tu ya kusema, nimemuuwa bila kuagizwa na Mtu  yeyote” Zola akachukua rungu la polisi akawa anampiga polisi  huyo sehemu za mbavu ili kuhakikisha anasema ni nani  aliyemtuma kufanya mauwaji ndani ya kituo hicho cha polisi.  Askari huyo alikuwa akipiga kelele za maumivu, Zola  aliendelea kumpiga hadi akawa anatema damu mdomoni, Zola  alionekana kujawa na jazba sana. Muda huo simu yake iliita,  ikawa auheni kwa Askari huyo ambaye alikuwa akipunguza sauti  ya kulalamika. 

Zola akatupa lile rungu chini kisha akasogea ukutani  akaipokea simu hiyo ambayo ilimfanya Zola kwanza awe mtii,  mwenye kufuata maagizo, simu hiyo ilitoka ikulu, Zola alikuwa  akizungumza na Rais aliyeitwa Jacob Zagamba. 

“Nakuja Mkuu” Alisema Zola kisha simu ilionekana kukatika,  kijasho kilichokuwa kinamtoka Zola kilimwagika hadi kwenye  singlendi yake nyeupe 

“Shiti!!” Akasema kisha akamtazama yule Askari ambaye alikuwa  akicheka kwa maumivu makali, Zola akachukua shati lake kisha  akaondoka pale mara moja. Safari hii Zola alikuwa akielekea  Ikulu kuitika wito wa Rais wa Nchi hiyo, akiwa kwenye gari  akawasha Intaneti kisha akampigia simu ya Video Sande Olise  aliyeko Botswana, bahati nzuri simu ilipokelewa haraka sana  na Sande Olise 

“Sande!! Mkuu wa Nchi ameniita, naelekea Ikulu sasa” Alisema  Zola huku akiendelea kukanyaga mafuta kuelekea Ikulu. 

“Nayaamini maneno yako, kuna mawili unaweza itiwa hapo, moja  kuhamishwa kwenda Nchi nyingine au kuonywa” 

“Kwa vyovyote Rais ni mhusika nambari moja wa Matukio yote,  hajui kama ninafanya kazi na Dawson” Alieleza Zola 

“Safi sana! Mchezo umeisha hapo, soma kauli yake kisha  jiongeze Zola….Kifo chako kinaweza kutokea leo baada ya kukoswa sana Miaka mingi tulipokuwa tukifanya Operesheni  Upepo, ulikuwa Simba usiyejulikana unayelipigania Taifa lako,  Dawson anahitaji pongezi kwa kuwaficha Askari tunao tumika  kwenye idara kwa siri sana vinginevyo tungekuwa tunakufa kama  Kuku huku tukizungukwa na siasa Chafu” Ilikuwa ni sauti ya  Sande Olise akizungumza kwa unakini mkubwa. 

“Kama Maisha yangu yatakoma leo Ikulu, Sande uje kufanya hii  kazi kuliokoa Taifa mara moja” Alisema Zola kisha chozi  lilimtoka, akakata simu hiyo. Visa vya baadhi ya Askari  kupotea vilikuwa vingi katika Taifa hilo, Zola baada ya Masaa  mawili alikuwa akikaguliwa kwa ajili ya kuingia Ikulu,  ilikuwa ni mara ya kwanza Zola kuitwa na Rais huyo, si Rais  huyu Pekee bali Zola hakupata kujulikana na Rais yeyote  aliyepita, hii ilimpa shaka sana Zola kwanini Rais ampigie  simu wakati ambao alikuwa akimbana yule Askari amwambie  ukweli kuwa Nani anafanya Mauwaji yale.  Comments zikiwa nyingi naachia ya 7 leoleo

Nini Kitaendelea? USIKOSE SEHEMU YA SABA  USISAHAU PIA Kununua Kitabu Cha KOTI JEUSI Kupiga Namba+255760871896 Ufikishiwe Mpaka Ulipo

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

SOMA RIWAYA YA MSALA HAPA

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa 

  Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx   Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx   Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx   Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx

38 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version