IlipoishiaKuna kundi linaitwa MAFIA GANG, ni kundi maalum kwa ajili ya  Ugaidi…Mkuu wa kundi hili anaitwa John Brain ni mzungu  anayeishi Uskochi, Kazi yake ni kuratibu mauwaji. Amefanya  kazi katika Nchi nyingi na sasa yupo hapa Nchini ndiye  anayeratibu mauwaji ya viongozi kwa maslahi yake binafsi.  Mwaka 2003 nchini Congo walifanya mauwaji mengi sana,  nakuamini Zola ndio maana nataka ufanye upelelezi wa kina,  ukomeshe kabisa kundi hili hapa Nchini” Yalikua ni maneno ya  Mzee Dawson yalitoka na moshi wa sigara. 

“Kila kitu kipo tayari kwa ajili yako Zola, unahitaji  kuikomboa Nchi yako. Nakufahamu vizuri linapokuja suala la  kesi tata” Akamaliza kwa kumtakia kila la Kheri kwenye jukumu  lake zito la kuliondoa kundi la MAFIA GANG lakini kichwani  bado alikua anauwaza ule mkasa wa akina Robert, akajiuliza  waliingiaje huko na nini kilipelekea? Endelea 

SEHEMU YA PILI 

“Oooh! Jesus!” Akasema Zola huku akilikodolea macho gari la  kifahari la Mzee Dawson ambalo lilikua likitokomea, mkononi  alikuwa ameshikilia bahasha nyeusi ambayo ilikua maalum kwa  ajili ya kazi za siri, alijua ni vitu gani vitakuwepo kwenye  Bahasha hiyo. 

Safari ya Inspekta Zola ilimchukua masaa takribani matatu  kufikia yalipo makazi yake ya siri ambayo alikua akiyatumia  kwenye upelelezi kila alipopata kazi ngumu mbele yake alijificha kwenye makazi hayo ambayo aliyapa jina la HOME  TOWN. 

Lilikua ni jumba lililopo karibu na fukwe ya Bahari ya Hindi,  alichagua eneo hili sababu lilikua tulivu sana, licha ya kuwa  ni eneo ghali sana lakini alimudu gharama ambazo alikuwa  akilipiwa na kitengo cha Siri cha Mzee Dawson ( MPA ) 

Akabandua karatasi zilizopo kwenye ubao maalum, kisha  akabandika karatasi nyeupe akachora kwa kalamu na maandishi  yakapata kusomeka kama MAFIA GANG akimaanisha ndio kwanza  alikua akiingia kazini kwa ajili ya kupambana na kikosi hicho  hatari cha Bwana John Brain. 

Ilikua tayari usiku umeshaingia, akapiga simu kwa Waangalizi  wa zile maiti Hospitali kuwa hazipaswi kutolewa hadi pale  upelelezi utakapo kamilika, Hivyo familia zisubirie kwanza  kabla ya maiti za akina Robert kupatikana kwa ajili ya  mazishi, alikua na lengo lake ndani ya kichwa chake  kilichojaa nywele za mvi, akakuna kidevu chake baada kuwa  tayari ametoa maelekezo muhimu sana. 

Inspekta Zola licha ya kuwa umri ulikua umeenda kidogo lakini  alikua akipenda sana visichana vidogo vidogo, akaondoka  kwenye makazi yale akaelekea Baa kwa ajili ya kupata mvinyo  na kuangalia Mwanamke wa Kustarehe naye usiku huo. 

Akaagiza White Wine huku akikodolea macho baadhi ya visichana  vilivyokua ndani ya Baa hiyo, alipomaliza kunywa akawa  ameshapata Msichana wa kustarehe naye usiku huo ambapo  akaelekea Kwenye Hoteli moja iliyopo mita kadhaa kutoka  kwenye makazi yake ya siri. Akastarehe naye kisha akamuondoa  usiku huo huo, akabadili hoteli ambako alilala hadi asubuhi. 

Aliamka na uchovu kiasi, akapata Kahawa kisha akaondoka  hotelini hapo akaelekea Hospitali, akaagiza iletwe maiti ya  Sandra. Akaanza sasa kuikagua rasmi kwa kutumia jicho lake  kali la kijasusi, akiwa amevalia miwani yake ya macho  akagundua jambo, akaagiza mkasi na kisu, akavalia gloves  kwanza. 

Akawaambia Watu wa Maabara waongeze mwanga wa taa, wakafanya  hivyo. Akaona alama kwenye sura ya Sandra ambayo ilionesha  kuwa sura ile haikuwa halisi. Akafwatisha ile alama kwa kisu  ndipo akaona sura ikijivua. Wote waliokuwa ndani ya chumba  cha Maabara wakaingiwa na ganzi, lilikua ni jambo lililo  hitaji umakini wa hali ya juu zaidi.

Sura ilipovuka wakaikuta sura nyingine kabisa, pale pale  akavua gloves akachukua simu na kupiga picha kisha akapiga  simu kwenye kitengo cha siri cha Mzee Dawson ( MPA ) 

“Nahitaji wataalam wa Maabara haraka sana kwenye Hospitali ya  ST. James karibu na chuo cha Biashara” Ilikua ni sauti yake  iliyojaa umakini zaidi, haraka wale wataalam wakawa  wamewasili hospitalini hapo 

“Chunguzeni maiti mbili za Robert na Bosco, vueni sura zao za  Bandia kisha mpige picha mnitumie” Akawaachia maagizo,  Inspekta Zola akaondoka pale Hospitalini akiwa na jambo jipya  ndani ya akili yake, sasa ndio akawa na mashaka juu ya wapi  walipo Akina Robert wa ukweli na kwanini wale wajitoe muhanga  kupoteza maisha yao? 

“Kuna jambo limejificha sio bure” Akasema Inspekta Zola akiwa  kwenye gari yake, alikua akielekea ofisini kwa Mzee Dawson  ambaye ni mtaalam wa Taarifa kutoka usalama wa Taifa. 

“Naam! Zola , kuna jipya umeligundua?” akauliza Mzee Dawson  baada ya kukutana ana kwa ana na Inspekta Zola 

“Dawson!! hili jambo lina mchakato wa hatari unaohitaji  utulivu zaidi” 

“Hilo ndilo nililotegemea kulisikia kutoka kwako Zola, hii  sio kazi ya kitoto ndio maana nimeileta kwenye meza yako,  umekutana na kazi nyingi za hatari na zote umefanikiwa, hili  haliwezi kuwa jepesi pia” 

“Maiti zile zina sura za Bandia, inaonesha kuna mwamvuli wa  Kifo uliotumika hapa ili kupumbaza akili za kipelelezi” 

“Una maana maiti sio halisi kwa sura tambuliwa?” 

“Ndio, hii moja wapo” Akamuonesha sura iliyokutwa kwenye  maiti iliyotambuliwa kama Sandra. 

“Wauwaji ni Watu wenye akili kubwa sana na inaonesha ni  wazoefu wa hii kazi Zola, unatakiwa kuwa makini sana endapo  watakugundua hali itakua mbaya, unatakiwa upate sura ya  Bandia ili kuficha uhalisia wako” Akasema Mzee Dawson  akionesha kuanza kulitazama jambo hilo kwa jicho la tatu. 

******** 

Ndani ya Uwanja wa ndege wa Kimataifa, Six na yule Mdada  aliyejitambulisha kwa Inspekta Zola kama Judith lakini huku alikua akiitwa Malaika walikua wakisubiria ugeni ndani ya  Uwanja huu. 

Malaika alikua kwenye sura yake halisi, akionekana kama mdada  mwenye majivuno sana, shingo yake ilikua na tatuu ya maua ya  rangi aina ya Rose, iliwabidi kukaa hapo kwa zaidi ya nusu  saa. Punde wakapata kumuona Mtu waliyekuja kumpokea, alikua  ni Mzungu mwenye kibegi kidogo. 

Safari ya kutoka Uwanja wa ndege kuelekea kwenye makazi yao  ya siri ilianza, Mzungu alipofika kwenye gari akavua sura  bandia. Yes! huyu ndiye John Brain ambaye idara nyingi za  Usalama Duniani zilikua zikimtafuta lakini ilikua ngumu sana  kumnasa, licha ya kuwa yeye ndio Bosi wa kundi la MAFIA GANG  lakini pia alikua akipokea oda kutoka kwa Mabosi wake ambao  walikuwa wa siri sana. 

“Umefanikisha kuchukua nyaraka?” akauliza John Brain huku  akiwa anaiweka ile sura ndani ya begi lake dogo ambalo  lilikua na sura nyingine za Bandia ambazo alikua akizitumia  mara kwa mara ili kuficha utambulisho wake. 

“Nimefanikisha lakini kuna Mpelelezi mmoja makini anafwatilia  jambo hili” 

“Dammn!! niliwaambia mnatakiwa kwanza kusafisha kikosi cha  Usalama wa Taifa ndipo kazi nzito ianze” John Brain akachukua  nyaraka na kuanza kuzipitia, alifahamu lugha zaidi ya 20  hivyo hakupata shida pindi alipokuwa akiratibu mpango fulani  kwenye Nchi tofauti tofauti. 

  • •••••••• 

Ndani ya Ikulu, Mzee Dawson alikua akifanya mazungumzo na  Rais wa Nchi ili kujua wamefikia wapi. Ilikua ni lazima  wadhibiti MAFIA GANG kabla haijaleta mpasuko na taharuki kwa  Wananchi, tayari Watu ambao hawakua Usalama wa Taifa walianza  kufa, vifo vya Askari 15 ndani ya kituo cha polisi ilikua ni  miongoni mwa taarifa zilizomkasirisha sana Rais. 

“Dawson! Unasifika kwa Ujasusi, tayari kazi hii iko mikononi  mwako na hakuna namna tunaweza kufanya bali kusikiliza  maendeleo yako” Yalikua ni maneno ya Rais, Mzee Dawson alikua  akichezea karamu kuonesha alikua akitafakari namna ya  kumjibu, Rais akagonga meza kama ishara ya kuhimiza kupata  jibu kutoka kwa Mzee Dawson 

“Kazi iko kwenye mikono yangu Mkuu, ni lazima nilifyeke kundi  hili kabla halija leta madhara zaidi”

“Madhara zaidi? tayari wameleta madhara na hofu imetanda kwa  watendaji wa Serikali, najiuliza ni Watu wa namna gani hawa  wameweza kuingia kwenye nyumba ya Msaidizi wangu ( Makam wa  Rais ) na kufanya mauwaji bila Askari na walinzi wengine  kujua, hali sio shwari Dawson” Rais akapaza sauti iliyoambata  na kukauka kwa koo lake, akahitaji maji ya Baridi kutoka  kwenye friza, Dawson akampatia maji kwenye glasi, yalikua ni  maongezi ya siri kati ya Dawson na Rais huyu. Baada ya  kumaliza kunywa glasi moja ya maji baridi, akawa ametuliza  mzuka wake. 

“Dawson! nakuamini” akasema Rais akiwa anaweka glasi juu ya  meza kisha akavuta tai yake 

“Sitakuangusha Mkuu ni jukumu langu zito, nimekula kiapo  kuilinda nchi yangu” akasema kwa utii na heshima kubwa mbele  ya Rais huyu Kijana 

“Wanataka nini?” 

“Mapema tutalibaini hilo, kuanzia hapo tutawadhibiti Mkuu.  Wamefanya mauwaji Nchi nyingi lakini hapa wameingia sehemu  isiyo salama kwao, nakuhakikishia nitawafyeka haraka  iwezekanavyo” 

“Dawson! Nchi inakuangalia wewe na kitengo chako cha Usalama  wa Taifa” Akamaliza kwa kumrunusu Dawson akaendelee na  majukumu yake mazito, jasho likiwa linamvuja…Mzee Dawson  akachukua Lifti kushuka chini, akaingia ndani ya gari yake. 

Jua lilikua tamu sana siku hii, hali ya ubaridi ikiwa  inachukua nafasi kubwa. Inspekta Zola akaelekea nyumbani kwa  Marehemu Robert, Waombolezaji walikua wengi sana lakini Zola  akahitaji kuonana na Mama yake na Robert, akaoneshwa mahali  ambapo Mama huyo alikuwepo. 

“Pole Mama, Naitwa Inspekta Zola nafikiri unanikumbuka?”  akaongea baada ya kuketi, akahitaji kuzungumza na Mama yake  Robert pekee, waombolezaji wengine wakaamriwa kutoka. 

“Mara ya Mwisho ulionana wapi na Robert?” Mama akafuta chozi  lake, akajiweka sawa kuongea 

“Nilizungumza na Robert kupitia simu, akaniambia nije huku  kwa ajili ya harusi yake. Nilichelewa kufika huku kutokana na  mazingira yaliyo nje ya uwezo wangu, Alinisistiza sana  natakiwa kuwepo lakini nilifika siku ya harusi…” 

“Ulionana na Mwanao baada ya kufika?”

“Hapana, alipofika kanisani hakupata hata kunitazama. Ndio  tukio likatokea…” 

“Mwanao alikua anafanya kazi gani?” 

“Robert alikua na duka la kuuza Maua mjini, ndio biashara  yake ya muda mrefu” 

“Unamfahamu vipi Bosco?” Mama akaanza kulia, Zola akajitahidi  kumtuliza 

“Bosco ni kama Mwanangu, walikuwa wakija pamoja kunitembelea,  sijui wamepatwa na nini hadi wakauwana” Inspekta Zola  alipomaliza kuzungumza na Mama Robert, akaelekea kuonana na  Mzee Dawson ambaye alimpigia simu kuwa kuna ujumbe kutoka kwa  Rais 

Ndani ya mkoba wa Inspekta Zola kulikua na sura za bandia  ambazo alikua amepewa na Mzee Dawson ili kuficha uhalisia  wake, alipofika kwenye gari akaivaa kisha akaelekea kuonana  na Dawson. 

Kama kawaida yao walikutana sehemu iliyojificha huku wakipata  pombe ambayo kwao waliita kama kifungua kinywa, sura ya Mzee  Dawson ilikua imekosa neema ya furaha, tabasamu lake  halikuonekana hata chembe na kumfanya Zola atamani kusikia  kutoka kwa Mzee Dawson ( Google ) 

“Hali ni mbaya Zola, Mkuu amewaka sana leo anahitaji kazi  iishe ndani ya muda mfupi vinginevyo anaweza akaajili Watu  kutoka nje ya Nchi kwa ajili ya upelelezi wa kina kuhusu  MAFIA GANG” akasema kwa sauti iliyotoka kwa vituo vituo huku  akiwa anameza funda za pombe 

“Dawson! umenipa kazi ndani ya masaa 24, ndani ya Upelelezi  huu kuna visa tata sana ambavyo vinahitaji umakini wa hali ya  juu sana vinginevyo tutakuja kupoteza kila kitu” 

“Kuna Mtu nitakuunganisha naye, ni rafiki yangu wa muda mrefu  anaitwa Pacho…atakusaidia baadhi ya mambo ili kuendana na  muda” 

Punde simu ya Mzee Dawson ikaanza kuita, akaisikilizia kwa  miito mitatu kisha akaipokea na kuiweka kwenye sikio lake  lililojaa Usikivu wa kupokea taarifa, alichokisikia  kilimshtua sana mara simu ikakatika. 

“Barabara namba 8 kuna mauwaji yametokea ya Afisa wa Usalama  akiwa anatoka kanisani” Ilikua ni sauti ya Mzee Dawson  iliyotawaliwa na utulivu sana

“Ooh God” 

“Ndio hivyo Zola, hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa wiki hii  na kuendelea” 

“Ngoja nielekee eneo la tukio” Inspekta Zola akajikusanya na  kuondoka pale akimuacha Mzee Dawson akiendelea kugida pombe  kali. 

Yalikua ni majukumu yake ya kazi, akafika eneo la tukio na  kuukuta mwili wa Afsa aliyeuwa ukiwa juu ya daraja, gari ya  Afsa huyo ikiwa imesimama katikati ya Barabara na kusababisha  msongamano. 

Taratibu za kiusalama zikaanza mara moja huku mwili  ukichukuliwa na kupelekwa Hospitalini, mara simu ya Zola  ikaingia ujumbe kutoka kwa wataalam wa Maabara kutoka kwenye  kitengo cha Siri cha Mzee Dawson kilichoitwa MPA, akapewa  taarifa juu ya Maiti ya Robert na Bosco. 

Milii ile ilikuwa ndio pekee yenye sura halisi tofauti na  Maiti ya Sandra ambayo ilikutwa na sura bandia, akajikuta  akiwa njia panda hajui aanze na lipi amalizie lipi, simu yake  ikaingia ujumbe mfupi kutoka kwenye namba ambayo ilikuwa ya  siri 

“ZOLA TOKA ENEO HILO HARAKA SANA” Ujumbe ulisomeka hivyo,  akajaribu kutafakari kwa kina lakini hakupata majibu kwa  haraka, akajaribu kuujibu ujumbe huo lakini hakufanikiwa  kupata majibu. Kwa akili yake ya kipelelezi akajuwa mara moja  yupo Mtu anayemuona pale, haraka akaondoka pale na kuelekea  kwenye gari lake ambalo lilikuwa kando na eneo lile, mara  akasikia mlipuko mkubwa. Alipogeuka akaona gari moja ikiwa  inawaka moto, ndio gari ambalo alikuwa karibu nalo pale  alipokuwa amesimama eneo la tukio. 

Hapo akafanikiwa kujua kuwa kuna Watu wanamfuatilia kwa  karibu sana lakini akawa na maswali mengi kuwa ni nani  aliyemuokoa kwenye ile hatari? Mlipuko ulisababisha majeruhi  wengi sana ambao walikuwa ni Askari na wapita njia. 

Alipofika kwenye gari yake akapata shahuku ya kutaka  kumfahamu aliyemuokoa kwenye kifo, akachukua simu yake na  kujaribu kuujibu ule ujumbe lakini hakupata majibu mengine,  akamtafuta Mzee Dawson na kumtaarifu juu ya tukio hilo la  mlipuko 

“Aliyekuokoa anaitwa Pacho, ndiye msaidizi wako kwenye  majukumu”

“Oooh! niliona kifo changu pale” 

“Kuwa makini sana, Watu wa Usalama wanauawa sana….” yalikua  ni maneno ya mwisho ya Mzee Dawson kisha simu ilikatika,  ikampa wasaa Inspekta Zola kuelekea kwenye makazi yake ya  Siri karibu na ufukwe. 

Masaa mawili baadaye yalimkuta Inspekta Zola akiwa amekalia  kiti kwenye makazi yake ya siri, mbele yake kulikuwa na meza  nyeusi ngumu iliyotengenezwa kwa kioo. Alionekana kuzama  kwenye lindi la mawazo, akafikiria namna Muuwaji alivyokuwa  akifanya mauwaji kila kukicha, bado alitakiwa kujuwa ni wapi  alipo Sandra wa Ukweli kama Bosco na Robert ni Watu halisi,  presha ya Rais ya kulazikisha kazi ifanyike upesi  ilimkasirisha sana. 

***************** 

Anga lilibadilika kuwa jeusi machoni pa Idara za usalama wa  Taifa, Mauwaji ya Polisi na Maafisa yalitaarifiwa kila kona  ya Jiji, Hofu ikachukua nafasi kubwa kila mmoja akijiuliza ni  nani atafuata Kufa. Ujio wa John Brain Nchini ulikuwa na  lengo moja kubwa, akakutana na Vijana wake wawili  aliowatumainia sana mmoja aliyeitwa Six na mwingine aliyeitwa  Malaika akawaambia 

“Wakati Polisi wanahangaika kutafuta ufumbuzi wa vifo hivi  vya utata sisi tutakuwa bize kumalizia mpango wetu hapa  Nchini, Rais wa Nchi hii alitutuma kazi na tumeimaliza sasa  kwanini idara yake inamshikilia Jamaal?” Alihoji John Brain 

“Huyu Kenge anayeitwa Zola atakuwa kikwazo kikubwa sana  kwenye mpango huu, lazima aondoke kwanza” Alisema Malaika  akakumbuka jinsi Inspekta Zola alivyo makini 

“Udhaifi wa Zola ni Wanawake, kilevi chake kitamuuwa muda  mchache ujao” Alisema John Brain aliyeonekana kujaza mambo  mengi kichwani pake 

“Kazi hiyo niachieni mimi” Six akaomba apewe huo mpango wa  kuondoa uhai wa Inspekta Zola 

“Unatakiwa kuwa makini sana sababu kwa namna alivyo huyo Mtu  si rahisi akamuamini Mtu kwa Mara ya kwanza, unapaswa pia  kujuwa kuwa ukibainika basi kila kitu kitaharibika. Zola ni  Jasusi mbobezi, kabla hujampeleleza anakuwa tayari  amekupeleleza.” Alisema John Brain, kisha Malaika kasema

“Zola anatumika kama Mwanvuli wa Serikali katika kutekeleza  mipango ya siri, najiuliza aliwezaje kukwepa mtego wa Bomu” 

Nini Kitaendelea? USIKOSE SEHEMU YA TATU  USISAHAU PIA Kununua Kitabu Cha KOTI JEUSI Kupiga Namba+255760871896 Ufikishiwe Mpaka Ulipo

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

SOMA RIWAYA YA MSALA HAPA

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa 

  

  

2 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version