IlipoishiaAaaah Zola” ilisikika sauti upande wa Mzee Dawson, ikionesha  alikuwa akijigeuza. 

“Hebu fanya taratibu tuonane ana kwa ana Mzee Dawson, nahisi  kuchanganikiwa sasa” Zola alikata simu bila kusikiliza sauti  ya Mzee Dawson, baada ya hapo akapiga simu sehemu nyingine  ndani ya kitengo cha siri cha Mzee Dawson kinachoitwa MPA,  akaomba madaktari waweze kufika eneo la tukio, akawapa Ramani  kamili lilipo eneo hilo.  Endelea

SEHEMU YA NNE

Hakuwa na muda wa kukaa pale, akatoka taratibu hadi nje,  akayaangalia vizuri mazingira yale kwa jicho na akili ya  kipelelezi akajua tu kifo kile kimetokea masaa machache  yaliyopita na kwa vyovyote mwenye chumba kilichokuwa  kinaangaliana na mlango lilikofanyika tukio atakuwa labda  amesikia au kuona chochote kile, akakumbuka kuwa mlango huo  ulifungwa na funguo kuondolewa, akajiuliza haraka akiwa  analitazama dirisha la Chumba jirani 

“Kama funguo imetolewa maana yake kuna Mtu amefunga mlango na  kumfungia Mtu ndani, Nani amefanya hivi?” Akapata akili ya  kusogea chumba cha jirani, alipogonga akatoka yule Msichana  ambaye alimuelekeza chumbani kwa Anastanzia, yule Mdada  alipomuona Zola akaanza kujishebedua kwa kuhisi kuwa Zola  alikuwa akimtaka, alionekana kuvutiwa na Mzee Zola kutokana  na muonekana wa kitajiri alionao bila kujuwa kuwa alikuwa  amesimama mbele ya Mtu hatari kwa upelelezi 

“Nilijua tu utakuja kwangu, Anastanzia sio aina ya Mwanamke  ambaye anakufaa wewe. Wazee kama nyie mnatakiwa kupetiwa  vizuri ili msiwe na mawazo ya kufa kufa” Alisema huku  akitabasamu mbele ya Zola, kisha Zola akamuuliza yule  msichana

“Mara ya mwisho umemuona Anastanzia lini?” Mdada akaacha  kujishebedua baada ya Zola kuonesha sura ya mbuzi 

“Wiki sasa sijamuona ila rafiki yake si umeonana nae? Maana  nimekuona ukitoka humo ndani” Zola akatoa kitambulisho cha  uaskari akamuonesha yule mdada kisha akamuuliza 

“Unaitwa nani?” Mdada akawa anatetemeka 

“Naitwa Scolastica” 

“Rafiki yake Anastanzia amekufa, naomba uniambie ni nani  umemuona akiingia au kutoka mle ndani kabla yangu Mimi” 

“Kulikuwa na Mkaka mmoja hivi, aliingia kisha akafunga mlango  akatoka, sikumuona tena” 

“Anafananaje?” 

“Mrefu kiasi, mweusi ana rasta” 

“Sikia, watakuja polisi kuchukua mwili wa Marehemu, asante  kwa ushirikiano wako” Zola akaingia kwenye gari yake  akatokomea eneo hilo, akawasiliana na Mzee Dawson ili wapate  kukutana na kuzungumza, Mzee Dawson kama kawaida yake  akamueleza Zola wakutane sehemu ya siri. 

Alipofika Zola, Mzee Dawson aligundua ni jinsi gani Zola  alikuwa katika nyakati ngumu ambayo hakupata kumuona nayo,  akamimina mvinyo kwenye glasi na kumpatia, akapiga funda moja  la mvinyo ukawa umeisha kwenye Glasi, kisha akaitua Glasi  hiyo mezani kama Mtu aliyechoshwa na kinachoendelea. 

“Dawson! Hili jambo ni zito sana, kulifahamu lilipo kundi la  Mafia Gang, na kuwajua Watu hao inakuwa kazi ngumu sana.  Sijui ni mafunzo ya namna gani watu hao wanapatiwa kabla ya  kutekeleza jambo fulani” Alisema Zola huku akakunja midomo  yake, akampa Glasi Mzee Dawson ili amuongeze mvinyo,  ukamiminwa mvinyo kwenye Glasi ya Zola haraka kisha Dawson  akakaa vizuri ili amjibu Zola, kwanza akajikoholesha kisha  akasema 

“Mauwaji yaliyofanywa na Mafia Gang huko Congo yanatisha  sana, hapa bado kabisa hawajavuruga kisawasawa! John Brain  kama lilivyo jina lake ni Mzungu hatari sana Zola, nahisi  yupo hapa Nchini na kuna mpango wanautekeleza, umejaribu  kufuatilia ni mafaili gani yaliibiwa na huyo Msichana katika  kituo cha polisi” Zola alitikisa kichwa kuashiria  hakufuatilia suala hilo, Dawson akapiga tena fundo la Mvinyo  kisha akabeua kidogo

“Zola ninayemjua Mimi hawezi kukosa kujuwa mambo kama hayo,  akili yako haipo kabisa Zola, John Brain ana akili sana na  anachezea ubongo wako! Huenda ameshakujua na kukufuatilia,  anachofanya ni kukuchezesha, hapa kuna mambo mawili huenda  yanafanyika kwa wakati mmoja” 

“Mambo gani hayo?” 

“Wananunua Muda wako na muda wa Wapelelezi wengine ili  watekeleze mipango yao, hata haya mauwaji yanayotokea huwenda  wanakuhadaa ili usipate muda wa kutuliza akili yako, wanajuwa  wewe ni hatari kiasi gani, hilo lipo wazi Zola” 

“Hili suala linaninyima usingizi Dawson, nahisi nipo katika  chumba chenye giza ambacho siwezi kuona kuna nini ndani yake  hata kusikia sauti inayonipa ishara, nahisi kushindwa” 

“Ha!ha!ha! Zola, huwezi kukata tamaa mapema hivi, umekula  kiapo cha kulinda Taifa hili ikiwemo kupambana na Watu aina  ya John Brain, nafikiri muda unaenda, umekuja na gari yako?” 

“Ndio” 

“Tuitumie sasa hivi” 

“Tunaenda wapi?” Aliuliza Zola huku akimtazama kwa makini  Mzee Dawson ambaye tayali alionekana kuwa ameshaanza kulewa  lakini alimjuwa sawa sawa jinsi alivyo, akilewa huwa anaamuwa  mambo kwa kutumia akili sana. 

“Tunaenda Hospitali kuruhusu ile Maiti moja iliyosalia kwenda  kuzikwa” 

“Tutawapa vipi Maiti ambayo si yao, kumbuka ile ni Maiti ya  Anastanzia na sio Sandra” 

“Tunairudisha sura ya Bandia kama ilivyo Mwanzo, huu sio  wakati wa wao kujuwa ukweli, acha waamini wanamzika Mtu wao”  Waliitumia gari ya Zola hadi walipofika Hospitali, tayari  maiti mbili zilikuwa zimeruhusiwa kwenda kwa wahusika ambazo  ni Maiti ya Bosco na Robert. 

Wakasimamia zoezi la kuveshwa sura kwa Mwili wa Anastanzia,  dakika chache muonekano ulibadirika, 

“Yes! Acha wamzike wanayemuamini huku sisi tukiwa bize  kufuatilia” Alisema Dawson kisha alikohoa kama kawaida yake,  Zola akampa kitambaa akawema mdomoni lakini alipokitoa  ilionekana damu katika kitambaa hicho cheupe kuashiria kuwa  mapafu ya Mzee Dawson yalikuwa katika hali mbaya

“Usijali” akasema Dawson, kisha Zola akapiga simu kwenye  familia ya Mama Sandra ili waende kuuchukuwa mwili walioamini  ni wa Sandra ili wakauzike. 

“Naingia kazini sasa Zola, tuna muda mchache sana kuhakikisha  Nchi inakuwa shwari” alisema Dawson na kumfanya Zola  atabasamu maana mzigo ulikuwa ukimuelemea sana. Siku  iliyofuata Mazishi ya Sandra yalifanyika, Zola alikuwa  miongoni mwa waliohudhuria lakini uwepo wa Zola msibani  ulikuwa na melengo makuu mawili, moja kuhakikisha familia  haitambui kama anayezikwa si Sandra, jambo la pili aliamini  kama Mpango ule ulisukwa basi wasukaji wangefika pale Msibani  kwa ajili ya kufuatilia, lakini Pia Zola alimtilia shaka Baba  yake Sandra akiamini anajuwa jambo fulani. 

Akiwa ameketi alivalia miwani nyeusi na sura ya Bandia kama  alivyoambiwa na Mzee Dawson kuwa Huenda Mafia Gang  wameshamjuwa ndio maana walitaka kumuuwa katika jaribio la  bomu, hakutambuliwa na yeyote pale lakini alionekana kuwa  miongoni mwa waliokuja Msibani, Watu walikuwa wengi mno. Kifo  kile kilishika mioyo ya wengi. 

Naam!! Zola alikuwa bize sana kuhakikisha anazungusha macho  yake kila kona, macho yake yakajikuta yametua kwa jamaa mmoja  ambaye naye alikuwa bize sana kuzungusha macho yake, Zola  hakufanikiwa kugundulika baada ya kubadilisha sura kisha  kuvaa miwani, ingehitaji utaalam mkubwa sana kumtambua.  Kilikuwa ni kipindi ambacho Msemaji wa Familia alikuwa  akiwashukuru Watu waliokuja pale kwa ajili ya maziko ya  Sandra ambaye alizikwa pale pale nyumbani kwao, Zola hapo  ndipo akajithibitishia kuwa familia ya Sandra haikusanuka  kuwa walikuwa wakizika Maiti ya Mtu mwingine, lakini hakusita  kukubali uwezo wa Maadui zao ambao walifanikiwa kuuhadaa  ulimwengu wa vipofu ambao macho yao hayakuweza kuona mbali  zaidi ya Jicho la kipelelezi lenye mafunzo ya kijeshi ambalo  Zola alikuwa nalo. 

Kwa mantiki hiyo, Maadui walifanya tafiti zao kabla ya  kumtumia Anastanzia kuvaa sura ya Sandra maana miili yao  ilifanana sana ndio maana hawakuweza kuhisi kama kuna tatizo,  akashusha pumzi zake, alijuwa ilitumika akili kubwa sana pale  hadi Anastanzia akaingizwa kwenye mwanvuli ule wa Umauti,  swali lililomjia akilini mwake haraka ni wapi alipo Sandra  mwenyewe?. Aliporejesha macho eneo la yule jamaa aliyekuwa  akimfuatilia, aliona kiti kikiwa kitupu kabisa, akaangaza  huku na kule bila mafanikio yoyote ndipo akaona ni bora atoke  nje ili apeleleze yule jamaa ni nani na kwanini alikuwa  akichezesha yale macho ya kipelelezi, akamkubuka sawasawa  jamaa huyo mwenye upara na ndevu nyingi.

Alinyanyuka kutoka kitini kama Mtu aliyemaliza tukio la  mazishi, hakutaka kuonesha dalili zozote kuwa alikuwa  akifuatilia chochote maana aliamini Maadui walikuwepo pale  Msibani, akiwa anatoka aligongana na Mwanamke mmoja mrefu,  mweupe na mwenye nywele nyingi. 

“Samahani?” Alisema Mwanamke huyo ambaye alikuwa na uzuri wa  kutosha, macho ya Zola yakautalii mwili wa Mwanamke huyo bila  stara 

“Usijali!” Akasema Zola kisha akatoka pale taratibu bila  kugeuka nyuma. 

Yule Mwanamke alimtazama sana Zola hadi alipozama, kisha  akaketi kitini. Zola alipofika nje alimuona yule jamaa  akizungumza na simu kisha akaingia kwenye gari, Zola  hakuchelewa naye akaingia kwenye gari na kuanza kumfuatilia  jamaa huyo ambaye alionekana kutokuwa na wasiwasi wowote ule  maana hata alivyoendesha gari hilo ilionesha wazi kuwa  alikuwa katika hali ya kawaida, akaingia Barabara ya tano  kisha akashika barabara kuu ambayo ilikuwa ikitoka Uwanja wa  ndege kuelekea eneo ambalo lilikuwa na Hoteli nyingi za nyota  tano. 

Bila kupoteza muda Zola alimpigia Dawson simu, akamueleza  hali ilivyo kisha akasubiria jibu la Mzee huyo. 

“Washa GPS ya Gari” ilisikika sauti kutoka upande wa pili,  ikampa ishara Zola kuwa Mzee Dawson alikuwa na maelekezo  maalum ya nini cha kufanya. 

“Nakuona!” Alisema Dawson kisha alikata simu mara moja, baada  ya dakika tano akampigia tena na kumwambia 

“Fuata maelekezo yangu, kuwa makini hao Watu wana akili ya  ziada sana wakati mwingine Watu hawaamini kama Huyo Mzungu ni  Binadamu, wana akili iliyozidi…unaweza kuwa umetegwa, kabla  ya kutoka Msibani hakuna ishara tata?” Alimpa wakati wa  kufikria, Zola akasema 

“Nilikuwa makini kuliko kawaida, hakuna aliyeniona ila wakati  natoka…” Ukimya ukatawala, Mzee Dawson akamuuliza Zola 

“Enhee ilikuwaje?” Zola akafikiria alipokuwa akitoka pale  aliparamiana na Mwanamke mmoja mzuri sana, hakutaka kulisema  hilo akiamini sio ishara ya kumueleza Mzee Dawson 

“Sio ishara!” 

Nini Kitaendelea? USIKOSE SEHEMU YA TANO  USISAHAU PIA Kununua Kitabu Cha KOTI JEUSI Kupiga Namba+255760871896 Ufikishiwe Mpaka Ulipo

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

SOMA RIWAYA YA MSALA HAPA

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa 

  Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx   Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx   Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx   Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx

7 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version