Robert akiwa kwenye gari lake alianza kulia, akashindwa hata  kuendesha akaamua kusimama kando ya Barabara akiwa  anabubujikwa na machozi. 

Machozi yakawa yanamtiririka Robert huku akizidi kulia kwa  uchungu mkubwa, jua lilikua likiwaka huku Watu wakiendelea na  shughuli zao lakini kwa Robert ilikua tofauti sana, alijikuta  yupo kwenye kisa chenye utata sana. 

Alikua amevalia Suti nyeusi, kiatu cheusi lakini sura yake  hofu na hali ya majuto ilikua imetanda sana. Akajikuta  akipiga usukani kutokana na hali aliyokuwa nayo, akageuka  nyuma ya gari. 

Kulikuwa na Mwili wa Mtu uliokuwa ukivuja damu, mwili huo  hapana shaka ulikuwa ni wa kike kwani ulikuwa na vazi la  Shela. 

Robert akaliondoa gari pale kando ya ile barabara, sasa akawa  barabarani kuelekea alipokusudia huku ile hali ya kulia ikiwa  imekata. Simu yake ilikua ikiita mno lakini hakutaka  kuipokea, Alipofika mbele akaachana na barabara kuu akaingia  barabara ya vumbi ambayo ilikua ikielekea ufukweni. 

Robert alipofika juu ya kilima akaongeza mwendo  akalitumbukiza gari hilo ndani ya bahari na kuzua taharuki  kwa Watu waliokuwa upande mwingine wa ufukwe, kelele na  taharuki vikaamka pale Ufukweni, Watu wa uokozi wakawa tayari  kwa ajili ya kuzama majini kulitoa gari hilo. 

Kwa muda mfupi lile gari lilikuwa limezama ndani ya yale maji  ya Bahari ambapo kwa upande ule kulikuwa na kina kirefu  ambacho Watu walikuwa hawaendi kuogelea, Punde polisi wakaja  pale huku Watu wakiendelea kupigiana simu kuwa kuna gari  limezama ndani ya Bahari, kilikuwa ni kituko kwa kila  aliyesikia, kila Mtu akataka kujua ilikuwaje.

Polisi wakazungusha utepe wao kuashiria kuwa eneo hilo  halikuwa salama kwa wakati huo, ziliwachukua zaidi ya dakika  45 waogeleaji kuchopoa miili miwili. Moja ilikuwa ni ile ya  kike na nyingine ilikua ni ya Robert, gari ya huduma ya  kwanza ikaichukua miili ambapo yote ilikuwa tayari haina  uhai. 

Taarifa hii ikawa na mkanganyiko mkubwa kwa Watu walioisikia,  haikuhitaji uchunguzi mkubwa sana kugundua kuwa walikuwa ni  Wanandoa au watarajiwa, mwili wa Mwanamke ulikutwa na risasi  shingoni. 

“Ufanyike uchunguzi haraka sana kuhusu hili tukio” Akaagiza  mkuu wa Upelelezi. 

  • •••••••• 

Vilio vilikuwa vimetanda ndani ya kanisa moja lililopo  katikati ya Jiji, tayari polisi walikuwa wamefika na kuukuta  mwili mwingine uliokuwa umejeruhiwa kwa risasi, ulikuwa ni  mwili wa Mwanaume mmoja ambaye alitambulika kama Bosco, naye  alikuwa amevalia suti. 

Polisi wenyewe walipigwa na butwaa kwa jinsi hali ya vilio  ilivyokua imetanda ndani ya kanisa hilo kubwa na lenye hadhi,  Watu wengi walikuwa wakisimuliana kilichotokea hapo. 

Mama mmoja alikua akilia kwa uchungu huku akiutikisa mwili wa  Bosco uliokuwa umeloa damu, shati jeupe alilovaa lilikua  limetapakaa damu mno. 

“Mwanangu mimi! Eeeh Mungu mtihani gani huu umenipa mimi leo  tena mbele ya Kanisa” Sauti ya kilio iliyotoka kwa kwikwi  ilimtoka Mama huyo, mmoja wa Askari akapata shahuku ya  kumfuata huyo Mama. 

“Pole Mama!” Akasema huku akiwaambia watu wa Huduma ya kwanza  wauchukue ule mwili kwa ajili ya taratibu za kiupelelezi  zaidi. 

Lilikua ni pigo lililoamsha kilio chake, Mwili wa Bosco  ulikuwa ukiwekwa kwenye gari maalum kwa ajili ya kuupeleka  Hospitali, mkononi Askari huyo aliyejitambulisha kama  Inspekta Zola alikua ameshikilia karatasi yenye majina ya  Watu waliopoteza Maisha kwenye kisa kile cha kutisha. Jina la  Robert lilikua la kwanza, la pili ni Sandra na la tatu ni  Bosco. Akajiuliza Watu wale walikua kwenye kisa gani  kilichopelekea vifo vyao.

Akamfwata Mtu mmoja aliyekua amekaa kando, alikua amejitenga  sana na wengine. Kupitia jicho la Kipelelezi Inspekta Zola  akagundua jambo, alipomfikia akamuuliza 

“Nini kimetokea?” Ilikua ni kama vile ameamshwa kutoka kifo,  akajikuta akishtuka sana. Naam! alikuwa ni Mdada mwenye sura  ya upole, mweupe mwembamba, kwa jinsi alivyovaa ilikua rahisi  kutambua kuwa hakua miongoni mwa Watu waliofika kwa ajili ya  ile shughuli pale Kanisani. 

“Unaitwa nani?” 

“Judith!!” 

“Huonekani kama mmoja wa Waalikwa hapa, kimekuleta nini?”  Swali hili likaambatana na jicho kavu la kipelelezi 

“Mimi?” 

“Ndio wewe kwani naongea na nani?” Mdada akakaa kimya bila  kujibu chochote huku akionesha kutetemeka, Yule Askari  akamchukua Mdada kwa ajili ya mahojiano zaidi pamoja na  baadhi ya Watu ambao walitambulika kama ndugu wa Bosco ambaye  amefariki kwa kupigwa risasi. 

Ilikua ni siku ya majonzi sana, vilio vilitanda hadi kituo  cha polisi ambapo baada ya polisi kuwataka watulie ndipo  vilio vilipokoma. 

“Nini kimesababisha vifo vyao?” Aliuliza Inspekta Zola ambaye  alikua makini, mbele yake kulikua na Ndugu zake Bosco na  wengine ambao walijitambulisha kama ndugu wa Sandra, yule  Mdada alikua amekaa pembeni akiwa katika hali ya hofu. 

“Inatisha na kusikitisha Afande, marafiki walioshibana leo  wanauwana” akaongea Mama yule ambaye alifahamika kama Ndiye  Mama yake na Bosco, kilio kilianza tena ikabidi sasa Inspekta  Zola amuondoe Huyo Mama kwasababu asingeliweza kuzungumza  chochote zaidi ya kilio. 

“Nini kimetokea?” akauliza tena Inspekta Zola akiwatazama  walioko mbele yake, mmoja akatikisa kichwa ishara ya kuwa  hajui hasa kilichosababisha vifo vya Watu watatu, Inspekta  Zola akapata wazo la kumuuliza yule Mdada, akamuita 

“Nini kimetokea?” Akamuuliza yule Mdada ambaye hata baada ya  kuulizwa alikaa kimya kwa kitambo kidogo kabla ya kuanza  kuzungumza. 

Chozi likianza kumbubujika akajikuta akianza kuongea.

“Mapenzi! Najiuliza kwanini yameumbwa, kwanini yanatesa,  yanafanya Watu wawe maadui, watu wapoteze furaha walizonazo!  Ni mapenzi” Kila mmoja alikaa kimya baada ya huyo Mdada  kuanza kuzungumza, Familia zote zilizopo pale polisi zilikaa  kimya kumsikiliza Mtu ambaye hawakumfahamu. 

“Huyu ni Muongo” Akadakia Dada Mmoja aliyekuwa akibubujikwa  machozi 

“Hebu subiri aongee alafu sisi tutapima maneno yake kama  yamejaa ukweli au uwongo” akaongea Inspekta Zola 

“Nawaomba polisi mufanye kazi yenu lakini sio kusikiliza  maneno ya Mtu huyu, Mdogo wangu Sandra hakuwahi kuingia  kwenye vita ya Mapenzi, anaongea Uwongo Mtupu…” 

“Mpaka hapa tunapozungumza hakuna aliye hai ambaye anayeweza  akatueleza kilichotokea, ni vema tukamsikiliza huyu Binti” 

“Una maanisha nini? Mdogo wangu Robert amekufa?” akauliza kwa  Mshituko kuhusu Robert ambaye mwili wake uliopolewa Baharini  baada ya kulitosa gari lake ndani ya Bahari. 

“Sandra na Robert wamekutwa wakiwa tayari wamekufa ndani ya  maji, ndio maana nasema tukae kimya kumsikiliza ili kama kuna  ukweli unazungumzwa basi ndio utatupa uelekeo wa kujua chanzo  cha vifo hivi vya Kutisha” Akajibu Inspekta Zola, taarifa  ikaamsha tena vilio 

“Nilijua Robert atakuwa salama jamani” 

“Nini kimetokea Robert Mwanangu…Nini Babaaa??” 

“Bosco mlikuwa mnaficha nini kwenye maisha yenu wanangu?”  Zilikuwa ni sauti zilizojaa vilio hadi Inspekta Zola akaamuru  sasa watolewe nje ili afanye mahojiano na huyo Mdada ambaye  alionesha kufahamu baadhi ya mambo! 

“Judith sitaki uingie matatizoni, unaonekana sio mtu  mbaya…sura yako inaonesha hujahusika kwenye jambo hili  lakini unafahamu kitu..lisaidie jeshi la polisi, nini  kimesababisha vifo hivi vya kutisha na ilikuwaje pale  kanisani?” Chozi likaanza kumbubujika Judith akiwa anamtazama  Inspekta Zola ambaye alikua makini kusikiliza atakacho  kisema. 

“Judith…unafahamu nini kuhusu Maisha ya Bosco, Sandra na  Robert?” akauliza tena Inspekta Zola lakini bado Judith  aliendelea kulia.

“Mapenzi yamefanyaje Judith? wewe ni sawa na binti yangu na  huwa naumia sana kumuona Binti kama wewe ukiingia kwenye  matatizo” 

Judith akajifuta mchozi uliokua ukitiririka kwenye mashavu  yake akavuta hewa kama Mtu mwenye mafua kisha akamkodolea  macho Inspekta Zola 

“Tupo mimi na wewe tu, tuongee kama Mtu na Baba yake  Judith…Nini kimetokea?” Kauli hii ikamfanya Judith avute  hewa, akajisikia uhuru fulani wa kuzungumza. Macho ya  Inspekta Zola yaliyokomaa Kijasusi yakawa yana Mmulika Judith  ndani ya Chumba kimoja cha mahojiano. 

“Unawafahamu vipi hawa Watu?” aliuliza tena Inspekta zola  tena bila kuchoka 

Judith akanyanyua kinywa chake ili aanze kueleza  kilichotokea, mara mlango ukafunguliwa akaingia Polisi mmoja  aliyevalia sare za kipolisi, akapiga saluti kwa Inspekta  Zola. 

“Ripoti ya uchunguzi wa miili ya Marehemu wote Watatu”  Akaongea polisi aliyeingia, akamkabidhi baasha Inspekta Zola,  akaifungua ili asome ripoti hiyo. 

Akazisoma ripoti zote lakini ripoti ya mwili wa Sandra  ilimshangaza kidogo licha ya kukutwa kwa risasi sehemu ya  shingo pia Mwili ulikutwa na tatuu ya jina la Bosco upande wa  kulia wa paja lake lakini pia upande wa kushoto wa paja lake  lilikutwa jina la Robert. Inspekta Zola akamtazama yule  polisi kisha akarudisha macho yake kwa Judith, akawa na  maswali mengi yaliyohitaji majibu ya haraka. 

“Sandra alikua na mahusiano na Bosco na Robert kwa wakati  mmoja?” 

“Ndio” 

“Je, Robert na Bosco walikua wakijuana kwenye penzi la  Sandra?” 

“Hapana” 

“Walikua marafiki walioshibana sasa waliwezaje kuishi kwenye  penzi la Mtu mmoja?” Akauliza Inspekta Zola, kisha akatazama  saa yake tayari usiku ulikua umeingia.

“Afande utahakikisha anakua salama huyu binti hadi kesho  asubuhi” akasema Inspekta Zola kisha akaondoka zake pale  kituo cha polisi, Judith akachukuliwa kwa maelekezo maalum ya  Inspekta Zola akapelekwa sehemu ili apumzike ndani ya kituo  kile cha polisi. 

  • •••••••• 

Nyumbani kwenye familia ya Robert bado vilio vilikua  vimetawala kila mmoja akijiuliza Robert alikua amepatwa na  nini hadi akawapiga risasi Sandra na Bosco, wote walishuhudia  tukio hilo ndani ya kanisa. Ndugu walikua wakifika kwa ajili  ya mazishi ya Robert, pia upande wa Bosco hali ilikua hivyo  hivyo, pia kwa Sandra hali ikawa hivyo hivyo. 

Hakuna aliyejua hasa sababu ya Marafiki hawa walioshibana  kuangukia kwenye kivuli cha Umauti. 

Baada ya kutoka kituo cha Polisi Inspekta Zola akaelekea  nyumbani kwake, siku hii hakuwa katika hali ya kawaida bali  kwenye tafakari nzito kuhusu kisa kile kizito ambacho kilikua  mikononi mwake. Taarifa iliyopo kwenye meza yake ilikua ni  Robert kumpiga risasi Bosco, kisha kumpiga risasi Sandra na  kwenda kujitosa ndani ya Bahari. 

Akiwa kwenye chumba chake maalum kwa ajili ya upelelezi  akaanza kuvuta picha tofauti tofauti ambazo alikua  akizifikiria lakini hakufanikiwa kupata picha halisi ya tukio  lile, umri wake wa miaka 60 ulitosha kumwambia kuwa kisa kile  kilikuwa na simulizi ya kusisimua ndani yake. 

Akachukua karamu na karatasi akaandika ” ROMEO NA JULIET”  kisha akafuta kwa kuamini kuwa visa hivyo ni tofauti,  akamaliza kwenda kitandani na kujitupa, akajigalagaza hadi  Usingizi ulipomchukua. 

Asubuhi jua likiwa tayari limetoka akaamshwa na mlio wa simu  yake ya mkononi iliyokua pembezoni mwa Kitanda chake. Akaamka  na kuipokea, akajua kuwa siku ilikua imeanza. Akajiandaa na  kuelekea kituo cha polisi, akaelekea moja kwa moja chumba cha  mahojiano akamkuta Judith akiwa anamsubiria. 

Kabla hajaanza na Judith, akaikuta baasha pale mezani, hapana  shaka ilikua ikimsubira yeye. Alipofungua akakutana na ujumbe  mwingine uliomkata maini yake, Naam! haraka akachomoka pale  na kumuacha Judith akiwa kwenye uangalizi, akachukua gari  yake ndogo na kuelekea Hospitali ambako maiti zilikua  zimehifadhiwa.

Akaiomba maiti ya Sandra, ikaletwa kwenye chumba maalum kisha  paja la Sandra likafunuliwa, akaiona Tatuu yenye jina la  Bosco kisha akaifungua ile taarifa iliyopo kwenye baasha  akagundua ufanano wa jambo fulani, pale pale simu yake  ikaita. Akaweka miwani yake vizuri kisha akaipokea hiyo simu 

“Zola! nafikiri umeupata Ujumbe wangu, Haraka sana anza na  upelelezi wa kina…Hawa marehemu watatu huenda wakawa  wanahusika na kifo cha Makam wa Rais” Ulikuwa ni ujumbe tata  sana kwenye kichwa cha Inspekta Zola, jasho likawa linamtoka. 

“Inawezekanaje? Wauwaji wakauwana wenyewe kwa wenyewe?”  Akauliza Zola 

“Zola, fanya upelelezi wako upesi. Idara yangu ya Usalama wa  Taifa inakuamini sana ndio maana sijaona Mtu wa Kumpa hiyo  kazi zaidi yako”. 

“Oooops! sawa Mkuu” Akajibu kwa utiifu wa hali ya juu sana,  Hofu ikatanda na hali ya tahadhari ikapanda kwenye kichwa cha  Inspekta Zola, akajua sasa alikua kwenye kazi rahisi  iliyogeuka kuwa ngumu kupita maelezo. 

Kwenye Tatuu ya Jina ka Bosco kulikua na alama ya vidole  viwili, alama hii ilikua maarufu sana miezi michache  iliyopita baada ya kutokea kwa vifo vingi vya Watu wa  Usalama, na viongozi wa juu wa Serikali, kila aliyeuawa  alikutwa na muuli wa alama ile ya Vidole, hapo ndipo wasiwasi  ulipoibuka baada ya kukutwa kwa Tatuu kwenye mwili wa Sandra. 

Mara moja simu ya Inspekta Zola ikaanza kuita, ilikua ni simu  kutoka kituo cha Polisi. 

“Unasemaje?” akauliza Inspekta Zola akiwa amesimama kando ya  maiti ya Sandra 

“Nakuja haraka sana” akasema Zola kisha akachukua gari  kurejea kituo cha Polisi, akasikia Milio ya gari za kubebea  wagonjwa kutoka kituo cha polisi, maiti zilikua zimezagaa  eneo la kituo cha polisi. 

Zola hakuamini macho yake, Polisi mmoja akamfwata Zola na  kumwambia kuwa yule Binti aliyekuwa akihojiwa ndani ya kituo  hicho ndiye aliyekuwa amesababisha madhara yale 

“Inawezekanaje binti dhahifu kama yule awashinde zaidi ya  Askari 15 na kuwauwa wote?” Akauliza Zola huku akiwa  anatazama jinsi maiti zilivyokuwa zikichukuliwa na kuwekwa  kwenye Magari ya kubebea wagonjwa.

“Inspekta, Binti anaonekana kuwa na mafunzo ya kimapigano na  ujasusi wa hali ya juu sana” Baada ya kusikia hivi Inspekta  Zola akaelekea ndani ya kituo, damu zilikua zimetapakaa huku  matundu ya risasi yakiwa kwenye miili ya askari waliokuwa  tayari wameuawa. 

“Amechukua baadhi ya nyaraka kwenye masanduku” akaongeza  askari ambaye alikuwa akimfwata Inspekta Zola kwa nyuma,  akaingia moja kwa moja hadi kwenye kile chumba cha mahojiano  ambacho alimuacha yule Mdada aliyejitambulisha kama Judith,  akaona kuna ujumbe juu ya meza, akaufungua ukiwa kwenye  baasha akakutana na ujumbe ulioandikwa “KIVULI CHA UMAUTI”  alafu alama ile ya vidole ikawa chini ya maneno hayo. 

“Uuupsss” Akashusha pumzi kisha akaketi kwenye kiti na  kuegemea ile meza 

“Ngoma hii ni ngumu sana kuicheza” akajisemea kwa sauti kuu  huku akitikisa kichwa chake. 

  • •••••••••••••••

Ndani ya Jengo moja refu zaidi katika Jiji hili, kulikuwa na  jamaa mmoja aliyeitwa Six, alikua ameketi huku akivuta sigara  yake, mwili wa Six ulikua na tatuu nyingi sana za rangi, simu  yake ilikua bize sana akionekana kupokea na kutoa taarifa. 

Mara akaingia Judith Mdada ambaye alikua kwenye kile kituo  cha polisi, alionekana kuwa mwenye msongo wa mawazo. Akafikia  kuketi kwenye sofa karibu na Six, Six akatikisa rasta zake 

“Mbona uko juu juu sana?” Akauliza huku akizima sigara yake,  akatoa moshi mwingi mdomoni 

“It’s a bit Strange ( Inatisha kidogo )” 

“Kumetokea nini?” 

“Walinishtukia ikabidi nipambane kujiokoa pale” 

“Oooh! Shit” Six akaongea kwa hasira sana, Mdada  aliyejitambulisha kwa polisi kama Judith akavua sura ya  bandia. 

“Hawajafanikiwa kukufahamu?” 

“Yes! hawajanifahamu”

“Ok! Malaika usiye na dhambi” akaongea huku akiwa anapokea  nyaraka zilizoibwa ndani ya kituo cha polisi. 

Nje kidogo ya Jiji hili, Inspekta Zola alikua akipokea kazi  kamili ya kuwasaka waliokuwa wakifanya mauwaji ikiwemo kifo  cha Makam wa Rais ambaye alipigwa risasi akiwa nyumbani kwake  na kuzua taharuki kubwa. 

Mbele yake alikua amesimama Mtu mmoja mwenye umri sawa na  wake, wote walikua Wazee wenye utaalam wa upelelezi, Mzee  huyu alijulikana kama Dawson maarufu kama Google. Jina hili  la utani alipewa sababu ya taarifa nyingi alizonazo ndani ya  kichwa chake, licha ya Mzee Dawson kuwa Mtu wa Usalama wa  Taifa pia alikua ana kitengo chake cha Siri alichokipa jina  la MPA ambacho kilikua kikidili na masuala ya Upelelezi wa  kesi kubwa kubwa ndani na nje ya Nchi. 

Walifanana sana tabia zao, walikua walevi wa sigara na  nyakati fulani walikua wakitumia pombe kali, ilikua ni  kawaida kwao tangu wakiwa vijana kwani kazi waliyokua  wakiifanya iliwafanya watumie akili nyingi ili kupambana na  uharifu, 

“Kuna kundi linaitwa MAFIA GANG, ni kundi maalum kwa ajili ya  Ugaidi…Mkuu wa kundi hili anaitwa John Brain ni mzungu  anayeishi Uskochi, Kazi yake ni kuratibu mauwaji. Amefanya  kazi katika Nchi nyingi na sasa yupo hapa Nchini ndiye  anayeratibu mauwaji ya viongozi kwa maslahi yake binafsi.  Mwaka 2003 nchini Congo walifanya mauwaji mengi sana,  nakuamini Zola ndio maana nataka ufanye upelelezi wa kina,  ukomeshe kabisa kundi hili hapa Nchini” Yalikua ni maneno ya  Mzee Dawson yalitoka na moshi wa sigara. 

“Kila kitu kipo tayari kwa ajili yako Zola, unahitaji  kuikomboa Nchi yako. Nakufahamu vizuri linapokuja suala la  kesi tata” Akamaliza kwa kumtakia kila la Kheri kwenye jukumu  lake zito la kuliondoa kundi la MAFIA GANG lakini kichwani  bado alikua anauwaza ule mkasa wa akina Robert, akajiuliza  waliingiaje huko na nini kilipelekea wauwane. 

Nini Kitaendelea? USIKOSE SEHEMU YA PILI 

SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA 

SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI 

SOMA RIWAYA YA GORYANAH HAPA 

SOMA KISASI CHANGU HAPA  

SOMA RIWAYA YA MSALA HAPA

JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa 

  

5 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version