Akiwa katika hatua ya robo fainali ya michuano ya mataifa barani Afrika na timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo) mlinzi wa kati wa klabu ya Simba Henock Inonga Baka ni wazi sasa uongozi wa klabu ya Simba unakuna vichwa kuona watafanya mbinu gani kumshawishi kubaki katika mitaa ya Msimbazi.

Tumeitazama michuano hii kuanzia hatua ya awali yaani ya makundi mpaka hatua hii ya robo fainali inayotarajiwa kuanza siku chache zijazo na hakuna atakayepinga kuwa Inonga amekua na kiwango bora sana ambacho mpaka kupata nafasi ya kuanza katika kikosi chao inaonesha si lelemama kwani DR Congo imejaa wachezaji wengi kutoka ligi kubwa barani Ulaya.

Kuna taarifa zimekua zinazagaa mitandaoni kwamba beki huyu kisiki amemalizana na klabu ya FAR Rabat kutoka nchini Morocco kwa mkataba wa awali ili akimaliza mkataba wake katika klabu ya Simba basi wamchukue na mara nyingi watu husema tetesi muda mwingine huwa ni kweli na ikumbukwe kuwa kikosi cha FAR kinaongozwa na kocha wa zamani wa klabu ya Yanga Nasreddine Nabi.

Ukiachana na kocha Nabi lakini pia inadaiwa Al Ahly ya Misri nao wameonyesha nia  kumtaka beki huyo mwenye thamani ya Dola laki tano ambayo sawa na shilingi bilioni 1.2 ambaye amebakisha mkataba wa mwaka mmoja ndani ya timu hiyo.

Hivi karibuni uongozi wa klabu ya Simba ambao ndio wamiliki halali wa mchezaji huyo umeweka wazi kuwa endapo itakuja ofa kubwa ya mabilioni ya fedha watatengeza msimamo na kuzungumza na klabu ambayo inahitaji huduma ya beki wao wa kimataifa, Enock Inonga Baka.

Kwa haya yote yanayotokea nadhani pia ni funzo kwa wachezaji wetu wa Tanzania kuamini na kuonesha kuwa wanatakiwa kupambana ili kuhakikisha kuwa wanapata mafanikio makubwa na kutumikia vyema vilabu vyao.

SOMA ZAIDI:Walioleta VAR AFCON Wana Nafasi Yao Moyoni Mwangu

2 Comments

  1. Pingback: Chama Amedhihirisha Kuwa Viongozi Simba Ni Wababaifu - Kijiweni

  2. Pingback: Safari Ya Afcon Na Heshima Kubwa Kwa Ligi Za Afrika - Kijiweni

Leave A Reply


Exit mobile version