Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema almanusura azimie baada ya wapinzani wao USM Alger kupata penalti katika fainali ya pili, hapo hapo anafanya maamuzi magumu ya kumpiga stop beki wake, Ibrahim Bacca aliyeisababisha japo penalti hiyo iliokolewa na kipa Djigui Diarra.

Nabi, aliweka wazi kuwa, baada ya tukio lile la Algeria ambapo Yanga ilishinda 1-0, lakini ikashindwa kubeba taji kwa kanuni ya bao la ugenini lililowabeba wenyeji wao, alikaa kikao na Bacca na kwamba kuanzia sasa hataki kumuona anafanya ‘Tackling’ tena karibu au ndani ya eneo la hatari.

Nabi alisema licha ya kwamba Bacca anazipatia ‘tackling’ lakini hatakiwi kuzifanya tena kwa kuwa Kuna wakati zinaweza kuwaletea shida kama ambavyo ilikaribia kuwaumiza dhidi ya USM Alger.

“Ilipotolewa Ile penalti nilihisi naweza kuzimia ilinishtua sana, unajua ilikuja penalti Ile wakati tunatafuta bao na hatukutakiwa kuruhusu bao lakini jambo zuri la kumshukuru Mungu kipa wetu (Diarra) alikuwa na siku nzuri kazini,” alisema Nabi na kuongeza;

“Nimemwambia Bacca kuanzia sasa sitaki kumuona tena anafanya kitu kama kile, sitaki kuona anafanya tekolingi ndani ya eneo la hatari au hata Karibu na hapo Kuna wakati huwezi kufanikiwa kama kilivyotokea.”

Nabi alisema anaruhusu Bacca kuendelea na njia hiyo ya uzuiaji kwa kuwa ni moja ya ubora wake lakini anatakiwa kufanyia mbali na eneo la hatari ambapo wanaweza kujipanga kuzuia kuliko kuzalisha matukio ya hatari kwa timu yao.
Alisema Bacca akiendelea kufanyia kazi dosari zake ndogondogo anaweza kuja kuwa beki bora na mkubwa hapa nchini kutokana na upambanaji wake.

“Nampenda sana Bacca ni beki ambaye anacheza kama mwanajeshi uwanjani muda wote anatamani kukaba hataki kuona mshambuliaji anapata utulivu lakini anatakiwa kuendelea kufanyia kazi dosari ambazo tunaendelea kuzifanyia kazi kwake.”

Endelea kufatilia taarifa zaidi za Michezo hapa.

Leave A Reply


Exit mobile version