Kwa miaka ya hivi karibuni kumekua na idadi kubwa ya wachezaji ambao wamekua wakijitokeza na kusema kuwa wana asili ya Tanzania na hivyo kuomba uraia ili kupata nafasi ya kuchezea timu ya Taifa yaani Taifa Stars. Ukiachilia mbali hao wanaojitokeza lakini pia wapo ambao Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania (TFF) huwafuatilia ili kuwashawishi kuchezea Taifa Stars.

Ukiwa mmoja ya wale ambao wanafuatilia michuano ya Mataifa barani Afrika (AFCON) bila shaka utakua unajizuliza mengi kuhusu baadhi ya wachezaji ambao wamepata nafasi ya kucheza kabisa ambao wanaasili ya Tanzania.

Nadhani kwa sasa kama ambavyo tumejaribu kwa muda mrefu na imekuwa ngumu kupata wachezaji ambao watatuvusha kuelekea mbele zaidi kimataifa ni wakati sasa wa serikali kukaa chini na kulitazama suala hili la uraia pacha na faida yake haswa katika ukuwaji wa soka la Tanzania na timu ya Taifa katika michuano mbalimbali watakayokuwa wanashiriki.

Ishu hii ya uraia pacha kwa wanamichezo ni kati ya mijadala ambayo imekuwa ikiibuka na kupotea huku wadau wakitamani kuona suala hilo likipitishwa ili wachezaji wenye asili ya Tanzania waanze kutumika kwa kasi kwenye kikosi cha Taifa Stars.

Suala hili ni pana na limekuwa na mvutano wa aina yake hata kwenye vikao vya Bunge ambako sheria na kanuni mbalimbali za nchi zimekuwa zikijadiliwa na kufanyiwa maboresho lakini kwa bahati nzuri wakati hilo likiendelea ipo hadhi maalumu ya uraia ambayo inaweza kuanza kutumika. Hadhi hiyo inaweza kumfanya mchezaji mwenye asili ya Tanzania kuwa na uhalali wa kuitumikia Taifa Stars bila ya kulikana taifa lake jingine.

Wapo ambao watajiuliza kwanini sana watu wanahitaji uraia pacha utumike kwa Taifa Stars kwanza tufahamu kuwa hili ni jambo la kawaida katika timu za taifa duniani kote. Hata hivyo, kwa Tanzania, kuingizwa kwa wachezaji wenye uraia pacha kutakuwa na athari kubwa kwani watakuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya Timu ya Taifa ya Tanzania.

Kupitia mchango wao, timu itaimarika kimbinu, kiufundi, na kimchezo. Uzoefu wao katika ligi za kimataifa utachangia katika kuleta ushindani na kujenga heshima ya Tanzania kwenye jukwaa la kimataifa mfano mchezaji kama Haji Mnoga anayekipiga katika nchi ya Uingereza.

Tunafahamu namna ambavyo nchi yetu imebarikiwa kuwa na wachezaji wengi wazuri wanaokipiga ligi ya ndani na wale ambao wanakipiga katika baadhi ya ligi za nje ya Tanzania hii isitupe kiburi cha kuamini kuwa hao wanatosha kutuvusha katika mafanikio ya soka bali tuukubali Uraia pacha na kuwapa nafasi vijana wenye vipaji kutoka kote duniani kunaweza kuongeza kushindana kwenye michuano mikubwa zaidi. Hivyo, kuwekeza katika maendeleo ya wachezaji hawa na kuwajumuisha kikamilifu katika programu za maandalizi kunaweza kuwa msingi muhimu wa mafanikio ya baadaye.

Uraia pacha katika Timu ya Taifa ya Tanzania ni fursa muhimu ya kuleta mabadiliko na kuleta mafanikio makubwa. Kwa kuwaunganisha wachezaji wenye asili mbalimbali kwa lengo moja, Taifa Stars inaweza kuendelea kuchora sura nzuri ya Tanzania kwenye ramani ya mpira wa miguu duniani.

Hata hivyo, ni muhimu kwa timu za taifa kusimamia kwa busara mchakato wa kuingiza wachezaji wenye uraia pacha ili kuhakikisha wanachangia kikamilifu kwenye maendeleo na mafanikio ya timu bila kusababisha migogoro ya utaifa au kuvuruga umoja wa timu.

Kama ulikua hufahamu nikutaarifu kuwa sheria na kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na FIFA, wachezaji wanaoruhusiwa kuichezea Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) wanapaswa kuwa na uraia wa Tanzania pekee. Hii ina maana kwamba wachezaji wanaotaka kuwakilisha Tanzania lazima wawe na uraia wa Tanzania na wasiwe na uraia wa nchi nyingine.

Sheria hii inaweza kutofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine, na kila shirikisho la mpira wa miguu linaweza kuwa na kanuni zake. Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo, wachezaji wanaweza kupata uraia pacha kulingana na sheria za nchi husika. Hii inaruhusu wachezaji kuwa na uraia wa zaidi ya nchi moja na bado wanaweza kuichezea timu ya taifa ya nchi zote wanazohitaji kuchezea.

Wapo ambao wanapinga hili wakiwa na hoja ya kuwa kutokuruhusu uraia pacha kutadumisha utaifa na kuhakikisha kwamba wachezaji wanaowakilisha timu ya taifa wanaunganishwa kwa nguvu na utamaduni wa nchi husika. Pia, inaweza kuwa njia ya kuhakikisha kwamba mafanikio na heshima inayopatikana kupitia michezo inaunganishwa moja kwa moja na raia wa nchi hiyo.

Nadhani ni wakati sahihi sasa wa serikali kulifikiria upya suala hili la uraia pacha na haswa katika upande wa sekta ya michezo.

Endelea kusoma makala zetu mbalimbali kwa kugusa hapa.

Leave A Reply


Exit mobile version