Nyakati zinasogea sana. Mambo yanayotokea unaweza ukastaajabu na kuishia kuguna tu. Mnara kwa sasa unasoma katika mitaa ya Twiga na Jangwani, Tanzania nzima na pengine Afrika Mashariki yote baada ya klabu ya Yanga kukamilisha kuinasa saini ya nyota wa Zambia Clatous Chama  kutoka kwa watani zao na mahasimu wao katika soka la Tanzania Simba sports Club.

Kwa Chama ni kama ilivyo kwa mchezaji mwingine yeyote mashabiki wa Simba lazima waelewe hili. Majuzi hapa tulimsikia nyota wa Ubelgiji na Manchester City, Kevin Debryune akiizungumzia ofa aliyoahidiwa nchini Saudia. Ni pesa nyingi ambayo miaka 15 aliyocheza Ulaya hajaipata lakini Saudia anaweza ipata ndani ya msimu mmoja. Sasa nani anajua labda Chama ameahidiwa dau nono kutoka kwa mabwanyenye wa Jangwani?

Achana na upuuzi wa dau nono au ni usajili wa kukomoana kwa timu hizi mbili ambazo huitwa timu kubwa. Kinachonipa mashaka ni je majukwaa ya jezi nyekundu na nyeupe hayawezi kumgeuka mwamba wa Lusaka?

Ni mara chache sana inatokea katika duniani mchezaji fulani mkubwa kabisa ambaye alikuwa kipenzi cha mashabiki wa timu fulani kisha akahama na bado watu watamfuata na wengine wataendelea kuimba jina lake, kwangu mimi sijapata kuona mchezaji mwingine yeyote kando ya gwiji wa kandanda ulimwenguni Cristiano Ronaldo  ambaye anapendwa Sporting Lisbon, anapendwa Manchester United, anapendwa Real Madrid, anapendwa Juventus na sasa Dunia imehama nae Saudia kwenye klabu ya Al Nassr.  Kwenye viwanja vyote kuanzia Old Trafford, Santiago Bernabeu na Allianz Ronaldo ni mfalme.

Sasa je Chama anaweza akawa kama Cristiano Ronaldo? Ni swali. Kwa mashabiki wa Simba kumshangilia mchezaji wa Yanga au mashabiki wa Yanga kumshangilia mchezaji wa Simba haitofautiani sana sawa na jua kuzama mashariki, achilia mbali mashabiki wa Simba kuishangilia Yanga hilo ni sawa na kutukana kabila tena ni uchuro ambao haujapata kutokea tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

Swali lingine ambalo naendelea kujiuliza ni je ikiwa mashabiki wa Simba watamsaliti Chama je mashabiki wa Yanga watampenda kama ambavyo wa Simba walimpenda na kuimba jina lake miaka yote hii?

Mifano tunayo katika soka la kimataifa. Januari mwaka 2011 Fernando Torres alihama kutoka Liverpool na kujiunga Chelsea, kilichofuata baada ya hapo ni kusahaulika. Mashabiki wa Liverpool walikuwa wakiimba jina lake uwanjani Anfield kila mechi lakini alipoondoka walimuona msaliti, wao pia wakamsaliti na kumfuta mioyoni mwao. Torres kwa sasa haheshimiki Liverpool wala Chelsea kote huko anaonekana ni mchezaji mzuri wa kawaida aliyepita kisha akaondoka zake.

Mashabiki wa Barcelona hawajamsamehe Luis Figo mpaka leo tangu alipowasaliti akajiunga na mahasimu wao Real Madrid mwaka 2000. Tangu hapo hawamuhesebu kama alikuwa nyota wa timu yao. Katika pambano la El Clasco uwanjani Camp Nou walimtupia kichwa Cha nguruwe alipokwenda kupiga kona. Mashabiki wa Liverpool pia hawajamsamehe Michael Owen tangu alipojiunga na Manchester United mwaka 2009 na hapo hakutokea Liverpool moja kwa moja alizurula kwanza Rela Madrid kisha akajitia New Castle United kabla ya kuhamia kwa Sir Alex Ferguson ambako alishinda ubingwa wa ligi mara moja.

Ni wachezaji wachache sana ndio waliamua kubaki na timu zao na hawakutaka kuwakera  mashabiki zao kipindi walipotakiwa kuhamia mahala pengine. Nyumbani hapa tunae nahodha wa zamani wa Yanga Nadir Haroub Ally Canavaro, Mussa Mgosi na wachache wengine.

Barani Ulaya yupo Fransesco Totti, nyota wa zamani wa As Roma ya nchini Italia. Totti alizaliwa Roma, alisoma Roma, ameoa Roma, amecheza Roma na amestaafia Roma na huenda atafia hapo hapo Roma. Ukiwa katika jiji la Roma Totti ni kama Mfalme. Nilishuhudia hili nilipokuwa huko mwaka 2016😀. Kuna muda Totti alikuwa mkubwa kuliko timu lakini hakutaka kuwasaliti watu wa Roma. Wengine ni Paul Scholes na Ryan Giggs ndani ya Manchester United. Walianzia hapo na wakastaafia hapo.

Kwa Chama sioni kama mashabiki wa Yanga watampenda kama ilivyokuwa kwa  Simba kwa sababu umri wake umesogea na kiwango pia kinashuka na kibaya zaidi simuoni Chama atakayedumu na Yanga kwa zaidi ya misimu mitatu. Mashabiki watamfurahia tu kwa sababu ni kama ameikomoa Simba lakini sio kwa kile ambacho Chama atakitoa uwanjani.

Mpira wa kibongo unajulikana na hasa unapoona sajili za mchezaji aina ya Chama ndani ya Yanga. Ndio sawa unaweza kuongea lugha yoyote kwamba Chama anajua hilo halina ubishi ni mjinga pekee ndiye atakayebisha. Pamoja na hayo nani anajua labda sio usajili wa pendekezo la kocha Gamondi bali ni usajili tu wa viongozi fulani na kwa lengo fulani? Huenda Gamondi hakumtaka Chama hivyo tutegemee kutomuona Chama muda mwingi uwanjani kama ambavyo ilikuwa kwa Simba na hasa ukizingatia tayari Yanga inao kina Aziz Ki, Pacome,  na Max katika eneo la mbele.

Tusubiri na kuona kama Chama atakuwa kama Cristiano Ronaldo au atakuwa ni Fernando Torres mwingine atakayesahaulika? Kama atakuwa kama Ronaldo kongole kwake na ikiwa sivyo basi pole yake.

MUDA UTAONGEA.

Luqman Van Maliki

Chamwino Dodoma 

SOMA ZAIDI: Chama, Aziz Ki Na Pacome Watachezaje Yanga?

3 Comments

Leave A Reply


Exit mobile version