Historia ya Klabu ya Yanga SC inaanzia tangu enzi za miaka ya 1910 ingawaje historia kamili ilianza kuandikwa mwaka 1935.
Klabu hii ilitokana na desturi ya vijana wa Dar es salaam waliokuwa wakikutana viwanja vya jangwani kufanya mazoezi na baada ya muda wakaamua kuunda timu yao iliyojulikana kwa jina la Jangwani Boys.
Ndani ya kipindi kifupi timu hiyo iliteka hisia za wengi, waliojitokeza kujiandikisha uanachama wa klabu hiyo, miongoni mwao waliovutiwa na uanachama wa klabu hiyo ni Tabu Mangala (Sasa marehemu) na ilipofika mwaka 1926 walifanya mkutano wa kwanza katika eneo ambalo hivi sasa kuna shule ya sekondari ya Tambaza.
Miongoni mwa yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuiboresha timu hiyo ambayo wachezaji wake wengi walikuwa wafanyakazi wa bandarini na mashabiki wake wengi walikuwa wabeba mizigo bandarini.
Baada ya mkutano huo, timu ilibadilishwa jina na kuwa Navigation, iliyotokea kuwa moto wa kuotea mbali katika timu za waafrika enzi hizo, kabla ya uhuru wa Tanganyika. Timu kama Kisutu, Kitumbini, Gerezani na Mtendeni zilikuwa hazifui dafu kwa wana wa Jangwani hao.
Ikiwa inatamba kwa jina la Navigation, wanachama na washabiki wa timu hiyo walikuwa wanatembea kifua mbele na kuwatambia wapinzani wao, kwamba katika kipindi hicho wao ndiyo zaidi.
Kwasababu Italia ilikuwa inatamba kwenye ulimwengu wa soka wakati huo, wanachama wa timu hiyo nao waliamua kuibadilisha jina timu yao na kuiita Italiana. Italiana FC ilipata mafanikio ya haraka na haikushangaza ilipopanda ligi daraja la pili kanda ya Dar es Salaam. Mwanzoni mwa miaka ya 1930 Italiana waliamua kuachana na jina lao mapema kabla ya kuingia kwenye ligi hiyo, hivyo wakaanza kujiita New Youngs.
Kila ilipokuwa ikibadilisha jina, ilikuwa ikifanya vitu vipya pia, kwani wakiwa na jina la New Youngs waliweza kutwaa kombe la Kassum, lililoshirikisha timu mbalimbali za Dar es Salaam.
Mwaka 1935 uwezo wa Klabu ulishuka sana kusababisha wanachama kutofautiana na kuleta migogoro katika Klabu.
Mwaka 1936 utendaji na uwezo Klabu ulishuka sana na kusababisha mgogoro mkubwa wa wanachama ambao ulisababisha baadhi ya wanachama kujiengua na kuanzisha Klabu nyingine. Wanachama walioasi Klabu waliunda Klabu ilijulikana kwa jina la Queens F.C. ambayoa baadae ilibadirisha jina na kuitwa Sunderland ambayo kwa sasa inajuliakana kama Simba
Baada ya mgawanyiko wanachama waliobaki waliifanyia marekebisho Klabu yaliyopelekea kubadilisha jina kutoka New Youngs to Young Africans. Washabiki wengi walishindwa kutamka jina la Young kwa ufasaha ambao ilipelekea kuzaliwa kwa jina la “Yanga”.
Yanga kama timu ya wananchi ilileta hamasa sana katika nchi na kusaidia kuunganisha wananchi kipindi cha kupigania uhuru wa nchi. Yanga imekuwa na mafanikio makubwa sana tangu kuanzishwa kwake na inajulikana kama timu bora Tanzania.
Ikiwa na miaka Zaidi ya 85 imekuwa na mafanikio yafuatayo;
1. Washindi wa Ligi Kuu ya Tanzania mara 27- 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000, 2005, 2006, 2007–08, 2008–09, 2010–11, 2012–13, 2014–15, 2015–16, 2016–17
2. Washindi wa Kombe la Tanzania mara 4 – 1975, 1994, 1999, 2015–16
3. CECAFA Club Cup/Kagame Interclub Cup mara 5 – 1975, 1993, 1999, 2011, 2012
4. Kombe la Mabingwa la CAF – Imeshiriki mara 11
1997 – Hatua ya Mwanzo (Preliminary Round)
1998 – Hatua ya Makundi (Group stage)
2001 – Hatua ya Pili (Second Round)
2006 – Hatua ya Mwanzo (Preliminary Round)
2007 – Hatua ya Pili (Second Round)
2009 – Hatua ya Kwanza (First Round)
2010 – Hatua ya Mwanzo (Preliminary Round)
2012 – Hatua ya Mwanzo (Preliminary Round)
2014 – Hatua ya Kwanza (First Round)
2016 – Hatua ya Pili (Second Round)
2017 –
5. Kombe la Klabu Bingwa Africa – Imeshiriki mara 11
1969 – Robo Finali (Quarter-finals)
1970 – Robo Finali (Quarter-finals)
1971 – Ilijitoa Hatua ya Pili (withdrew in Second Round)
1972 – Hauta ya Kwanza (First Round)
1973 – Hatua ya Kwanza (First Round)
1975 – Hatua ya Pili (Second Round)
1982 – Hatua ya Pili (Second Round)
1984 – Hatua ya Kwanza (First Round)
1988 – Hatua ya Kwanza (First Round)
1992 – Hatua ya Kwanza (First Round)
1996 – Hatua ya Mwanzo (Preliminary Round)
Je, Hayo ndio mafanikio pekee ya Yanga SC?
Yanga katika Harakati za ukombozi wa Tanganyika na Muungano wa Tanzania chini ya mzee Nyerere na Karume 
YANGA ni klabu iliyoshiriki kwa nguvu katika kutafuta Uhuru wa Tanganyika ambao baadaye ulipatikana mwaka 1961 na kujiondoa kwenye mikono ya Waingereza waliokuwa watawala.
Sehemu moja ya kuonyesha kuwa kweli Yanga ilishiriki ni nembo yake ambayo hadi leo imekuwa na alama ya Bara la Afrika ikiwa ni sehemu ya kusisitiza kuwa Waafrika wanapaswa kujitegemea bila ya kuongozwa na watu kutoka nje ya bara hilo.
Wakati wa utawala wa kikoloni, hakukuwa na nafasi ya kutosha kwa Waafrika kusimama na kujieleza kuhusiana na walichotaka kwa uwazi, badala yake mambo mengi yalilazimika kufanyika kwa siri kuhofia adhabu kutoka kwa wakoloni.
Jina la Young African ilikuwa ni sehemu ya dhana, kwamba linawabeba Waafrika vijana, hivyo ikawa rahisi kuihusisha klabu na wazalendo waliokuwa wakitaka kwa dhati uhuru wa nchi yao ambao ulikuwa lazima upiganiwe.
Kuanzia mwaka 1951, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikaribishwa na wazee waliokuwa Yanga na walikuwa tayari kushirikiana naye. Baadhi yao ni akina Dunstan Omar, Sheikh Suleiman Takadir, Idd Faiz Mafongo, Ally Sykes, Abdulwahid Sykes, Juma Sultan ‘Mabosti’, Said Chaurembo, Sheikh Jumbe Tambaza, Bibi Titi Mohammed, Tatu Binti Mzee na wengine wengi.
Wakati huo Nyerere alikuwa mwalimu katika Sekondari ya St Francis (sasa Pugu), mikutano ilianza kufanyika kwenye makao makuu ya Yanga ikiwa inahamasisha Watanganyika kuzungumzia unyonge wao ndani ya nchi yao na baada ya hapo kuanza kudai uhuru.
Mkutano hiyo haikuwafurahisha wakoloni hata kidogo, mara nyingi walituma mashushushu na kutaka kujua kilichokuwa kikiendelea ndani. Lakini Nyerere na wenzake wa Yanga waliamua kubuni mbinu tofauti kuwakwepa.
Kwa kuwa hakukuwa na ujanja wa kuhama katika eneo hilo na kufanya mikutano kwingine, mbinu mbadala moja wapo ilikuwa ni kukifanya kikundi cha taarabu cha Jipisheni kuendelea kutumbuiza kila walipoanza vikao.
Kikundi hicho ambacho baadaye kilipewa jina la Egyptian Musical Club, kiliendelea kutumbuiza huku watu wakishangilia kwa nguvu.
Ingawa kelele zilikuwa juu, lakini Nyerere na wanachama wengine wa Yanga ambao pia walikuwa wanachama wa Tanu waliendelea na mikutano yao kuhakikisha wanafikia malengo.
Mwasisi wa kikundi hicho cha taarabu, Maalim Bom Hambaroni, yeye alijitolea ikiwa ni sehemu ya mchango wake na wanamuziki wa kikundi hicho wakakubaliana na hilo kila mmoja akiwa amepania kuona siku moja wanakuwa huru.
Baadhi ya wanamuziki wa kikundi hicho na wanachama wa Yanga walipokezana kuimba huku wengine wakipika chakula ambacho Nyerere, viongozi wa Yanga na wanachama wa Tanu walikula na baadaye kuendelea na vikao vyao hivyo vya ukombozi wa Tanganyika.
Mara kadhaa, katika baadhi ya mechi, klabu ya Yanga ilitoa kiasi cha fedha na kuhakikisha kinaisaidia Tanu katika mambo yake kadhaa ya kichama kwa lengo la kufanikisha upatikanaji wa uhuru.
Kutokana na ushirikiano wa juu aliokuwa akiupata kutoka Tanu na Yanga, Nyerere aliamua kuacha kazi yake ya kufundisha ili apate nafasi ya kutosha kupambana kusaidia kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika.
Alianza kuzungumza kila sehemu Tanganyika, dereva akiwa ni Said Tanu, ambaye alikuwa shabiki wa ‘kulia’ wa Yanga na aliwahi kueleza kwamba nje ya siasa, mwalimu alizungumza sana kuhusu mpira na Yanga ndiyo iliyokuwa ikiukosha moyo wake.
Baadaye kwa ushirikiano wa Tanu, wananchi wengi, Nyerere alifanikiwa ku ipatia Uhuru wa Tanganyika, rasmi Desemba 9, 1961.
Uhuru wa Zanzibar:
Uhuru wa Zanzibar pia Yanga ilishiriki kwa kuwa mwanamapinduzi namba moja, Abeid Amani Karume alikuwa anapenda sana mpira na ndiye mwanzilishi wa klabu ya African Sports ya Zanzibar.
Wakati fulani hata kabla ya uhuru wa Tanganyika, viongozi wa Yanga walialikwa Zanzibar na Karume. Wakiwa kule Yanga na African Sports, wakafanya mkutano wa kutaka kudumishwa undugu kwa watu wa Bara na wale wa visiwani.
Mikutano ilikuwa miwili, mmoja ulifanyika Zanzibar na mwingine ukafanyika Dar es Salaam, lengo lilikuwa ni hilo kusaidia kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika pia Zanzibar.
Mfano timu hizo ziliandaa mapambano mawili, moja likachezwa visiwani na fedha zikaichangia ASP kuendelea kupambana dhidi ya wakoloni, halikadhalika mechi nyingine ikapigwa Bara na fedha zikaisaidia Tanu kwa lengo lilelile.
Katika mechi iliyochezwa Kajengwa Makunduchi, Zanzibar na ile ya Ghymkhana (sasa Karume), watazamaji walikuwa wakiingia wanalipa kwa kuweka fedha kwenye vibubu moja kwa moja ili kudhibiti mapato.
Ndiyo maana hata baada ya Zanzibar kupata uhuru, Karume alikuwa akizialika ikulu klabu za Yanga, Simba, African Sports ya Tanga na ile ya Zanzibar kwenda kusherekea sikukuu mbalimbali kama Pasaka au Idd.
Kwa hayo hii ni sehemu ya kuonyesha Yanga ilishiriki kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa uhuru wa Tangayika, Zanzibar au Tanzania kwa ujumla na ndiyo maana ilipewa jina la timu ya wananchi.
Muungano:
Yanga inaelezwa kuwa sehemu iliyochangia kwa kiasi fulani kupatikana kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ulizaa Tanzania. Maana ndiyo zilichangia Nyerere na Karume kuwa karibu na suala la kuungana likaanza.
Kwa kuwa Nyerere na Karume, wote waliamini jambo moja kuwa kuungana ni kuongeza nguvu, hivyo waliweza kuzungumza kwa urahisi zaidi kwa kuwa waliona walikuwa na sera zinazofanana.
Hivyo suala la muungano halikuwa na ugumu na ikawa pia lahisi kwa Tanu na ASP kuungana na kutengeneza Chama cha Mapinduzi (CCM).
Leave A Reply


Exit mobile version