Achana na njia ngumu waliyopita Ivory Coast hadi kuwa mabingwa wa AFCON 2023 kuna njia nyingine ngumu aliyopita mfungaji wa bao la ushindi, Sebastian Haller kwani aliyaanza mashindano haya akiwa na majeraha ya kifundo cha mguu na hii ndiyo maana mechi za mwanzo alizikosa na baadaye akawa anatokea benchi huku mechi yake ya kwanza kuanza ilikuwa nusu fainali dhidi ya DR Congo ambapo alifunga bao la ushindi.

Na kwenye fainali pia akafunga bao lililobakisha kombe nyumbani litakalodumu katika vichwa vya wananchi wa Ivory Coast bila kusahau na mashabiki wa soka barani Afrika ambao walikua wakiitazama fainali kati yao na Nigeria.

Lakini hilo sio jambo kubwa zaidi kwake kwani moja kati ya kitu kikubwa na cha kishujaa ni ile ya kurudi uwanjani baada ya kushinda vita dhidi ya ugonjwa hatari wa saratani ambapo Julai 2022, baada tu ya kujiunga na Dortmund akitokea Ajax, Sebastian Haller aligundulika kuwa na saratani ya korodani.

Akafanyiwa upasuaji mara mbili na kupigwa mionzi mara nne ili kuondoa mfumo wake wote wa korodani ulioathirika na saratani ambapo kila tiba moja katika hizo ilichukua siku tano za kulazwa hospitali lakini Septemba 2022 akatoka hospitali na Oktoba mwaka huo huo akahudhuria sherehe za utoaji tuzo za Ballon d’Or jijini Paris ambapo yeye mwenyewe alikuwa mmoja wa wanaowania tuzo hiyo na alishika nafasi ya 13 kutokana na mafanikio yake akiwa na Ajax ikiwa pamoja na kuwa mfungaii bora wa ligi ya Uholanzi.

Alipewa nafasi ya kupanda jukwaani kukabidhi tuzo ya Yashin kwa kipa bora, Thibaut Courtois. Haller alionekana kuathirika na mionzi ya tiba na nywele zake zilinyonyoka vibaya.Siku hiyo ambayo mtangazaji wa Balon d’Or, Didier Drogba, ambaye ni shujaa wake, akamuomba aseme kitu kuhusu maendeleo ya afya yake. Akasema anaendelea vizuri na anatarajia kurudi uwanjani.

Mwezi wa 12 Sebastian Haller akarudi hospitali kufanya tena vipimo na madaktari wakamthibitishia kwamba amepona kabisa hivyo akajiunga na kambi ya timu yake kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi na Januari 22, 2023 akacheza mechi yake ya kwanza rasmi tangu ajiunge na Dortmund ambapo ilikuwa mechi ya ushindi wa 4-3 dhidi ya Augsburg kwenye Bundesliga na Haller aliingia dakika ya 60 akivaa viatu vilivyoandikwa “F*CK CANCER”.

Februari 2024 anaisaidia Ivory Coast kushinda AFCON baada ya kuwavusha hatua ya nusu fainali na kufunga bao la 2 la ushindi katika hatua ya fainali dhidi ya Nigeria.

SOMA ZAIDI: Takwimu Na Rekodi Zote AFCON Unazopaswa Kuzifahamu

Leave A Reply


Exit mobile version