Mchezo ulianza kwa kasi kwa timu zote mbili Azam FC na Yanga SC wote wakifunguka kwa dakika 15 za mwanzo faida aliipata zaidi Yanga SC na ndiyo sababu ya goli la kwanza la Clement Mzize ilisababishwa na nini? Azam FC kufunguka na kuacha mianya eneo kubwa na zaidi ni press ya Yanga SC kuwa juu kwa dakika za mwanzo. Baada ya kufungwa Azam waliamua kurudi chini na kuwaachia mpira Yanga walifanikiwa? Ndiyo walifanikiwa kwa kufanikiwa kuwakaba vizuri ambapo Adolf Mtasigwa akibaki chini kuwalinda na Yahya Zayd akizunguka juu yake.

Azam FC wakaamua kutumia maeneo ya pembeni (winga) wakipiga pasi ndefu za “Caunter Attack” wakipata faida ya kuwa na wachezaji ambao wana uwezo mzuri wa kumiliki mpira na hata ukitazama goli lao la kusawazisha lilipita kwenye miguu ya wachezaji watatu tu baada ya kuvuka nusu yao na kuwa kwenye nusu ya Yanga SC Feisal Salum ambaye alikokota kwa umbali mrefu kidogo kitendo ambacho kiliwavuta mabeki wa Yanga SC kumfuata na kuacha nafasi kwa Kipre Junior ambaye naye alikokota kidogo kabla ya kuingiza mpira ndani, wapi Yanga SC walikosea na kupelekea kuruhusu goli ? Imechangiwa na umiliki wa Feisal Sakum ambao uliwavuta wapinzani kwake na kuacha nafasi kwa Kipre Junior.

Pigo kwa Yanga SC ni kuumia kwa Pacome Zouzoua jambo ambalo lilipelekea Azam FC kutawala eneo la kati kivipi? Uwezo wa Pacome kumiliki na kutembea na mpira eneo kubwa la uwanja ulisababisha kupiga mipira mingi mirefu na kupelekea umiliki kuwa kwa Azam FC zaidi wakitokea pembeni na kuwapa shida mabeki wa pembeni Yao Attouhula pamoja na Nickson Kibabage.

Kipindi cha pili kilitawaliwa zaidi na Yanga SC na muda mwingi walikuwa wakijaribu kupitia katikati mwa uwanja wakimtumia Aziz Ki lakini ilishindikana kwa Azam FC kuwa wengi wakilinda goli lao, jambo ambalo uchezaji ulibadilika na kuwaingiza Kennedy Musonda na Augustine Okrah ili wawe wanatokea pembeni mwa uwanja ila bado Azam FC walikuwa bora sana kwenye kukaba ndani ya nusu yao.

Namna walivyocheza kipindi cha kwanza ndiyo hivyo hivyo walicheza kipindi cha pili wakiamua kutumia “Caunter Attack” kupitia pembeni mwa uwanja huku silaha yao kubwa ikiwa ni Gibril Sylla pamoja na Kipre Junior wakipitia pembeni huku Feisal Salum akiwa anatokea katikati na iliwapa faida wakapata goli la pili kupitia njia hiyo. Azam FC walikuwa bora kiwanjani wakitekeleza majukumu yao kwa usahihi huku Yanga SC wakiwa na mchezo wa taratibu sana tofauti na wanavyocheza walikosa wachezaji ambao watakokota mpira eneo kubwa la uwanja pengo la Pacome Zouzoua na Khalid Aucho likionekana.

Kile kitasa cha Azam FC Fuentes bonge moja la beki utulivu wake akiwa na mpira ni “superb” ni mtulivu kweli kweli, mabeki wa Yanga SC hawatamsahau Kipre Junior amewasumbua sana kiwanjani atulii eneo moja kati yupo pembeni yuko ndiyo mchezaji bora wa mchezo, wanapokutana Yanga SC na Azam FC lazima magoli yapatikane na ilo limetokea.

SOMA ZAIDI: Barua Kwenu Washirikina Wa Mpira Wa Miguu Tanzania

1 Comment

  1. Pingback: Pacome Na Aucho Ni Pasua Kichwa Dhidi Ya Mamelodi? - Kijiweni

Leave A Reply


Exit mobile version