Ilipoishia ” Walipomaliza kunywa chai walikodi Tax hadi nyumbani kwa Mage, Wakatumia ukuta kuingilia, kisha Robson akajificha mahali, Mark akagonga mlango. Kelele za kugongwa mlango zilimshtua Mage ambaye alikuwa Usingizni, akajiuliza ni Nani anayegonga mlango wake bila kupitia getini, akajiuliza au aliacha geti wazi ila hakukubaliana na wazo hilo sababu alikumbuka kuwa alifunga milango yote kwasababu ya woga.

Tuendelee

SEHEMU YA SABA-07

Alienda kuchungulia dirishani, akamwona Mark, akamkumbuka kuwa alisoma naye lakini akajiuliza Mark amefuata nini nyumbani kwake tena bila taarifa. Angalau kumwona Mtu anayemjuwa kulimfanya aondoe hofu yake, akafungua mlango akiwa amevalia Khanga tuu

“Mark!!” alisema Mage akijifanya kushtuka kumwona Mark hapo

“Mambo Mage!!”

“Powa tu, umepafahamu vipi hapa Mark, alafu umeingiaje?” aliuliza Mage

“Nimeelekezwa hapa hadi nikafika, nimekuta geti lipo wazi ndiyo nikaja kugonga hapa” Alisema Mark akiwa mwenye kutabasamu

“Kimekuleta nini hapa kwangu?”

“Mimi ni rafiki tu kwani kuna ubaya nikifika hapa?”

“Mark plzz sema kimekuleta nini hapa au ni wewe ndiye uliyekuwa ukinifwatilia kutwa nzima?” aliuliza Mage akiwa ameanza kuingiwa na hofu

“Hapana siyo Mimi, aliyekuwa anakufwatilia jana ni Robson”

Aliposikia kuwa ni Robson akataka kuufunga mlango haraka lakini Mark alimuwahi akamzuia kisha akaingia ndani kwa nguvu, Robson naye akaingia ndani, alipomuona Robson akataka kupiga simu kwa Brahama lakini wakamuwahi tena wakamnyang’anya simu, wakaona jina la Brahama kwenye kioo

“Oooh kumbe unajuwa kilichotuleta hapa si ndiyo Mage? Mimi na wewe hatukuwahi kuwa maadui wala marafiki chuoni, ulichagua kuwa upande wa Brahama” Alisema Robson akiwa ameishikilia simu ya Mage

“Hebu kaa tuzungumze Mage” Alisema tena Robson kisha aliketi, Mage aliketi pia taratibu huku akiwatazama Wanaume hao

“Hapana shaka unaishi mwenyewe hivyo kitakachotokea hapa hakitakuwa na shahidi ispokuwa Mimi na Mark” Alisema tena Robson

“Robson unataka nini kwangu?” Aliuliza Mage

“Ni kuhusu Mke wangu Sylivia, alikuja hapa siku chache zilizopita, unaweza ukaniambia alikuja kufanya nini?” Aliuliza Robson

“Robson!! Sylivia alikuja kunisalimia tu sababu tulikutana sokoni, ina maana kuna ubaya Mimi nikiwasiliana na Sylivia?”

“Siyo Ubaya wewe kuwasiliana na Sylivia kwasababu ulisoma naye lakini Ubaya unaingia aendapo wewe unaposimama kama Mtu

kati…”

“Mtu kati unamanisha nini?”

“Usijitoe ufahamu Kima wewe, hivi unajuwa ni gharama kiasi gani zimetumika kwa ajili ya ndoa ya Robson na Sylivia?” Alidakia Mark kwa hasira.

“Mbona siwaelewi Robson mnataka nini?” Alipayuka Mage Robson akampiga kofi Mage kisha akamwambia

“Ndoa yangu ipo katika mgogoro mkubwa sana kwasababu ya Brahama, najuwa yupo Tanzania” Alisema Robson huku chozi likimbubujika, Mage akakaa kimya huku akiwa anamwangalia Robson

“Unajuwa ni jinsi gani naumia? Baada ya kuja hapa Mwanza kwenye fungate ndoa yangu ilianza kupata mpasuko mkubwa sana, labda nikukumbushe kuwa kuna siku Mke wangu alikuja kwako, baada ya hapo kila jambo liliharibika, hadi hivi sasa Mimi na Sylvia hatupatani kabisa, na hakuna Mwanaume anayeweza kuvuruga kichwa cha Sylvia zaidi ya Brahama, nataka uniambie ukweli Brahama anawasiliana na Mke wangu?” Alisema Robson

Akiwa anafuta chozi, macho ya Mark yakatua kwenye uso wa Robson ambao ulipoteza nuru akajisemea moyoni

“Kumbe mapenzi yanauma kiasi hiki?” Alijisemea kisha akamshika bega Robson ili kumtuliza maana alijuwa kuwa alikuwa akipitia magumu sana, hata sura ya Mage ilijawa na majonzi mno akawa anamtazama Robson jinsi alivyokuwa akilia

“Mage kuwa katika nafasi yangu, ingia ndani yangu uone jinsi ninavyoumia. Sylivia ndiyo furaha yangu Mimi…”

“Robson ukilia haisaidii cha msingi ajibu maswali basi hakuna kitu kingine” alisema Mark akiwa anamtazama Robson

“Sielewi Mark, hujui naumia Mimi. Nimefanya kazi ngumu hadi kumuowa Sylivia, kabla hata sijala tunda la ndoa yangu…”alisema Robson akashindwa kumalizia kuongea, alijiinamia.

Chozi likambubujika Mage, akalifuta kisha kwa sauti ya upole akamwambia Robson

“Pole Robson, sijui nisimame upande upi ili unione sina hatia katika hili. Ni kweli Brahama yupo Tanzania” Alisema Mage kisha aliweka kituo baada ya Robson kunyanyua kichwa kwa mshtuko

“Unasemaje?”

“Robson, sijui hata nielezee vipi, mara zote nimekuwa nikijaribu kuongea na Brahama apotezee kuhusu Sylivia lakini….Ahhh”

“Mage niambie…. Brahama amerudiana na Mke wangu sylvia si ndiyo?” Aliuliza Robson huku mwili wake ukizidi kupata joto kali na moyo ukizidi kumuuma

“Ndiyo lakini aaah kwanini haya mambo yanatokea sasa hivi, ni bora hata angebakia huko Ulaya….lakini nisamehe Mimi Robson sababu Mimi ndiyo chanzo cha Mkeo kukutana na Brahama….Nisamehe Robson” Alisema Mage kisha akapiga goti mbele ya Robson

“Unajuwa ni jinsi gani nampenda Sylivia? Aaaah” aligumia Robson kama Mtu aliyepandwa na kichaa

“Rob Mzee, punguza jazba sababu ukitumia hasira mwisho hauwezi kuwa mzuri, kikubwa tumeshajuwa tatizo lipo wapi..”

“Ok!ok! Nifanye nini Mimi? Nifanye nini nawauliza? Kwanza Brahama yupo wapi?” Alihoji Robson akiwa kama Mbwa kichaa, kilio kilikata huku hasira ikiwa imejaa kifuani pake, akawa anahema mithiri ya Mwanariadha aliyekimbia kilomita 20 kwa dakika chache

“Robson ikibidi kuniuwa niuwe tu lakini siwezi nikakwambia alipo Brahama, kama kujuwa alipo Brahama kunatatua tatizo lako basi nitakuwa nimeshindwa kukusaidia Robson” alisema

Mage kwa ujasiri Mkubwa sana, Robson akaanza kuingia chumba kimoja badala ya kingine kumtafuta Brahama, hakunwona Brahama sababu alikuwa Dar tena alikuwa na Mke wake Sylivia

Alipomaliza kupekua kila mahali alirudi sebleni akiwa na kisu mkononi, jasho likiwa linamvuja

“Robson unataka kufanya nini?” Aliuliza Mage, Robson hakujibu chochote alikuwa kama amechanganikiwa, akawa anamsogelea Mage, Hofu ikatanda moyoni kwa Mage, hata Mark alishangaa Robson anataka kufanya nini

“Tafadhali Robson nitasema alipo Brahama, yupo Dar anamtafuta Sylivia” alisema Mage.

“Una uhakika?” Akauliza Robson

“Wallai siwezi kudanganya Robson, Brahama yupo Dar mlipotoka”

“Sasa kama utakuwa umeniongopea Mage nakuapia siwezi kukusamehe katika Maisha yangu!” Alisema Robson kisha alikitupa kisu akatoka, Mark akamwambia Mage

“Usiwe sehemu ya hili jambo sababu mwisho hautokuwa mzuri, kaa kimya hata Brahama usimweleze chochote” Alipomaliza kuchimba mkwara akaondoka zake pamoja na Robson, kilichofuata kwao ni kuanza safari ya kurudi Dar Usiku kwa ndege.

Muda huo, Jijini Dar, Mishale ya saa tano asubuhi, Sylivia alifika nyumbani kwa wakwe zake lakini cha kushangaza aliwakuta na wazazi wake wakiwa aamekaa sebleni wakiteta jambo, alishangaa maana Wazazi wake hawakumwambia kabisa kama wataenda kwa wazazi wa Robson.

“Karibu Sylvia” alikaribisha Mama yake Robson huku Baba na Mama yake wakiwa wanamtazama

“Baba na Mama hamkuniambia kama mtakuja huku!” Alisema Sylivia huku akiwa katika hali ya mshangao, alijikuta akijitupa sofani kama mzigo, akatamani sana kujuwa alichoitiwa pale.

Baada ya kuketi akamtazama Baba yake Robson kusikia atasema nini

“Sylivia Mwanangu pole kwa mshangao lakini hilo lisikupe hofu, Sisi na Wazazi wako tulikuwa tunajadili jambo kuhusu ndoa yenu na Robson” Alitanguliza kusema Mama yake Robson kisha Baba Robson akasema

“Tunajua ndoa yenu inapitia misukosuko ya hapa na pale, licha ya kujaribu kuwapatanisha lakini bado Robson amekuwa akilalamika kuwa haumfurahii, tukajaribu kuwauliza wazazi wako wakatueleza jambo lililotushangaza sana, kuwa humpendi Robson, ulikubali kuolewa na Mwanetu sababu wazazi wako walitaka ufanye hivyo, je ni kweli?” Aliuliza Baba Robson

akiwa anamtazma Sylivia kisha akawatazama wazazi wa Sylivia ambao walikuwa wameinamia chini, Sylivia hakujibu chochote kile.

 

Mara simu ya Sylivia ilianza kuita, haikujulikana mpigaji alikuwa ni nani lakini aliwatazama Wazazi wake kisha wazazi wa Robson, kisha akaipokea pale pale, akaisikiliza kwa mshituko mkubwa kisha akaondoka mbio mbio bila kusema chochote.

Akawafanya Wazazi wote washangae sababu hawakujuwa alipokea simu ya nini, na ameenda wapi, wakabakia wanaulizana

“Kuna nini?”

“Ile simu ina nini?”

“Ooohh haya mambo yananichosha sana kusema ukweli wazazi wenzangu” akasema Baba Sylivia

“Hupaswi kumkatia tamaa, yule ni Mtoto. Tutajuwa tu kilichomtoa hapa” Akasema Mama yake Robson, Baba Robson akawa amechukizwa sanaa na tukio hilo akawaambia wazazi wa Sylivia

“Mtoto wenu amenikosea adabu hata Mimi, kwanini atoke bila kusema chochote, huku ni kutudharau sisi”

“Mtusamehe sisi Wazazi wenzetu, hii ndiyo shida ambayo sisi Wazazi tunakumbana nayo sana, kwa kifupi ni kama tulivyowaambia, Sylivia hataki kuwa na Mtoto wenu…..Anasema yupo anayempenda” Alisema Baba Sylivia

“Sasa nasimama Kama Baba wa Robson, atake asitake ataishi na Mwanangu, hatuwezi kuingia kwenye hiyo aibu,ni bora ndoa isingepita kuliko ndoa imepita kisha yatokee haya, Mwanzo nilimuona Kijana wetu anamakosa kumbe haya yote anayetengeneza Binti yenu, sasa nitalifanyia kazi hili jambo” akasema kisha akaingia chumbani.

Hebu tumtazame Sylivia, alikuwa ndani ya gari baada ya kutoka pale kwenye kikao, alionekana kukosa umakini kabisa, alikuwa akikosea hata kuvuka barabara ambayo ilikuwa na taa nyekunde, mara kadhaa akawa anakoswa kugongwa au kusababisha ajali mbaya.

Alipiga honi kila mahali kutaka apishwe barabarani, aliongoza hadi Masaki kwenye Hoteli ya Ocean view alipo Brahama, hakuhitaji kuingiza gari ndani ya Hoteli hiyo, moja kwa moja akakimbilia kwenye lifti akaitumia kufika alipo Brahama. Akamkuta Brahama akiwa anamsubiria,,Sylivia alikuwa amechoka mwili mzima

“Brahama nimeshindwa kuendelea na kikao, simu yako imenivuruga akili mno” akasema Sylivia akiwa anaketi kitandani

“Hiyo ndiyo hali halisi, nimemwambia Mage aende polisi kutoa taarifa ya uvamizi” akasema Brahama akiwa anamtazama Sylivia

“Oooh Mungu wangu, nilitaka kukwambia hili mapema sana lakini nikaona nisubirie hadi Hatma ya kikao.”

“Kumbe nawe ulikuwa unajuwa kuwa Robson yupo Mwanza?”

“Ndiyo, nimelijuwa hilo kupitia kampuni anayoifanyia kazi”

“Ooh shit!! Kwa vyovyote atakuwa ameambiwa kuwa nipo Dar japo

Mage amekanusha kuwa hakusema ila kwa jinsi ninavyomjuwa Robson sijui”

“Sasa itakuwaje kama ameambiwa kila kitu?” Aliuliza Sylivia

“Nitakabiliana naye kwa namna yoyote ile lakini siyo kuachana na wewe Sylivia, tumetoka mbali hatuwezi achana kirahisi”

“Unamaanisha kweli Brahama?”

“Siwezi ongopa, siogopi chochote kile Sylvia”

“Sijui upande wangu itakuwaje Brahama, basi ngoja nirudi nione namna ya kumkabili najuwa atarudi na hasira zote dhidi yangu na atakutafuta wewe kila kona ya Jiji hili”

“Sylvia nimekwambia siogopi chochote hata ikibidi kujitokeza mbele yake lakini siwezi kujisaliti kwenye ahadi yangu mwenyewe”

“Haya sawa basi tutawasiliana Brahama”

“Powa Sylvia”

Wakaagana, Sylvia akarudi nyumbani kwao, lakini alipofika alikuta Wazazi wake wakiwa wanamsubiria getini, alipowaona alijuwa lazima kutakuwa na maneno makali dhidi yake, akajipanga kukabiliana nao.

“Sylivia unajuwa unatutia aibu wewe mtoto?” Alisema Baba yake Sylvia kwa hasira sana akiwa anapiga gari anayoendesha

“Baba Sylvia!!” Mama Sylvia akajatibu kutaka kumpoza BabaSylvia

“Niache…Niache…hivi wewe Mtoto unatuona sisi hatuna akili si ndiyo? Unatuona mabwenyenye ama, kipi kinachokupagawisha Mtoto wa kike kipi? Kwanini hutulii unataka uonywe na nani wewe….Haya umeamua kututukanisha si ndiyo?” Alisema kwa

Jazba kubwa, Haraka Sylvia akashuka naye akiwa amepagawa maana mambo yalianza kuharibika

“Kwahiyo ulitakaje Baba? Niishi kwa furaha kwa Mwanaume ambaye simpendi si ndiyo? Haya ni makosa yenu kwanini mniozeshe kwa Mtu ambaye hakuwa chaguo langu” Alipaza sauti Sylvia, akapigwa kofi na Baba yake

“Mshenzi wewe, kwahiyo sisi ndiyo wenye makosa si ndiyo? Hivi tulikuzaa wewe au manesi walitubadilishia?” Baba Sylvia alijawa na hasira na uchungu hasa akikumbuka maneno ya Baba Robson

“Sasa bila nyie kunilazimisha leo hii yangetokea yote haya? Nisikilizeni kwa makini sana, Siku zote punda utamlazimisha kwenda mtoni lakini kunywa maji ni hiyari yake, Punda Mimi staki kunywa Maji” Alisema Sylvia kisha akaingia kwenye gari, Baba yake akazuia kwa mbele gari ya Sylvia

“Huwendi popote Sylvia hadi tufikie muafaka wa hilo suala, kama unataka sisi tuendelee kuwa wazazi wako basi amuwa moja, kuishi kwa amani na Robson” alisema Baba Sylvia, tayari Binti yake alikuwa na hasira sana, akarudisha gari nyuma kisha akapeleka mbele kwa spidi na kufunga breki, akajikuta amemsukuma Baba yake akaangukia chini, kisha akaingiza gari ndani na kufunga geti

Baba yake akawa analalamika pale chini kuwa anaumia, Mguu ulikuwa unatoka damu lakini Sylivia hakujali kabisa.

“Sylivia umemgonga Baba yako na hujali?” Alisema Mama Sylvia, Binti yake akasimama na kugeuka akamwambia Mama yake

“Kama ambavyo nyie hamkujali kuhusu Mimi basi ndivyo ambavyo Mimi siwezi kujali tena kuhusu nyie” Alisema Sylvia kisha akaingia ndani haraka sana.

“Msaaada Jamani Mume wangu….Uwiii atakufa hapa nifanyaje Mimi” Alisema Mama Sylvia akiwa katika hali ya kuchanganikiwa sana, Bahati nzuri kulikuwa na Bajaji ambayo ilikuwa ikipita hapo, akaomba msaada wa kumwaisha Baba Sylvia Hospitali

Sylvia alishajuwa ameharibu zaidi, hakutaka kujilaumu, akafikiria afanye nini Maana Robson tayari ameshaujuwa ukweli, akakusanya mabegi yake kisha akaita Tax. Akapakiza mabegi yote akaondoka nyumbani kwa Robson.

  • ••••••

Masaa yalikatika, Hekaheka ikawa nzito kwa Baba Sylvia ambaye alikuwa amelala kitandani akitafari kilichotokea, Mguu wake ukiwa umetundikwa kwa kamba maalum za kumsaidia kupunguza maumivu. Mama Sylvia akiwa pembeni ya Mume wake akiwa amejishika tama, Mara akaingia Baba yake Robson na Mama Robson

“Jamani imekuwaje tena?” Aliuliza Baba Robson akiwa anavua miwani yake

“Hali ndiyo kama unavyoiyona, kilichotokea ndiyo kile nilichokuhadithia kwenye simu” Alisema Mama yake Sylvia

“Huyu Binti amekuwa mwenda wazimu sana, yupo wapi?” Alihoji Baba yake Robson

“Tumemuacha nyumbani kwake hakujali chochote kuhusu Baba yake” Alisema Mama Robson huku Baba Robson akiwa anaugulia maumivu ya Mguu uliopata hitilafu

“Baba Sylvia pole kwa yote, sijui kwanini yote yanatokea wakati huu, furaha imegeuka kuwa huzuni, wiki chache baada ya ndoa Hekaheka imekuwa nzito sana” Akasema Mama yake Robson

“Naumia sana sijui Binti yangu kapatwa na ukichaa gani, nini kimembadilisha ghafla hivi lakini pengine sisi tuna makosa sababu tulilazimisha aolewe na Kijana wenu” alisema Baba

Sylvia huku chozi likimbubujika

“Usiseme hivyo, mlifanya maamuzi kama Wazazi na ndiyo jukumu lenu kuhakikisha Binti yenu anaishi Maisha bora” Alisema Baba yake Robson, ilikuwa ni mishale ya jioni kigiza kikianza kuingia, Mara simu ya Baba Robson iliitaAlipoangalia aliyekuwa akipiga aliona ni Kijana wake Robson

“Eeeh Robson ndiyo anapatikana sasa hivi” Alisema Baba Robson, kila mmoja akawa makini kusikiliza lakini Baba Sylvia akasema

“Tafadhali usimwambie chochote kilichotokea hadi atakaporudi kwenye hiyo safari ya kikazi” Alisema, Hapana shaka Robson aliwaaga kama alivyomuaga Mke wake Sylvia

“Pokea Baba Robson” alisema Mama Robson, haraka Simu ikapokelewa, ikasikika sauti ya Robson ikisema

“Baba nimekamatwa na polisi Mwanza, nipo kituo cha polisi sasa hivi!!l

“Umekamatwa na polisi Mwanza? Ilikuwaje na ulienda lini huko si ulisema upo Dodoma?” Alihoji Baba Robson

“Baba hilo siyo jambo la Msingi kwasasa, kikubwa nitumie wakili kwa ajili ya hii kesi” Alisema Robson, wote walishangaa

“Kesi gani hiyo Robson mbona unaniweka kwenye funbo zito hivi?”

“Baba mtajuwa tu kikubwa aje Wakili mzuri” Alisema Robson.

“Sawa nakuja huko Usiku huu” Alisema Baba yake Robson kisha simu ilikatwa

Baba Robson alijiinamia akiwa ametingwa zaidi hakujuwa ni jambo gani ambalo lilimfanya Robson akamatwe Mwanza

“Jamani huu ni mtihani mzito sana, linaingia hili linatoka hili, kwasasa Robson anashikiliwa Mwanza, sijui alifikaje huko. Baba Sylvia ugua pole wacha nikamfwatilie Robson” alisema Baba Robson, haraka waliondoka hapo na Mama Robson

Walipofika nyumbani kwao Baba Robson alijiandaa Usiku huo huo, akawahi Uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius nyerere. Bahati nzuri alipata ndege Binafsi ya askari ambao walikuwa wakienda Mwanza usiku huo hivyo ikawa rahisi kwake, alikuwa akifahamiana nao, wakamuuliza anaenda kufanya nini Mwanza akawaeleza kuwa Kijana wake anashikiliwa na jeshi la polisi huko.

“Kwanini usitumie cheo chako Mtoto akaachiwa Mzee Kibu?” Aliuliza Askari mmoja maana Baba Robson alikuwa askari Mstaafu mwenye cheo kikubwa jeshini

“Mambo kama haya ni lazima kwanza niyaelewe ndipo nifanye uamuzi japo nina imani hadi asubuhi kila kitu kitakuwa kimeisha” Alisema Baba yake Robson, waliondoka Usiku huo huo wakafika Mwanza Alfajiri.

Nini Kiliendelea? Usikose Sehemu Ya 08

 

Wewe Ni Mwandishi? Unapenda kuendeleza Taaluma yako ya uchambuzi kwenye masuala ya michezo? Mtandao wa uchambuzi wa michezo kijiweni.co.tz unakupa uwanja wa kuendeleza kipaji chako na kufikia maelfu ya wapenzi wa michezo Tanzania na nje ya Tanzania.

Tutumie makala au uchambuzi wa michezo katika barua pepe hii editor@kijiweni.co.tz  

Fungate Sehemu Ya Kwanza 

Fungate Sehemu Ya Pili

Fungate Sehemu Ya Tatu

FUNGATE (Sehemu Ya Nne) Fungate-04

 

 

 

30 Comments

  1. Chard michael on

    Sipendi riwaya wala kusomasoma

    LAKINI HII NI NOMA SANA, umetisha sana mkuu wa kijiwe,
    sema tupe muda maalum sasa tujue mishale gani uhakika kuingia maktaba bhn

  2. Mmmh mamb si mamb sasa fungate ni fire,patamu hapo🤣🤣admin utatisha kama sehem ya 8 itatok sa 4 asubuh

  3. Emmanuel Ngoma on

    Ukikaa ukafikiria unaweza usitamani kabisa mapenzi na ndoa
    Ila bila roho ngumu hautaweza
    Fungate Ina mambo Sana.

Leave A Reply


Exit mobile version