IlipoishiaShangwe na vigeregere viliibuka kanisani baada ya Familia ya Sylvia kuingia kanisani, waliopiga vigeregere hawakujuwa mioyo ya Sylvia na Robson ilikuwa kwenye msuguano mzito sana, wao walifurahia kuona Robson anamuowa Sylvia, taratibu zilifanyika kikamilifu.”

Endelea 

SEHEMU YA PILI-02

Padre alifungisha ndoa hiyo, ndoa ilifungwa siku ya Jumanne, saa nane Mchana, Padre aliwatangazia kuwa Wao ni Mume na Mke hivyo wanapaswa kuvumiliana kwa shida na raha, Sylvia alimsogelea Robson kama anataka kumbusu kisha alimnong’oneza kuwa

“Tumeshakuwa Mke na Mume” Alisema Sylvia kisha alitabasamu.

Waliondoka kanisani, sherehe nyingi zilifanyika ili kufurahia ndoa hiyo iliyojaa mpasuko ndani yake

“Sylvia! Nilipanga kukupeleka fungate Kilimanjaro na Mwanza”

Alisema Robson wakiwa chumbani usiku wa ndoa yao

“Mh! Kwanini umechagua Kilimanjaro?”

“Kwasababu ni sehemu niipendayo, naamini pia utaipenda sana, itatufanya tuzike tofauti zote na tujione kama tumezaliwa upya ili tule matunda ya ndoa yetu” Alisema Robson, Sylvia alikuwa akisoma kitabu akamjibu Robson

“Sawa”

Robson alimpenda sana Sylvia, alijiapiza kuwa atafanya kila awezalo ili Sylvia amsahau Brahama. Siku iliyofuata waliondoka Dar kwa ndege ya shirika la Air Tanzania hadi Kilimanjaro, ilikuwa ni safari iliyofanya vichwa vyao vijione vinaenda kuwa sawa!

“Karibuni Kilimanjaro, tunaweza tukawatembeza mbugani kwa gharama nafuu sana” Alisema Mwanamke mmoja aliyeonekana kuwa wakala wa kampuni ya Utalii, Robson alimtazama Sylvia akamwambia

“Unaonaje?”

“Ni sawa tu” Alijibu Sylvia

“Samahani tulikuwa tunahitaji Chumba karibu na Mlima Kilimanjaro na hiyo huduma ya utalii, kwa siku tano itakuwa shilingi ngapi?” Aliuliza Robson, ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufanya safari ya Kwenda mlima Kilimanjaro

“Gharama ya chumba inategemea na aina ya huduma mzitakazo, zipo za laki tano kwa siku hadi milioni mbili kwa siku, kuwatembeza ni gharma ndogo tu hivyo msiumize kichwa” Alisema Mwanamke huyo

Robson na Sylivia waliridhia kuambataba na Kampuni hiyo hadi Mlima Kilimanjaro, walipata Hoteli nzuri ambayo iliwapa urahisi wa kuuona Mlima Kilimanjaro kwa ukaribu zaidi, nyuso zao zilitabasamu sana kama ambavyo Robson alisema huwenda safari hiyo ikazika tofauti zao, ndani ya siku moja ya kuwa

hapo ilionekana wazi Fungate inaenda kuimarisha ndoa yao.

“Umeona palivyo pazuri?” Aliuliza Robson wakiwa wamekaa baada ya hekaheka za safari kwisha

“Ndiyo pazuri sana nimefurahi” Alijibu Sylvia huku akiwa mwenye kutabasamu, mabusu na mahaba moto moto yalifuatia kuonesha ni jinsi gani tofauti zao zilivyozikwa na safari hiyo.

“Sijutii kukuooa Sylvia, unanifanya niwe mwenye furaha zaidi tokea mara ya kwanza nilipokuona chuo” Alisema Robson, Sylvia alimtazama Robson, mara nyingi hakupendelea kukumbuka mambo ya chuo sababu humkumbusha kuhusu Brahama ambaye yupo nje ya Nchi, Mwanaume aliyempenda kuliko Wanaume wote Duniani, Sura ya Sylvia ilibadilika akawa mnyonge ghafla

“Dear kuna tatizo?” Aliuliza Robson

“Sipendi kukumbushwa kuhusu Chuo Robson, nakumbuka mengi hivyo sihitaji kuyakumbuka yote yanayoumiza moyo wangu”

Alisema Sylvia

“Pole Mke wangu” Alisema Robson kisha alimkumbatia Sylvia mithili ya Kuku anavyokumbatia kifaranga chake.Fungate yao ilienda vizuri wakiwa Kilimanjaro, walitembea mbugani kuzunguka Mlima Kilimanjaro, ilikuwa ndiyo mara ya kwanza kwao kuona wanyama hasa Twiga ambao hupendezesha mandhari ya Mlima Kilimanjaro, Baada ya siku tano waliondoka wakaenda Mwanza kumalizia fungate yao.

Huko walikuwa na marafiki waliosoma wote, walipanga kwenye apartment kwa siku tano za kuishi Mwanza. Siku moja Sylvia alitoka kwenda kununua matunda kwenye moja ya masoko huko Mwanza, alimuacha Robson akiwa na rafiki yake.

Alipofika huko Sylvia alikutana na rafiki yake wa muda mrefu waliyesoma wote chuo

“Eeeeh siamini Mage kama nimekuona tena jamani” Alisema Sylvia

“Haaa Usijali Bwana, Milima pekee ndiyo haiwezi kukutana, kwanza ukutane nami kwa lipi Sylvia wakati umeamua kutukimbia” Alisema Mage, Sylvia alishusha pumzi zake kisha akamvuta Mage pembeni

“Unamaanisha nini Mage?” Aliuliza Sylvia

“Brahama ndiye aliyetufanya tukajuwana, nimesikia umeolewa na Rafiki yako Robson, ina maana mmekuja kuishi Mwanza?” Aliuliza Mage, Sylvia aliposikia kuhusu Brahama alipoa kidogo, alionekana kuwa mnyonge sana

“Hapana tunaishi Dar Mage, ningefanya nini Mage wakati Brahama alinipotezea, alipoondoka kwenda Ulaya kwa wazazi wake hakupatikana kwa zaidi ya Mwaka mzima, ikabidi niingie kwenye mahusiano na Robson” Alisema Sylvia akiwa analengwa na mchozi

“Mbona unaniambia stori nyingine na Brahama anasema stori nyingine?”

“Kwani unawasiliana na Brahama?” Aliuliza Sylvia

“Ndiyo!! Brahama yupo hapa Mwanza kwa zaidi ya wiki mbili, alisikia kuhusu wewe kuolewa” Alisema Mage

“Unasemaje? Brahama yupo Tanzania?”

“Siyo Tanzania tu bali ni hapa hapa Mwanza ambapo nyie mmekuja” Alisema Mage, moyo wa Sylvia ulianza kuweweseka kwa jinsi alivyompenda Mwanaume huyo.

“Mungu wangu kwanini hakunitafuta?”

“Angekutafuta vipi Sylvia na tayari wewe ni Mke wa Mtu, yaani ulishindwa hata kunipa taarifa juu ya wewe kufunga ndoa na Robson?” Alisema Mage kisha alijishika kiuno

“Nisamehe kwa hilo Mage, ndoa yenyewe aaaah!!!”

“Aaah!! Nini?”

“Tuachane na hilo basi mwambie Brahama kuwa namfikiria sana Mage, naomba namba yako basi” Alisema Sylvia kisha alimpatia simu Mage

“Sylvia Mtoe kabisa Brahama kwenye fikra zako sababu wewe ni Mke wa Mtu, hata hivyo mimi siwezi kumwambia kama. Nimekutana na wewe Sylvia, sitaki kuwa sababu ya kuvuruga ndoa yenu changa” Alisema Mage

“Mageee!!! Unasema nini sasa aaaah!!”

“Sylvia naomba niende tutaongea” Alisema Mage akiwa mwenye haraka kisha aliondoka zake

“Mageeee!! Mageee!!”

“Tutaongea Sylvia” Alisema Mage kwa sauti ya kuondoka, alimuacha Sylvia akiwa mwenye mawazo sana Kichwani pake, aliitazama pete ya ndoa kisha aliendelea kununua alivyovihitaji katika soko hilo, kisha alirudi Hotelini ambako alimuacha Robson akiwa na rafiki yakeSylvia alipita bila kumsemesha chochote Robson wala rafiki yake Robson kitu ambacho kilimshangaza Robson, alimuona Sylvia akiwa mnyonge mno tena mwenye maumivu ya ndani

“Hebu subiria niongee naye!!” Alisema Robson kisha alielekea jikoni ambako Sylvia alienda

“Mke wangu una nini?” Aliuliza Robson

“Siko sawa Rob!! Naomba tu uniache nipate muda wa kupumzika”

Alisema Sylvia kisha alielekea chumbani, Robson alimfuata Sylvia huko huko Chumbani

“Huwezi kuniambia?”

“Nikwambie nini Robson?”

“Ooooh! Shit….sawa akili yako ikitulia utaniambia” Alisema Robson kisha alirudi sebleni alipokuwa amekaa na rafiki yake.

Sylvia akiwa chumbani alijikuta akikumbuka mambo mengi sana kuhusu Udom, hasa alimkumbuka sana Brahama Mwanaume ambaye nafsi yake haiwezi kukana kuwa anampenda sana, alipekua simu yake akaitafuta namba ya Mage ambaye ndiye aliyempa taarifa za Brahama kule sokoni kisha akamtumia meseji

“Mambo Mage ni Mimi Sylvia” Aliutuma kwa Mage lakini haukujibiwa, Sylvia alijikuta akiwa katika nyakati ngumu sana katika maisha yake.

Aliporudi sebleni Robson alionekana naye kutokuwa sawa, mchana ulikuwa umeingia akamwambia rafiki yake

“Tutaonana wakati mwingine” alisema akiwa amekunja sura yake huku mikono yake ikipikicha sura hiyo pana iliyo na ngozi laini

“Kwani shemeji amepatwa na nini Kiongozi?” Aliuliza rafiki yake Robson

“Nimekwambia nenda tutaonana Bwana, Mimi ni Mume wa Mtu siyo mshikaji tena hivyo siwezi kufunguka kuhusu ndoa yangu”

Alisema Robson akionekana kumbadilikia rafiki yake, haikuwa mara ya kwanza kwa Robson kuwa hivyo kwani mara kadhaa amekuwa akiwa mwenye hasira pindi anapokuwa hayupo kwenye maelewano mazuri na Sylvia

“Si tutaonana jioni?” Aliuliza rafiki yake huyo

“Hivi huwezi kumsoma Mtu kiutu uzima Mzee, nenda basi” alikereka zaidi Robson, alimpa upenyo rafiki yake kutimka hapo kisha Robson alituliza akili yake akajiuliza

“Nini kimemvuruga Sylvia, amekutana na nini huko sokoni, yaani kama kuna Mtu amemkwaza nipo tayari kutoa roho ya Mtu”

Alijisema Robson ndani ya Nafsi yake kisha alishushia na maji kisha alijiegemeza kochini, kabla hajapata utulivu alioukusudia, Sylvia aliingia hapo Sebleni akiwa mwenye kumtazama Robson kwa jicho lenye ukakasi kidogoRobson alijiweka sawa akamuuliza Sylvia

“Una nini Mke wangu?” Alihoji kwa utaratibu kama siyo yeye aliyemfokea rafiki yake muda mchache uliopita, Sylvia aliketi bila kusema chochote huku ndani yake akiwa kwenye vita kubwa, alijiuliza amweleze Robson kuwa Brahama amerejea Nchini au akae kimya, alijiwazia kwa sekunde kadhaa kabla ya kupata jibu

Sylvia Alimjibu Nini Mumewe? Amemwambia ukweli kurejea kwa Brahama Tanzania? USIKOSE SEHEMU YA O3

 

Wewe Ni Mwandishi? Unapenda kuendeleza Taaluma yako ya uchambuzi kwenye masuala ya michezo? Mtandao wa uchambuzi wa michezo kijiweni.co.tz unakupa uwanja wa kuendeleza kipaji chako na kufikia maelfu ya wapenzi wa michezo Tanzania na nje ya Tanzania.

Tutumie makala au uchambuzi wa michezo katika barua pepe hii editor@kijiweni.co.tz  

 

 

13 Comments

  1. Pingback: FUNGATE (Sehemu Ya Kwanza) Fungate-01 - Kijiweni

  2. Pingback: FUNGATE (Sehemu Ya Tatu) Fungate-03 - Kijiweni

  3. Pingback: FUNGATE (Sehemu Ya Nne) Fungate-04 - Kijiweni

Leave A Reply


Exit mobile version