Katika Maisha, kila mmoja anakuwa na ndoto kubwa yenye kumpa furaha Maishani mwake,hata wewe una ndoto ambayo siku moja ikitimia utakuwa ni mwenye kufurahi sana.Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Robson, alisoma, alipata kazi nzuri iliyomuingizia pesa nyingi, alikuwa na muonekano mzuri, mtanashati lakini alikuwa na ndoto ambayo alitamani kuiona siku moja ikitimia, ndoto yake kubwa ilikuwa ni kumuoa  Sylvia.

Ndoto ya Robson ilitimia, Sylvia aliridhia kuolewa na Robson, maandalizi yote yalienda sawa na ndicho ambacho Robson alikuwa akikitaka, nafsi ya Robson ilikunjuka akawa mwingi wa furaha, si kazini hata nyumbani kwake alikuwa mwingi wa  kutabasamu

“Hakika Robson unaenda kutimiza ndoto zako za muda mrefu Kaka” Alisema rafiki yake Robson aliyeitwa Mark

“Zaidi ya Sylvia sijaiona furaha nyingine Mark, kumuoa yeye ni jambo linaloenda kunipa furaha sana” Alisema Robson wakiwa wanapata chakula cha mchana nje ya ofisi yao

“Mna mpango wa Fungate?” Aliuliza Mark

“Ndiyo! Nimepanga kumpeleka Kilimanjaro Kaka, tena tukaishi karibu na Mlima kwa wiki mbili za mwanzo kisha tukamalizie Mwanza kula sato” Alisema Robson kisha walicheka kwa pamoja

“Umetisha sana, Unyama mwingi Rob!!”

Tukiachana na upande wa Robson, Nyumbani kwao Sylvia hali haikuwa hivyo kabisa, Sylvia hakuhitaji kabisa kuolewa na Robson, alikubali kwasababu Baba yake alimlazimisha kufanya hivyo, Sylvia aliwaambia Wazazi wake kuwa ana Mwanaume anayempenda sana hivyo ataolewa na huyo na siyo Robson

“Hili linaenda kufanyika Silvia, unaolewa na Robson, Kijana Mtanashati, mchapakazi..” alisema Baba yake Sylvia siku mbili kabla ya ndoa ya Robson na Sylvia, hakukuwa na mjadala tena.

Usiku wa kuamkia siku ya ndoa, Sylvia alimwambia Mama yake kuwa waliangalie upya jambo walilolitaka yeye alifanye

“Mama naolewana Mtu ambaye hayupo ndani ya moyo wangu” alisema Sylvia

“Usiseme hivyo Mwanangu, mbona Robson ni Kijana mpole, mzuri na anaonekana anakupenda sana”

“Mama, suala siyo Robson kunipenda bali ni Mimi kumpenda yeye, hii itakuwa ndoa ya upande mmoja Mama, naomba tafadhali tusitishe hii ndoa Mama yangu” alisema Sylvia, alimpa wakati mgumu Mama yake wakati mipango yote ilipangwa na maandalizi yalishafanyika

“Hadi hapa tulipofikia Sylvia hakuna namna tunaweza rudi nyuma, huna budi kuingia kwenye ndoa, nina imani Utampenda Robson” Alisema Mama yake Sylvia kisha aliondoka chumbani na kumuacha Sylvia akilia

“Kwakuwa mmenilazimisha, nitamfanya Robson ajutie kuniowa”

Alijisemea Sylvia kwa hasira kubwa sana.Siku iliyofuata ndiyo ilikuwa siku ya ndoa ya Robson na

Sylvia, Robson alikuwa mwenye kufurahi sana wakati Sylvia akiwa mwenye kuchukizwa lakini mbele za Watu alionesha tabasamu, Sylvia alikumbuka jinsi alivyokutana na Robson kwa mara ya kwanza.

Alikutana naye chuoni Udom, wote walikuwa wakisomea masuala ya fedha. Walijenga urafiki kwa zaidi ya miaka miwili, Mwaka wa tatu Robson alimueleza Sylvia kuwa anampenda, kutokana na urafiki wao Sylvia alimwambia Robson

“Siwezi kuwa na mahusiano na wewe sababu sisi ni marafiki, pia unajuwa kuwa nina Mtu wangu Robson” Alisema Sylvia

“Mtu wako amekutelekeza yupo nje ya Nchi kwa zaidi ya mwaka bila mawasiliano na wewe, unaweza vipi kujihesabu kuwa upo naye? Alafu kuhusu urafiki wetu nina imani tukiwa wapenzi tutazidi kupendana” Alisema Robson

“Hilo haliwezekani Robson, nakuchukulia kama rafiki yangu, nakupenda kama rafiki na si vinginevyo”

“Sylvia ninayosema yanatoka ndani ya moyo wangu, tafadhali kubali kuwa wangu” Alisema Robson, Sylvia alimtazama Robson kisha alimuuliza

“Itakuwaje kama Brahama atarudi Tanzania?”

“Kama atarudi nipo tayari kukuacha uendelee naye Sylvia”

Alisema Robson, kutokana na sharti hilo Sylvia alikubali kuwa na Robson, Mapenzi yao yalikuwa ya kuvutana sana sababu bado Sylvia alikuwa akimuwaza sana Brahama ambaye alikuwa ndiye Mwanaume wake wa kwanza.

Zilikuwa ni kumbukumbu za Sylvia akiwa anajiandaa kuelekea kanisani, alishika simu yake akajaribu kuipiga namba ya Brahama lakini haikupatikana, kisha akamtumia meseji Robson akamuuliza

“Tunaenda kuwa Mke na Mume, unaikumbuka ahadi yako?” Baada ya kutuma ujumbe, Sylvia aliendelea kuvalia gauni la harusi, mara ujumbe uliingia

“Nakumbuka si kuhusu Brahama?”

“Ndiyo, kama atarudi kwa ajili yangu itakuwaje utakubali Matokeo?” Aliuliza Sylvia lakini ujumbe wake haukujibiwa na Robson hadi muda ambao alikuwa tayari amemaliza kujiandaa

Gari lilipofika waliingia kwenye gari, familia ya Sylvia ilienda kanisani Magomeni, muda wote Sylvia alikuwa akijaribu kumpigia Brahama lakini simu haikupatikana, Mama yake Sylvia aligundua kuwa Mwanaye hana furaha kabisa, alimshika na kumwambia

“Tuliza akili yako Sylvia kwani unaenda kupiga hatua kubwa sana katika Maisha yako” Alisema Mama yake Sylvia baada ya kugundua Mwanaye hayupo sawa , Robson na familia yake walikuwa wa kwanza kufika kanisani, hakika alipendeza sana kwa nje lakini ndani ya moyo wake alianza kuwa na mashaka kutokana na zile meseji ambazo alitumiwa na Sylvia muda mchache kabla ya kuingia kanisani.

Shangwe na vigeregere viliibuka kanisani baada ya Familia ya Sylvia kuingia kanisani, waliopiga vigeregere hawakujuwa mioyo ya Sylvia na Robson ilikuwa kwenye msuguano mzito sana, wao walifurahia kuona Robson anamuowa Sylvia, taratibu zilifanyika kikamilifu.

Ndoa ilifungwa? Nini kilitokea? Gusa Hapa Kusoma Sehemu Ya Pili

 

Wewe Ni Mwandishi? Unapenda kuendeleza Taaluma yako ya uchambuzi kwenye masuala ya michezo? Mtandao wa uchambuzi wa michezo kijiweni.co.tz unakupa uwanja wa kuendeleza kipaji chako na kufikia maelfu ya wapenzi wa michezo Tanzania na nje ya Tanzania.

Tutumie makala au uchambuzi wa michezo katika barua pepe hii editor@kijiweni.co.tz  

21 Comments

  1. Pingback: FUNGATE (Sehemu Ya Tatu) Fungate-03 - Kijiweni

  2. Pingback: FUNGATE (Sehemu Ya Nne) Fungate-04 - Kijiweni

  3. Pingback: FUNGATE (Sehemu Ya Tano) Fungate-05 - Kijiweni

  4. Pingback: FUNGATE (Sehemu Ya Sita) Fungate-06 - Kijiweni

Leave A Reply


Exit mobile version