Licha ya USM Alger kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 wakiwa ugenini kwenye mchezo wa fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Yanga, kocha wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha anaumiza kichwa namna ya kumdhibiti Fiston Kalala Mayele ambaye anaonekana kuwa moto wa kuotea mbali.

Juni 3, Yanga itakuwa ugenini, Stade du 5 Juillet, Algiers kuvuja jasho kwa mara nyingine tena ili kupindua matokeo kwenye fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika ambalo huu ni msimu wa 20 tangu kuanzishwa kwake 2004.

Benchikha alisema bado wana kazi kubwa na ngumu ya kufanya wakiwa nyumbani kwenye mchezo wa marudiano kutokana na ubora wa Yanga ambao wamekuwa wakiuonyesha kwenye michezo ya ugenini.

“Zitakuwa dakika 90 nyingine ngumu hasa kutokana na aina ya matokeo ambayo yamepatikana kwenye mchezo wa kwanza, tunatakiwa kuwa makini licha ya kwamba tutakuwa nyumbani huku tukiwa na faida ya mashabiki wetu.

“Hatuwezi kusema kazi imemalizika kwa sababu kwenye soka lolote linaweza kutokea tunatakiwa kuona ni kama tumepoteza hivyo tunatakiwa kufanya kila ambalo linawezekana ili kufanya vizuri tena kwenye fainali ya pili,” alisema Kocha wa USM Alger.

Kwa sasa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa DR Congo ndiye kinara wa mabao kwenye michuano hiyo ambayo Yanga imeingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa kutinga hatua ya fainali kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake miaka 19, iliyopita.

Licha ya Yanga kupoteza kwenye fainali ya kwanza ikiwa nyumbani, inarekodi ya kufanya vizuri ugenini, ilifanya hivyo dhidi ya Club Africain (1-0) kwenye hatua ya mchujo, ikaifunga TP Mazembe (1-0) kwenye hatua ya makundi, pia Rivers United (2-0) na Marumo Gallants (2-1) kwenye hatua ya robo na nusu fainali.

Leave A Reply


Exit mobile version