Lucas Hoeler aliifungia Freiburg bao la dakika ya 95 kwa mkwaju wa penalti na kuwaondoa Bayern Munich katika robo fainali ya Kombe la Ujerumani.

Bayern walitangulia kupata bao kupitia kichwa cha Dayot Upamecano lakini Nicolas Hoefler aliisawazishia Freiburg baada ya dakika nane.

Hoeler alifunga penalti baada ya Jamal Musiala kumchezea rafu ndani ya eneo la hatari, na kuiwezesha Freiburg kufuzu kucheza nusu fainali.

Hii ilikuwa mechi ya pili ya Thomas Tuchel tangu achukue usukani wa Bayern Munich, baada ya kuifunga Borussia Dortmund 4-2 katika ligi siku ya Jumamosi.

Klabu ya Munich ilimfuta kazi kocha Julian Nagelsmann baada ya kushindwa na Dortmund kwenye msimamo wa Bundesliga na kumleta Tuchel, ambaye aliwahi kuwa kocha wa Dortmund kati ya mwaka 2015 na 2017.

Upande wa Tuchel ulidhibiti mechi hiyo kwa sehemu kubwa lakini kombora la Hoefler kutoka nje ya eneo la hatari, baada ya Kingsley Coman kushindwa kutoa pasi safi, lilisawazisha kwa Freiburg kabla ya Hoeler kuipatia timu yake ushindi wa kushangaza kwa mkwaju wa penalti dakika za mwisho.

Freiburg ilipoteza fainali ya mwaka jana kwa mikwaju ya penalti dhidi ya RB Leipzig wakati Bayern haijafuzu kucheza robo fainali kwa miaka mitatu mfululizo.

Kwingineko, Randal Kolo Muani aliifungia Eintracht Frankfurt mabao mawili ndani ya dakika mbili na kuwaondoa Union Berlin kwenye Kombe la Ujerumani. Frankfurt ilishinda kwa 2-0.

Leave A Reply


Exit mobile version