Karibuni Ligi kuu ya NBC, karibuni kwenye soka la nyumbani njia yenu ilikuwa ngumu kidogo kupanda Ligi kuu, dhamira halisi ya kupambana na kupata nafasi kwenu ilionekana na nafasi mkapata bila iana na hatua moja ya kufanikiwa mkaipata kama mlivyotaka.

Pamba Jiji FC wewe ni mkongwe uliyosota muda mwingi kwenye Ligi za chini kutafuta nafasi ya kurudi Ligi kuu na sisi tunasema karibu sana, nikukumbushe kuwa Ligi uliyoiacha kipindi kile siyo ya sasa ushindani umeongezekana na uwekezaji ndiyo kipaumbele halisi.

Tunahitaji wachezaji wenye ubora na timu yenye mshikamano, ila hatutaki timu yenye migogoro ndumba na maneno yasiyo na utekelezaji. Niwakumbushe mpira wa sasa ni mbinu ufundi na mifumo ya kocha ndiyo inayocheza siyo ndumba wala upendeleo ukifanya vizuri, ukiwa na timu nzuri itaonekana tu na wengi.

Pamba ni timu ya watu ila mnapaswa kuwa na uongozi imara wa juu utakaojali maslahi mapana ya timu na maendeleo yake na siyo mtu mmoja mmoja, soka linahitaji watu wa mpira maana sasa mpira utahitaji watu wenye taaluma ya mpira mwenye uchu wa mafanikio na siyo mtu yoyote tu.

Majirani zangu kutokea Nyanda za juu Kusini niwasalimie kwa kihehe “Kamwene” KenGold FC timu ambayo inatokeo mkoa wa kisoka uliyona timu mbili za Ligi kuu.

Dhahiri shahiri mmejifunza na mmepata somo kutaka kwa wenzenu Mbeya Kwanza, mnahitaji muda na umakini wenye malengo makubwa ya mbali na ya karibu pia kwa ajili ya kuishi muda mrefu Ligi kuu uwekezaji mkubwa utakaoambatana na uvumilivu na imani ndiyo tunahitaji kutoka kwenu, niwakumbushe tu uwekezaji mzuri haudanganyi.

Mmeingia kwenye “Show” za soka letu kivyetuvyetu karibuni sana tena sana mabingwa wa NBC Championship msimu uliyopita machache ndiyo niliyonayo ila kubwa zaidi ni nyie kutengeneza timu imara ya kupambana kwenye michezo 30 ndiyo timu ambayo itakuwa na matarajio makubwa ya kubaki Ligi kuu na siyo kuchukua ubingwa kwa msimu wenu wa kwanza tu.

Huku kwetu hatuhitaji mapambano ya kuchukua ubingwa tunahitaji kuwaona mkifanya vizuri na kushuhudia soka lenu kwa msimu mwingine tena ndani ya NBC PL, ndoto yenu imechukua zaidi ya misimu minne (4) kupata na hatimaye mmeitimiza, ugumu mmeuona msikubali kushuka bila sisi kufaidi ladha ya soka lenu kutokea ardhi ya “Mwaisa”.

Mimi sina mengi juu yako ila ukihitaji kujazia basi muulize Pamba Jiji mengi nimemueleza, kazi sasa imebaki kwenu sisi wapenzi na watu wa mpira tunasema kuwa tunawasubiri kwa hamu sana kuona soka lenu na namna mlivyosuka vikosi vyenu.

Ligi kuu ya NBC inatarajia kuanza kwa msimu mpya wa 2024/2025 hivi karibuni ikiwa imebaki siku 21 kuweza kuanza, huku ikitarajia kuwa na timu 16 ambapo kila timu itatakiwa kucheza jumla ya michezo 30.

Jumla ya michezo 480 inatarajiwa kutimuwa vumbi ndani ya Ligi kuu ya NBC yenye jumla ya raundi 30 kwa kila timu, msimu ujao utashuhudiwa timu mbili (2) mpya ambazo zimepanda daraja kutokea NBC Championship ambazo ni Pamba Jiji FC na KenGold FC.

SOMA ZAIDI:  Muda Utatuonesha Tofauti Kati Ya TIMU Na MASTAA

1 Comment

Leave A Reply


Exit mobile version