Kwako Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas NdumbaroNdumbaro,

Nikiri kuwa nimeisikia kauli yako Mheshimiwa Waziri kuwa haitaruhusiwa kwa mtanzania kuingia na jezi ya timu pinzani uwanjani wakati timu mgeni ikija kucheza na klabu zetu za hapa nyumbani, kwa kuwa utakuwa siyo uzalendo.

Kwanza ningependa kusema kuwa uzalendo haupo na haukai katika jezi au rangi ya nguo au tisheti aliyovaa mtu bali uzalendo upo katika moyo wa mtu ambao utajionesha nje kupitia matendo yake na hii ndio maana kuna watu wana kaa maofisini tena ofisi kubwa na za hadhi kubwa lakini wanafanya ufisadi,wanapokea rushwa na kuiba mali za umma ikiwepo pesa au kusaini vitu kwa maslahi binafsi huku ukutani mwa ofisi zao kukiwa na Picha ya Rais ikiwatizama.

Wapo wengine wanapokea rushwa kutoka kwa maskini bila hofu ya aina yoyote ile huku katika viuno vyao wakiwa wamevaa mkanda wenye rangi ya bendera ya Taifa. Kwa hiyo ni lazima tujifunze kupanda mbegu za uzalendo katika mioyo ya watu wetu na siyo kuupima uzalendo wa mtu kwa kuangalia mavazi aliyo yavaa.maana kama nimavazi ndio yangekuwa ni kipimo na tafsiri ya uzalendo basi tungekuwa tunaamua tu vazi fulani wavae viongozi wetu ili wafanye mambo yao kwa uzalendo.

Katika suala la jezi wapo watu mitaani utakuta anajezi ama tisheti ameinunua kama sehemu tu ya mavazi yake na wala siyo kwa kuwa ni mshabiki wa timu hiyo lakini pia mwingine anaweza ipenda mwonekano tu au rangi yake tu.ndio maana unaweza mkuta mtu amejivalia zake leo jezi ya Manchester United au Man City au Liverpool kutoka Uingereza ,au Madrid au Barcelona kutoka Spain. Mtu anavaa tu japo siyo Raia wa nchi mojawapo ya Ulaya na wala hajawahi kufika huko.

Mimi mwenyewe nimekua ni mpenzi wa kuvaa jezi mbalimbali nilinunua na niliivaa tu kama sehemu ya nguo yangu kama zilivyo zingine.kwa hiyo kumzuia mtu kwasababu amevaa jezi ya klabu nyingine mtu aliyelipia tiketi kutizama mchezo huo inakuwa siyo sawa na ni kumuonea sana na kujenga chuki na hasira kwa watu zisizo na sababu ya aina yoyote ile kwa sababu hakuna mahali sheria inapokataza mtu kufanya hivyo.

Lakini pia inakuwa ni kupoteza na kuondoa ladha ya mpira ambao siku zote ni burudani, furaha na utani na siyo amri amri tu. Utani na kuzodoana kwa Simba na Yanga ndiko kumefanya klabu zetu hizi kupata mafanikio yanaonekana leo hii kwa maana kila mchezaji akiingia uwanjani anataka kupambana sana ili timu yake ipate ushindi na kuwapa raha mashabiki wake wanaokuwa wamefurika uwanjani dhidi ya wale wanaokuwa wapinzani wao bila kujali ni watanzania waliovaa jezi za timu pinzani kutoka nje au ni wa kutoka nje moja kwa moja.

Uzalendo ni lazima tuusisitize kwenye timu za Taifa maana huko tunaunganishwa na Utaifa wetu na utanzania wetu lakini siyo huku kwenye club.huku tuombeanage tu zote zisongage mbele ili sifa zijage sana Tanzania na kuipa nchi nafasi ya kujitangaza na hata serikali kuchukua nafasi hiyo kutangaza vivutio vya utalii .kama ambavyo simba kwenye jezi zao waliandika kuwa Visit Tanzania.

Uzalendo tuusisitize lakini si katika namna hii ya kupangiana hadi aina ya nguo za kuvaa kwa ngazi za mashindano ya Club. sisi wenyewe huwa tukienda nje ya nchi wakati mwingine tunapata washabiki huko huko wa ugenini wanaokuwa nao wanataka wapinzani wao watoke.

Kikubwa ambacho kingesisitiizwa ni kuwa hawa watakao vaa jezi za timu pinzani basi wakae eneo lao na siyo kwenda kukaa kwenye mashabiki wa club nyingine ili kuepusha vurugu zinazoweza kutokea hasa kutoka kwa wale waliofungwa.na hivyo kufanya au kuchochea au kupelekea uharibifu wa miundombinu ya uwanjani kama vile kung’oa viti, kurushiana chupa za maji, kupigana ngumi na wakati mwingine kuharibu hata utulivu wa mchezo wenyewe na hata kupelekea vifo.

Nimalize kwa kusema kuwa mpira ni uwekezaji kwa hiyo tuendelee kusisitiza na kujikita katika uwekezaji na kuvutia wawekezaji katika Secta ya michezo.

SOMA ZAIDI: Barua Kwako Pacome Zouzoua Profesa Wa Boli

2 Comments

  1. Pingback: Tanzania Tukubaliane Kuondoka Kwenye Mpira Wa Mdomoni - Kijiweni

  2. Pingback: Kwanini Yanga vs Mamelodi Na Sio Simba vs Al Ahly? - Kijiweni

Leave A Reply


Exit mobile version