Ukizungumzia klabu kubwa za mpira wa miguu zinazopatikana katika Ligi Kuu Tanzania bara huwezi kuacha kuwataja matajiri wa jiji la Dar Es Salaam kutoka Mbande hukooo Mbagala klabu ya Azam Fc miongoni mwa klabu kubwa kutoka hapa Tanzania ambazo zimechukua hatua muhimu kwa maendeleo ya soka nchini kwa kuwekeza katika akademi rasmi za vijana inayopatikana Azam Complex huko Mbande.

Ukitazama namna ambavyo klabu hii imekua na uwekezaji mzuri kuanzia katika miundombinu yote ya michezo huwezi kuamini kuwa imeanzishwa miaka 19 iliyopita yaani mwaka 2004 tofauti na vilabu vikongwe vya Simba na Yanga ambavyo kwa umri wao na jinsi ambavyo mpaka sasa kumekua na danadana za kuwa na viwanja Pamoja na akademi rasmi ya mpira imekua ni maneno bila utekelezaji.

Uwepo wa akademi ya Azam umekua na faida kubwa kwa soka la Tanzania kwani wapo wachezaji mbalimbali ambao wametokea katika akademi yao wanaochezea timu yao kubwa lakini pia wapo ambao baada ya kupata malezi ya akademi hiyo hutafuta maisha katika timu nyingine mbalimbali kutoka ligi kuu Tanzania bara lakini pia za kutoka ligi zingine za Tanzania.

Ukizungumzia majina kama Mudathir Yahya , Farid Mussa, Idd Chilunda , Novatus Miroshi , Aishi Manul abasi kumbuka kuwa ni miongoni mwa wachezaji baadhi kati ya wengi ambao wamepita katika viunga vya Azam Complex na kupata malezi ya akademi hiyo.

Faida mojawapo ya kuwa na akademi za mpira ni Pamoja na kupata maandalizi mazuri ya mpira wa miguu kuanzia chini mpaka unapokua umekua mkubwa na ndio hichohicho wanachopata wachezaji wanaopitia mafunzo katika akademi za Azam FC kwani wanapata maandalizi bora kimichezo na kimafunzo. Hii inawawezesha kujenga ujuzi wao wa soka, maarifa ya mchezo, na nidhamu ya kitaaluma. Wachezaji hawa wanapofikia ngazi za juu wanakuwa tayari kwa changamoto za soka la kitaalamu.

Tunaona namna ambavyo matajiri hawa wa Chamazi walivyo na ushindani mkubwa katika ligi kuu kwani licha ya kutumia wachezaji wakubwa wanaowasajili kutoka klabu kadhaa lakini pia wanachochea ushindani mkubwa wa vilabu vya soka nchini. Hii inapelekea vilabu vingine kujitahidi kuendeleza akademi zao na hivyo kuongeza kiwango cha soka kitaifa. Ushindani huu wa ndani unachangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha timu za taifa.

Kwa upande wa timu ya Taifa ya Tanzania tumeona namna ambavyo imekuwa ikiweka msisitizo katika kuimarisha uhusiano wake na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na timu za taifa na hii ni kwa kwa kutoa wachezaji wenye viwango bora kutoka akademi zao, Azam FC inachangia moja kwa moja kwenye maendeleo ya timu za taifa kuanzia ngazi za vijana.

Kwa kuhimiza maendeleo ya vijana na kutoa mchango muhimu kwa timu za taifa, Azam FC inaonyesha mfano wa jinsi uwekezaji katika akademi za vijana unaweza kuwa na athari kubwa kwa soka la kitaifa. Ni matumaini kwamba vilabu vingine nchini vitachukua hatua kama hizi ili kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kung’ara katika medani ya soka duniani.

 

SOMA ZAIDI: TFF Ni Wakati Wa Kuwafungulia Fursa Nje Makocha Wazawa 

Leave A Reply


Exit mobile version