Mabosi wa klabu ya Azam FC hawalali kwa mipango ya kusuka jeshi jipya la msimu ujao na sasa inakaribia kumleta beki wa kushoto wa timu ya Taifa ya Senegal na klabu ya Teungueth, Cheikh Sidibe (24) ili kuziba pengo la Bruce Kangwa aliye mbioni kuachwa.

Awali iliripotiwa kuwepo kwa mvutano wa maamuzi kwa viongozi wa timu hiyo juu ya mustakali wa Kangwa ambaye umri wa miaka 34 unaonekana kutumpa mkono, upo upande ambao wanataka aendelee kuwa kikosini huku mwingine ukitaka aondoke.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani inaelezwa kati ya majina ambayo yapo mezani na yanatazamwa kama mbadala sahihi wa Mzimbabwe huyo ni Sidine ambaye katika fainali za CHAN  pale Algeria alifanya vizuri na kuwaongoza Senegal kutwaa taji kisha kuingia kikosi Bora cha michuano hiyo.

Kushindwa kwa wachezaji wa ndani kufua dafu mbele ya Kangwa, kumewafanya Azam kufanya mazungumzo na Msenegal huyo na tayari ameonyesha nia ya kujiunga na matajiri hao ambao siku chache zilizopita walimtambulisha, Feisal Salum kuwa sehemu ya kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao.

Mmoja wa viongozi wa Azam (jina tumehifadhi) alithibitishia uwepo wa dili hilo kutokana na timu hiyo kuwa na mpango wa kuachana na Kangwa,”Ambacho watu hawajui ni kwamba tajiri (Yusuf) kwa sasa anataka kuona timu ikifanya vizuri kuanzia kwenye ligi ya ndani na Afrika ndio maana yupo mbele kwenye kila jambo,”

“Baada ya fainali tegemeeni kuona wachezaji wengine wakubwa wakitambulishwa, wakubwa (viongozi) wamekuwa na vikao vingi hasa vikijikita kwenye namna ya kukiboresha kikosi kulingana na mapungufu ambayo yameonakana msimu huu,” alisema kiongozi huyo.

Mbali na eneo la beki ya kushoto pia inaelezwa kuwa Azam inataka kuboresha upande wa kulia ambao ameonekana zaidi msimu huu kwenye michezo mikubwa na migumu, Lusajo Mwaikenda akicheza ambaye hiyo sio nafasi yake kiasili.

Eneo lingine ambalo Azam FC itashusha kifaa ni ushambuliaji, wanataka kuleta mashine ya mabao ambayo itasaidiana na Price Dube, huku Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutoka Yanga akiwa ameshasainiwa.

Soma zaidi hapa kwa taarifa za usajili duniani.

Leave A Reply


Exit mobile version