Klabu ya Al Ahly kutoka nchini Misri imefuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya kombe la dunia kwa klabu baada ya ushindi mzito wa bao 3-1 dhidi ya Al Ittihad ya Saudi Arabia.
Al Ittihad kutoka Saudi yenye Mastaa kama Benzema, Ngolo Kante na Fabinho walikumbana na kipigo hicho pasi na huruma huku mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid anayekipiga katika kikosi cha Ittihad Karim Benzema akikosa penati kwa kazi nzuri ya Mohammed El Shenawy, penati ambayo ingewasaidia kusawazisha bao la Ali Maâloul aliyefunga kwa mkwaju wa penati dakika ya 21.
Kazi nzuri sana ya Mohammed El Shenawy iliendelea kuwaweka salama Al Ahly na kipindi cha pili Ahly walicharuka na kufunga mabao mawili kupitia kwa Hussein El Shahat dakika ya 59 na Emam Ashour dakika ya 62 na kwenye dakika za fidia Karim Benzema aliipa Ittihad bao la kufutia machozi.
Huenda ukawa mwisho wa mshambuliaji Anton Modeste wa Al Ahly ambaye ameoneshwa kadi nyekundu na hajawa kwenye kiwango bora tangu ajiunge na timu hiyo huku tetesi zikidai Januari hii huenda akatemwa na mabingwa hao mara nyingi wa bara la Afrika.
Urejeo wa Mohammed Abdelmonem ulikuwa muhimu sana kwenye safu ya ulinzi lakini pia kiwango bora zaidi kutoka kwa Mahmoud Kahraba aliyetoa asisti ya bao moja kiwango bora zaidi ndani ya miezi miwili ya karibuni kwa Ahly.
Mchezo wa mapema zaidi Club Leon walifungwa na Urawa kutoka Japan bao 1:0 goli la Schalk dakika ya 76 ya mchezo.
Baada ya kutinga nusu fainali Al Ahly anakutana na bingwa wa bara la Amerika kutoka nchini Brazil , Fluminese huku nusu fainali nyingine ikiwakutanisha Urawa Red Diamonds kutoka nchini Japan dhidi ya mabingwa wa bara la Ulaya Manchester City. Unadhani kwa kiwango walichokionesha leo Al Ahly wana nafasi ya kuwa bingwa wa dunia kwa vilabu?
Endelea kufuatilia habari zetu kuhusu kombe la dunia kwa klabu kwa kusoma zaidi hapa.