Ndege aina ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 260 ndiyo itakayowabeba wachezaji wa Yanga na mashabiki kwenda Algiers nchini Algeria kwa ajili ya mchezo wao wa fainali dhidi ya USM Alger.
Yanga wanaondoka kesho Juni Mosi, 2023 kwenye mchezo kwa ajili ya mchezo wao wa marudiano na USM Alger utakaochezwa Juni 3, 2023. Mchezo wa kwanza Yanga ilifungwa magoli 2-1 katika Uwanja wa Mkapa, Dar.
Yanga kwenye mchezo huo wa fainali hiyo ya kombe la shirikisho la CAF itaongozwa na Waziri wa Utamaduni na Michezo, Balozi Dk Pindi Chana.
Akimzungumza na waandishi wa habari leo Jumatano ya Mei 31, 2023, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametimiza ahadi yake ya kuipa ndege Yanga kwa ajili ya kwenda kuipeperusha bendera ya Taifa kwenye mchezo wa fainali dhidi ya USM Alger.
Msigwa amesema zaidi ya mashabiki 3,000 wamejitokeza kwa kupeleka majina yao kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni na Michezo.
“Katibu Mkuu amekuwa na kazi kwa siku mbili kwa kuwa ndege inabeba zaidi ya watu 260, huku timu ya Yanga na maofisa wake wakiwa 90,” amesema Msigwa
Amesema ndege hiyo itakuwa na Yanga huko na itarejea nchini Juni 4, 2023.
“Kwanza kabla ya kutua Algeria itazunguka pale kama mara tatu hivi na huo ni ushindi wa kurudi na kombe” amesema Msigwa
Amesema mashabiki watakaokwenda hawatalipia gharama za usafiri kwa ndege imetolewa na Rais Samia, ni bure.
“Ndege ni bure watakao kwenda watatakiwa kulipia huko gharama za malazi na kula. Tunataka wachezaji wa 12 nje ya uwanja, washangiliaji” amesema