Klabu inaposajili mchezaji inakuwa na malengo ya kufaidika na huduma yake, bahati mbaya wengi wao wanashindwa kutimiza kusudi wakikabiliwa na changamoto kama majeraha na kukosa ushindani dhidi ya wapinzani wao wa namba.
Kijiweni linakuchambulia mastaa wanaokipiga Simba, Yanga, Singida Big Stars na Azam FC ambao ni kama watumishi hewa baada ya baadhi yao kucheza kwa nadra na wengine kukosa nafasi kabisa.
Erick Johora (Yanga)
Tangu kipa Erick Johora ajiunge Yanga 2021 hana nafasi, zaidi ya kucheza Kombe la Mapinduzi msimu huu, tofauti na makipa waliokuja nyuma yake kama Aboutwalib Mshery na Metacha Mnata ambao angalau wanapata nafasi mbele ya namba moja Djigui Diarra. Jumanne alipewa mechi dhidi ya Mbeya City na kukubali kufungwa mabao matatu katika sare ya 3-3 iliyopatikana Uwanja wa Sokoine.
Abdallah Shaibu ‘Ninja'(Yanga)
Beki wa kati Abdallah Shaibu ‘Ninja’ baada ya kusumbuliwa na majeraha ya hapa na pale, alipopona akakuta washindani wake wa namba wapo kwenye viwango vya juu,hivyo isingekuwa rahisi kwake kuingia kikosini, hadi ilifikia hatua ya kwenda kwa mkopo wa miezi sita Dodoma Jiji.
David Bryson-(Yanga)
Beki wa kushoto, David Bryson tangu ajiunge Yanga 2021 hana nafasi ndani ya kikosi cha kwanza, uwepo wa Joyce Lomalisa na Kibwana Shomari ambao viwango vyao vipo juu na ndio wanaobadilishana kucheza, hivyo ana kazi ya ziada kuhakikisha anamshawishi kocha kupata nafasi.
Dickson Ambundo (Yanga)
Yanga ina mawinga wanaofanya vizuri, jambo linalompa wakati mgumu Dickson Ambundo ambaye wakati fulani alikuwa kwenye kiwango kikubwa cha kuisaidia timu, hivyo ana kazi ya ziada kuaminiwa upya.
Chrispin Ngushi (Yanga)
Kuna wakati alikuwa anasumbuliwa na majeraha, ndipo akaibuka Clement mziza aliyepandishwa kikosi B na matunda yake yameonekana ana mabao matano ya Ligi Kuu na sita ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), hilo ni changamoto kwa Chrispin Ngushi kupambana zaidi kupata nafasi ya kucheza.
Mamadou Doumbia (Yanga)
Imekuwa ngumu kwa Doumbia kupenya katikati ya mabeki wa kati kama Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na sasa ameibuka Ibrahim Bacca, japokuwa ni mgeni ana kazi ya kupambania namba kikosi cha kwanza.
Peter Banda (Simba)
Wakati anasajiliwa Simba alichukuliwa kama chipukizi lakini miaka inaenda bado Banda hajaonyesha kile kiwango kilichotarajiwa kama mgeni na msimu huu hakuwa wa kiwango kwake, hivyo ana kazi ya kufanya ili kujipa umuhimu kikosi cha kwanza.
Gadiel Michael (Simba)
Inasemekana ni kati ya wachezaji waliopewa barua ya mkono wa kwa kheri, tangu ajiunge Simba akitokea Yanga hajaweza kumuweka benchi, nahodha msaidizi Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ panga pangua kikosi cha kwanza na kamzima mazima hadi kikosi cha Stars.
Habib Kyombo (Simba)
Simba ilimsajili Habibu Kyombo kuongeza idadi ya mabao akitokea Mbeya Kwanza, hadi sasa ana mabao mawili aliyofunga KMC na Dodoma Jiji na hana nafasi kikosi cha kwanza, ambacho kina washambuliaji kama Moses Phiri mwenye mabao 10, John Bocco tisa na mwingine mwenye mawili ni Kibu Dinis huyo kafunga na Geita Gold na Yanga angalau kidogo anapata nafasi.
Hemed Ismael Sawadogo (Simba)
Kiungo mkabaji Sawadogo alisajiliwa dirisha dogo kuongeza nguvu, ajabu hajawa na mchango kwenye timu na ni kati ya wachezaji wa kigeni wanaotarajiwa kupewa mkono wa baibai na mastaa wengine atakaoungana nao ni Nelson Okwa,Augustine Okrah, Mohamed Outtara, Victor Akphan huku Ousmane Sakho ikitajwa anaweza akapelekwa kwa mkopo.
Wakati huo huo wazawa nje na Gadiel anatajwa Nassor Kapama, Mohamed Mussa kuhusu mkongwe Jonas Mkude jina lake linatajwa kujadiliwa wapo wanaosema aondoke, wengine wakitaka abaki, bado mambo hajaamuliwa kipi kitatendeka kwa staa huyo.
Ukiachana na Simba na Yanga baadhi ya timu nyingine kama Singida Big Stars kuna Amissi Tambwe,Ibrahim Ajibu, Yassin Mustapha kwa Azam FC ni Cleophas Mkandala,Rodgers Kola, kipa wa kigeni Ali Ahamada,Wilbol Maseke (kipa).