Mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara uliowakutanisha mabingwa watetezi Yanga SC, umemalizika kwa Yanga kuendeleza ubabe katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo mabao ya klabu ya Yanga yamefungwa na kiungo Stephane Aziz Ki akifunga mawili, la kwanza kwa penalti dakika ya 45 na la pili dakika ya 65, mengine mshambulaji Mzambia Kennedy Musonda dakika ya 76 na winga Muafrika Kusini, Mahlatsi ‘Skudu’ Makudubela dakika ya 83.Bao pekee la Mtibwa Sugar limefungwa na Seif Abdallah Karihe dakika ya 90.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 27 katika mchezo wa 10, ingawa inabaki nafasi ya pili ikizidiwa pointi moja na Azam FC ambayo pia imecheza mechi mbili zaidi huku hali ikizidi kuwa mbaya kwa Mtibwa Sugar baada ya kichapo cha leo, kwani wanaendelea kushika mkia wakiwa na pointi tano kufuatia kushuka dimbani mara 13.
Endelea kusoma zaidi habari zetu kwa kugusa hapa.