Simba maarufu Kaskazini mwa Tanzania aliyeishi katika Hifadhi ya Serengeti, ‘Bob Junior’ ameuawa baada ya kushambuliwa na kundi la Simba watatu waliokuwa na lengo la muda mrefu la kuuangusha utawala wake, Mamlaka za hifadhi nchini humo zimethibitisha kifo hicho kilichotokea Jumamosi iliyopita.
Simba hao watatu waliowahi kujaribu kujisimika ufalme walilelewa na ‘Bob Junior’ tangu wakiwa wadogo lakini majaribio ya kufanya mapinduzi mara kadhaa ili kuuangusha utawala wa Bob Junior haukufanikiwa na badala yake walikimbizwa katika maeneo hayo, yaliyopo mashariki mwa hifadhi hiyo.
Simba ‘Bob Junior’ akisaidiana na kaka yake, Joel walitawala kwa zaidi ya miaka mitano na kuwa miongoni mwa Simba waliotawala kwa kipindi kirefu zaidi kabla ya kufanyika mapinduzi.
Mhifadhi Mwandamizi wa hifadhi hiyo, Fredy Shirima ameieleza kuwa tukio hilo ni asilia katika uhifadhi lakini pia hutokea zaidi kwa Simba ambao hushikilia ngome dhidi ya wengine wanaoitaka ngome.
Shirima anasema, “Bob Junior aliuawa siku ya Machi 11, akishambuliwa na Simba watatu ambao walikuwa sehemu ya kundi la simba saba waliokuwa wanapanga mapinduzi. “…kwa kawaida hatuwezi kuingilia maisha ya wanyama pori… hivyo kilichotokea kilipangwa miongoni mwao ikiwa ni vita vya kimapinduzi na simba huwa wana tabia hiyo ambapo mtawala anapozeeka hutolewa kimabavu,” alieleza.
CHIMBUKO LA UMAARUFU WA ‘BOB JUNIOR’
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, ni Simba aliyejibebea sifa kwa kuwa mpole na anayekuwa na utulivu anapoona watalii.
Shirima anasema, ‘Bob Junior’ pia alikuwa na sifa za kipekee kama vile kuwa na manyoya mengi zaidi kuliko simba wengine lakini mwenye kuvutia kwa muonekano na hutulia pale anapopigwa picha.
Wadau wa utalii wamesikitishwa na kifo cha simba huyo, huku ikimtaja kuwa ndiyo Simba bora na mtulivu kuwahi kuonekana katika hifadhi ya Serengeti.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali,Tanzania ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya simba kuliko nchi nyingine yoyote barani Afrika.
Inakadiriwa kuwa na simba 15,000 huku hifadhi ya Serengeti pekee ikiwa na takribani simba 3,000.