Ilipoishia “Kwanza pole sana Jacklin, Dunia yako imekugeuka lakini ndivyo ilivyo sababu siyo Watu wote wanakuwa na simulizi tamu za Maisha yao, yako chungu sana. Osman alikutafuta sana, ilisadikika kuwa Mlikuwa mmeuza kila kitu na kuondoka” Alisema Dokta Simon, stori yake ilikuwa ngeni masikioni mwangu
“Tuliuza kila kitu?” Nilimuuliza
“Ndiyo! Mzee Dhabi pia alihangaika kuwatafuta bila mafanikio, mwisho alikata tamaa baada ya kupata taarifa kuwa mliuza nyumba na kuondoka wewe na Mama yako!”
Haraka niligundua kuwa Mzee Dhabi alifanya yote pasipo Osman kujuwa. Endelea
Sehemu Ya Kumi Na Tatu
“Hapana Baba yake Osman alitumia hasira zake kutuondosha kwenye ile nyumba na kuchukua kila kitu tulichonunuliwa na Osman, hatukuuza nyumba wala mali yoyote ile vyote vilichukuliwa na Mzee Dhabi, tuliishi Maisha ya mateso sana Mimi na Mama yangu” nilisema, nilishindwa kuzuia uchungu ulio ndani ya moyo wangu, nililia sana tena kwa kwikwi
“Usilie Jacklin, kwasasa unaishi wapi?” Alihoji Dokta Simon, nilifuta chozi langu nilitulia kwa sekunde kadhaa kisha nilimjibu
“Uswahilini, tulikuwa tunaishi kwa kuuza Mboga mboga mtaani. Na hii hali yangu nitaweza vipi kuendesha Maisha yangu Dokta!” Chozi liliendelea kunibubujika
“Usijali nitakuchukua utaishi kwangu Jacklin wakati tunafanya utaratibu mwingine” Alisema Dokta
“Samahani hivi Osman yupo wapi?” Niliuliza
“Osman anaishi Marekani..” Alijibu Dokta Simon huku akionesha kutaka kusema kitu kingine ambacho alijizuia asikiseme
“Anaishi na Zahra?” Nilimuuliza
Alishusha pumzi zake kisha alinitazama akanijibu
“Ndio, wanatarajia kufunga ndoa miezi mitatu ijayo hapa Nchini” Alisema Dokta Simon
“Natamani kumuona Osman ili nimwambie kuwa sikukataa kuokoa Maisha yake ila nilikuwa nimechelewa” Nilisema kwa kilio kikubwa
“Jacklin, hayo yameshapita, kwasasa tuangalie Afya yako kwanza ndiyo jambo lenye umuhimu zaidi kuliko chochote kile” Alisema Dokta Simon, nilimkubalia. Hakuchelewa sana aliondoka wodini
Hakuna aliyekuja kuniona kwa siku nilizokuwa Hospitalini, moyo ulijaa upweke na maumivu makali, nilimkumbuka Mama yangu jinsi alivyonilea na kunipigani katika nyakati zote. Nilitokwa na machozi kila wakati, Mama yangu aliondoka bila hata kuniaga, ilinipa shida sana hadi kuwa sawa. Dokta Simon alijitahidi sana kila alipopata muda alikuja kuniangalia na kunipa faraja kwa kuniambia maneno yaliyojaa matumaini makubwa sana japo nilishajuwa kuwa thamani ya Maisha yangu ilikuwa imeshaondoka.
Bili za Hospitali alizilipa mwenyewe Dokta Simon, nilimshukuru sana kwa ubindamu aliouonyesha kwangu. Alinichukua na kunipeleka nyumbani kwake baada ya mwezi mmoja kupita, alikuwa akiishi na Mke wake aliyeitwa Lidia. Niliishi kwa upendo na amani ya hali ya juu sana, Mke wa Dokta Simon alikuwa na moyo kama wa Mume wake ndio maana ndege hawa wawili waliruka pamoja sababu walifanana kwa kila kitu
“Usijali Jacklin Mungu atakupa ufalme mwingine kupitia maumivu yako” Alisema Mke wa Dokta Simon wakati nilipokuwa najifunza kutembea kwa kutumia Magongo
“Nashukuru kwa ukarimu wenu Lidia, mmenionesha thamani kubwa iliyo ndani yangu ambayo niliona imeondoka, nilihisi sitotabasamu tena. Mwisho ninekubali hali halisi kuwa siwezi kutembea hivyo nashukuru kwa kila kitu Lidia” Nilisema tukiwa tumesimama kando ya Barabara.
“Dokta Simon alinieleza kuhusu wewe na Osman, alikutolea figo na kuokoa Maisha yako”
“Ni kweli, katika vitu ambavyo ninajuta katika Maisha yangu ni kutomshukuru Osman kwa wema wake alionitendea na kumuomba Msamaha sababu sikuweza kuokoa uhai wake, nilishindwa kulipa fadhila za Ubinadamu wake” Nilisema, nilihisi chozi likinilenga taratibu
“Usijali Jacklin, hayo yameshapita. Haina haja tena kuingia kwenye Maisha ya Mtu nwingine na kumkumbusha yaliyopita. Sahau tu na Maisha yaendelee ” Alisema Lidia, tuliendelea na mazoezi
“Pamoja na yote ila uzuri wako Jacklin upo pale pale, wewe ni mzuri sana” Alisema Lidia,, alinifanya nitabasamu
“Unanichokoza?” Nilisema kwa utani kisha tulicheka, tulikuwa marafiki wakubwa sana kwa kipindi kifupi ambacho niliishi nyumbani kwao, walijitahidi kuniondoa upweke, walinisaidia sana sikuwa na mawazo kama Mwanzo.
Usiku mmoja nikiwa nimelala, kutokana na dawa kali nilizokuwa nameza kwa ajili ya kupunguza maumivu nilijikuta nikizama ndotoni. Ndoto ilianza kwa furaha sana, Niliota Tukiwa tunacheka na Osman, ghafla alikuja Mwanamke akiwa ameshikilia Bastola, Mwanamke huyo sikuiyona sura yake ila alisema
“Jacklin una muda mchache sana wa kuendelea kupumua, siwezi kukubali furaha yangu ukaiharibu kirahisi, Pumzi yako ya Mwisho sema neno moja kabla sijakumaliza” Alisema Mwanamke huyo, nilimtazama Osman ambaye alikuwa akishangaa tukio hilo, nilisema
“Nakupenda Osman” Lilikuwa ndiyo neneo langu la Mwisho katika pumzi yangu ya Mwisho, alinipiga risasi. Ghafla nilishtuka kutoka Usingizini, nilihema sana, Jasho lilikuwa likinibubujika, niliamka na kwenda kuwasha taa. Jumba la kifahari la Dokta Simon lilikuwa kimya sana, sikutaka kuwasunbua ila ndoto niliyoiota ilinishtua mno.
Nilijiuliza ndoto hiyo ilikuwa na maana gani, nilisali ili Mungu aniweke mbali na hatari hiyo kabisa. Nilikesha nikimuomba Mungu, Usingizi ulinichukua Alfajiri, Asubuhi nilimsimulia Lidia kuhusu ndoto yangu, alicheka tuu kisha alisema
“Tatizo rafiki yangu unawaza sana kiasi kwamba unatengeneza hadi picha ya Uwongo kwenye akili yako, kumbuka kila unachokifikiria hutokea hivyo acha kutengeneza Maisha mabaya ya Baadaye” Alisema akiwa ananiandalia chai, alikuwa akinichukulia kama Mtoto mdogo yani kwa jinsi alivyokuwa akinidekeza
“Nimekuelewa Lidia” Nilisema.
- •••••••••••••••••••••••••••••••••
Osman aliwasili Nchini kwa ndege ya shirika la Fly Emirate akitokea Marekani. Alirudi Nchini kwa ajili ya kufunga ndoa na Zahra, tangu alipoondoka kwa ajili ya matibabu miezi kdhaa iliyopita hakurudi tena. Aliwasiliana na Rafiki yake Dokta Simon, ilikuwa ni furaha kwa marafiki hao kukutana tena Osman akiwa mwenye Afya, katika Maongezi yao Osman aliniulizia lakini Dokta Simon hakutaka kumwambia Osman kuwa Mimi nipo nyumbani kwake, sina Mguu. Alifanya hivyo ili kuruhusu kila kilichopita kasirudi tena.
Nilishangaa siku hiyo Lidia aliniambia kuwa twende Shamba tukakague, sikuwa na pingamizi sababu nilikuwa sina kazi yoyote ile kumbe ndiyo siku ambayo Osman alikuwa anakuja kutembelea nyumbani kwa Dokta Simon, hawakutaka nionane na Osman, hawakutaka nijisikie vibaya. Basi tulipoondoka nyuma Osman alienda nyumbani kwa Dokta Simon kwa ajili ya kupata chakula cha Mchana na mazungumzo mengine ya kirafiki.
Tukiwa njiani tunaenda Shamba nilihisi kama kuna kitu hakipo sawa kwangu, sikuwa na furaha ya kwenda huko shamba, nilimwambia Lidia kuwa sijisikii vizuri kuendelea na safari hivyo turudi nyumbani.
“Unaumwa?” Aliniuliza Lidia
“Hapana, sihisi kama natakiwa kuwa sehemu ya safari hii, samahani Lidia” nilisema ili kama nitakuwa nitakuwa nimemkwaza anisamehe, Lidia alisema
“Mbona tumekaribia Jacklin jamani, ni hapo tu wala siyo mbali hata hivyo hatuchelewi” Alisema Lidia, nilizungumza sasa kama Binadamu ambaye sijatumia viungo vya mwili, si unajuwa vilema jinsi ambavyo wanapenda kujiongelea madhaifu yao
“Turudi Bwana au sababu unajuwa siwezi kutembea ndiyo uniringie hivyo? Sijisikii na safari” Nilisema kisha niliuchuna, niliegemea kwenye kioo huku moyo ukiniambia niwahi kurudi nyumbani, hata mwenyewe sikujuwa ni kwanini nilikuwa nataka kurudi nyumbani wakati tulikubaliana kuwa twende Shambani.
“Usiseme hivyo Jacklin, Usimkufuru Mungu kiasi hicho, haya turudi” alisema Lidia kisha aligeuza gari, moyo ulianza kuchanua
Sasa kingine nilichokigundua ni kuwa Lidia alikuwa bize kupiga simu mahali alafu simu ilikuwa haiiti, nilijaribu kuchungulia niliona alikuwa akimpigia Mume wake, nilijuliza alikuwa anataka kumwambia nini?
Sikuwa na kifua cha kuweza kukaa na dukuduku, nilimuuliza
“Unampigia nani?” Niliuliza makusudi tu wakati nilishaona alikuwa akimpigia Mume wake Dokta Simon
“Nampigia Dada atuandalie chakula” Alisema kwa tabasamu ambalo hata yeye mwenyewe aligundua kuwa alikuwa akiongopa, niliguna
“Mh! Haya” Wala sikutaka eti kumuuliza zaidi wakati niliona alikuwa akimpigia Mume wake, hali ile iliendelea kwa muda mrefu, sijui sasa simu ilikuwa inaita alafu haipokelewi au vipi, sikutaka kuhoji zaidi bali nilihisi jambo ambalo sikuwa na uhakika nalo. Tulipofika Mjini kulikuwa na foleni kiasi hivyo angalau nilimuona akitabasamu hadi nilishangaa yaani Watu wanakasirika kisa foleni yeye anafurahia
Nilicheka chini chini baada ya kugundua alikuwa amepagawa, Basi haikutukuchukuwa muda mrefu kufika nyumbani. Niliiyona gari ya kifahari ikiwa imeegeshwa karibu na Bustani ya Mauwa, ilikuwa ya kifahari sana.
“Ile gari ni ya Nani?” Niliuliza maana sikuwahi kuiyona pale nyumbani
“Aaah ile?” Aliuliza Lidia kama vile hakuwa na jibu la kunipa, nilimkazia
“Ndiyo! Ile nyeusi sijapata kuiyona hapa nyumbani, inaonekana ni ya kifahari sana.” Nilisema huku Lidia akiwa anasogeza gari eneo la maegesho.
Kumbe Dokta Simon alikuwa tayari amewasiliana na Mke wake kwa njia ya ujumbe mfupi, lengo lao lilikuwa ni kutotaka Mimi na Osman tuonane pale. Huko ndani sasa ambako Osman na Dokta Simon walikuwepo walikuwa wakizungumza mambo yao ila waliposikia ngurumo ya gari, Osman alitaka kuchungulia huku akimuuliza Dokta Simon
“Shemeji Lidia huyo?” Simon alipoulizwa hivi alibakia akiwa anajiuma meno asijuwe ajibu vipi, ni kweli tulikuwa Mimi na Lidia sasa angemjibi vipi ikiwa hataki Mimi na Osman tuonane?
“Ndi…ndi…oo”
“Mh! Mbona unajibu kama hauna uhakika, ni bora ukaangalie kama ni yeye maana muda wangu umeisha hapa ingawa nilihitaji sana kumuona” Alisema Osman
“Sawa ngoja nikaangalie, jisikie huru rafiki yangu” alisema Dokta Simon kisha alikuja kwenye Maegesho akatukuta mimi na Lidia tukizozana maana alikuwa hataki nishuke kwenye gari
“Bora hata Shemu umefika yaani Mkeo simuelewi kabisa, huwezi amini ananizuia kushuka kwenye gari” nilisema
“Aaah Mke wangu kwanini unafanya hivyo?” Aliuliza Dokta Simon
“Jacklin hajanielewa, nilikuwa nimemwambia asubirie wewe ufike ili ukamuoneshe sapraizi yake” Alisema Lidia, nilijikuta nikitabasamu kusikia kuna Sapraiz
“Sapraiz gani hiyo?” Niliuliza, mkononi Dokta Simon alikuwa na kitambaa cheusi akaniambia anifunge machoni
“Jamani jamani Sapraizi gani hiyo mbona mnanitisha” Nilisema
“Hebu kwanza nikufunge ili ukaiangalie Sapraiz itakayo kufanya upagawe” Alisema Dokta Simon, Basi nilikubali kufungwa kitambaa kumbe lengo lao lilikuwa Nisimuone Osman, Walinipeleka nyuma ya nyumba
“Jamani nna hamu ya kuona hiyo Sapraiz” Nilisema
“Haya hebu nikufungue” Alisema Dokta Simon, moyo wangu ulijawa na furaha sana nilipomuona Kasuku akiwa kwenye kizizi chake, nilikuwa napenda sana Kasuku, sikuwaza chochote tena. Nilivuta Magongo yangu na kulisogelea Zizi la Kasuku, Dokta Simon alimpa Ishara Mke wake kuwa anatoka, muda huo akili yangu wala haikuwa hapo, walinipeleka sehemu ambayo hata nisingeliweza kusikia sauti ya gari
Osman alikuwa akimsubiria Dokta Simon ndani, alipofika alimdaka kwa swali
“Ni yeye?”
“Mke wangu?”
“Ndiyo!”
“Aah hapana, ni Kijana wangu wa kazi alikuwa akileta gari”
“Oooh! Sawa Basi ngoja Mimi niende” Osman aliaga, alielekea lilipo gari lake kisha aliondoka pale nyumbani bila kuhisi wala kujuwa kuwa nilikuwa pale.
Nilikuwa nacheza na kasuku wangu mzuri niliyepewa kama zawadi, nilisahau kila kitu. Lidia na Mume wake waliingia ndani
“Hajashtuka chochote” aliuliza Lidia
“Hapana sijui Jacklin!”
“Hapana japo alikuwa na wasiwasi kama nilivyokutumia meseji kuwa hatukufika shambami aligaili njiani” Alisema Lidia
“Mmmh kuna namna hawa Watu wawili wanawasiliana kifikra, sitaki waonane, sitaki turudi tulipotoka. Osman ameamua kuendelea na Maisha yake, nataka Jacklin naye aendelee na Maisha yake, atapata Mtu atakaye mpenda kwa jinsi alivyo” Alisema Dokta Simon, alikuwa ni Mtu safi sana, roho yake ilikuwa nzuri iliyojaa huruma
“Cha Msingi ni kuendelea kuhakikisha hajisikii mpweke” Alimalizia Dokta Simon.
Hayo ndiyo yalikuwa Maisha yangu, mipango ya Harusi ya Osman iliendelea kufanyika, kumbe katika kipindi hicho chote Osman alikuwa hajakata tamaa ya kunitafuta japo Baba yake alimuongopea kuwa tuliuza nyumba na kuhama mji, alinitafuta bila mafanikio lakini alijipa tumaini kuwa ipo siku ataniona,
Masikini hakujuwa kama Mimi ni kilema wa Mguu, hakujuwa kuwa Mama yangu ambaye alikuwa akihangaika naye kunitafutia figo alikuwa amefariki siku nyingi. Hakujuwa kama nilikuwa nikiishi kwa rafiki yake.
Wazazi wa Osman walikuja kutoka Dubai, Harusi ilipangwa kwa kuzingatia heshima aliyonayo Mzee Dhabi, umaarufu na utajiri wake. Moyo wa Mzee Dhabi ulificha unyama ambao alitutendea Mimi na Mama yangu.
Lidia na Osman walikuwa ni miongoni Mwa Watu wa karibu wa Familia ya Mzee Dhabi, walishiriki maandalizi kisiri sana bila Mimi kujuwa kwa kipindi chote, walikuwa wakiingia na kutoka alafu hakukuwa na stori zozote kuhusu Ndoa ya Osman, nakumbuka siku moja nilimuuliza Dokta Simon kama ndoa ya Osman ilikuwa imepita
“Imeshapita, walitaka kufanyia huku lakini walighaili, imefanyika huko Dubai ambako anaishi kwasasa” Ndicho alichonijibu Dokta Simon, nilikuwa mnyonge baada ya kusikia hivyo
“Usijali Jacklin, haikuwa ridhki yako ndiyo maana yalitokea yaliyotokea, sahau kila kitu Maisha yaendelee sawa?” Alisema tena Dokta Simon
“Sawa” Nilijibu huku moyo wangu ukiwa na maumivu makali sana, Osman kuowa haikuwa shida kwangu ila kilichoniuma zaidi ilikuwa ni kushindwa kumshukuru na kumwambia kuwa nipo Hai anisamehe kwa kila kitu.
Nilikaa na picha ya Osman kwa muda mrefu, siku moja niliichoma moto, nilifungua ukurasa mpya wa Maisha yangu, niliyapotezea maumivu kwa kucheza na Kasuku wangu, sikutaka kabisa kumfikiria Osman wala kukumbuka kilichomfika Mama yangu maana mambo hayo mawili yalikuwa yakinifanya nakuwa mnyonge sana. Niliamua kujisahaulisha hata alichonifanyia Mosses..
Siku moja ilikuwa Mchana nilimpigia simu Lidia nikamwambia kuwa nina hamu ya kula Ice Cream, alikuwa kazini hivyo alinitaka nivumilie kidogo, baadaye alimtuma dereva taxi aje kunichukua anipeleke mahali ambapo Lidia alikuwepo ili tukanunue Ice Cream. Nilipofika niliingia kwenye gari ya Lidia, tulielekea kwenye Ice Cream huku tukipiga stori za hapa na pale ambazo zilituburudisha kwa kiasi fulani.
Kutoka nilipomkuta Lidia hadi sehemu ambayo Ice cream zilikuwa zinauzwa hapakuwa mbali sana, mwendo mfupi tu tulikuwa tumefika. Kutokana na hali ya Mguu wangu Lidia aliniomba nisishuke kwenye gari badala yake nimsubirie! Basi Lidia alishuka na kuingia zinapouzwa Ice cream ambazo nilikuwa nikizipenda sana, alichelewa sana hadi nilianza kujiona mpweke ndani ya gari
Nilitamani kushuka lakini kabla wazo la kushuka halijaniingia sawa sawa, simu ya Lidia iliita, iliita kwa muda mrefu sana hadi nilitamani kuangalia ni nani alikuwa akipiga ila nilihisi uvivu fulani, sasa katika angalia angalia niliona kitu kama kadi hivi. Nilipata shahuku ya kuiangalia, nilinyoosha mkono na kuichukua.
Nilianza kuisoma, ilikuwa ni kadi ya harusi ya Osman na Zahra, moyo uliniripuka paa! Nikaangalia mlango ambao Lidia aliingia hakukuwa na Mtu aliyekuwa akitoka nikaendelea kuisoma. Cha ajabu kadi ile ilikuwa haijatumika kabisa yaani tarehe iliyoandikwa ilikuwa ni siku mbili mbele, zilikuwa kadi kama tano hivi zenye majina ila hiyo moja ilikuwa haina jina basi niliiweka kwenye mkoba wangu haraka ili nikitulia niisome vizuri, nilijikuta nikianza kuwa na huzuni sana.
Punde Lidia alirejea ndani ya gari akiwa na Ice Cream, nilimtazama sana hadi aliniuliza
“Vipi kuna tatizo?” Aliniuliza akiwa ananipatia Ice Cream, nilitabasamu tu baada ya kugundua kuwa nilikuwa nikifichwa jambo maana Dokta Simon alisema Harusi imeshapita ila cha ajabu kadi zile zilisema kuwa ni siku mbili baadaye
“Hakuna shida” nilimjibu
“Nimepata hiyo ile nyingine unayoipenda haipo” Alisema Lidia
“Hata hii siyo mbaya kikubwa ni Ice Cream” nilimjibu kisha nilianza kufakamia Ice Cream, nilikula kwa hasira sana baada ya kugundua Lidia na Mume wake hawakuwa wakweli
“Tunarudi nyumbani au kuna mahali unataka twende” aliuliza Lidia akiwa anawasha gari
“Nafikiri turudi nyumbani tu” Basi Tulirudi nyumbani.
Tulipofika nilielekea chumbani kwangu nilihakikisha nimefunga mlango vizuri ili niweze kuisoma ile kadi kwa utulivu, nilikaa kitandani, niliitoa na kuanza kuisoma tena. Kibaya zaidi ni kuwa waliokuwa wakizisambaza zile kadi walikuwa ni Dokta Simon na Mke wake Lidia.
Nilitamani kulia kwa uchungu ambao nilikuwa nikiusikia kwenye moyo wangu, mara nyingi nilikuwa nikiwauliza kuhusu Osman lakini walikuwa wakinipa majibu ya Hatuna mawasiliano naye sana kwa sasa
Nililia sana, niliona nimenyimwa haki ya kumuomba msamaha na kumshukuru Osman, niliihifadhi ile kadi kwenye Begi langu la nguo. Sikutaka kuwauliza chochote kile, siku hiyo Usiku Lidia alikuja chumbani kwangu na kuniambia kuwa anasafiri na Mume wake kwenda Nje ya Jiji watarudi baada ya wiki moja
“Nitawamiss sana jamani” nilisema
“Usijali Jacklin hata sisi tutakumiss mno, ubaki salama na kwa chochote usisite kutupigia simu” Alisema Lidia
Alipoondoka nilitafakari nifanye nini maana nilijuwa tu walitengeneza safri feki ili kunizuga kuhusu Ndoa ya Osman. Kweli siku iliyofuata asubuhi mapema waliniaga rasmi, waliingia kwenye gari niliwapungia mkono wa kuwaaga, waliniacha na Mdada wa kazi na Mlinzi.
Walipoondoka nilimfuata Mdada wa Kazi aliyekuwa anaitwa Scola nikamuuliza
“Unakunbuka siku ambayo Mimi na Lidia tulienda Shambani? Ile siku ya mwisho?..” nilimuuliza alionekana kutafakari sana
“Ndio nakumbuka” alinijibu baada ya kuwa tayari amemaliza kutafakari
“Kuna mgeni alikuja hapa si ndiyo?” Scola alinitolea macho yake Makubwa
“Scola nijibu alikuja Mgeni si ndiyo?” Nilimuuliza tena baada ya kuona alikuwa hanipi jibu
“Lakini Dada..” alisema Scola, nikahisi kuna jambo
“Sitaki cha lakini nataka uniambie ukweli ni nani alikuja hapa?” Nilimkazia sauti na jicho
“Baba alisema nisiseme unanipa wakati mgumu Dada Jacklin” Nilimshika mkono Scola nikamuingiza chumbani kwangu nikamwambia
“Tupo Mimi na wewe naomba unieleze ukweli ni nani alikuja hapa”
Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya KUMI NA NNE Ya PUMZI YA MWISHO
Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost RIWAYA Mpya Hapa Kijiweni
Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM
SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI
JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa
Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho xx Pumzi Ya Mwisho
4 Comments
Jamani Jackline😢
Mapenzi mabaya sana yasikie tu kwa mwenzako omba yasikukute
Leo umejitahidi sana admini
😇😇😇😇
https://whatsapp.com/channel/0029VanxLVYJ93wbHawAAh3H
Maisha Kitaa WhatsApp channel