Kiungo wa Juventus, Pogba, asimamishwa kwa muda baada ya kugundulika kutumia dawa za kuongeza nguvu mwilini Iwapo atapatikana na hatia ya kutumia dawa za kuongeza nguvu mwilini, Pogba, ambaye alikuwa nyota wa Ufaransa katika Kombe la Dunia la mwaka 2018, anaweza kusimamishwa kwa hadi miaka minne.
Kiungo wa kati wa Ufaransa wa Juventus, Paul Pogba, amesimamishwa kwa muda baada ya kupatikana na matokeo chanya kwa kutumia dutu iliyopigwa marufuku, kulingana na mahakama ya kitaifa ya kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini nchini Italia (NADO Italia), iliyosema siku ya Jumatatu.
Kipimo hicho, kilichofanywa baada ya ushindi wa Juventus wa 3-0 katika msimu wa Serie A dhidi ya Udinese mnamo Agosti 20, kiligundua testosterone, homoni inayosaidia kuongeza uvumilivu wa wanariadha.
“Kwa kukubali ombi lililotolewa na Mwendesha Mashtaka wa Kitaifa wa Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kuongeza Nguvu Mwili, imetoa kwa muda kusimamishwa kwa mwanariadha Paul Labile Pogba,” NADO Italia ilisema katika taarifa.
Mahakama hiyo ilisema Pogba alikiuka sheria za kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini walipogundua dutu iliyopigwa marufuku “metabolites ya testosterone isiyo ya asili”, na kuongeza kuwa matokeo hayo yalikuwa “yanalingana na asili ya nje ya misombo lengwa.”
Pogba mwenye umri wa miaka 30, alikuwa akiba katika ushindi dhidi ya Udinese.
Juventus ilisema wamepata habari za kusimamishwa kwa muda na wanafanya tathmini ya hatua zijazo.
Iwapo atapatikana na hatia ya kutumia dawa za kuongeza nguvu mwilini, Pogba anaweza kusimamishwa kwa kati ya miaka miwili hadi minne.
Mkataba wake na Juve unakamilika mnamo Juni 2026.
Pogba amekuwa na wakati mgumu katika kipindi chake cha pili na Juventus kutokana na majeraha tangu aliporejea katika klabu hiyo iliyoko Turin baada ya kuondoka Manchester United mwaka jana.
Mshindi wa Kombe la Dunia la mwaka 2018 hakucheza sana msimu uliopita kutokana na majeraha ya goti na nyama za paja pamoja na upasuaji wa goti uliomzuia kucheza kwa Ufaransa katika Kombe la Dunia nchini Qatar.
Pogba bado hajaanza mechi msimu huu lakini amecheza mechi mbili akiwa kama mchezaji wa akiba, mara ya mwisho akiwa uwanjani katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Empoli.
Soma zaidi: Habari zetu kama hizi hapa