Ilipoishia “Asante Yesu” Mikono yake ikiwa juu, Mchungaji akaja na kumwinua
“Matilda, kanisa linakuhitaji useme neno” Mchungaji George alimsogeza Matilda hadi Madhabauni, akampa kipaza sauti. Aseme nini? ndicho ambacho Matilda alikua akiwaza, umati ulikua mwingi hapo kanisani, macho yote yakawa kwa Matilda Msichana wa miaka 28
Alikua akitetemeka kwa kila alichofikiria kukisema, alikua kama amepigwa shoti vile, alimtazama Mama Naomi ambaye alimpa ishara ya kumtia moyo kua aseme chochote hapo kanisani. Endelea
SEHEMU YA NNE
“Asanteni kwa wote, asanteni sana. Nilikata tamaa kabisa lakini roho mtakatifu ameniinua kupitia nyie” Alisema Matilda, Chozi lilimbubujika kilio kikamzidi maarifa akaweka kipaza sauti huku akimpa ishara Mchungaji kua hawezi kuzungumza kabisa.
Kanisa kikazizima, hadithi ya Maisha ya Matilda ikawaliza wengi, bahati nzuri muda huo wataalam wa kuhesabu pesa walikuwa tayari wamemaliza, Mchungaji akawatangazia kua wamepata Milioni tano, Matilda hakuamini masikio yake
“Sikutegemea kabisa kama kwa taarifa hii iliyo ghafla tungeweza kukusanya kiasi kikubwa namna hii, pesa hii itaenda moja kwa moja Hospitali muda huu ili Mtoto aanze matibabu” Alisema Mchungaji, Akawaambia waumini waendelee na ratiba zingine, yeye, Mama Naomi na Matilda wakaingia kwenye gari ya kanisa, safari ya kuelekea Hospitali ikaanza.
“Mama Matilda, napata hisia mbaya juu ya Mtoto wetu” Alisema Baba Matilda akiwa ameketi kwenye Mkeka, Mama Matilda alikua akimalizia kuweka kuni jikoni, kauli ya Mume wake ikamfanya aache alichokua anakifanya, akapiga hatua za taratibu huku sura yake ikijawa na Mshangao akamsogelea Mume wake, akajishika kiuno
“Kwanini unasema hivyo Baba Matilda?”
“Jana usiku nimeota ndoto mbaya sana kuhusu Matilda, sina hakika kama Atakua hai na kama yupo hai basi anaishi kwa Mateso ya Golgota” Akasema Baba Matilda huku akikunja vizuri goti lake wakati huo Mama Matilda akivuta kigoda na kuketi huku macho yake yakiwa bize kwenye sura ya Mume wake
“Mungu amuepushe Binti yetu na majaribu yoyote yale, hujui jinsi roho yangu inavyouma Baba Matilda” Akasema Mama Matilda huku akifuta chozi lake
“Tokea nikiwa shambani leo sijisikii vizuri kabisa, nimeliweka jambo moyoni kama Mwanaume lakini Mwisho wa siku nimeshindwa nimeona ni bora nilitoe, Huu wasiwasi sijui utaondoka lini”
“Baba Matilda Mtoto yupo hai, na anatukumbuka sana. Ewe Yehova tenda kwa ajili ya Binti yetu popote alipo, mpe roho ya kurejea nyumbani ili sisi tuwe na Amani” Akasema Mama Matilda mikono ikiwa juu, Hakika familia hii ilikua yenye misingi thabiti ya dini.
“Kama siyo huu umasikini basi ningeenda Mjini kumtafuta Matilda, hatuna Mtoto mwingine sisi” Jinsi Baba Matilda alivyokua akilalamika alizidi kumfanya Mama Matilda adondoshe chozi lake.
“Baba Matilda moyo unaniuma sana tena zaidi ya sana, nikiwa kama Mama naumia kuliko unavyofikiria” Alisema Mama Matilda kisha akaingia ndani akiwa analia, alimuacha Baba Matilda akiwa amejishika tama.
Mchungaji, Matilda na Mama Naomi walikua kwenye kordo la Hospitali tayari kuelekea kwa daktari kwa lengo la kukabidhi pesa ili upasuaji uanze. Ghafla polisi waliwasimamisha, sintofahamu ikatawala
“Sisi ni Maafisa wa polisi, Matilda upo chini ya ulinzi kuanzia sasa..” Alisema askari mmoja, Matilda alishtuka
“Mimi?”
“Ndiyo” Akasema polisi
“Afande…huyu Binti amefanya nini?” alihoji Mchungaji George kwa Mshangao Mkubwa sana.
“Utajua ukifika kituoni, ruhusa ya kukamatwa kwake hii hapa” Alionesha
“Polisi nimefanya nini Mimi jamani, tafadhali msinifanyie hivyo. Binti yangu ni mgonjwa sana anahitaji matibabu” Alisema Kwa kilio Matilda lakini tayari pingu zilikua zimeshafungwa kwenye mikono yake, pesa zilikua mkononi mwake, haraka Mchungaji akataka kuzichukua lakini polisi wakazuia
“Chochote mtakachokifanya hapa kitatumika kama Ushahidi Mahakamani”
“Vijana, tafadhari sana hizo ni pesa kwa ajili ya matibabu ya Mtoto, kama mnamkamata Matilda basi hizo pesa hazihusiani na sababu yoyote ile ya Kumkamata, hizi ni pesa kutoka kanisani” Alisema Mchungaji George akitaka pesa ziachwe lakini polisi hao walikua tayari wameanza kumchukua kwa nguvu Matilda ambaye alikua akipiga mayowe ya kutaka aachwe ili akamtibie Binti yake Patra.
Aliyeucheza mchezo huu alikua amejibanza mahali akiangalia namna mpango wake unavyofanikiwa, Neema akashangilia baada ya Matilda kutupwa kwenye difenda ya polisi, gari hiyo ikaondoka haraka sana. Mchungaji na Mama Naomi wakatazamana kwa mshangao mkubwa hawakujua waende wapi, waingie kwa daktari bila pesa au waelekee Kituo cha polisi ambacho walikua wametajiwa.
“Mchungaji nenda Polisi Mimi naenda kwa Mzazi mwenzake” Alisema Mama Naomi huku taharuki ikizidi kuwa kubwa ndani yao
“Kwa Mzazi mwenzake wakati amemkataa Mtoto? Twende pamoja polisi kujua nini chanzo cha kukamatwa kwake”
“Na vipi kuhusu hali ya Mtoto Mchungaji?” Aliuliza Mama Naomi
“Oooh hapa sasa nachanganikiwa Mimi, basi baki hapa ukiangalia hali ya Mtoto, wacha Mimi nikimbilie Polisi” Alisema Mchungaji, akakimbilia kwenye gari na kuondoa gari kwa kasi sana, Mama Naomi alipoona Mchungaji ameondoka naye akaondoka kuelekea kwa James kumpa taarifa.
Neema akajitokeza kisha akajinasbu kua ni lazima Matilda aondoke Dar.
********
Mchungaji George alipofika kituo cha polisi alipaki gari kwenye maegesho, kisha akashuka haraka haraka na kukimbilia ndani ya kituo hicho cha polisi. Akapandisha ngazi kabla ya kukutana na polisi
“Afande nimekuja haraka sababu bado sijajua sababu ya kukamatwa kwa huyu Binti” Alisema Mchungaji akiwa anamwangalia Matilda ambaye alikua amekalishwa chini
“Nifuate” Alisema polisi huyo kisha akamnyanyua Matilda wakaelekea kwenye chumba kimoja ambacho kilionekana wazi kilikua chumba cha mahojiano, Mlango ukafungwa, ndani kulikua na askari wawili wengine ambao waliwakuta humo
“Huyu Binti ni mwizi, mahali anapoishi siyo pake kuna Mtu amemweka akae hapo lakini mwenye nyumba amelalamika juu ya upotevu wa vitu vyenye thamani ya Zaidi ya Milioni 10” Alisema polisi huyo akiwa na sura kavu sana.
“Ameiba?”
“Ndiyo”
“Afande Mimi siyo mwizi na sijawahi kuiba chochote kile, nimeishi pale kwa zaidi ya mwaka mmoja iweje leo ionekane Mimi ni Mwizi? James anakosea sana” Alisema kwa uchungu sana Matilda
“Kaa kimya hupaswi kuongea chochote kile hadi pale aliyekushtaki atakapofika hapa” Alisema polisi huyo
“Jamani kuweni na huruma, huyu Binti ana Mtoto mdogo ambaye ni mgonjwa sana na yupo Hospitalini, hizo pesa mlizomkamata nazo ni michango ya kanisa kwa ajili ya Matibabu” Alisema Mchungaji
“Kwakua umeshafahamu nini kilichopelekea akakamatwa basi ni vema ukakaa kimya huku ukisubiria uendeshwaji wa kesi hii, kama unahitaji kuwa shahidi wa hili basi tukutane mahakamani” Alisema Polisi huyo ambaye alishapewa Hongo na Neema ili kesi hiyo iwe hai
“Nenda nje” Akasema polisi huyo akimtaka Mchungaji aondoke
“Afande kua na moyo wa utu japo hata kidogo, Mtoto wake anaangamia kule Hospitali kwa kukosa matibabu, ninaomba sana na nipo chini ya Miguu yenu ikibidi hata kua Mdhamini wa hili, hizo pesa nazihitaji zikamtibie Binti yake” Alisema Mchungaji George akishinikiza apewe pesa hizo lakini polisi wakamtoa Nje Mchungaji George
Matilda alikua Mtu wa kulia muda wote huku akiomba kwa Mungu kuhusu hali ya Binti yake, dakika chache baadaye aliingia Neema akiwa ameambatana na yule Mwanaume anayeitwa Masudi, akavuta kiti na kuketi, Matilda alishtuka baada ya kumwona Neema
“Matilda, kama ulifikiria unaweza ukachomoka kwenye hili basi sahau kabisa” Alisema Neema, polisi wakatoka ili kuwaachia wazungumze
“Kumbe ni wewe ndiye uliyenifungulia hii kesi isiyo na kichwa wala Miguu, wewe ni Mzazi mtarajiwa si ndiyo? utajisikiaje ukitendewa namna nitendewavyo Mimi…Kumbuka Binti yangu yupo Hospitalini na anahitaji Matibabu…” alisema kwa uchungu Matilda huku chozi likimvuja, alishindwa kufuta chozi sababu alifungwa pingu mikononi
“Kumbe inaumiza eeeh? basi hivi ndivyo ambavyo Mimi pia naumia ninapokuona mbele ya macho yangu, una chaguo moja la kufanya, nalo ni kukubali kurudi kwenu kabla hujafikishwa mahakamani, ukikubali hii kesi naifuta haraka sana, sitaki kukuona ukiendelea kuwa karibu na James kwa lolote lile” Alisema Neema
“Dada yangu kama unafikiria Mimi ni dhahifu kwenye hilo naomba usahau kabisa, ikibidi mniuwe lakini siwezi kuidhurumu haki ya Mwanangu Kumjua Baba yake” Alisema Matilda, akapigwa kofi na Neema
“Mshenzi mkubwa wewe, sasa endelea kujifanya Mjuaji kwenye hili, mwisho wako unakuja” Alisema Neema kisha aliondoka hapo akiwa na Masudi, walipofika kwenye gari Neema alionekana kua na hasira sana sababu lengo halikua kesi bali ni kumtisha tu Matilda
“Usiwe na hasira, huu ni mwanzo tu Naamini mateso atakayoyapata atakubali kuondoka mwenyewe” Alisema Masudi, Mwanaume ambaye alionekana kua karibu sana na Neema
“Kama kuteswa inabidi ateswe haswa, kwasababu amekataa kuondoka kwa uhuru basi ataondoka kwa shari kama atakavyo” Alisema Neema kisha aliondoa gari haraka sana.
“Nikusaidie nini?” lilikua ni swali aliloulizwa Mama Matilda baada ya kufika ofisini kwa James, hakukaribishwa ofisini bali aliachwa getini azungumze
“Ni kuhusu Matilda” Alisema Mama Naomi akiwa anahema “Amefanyaje?”
“Amekamatwa na Polisi muda mchache uliopita, hadi sasa hatujui sababu ya kukamatwa kwake. Nakuomba James, hunijui lakini Mimi ni jirani wa Matilda kule anakoishi, fanya uwezalo ili aachiwe”
“Usinichekeshe ndugu yangu,, yaani umetoka kote huko hadi hapa ili kuniambia hicho tu? unaonekana kama Mwanamke mwenye busara zako lakini sikutegemea kama mwisho wa siku ungesimama na Mwizi” Alisema James akionekana hana wasiwasi kabisa
“Mwizi? nimeishi naye kwa siku zote hakuwahi kuonekana na tabia hiyo ya wizi, hata kama akawa mwizi lakini ana haki ya kuokoa Maisha ya Binti yake, fanya kwa ajili ya Patra ni Binti yako yule James” Alisema Mama Naomi, kofi likatua kwenye shavu lake la kulia
“usirudie tena hiyo kauli, hakuna unachojua kuhusu Mimi…..Ondoka” Alisema kwa hasira sana James
“Laiti kama ungelijua Maisha anayopitia Matilda sasa hivi wala usingethubutu kunipiga, basi siyo Mtoto wako lakini kumbuka wewe ndiye uliyemtoa kwao basi thamini utu kama Binadamu wa kawaida” Alisema Mama Naomi kwa uchungu sana huku Mtoto akiwa analia mgongoni
“Nini ambacho hujanielewa?” Alisema James kwa hasira akiwa anamsogelea Mama Naomi, kelele hizo zikamtoa Sekretari hadi nje
“Bosi kuna nini?” aliuliza
“Simjui ananilazimisha nimsaidie, amekua king’ang’anizi sana Jack!”
“Halafu kama alikuja jana huyu na Mdada mwingine, sura nishaikumbuka kumbe walikua wanahitaji msaada? kwanini usiwasaidie Bosi?” aliuliza Jack
“Hujui kitu hakuna msaada unaotolewa kwa kung’ang’ania namna hii, Kutoa ni moyo, sikia nenda ofisi zingine hapa hatusaidii omba omba” Alisema James kisha akarudi ofisini
Jack akamtazama Mama Naomi. Akiwa kama Mwanamke alimuonea huruma Mama Naomi na Mtoto aliye mgongoni, akatoa noti ya elfu tano akampa
“Chukua hii itakusaidia” Alisema Jack
“Asante lakini huu siyo msaada ambao Mimi niliutaka kutoka kwa Bosi wako” Alisema Mama Naomi
“Ulikua unahitaji msaada gani?” Jack akapata shahuku ya kutaka kujua zaidi maana hakuna ombaomba ambaye anaweza kukataa shilingi elfu tano, akasogea
“Bosi wako James amezaa na Msichana yule ambaye nilikuja naye jana, James amemkataa Mtoto sababu ni mlemavu, Mtoto yupo mahututi Hospitalini, Yule Msichana amekamatwa na polisi muda siyo mrefu ndiyo maana nilikuja hapa ili kumpa taarifa akamsaidie hata Mtoto sababu anahitaji matibabu, hakuna pesa ya kumtibia” Alisema kwa uchungu Mama Naomi huku akikaribia kudondosha chozi, Jack aliumia sana
“Sikia chukua hii kadi yangu, kwa lolote naomba unipigie, nenda sababu James ana hasira sana” Alisema Jack, kila alivyomtazama Mama Naomi akiwa anaondoka alisikitika kisha akarudi Ofisini, akamkuta Bosi wake akiwa anataka kutoka
“Yaani Watu wengine Bwana kutaka kuharibiana siku tu, kwani ni lazima kumsaidia Ombaomba….Mimi natoka sijisikii kufanya chochote kwa sasa, siku nyingine usiruhusu Omba omba katika ofisi yangu”
“Sawa Bosi” Aliitikia Jack
Jua lilikua kali lakini Mchungaji George alihitaji kujua hatma ya Maisha ya Matilda, Mateso yalianza upande wa Matilda, alipigwa bila kosa lolote lile. Lengo lilikua ni kumtaka aondoke Dar ili asiwe kero kwa James, ndicho alichokipanga Neema.
Baada ya Saa nzima aliingia Mama Naomi akamkuta Mchungaji George akiwa anachomwa na jua la Mchana
“Eeeh kulikoni Huko Hospitali kuna usalama?” aliuliza Mchungaji George kwa Mshtuko sababu alimuacha Mama Naomi Hospitali
“Sijui Mchungaji lakini natumaini hakuna kitakachoharibika, Mungu aliye hai anapigana vita nzito muda huu, vipi kuhusu Matilda?”
“Bado yupo kituoni, hizo sauti unazozisikia ni zake, anaonekana kua kwenye mateso makali” Alisema Mchungaji
“Jamani sasa amewakosea nini?”
“Wanasema ameiba vitu vyenye thamani kwenye nyumba anayoishi”
“Ameiba? si kweli, Maisha anayoishi Matilda ni ishara tosha kua hawezi kuiba, hawa Watu kwanini waneamua kumkatili Binti wa watu jamani”
“Hatuna namna Zaidi ya kusubiri muda utupe majibu sahihi, Kama hakufanya hivyo basi ataachiwa tu ila kinachonipa hofu ni kuhusu Binti yake, sijui itakuaje”
“Mchungaji hapo ni pazito zaidi sababu uliponiacha Hospitali nilitoka na kwenda kwa Mwanaume aliyezaa naye lakini huwezi amini kamkana mbele ya Macho yangu, kanipiga kofi pia” Alisema Mama Naomi akiwa anamweka vizuri Mtoto
“Sijui hata tufanye nini, kwani wazazi wa Matilda wapo wapi?”
“Wazazi wake wapo Njombe, pamoja na shida anazopitia lakini alisema hawezi kurudi kwao wala kusema chochote kwa Wazazi wake”
“Oooh Mungu wangu, basi wewe ungerudi tu nyumbani Mimi nitabakia hapa kwa masaa kadhaa kwa ajili ya kujua Hatma ya Matilda” Alisema Mchungaji George
“Sawa Mchungaji kwa chochote kile tuwasiliane” Alisema Mama Naomi kisha akaondoka kituoni hapo.
Upande wa pili, gari moja lilikua likiendeshwa kwa spidi kubwa sana, ndani yake alikuwepo James akionekana kuchanganikiwa, maneno ya Mama Naomi yaliendelea kujirudia ndani ya Kichwa chake, akawa anapiga usukani kwa hasira, alikanyaga mafuta hadi nyumbani kwake, akateremka haraka kisha akaingia ndani
Kama akili yake ilivyomtuma ndivyo alivyokuta, Neema alikua ameketi huku akitikisa miguu yake, pembeni kukiwa na embe bichi ambalo lilikua linasukuma tabasamu lake, baada ya kumwona James akiwa ameingia na taharuki akamuuliza
“Kulikoni Baby mbona una taharuki?” aliuliza Neema akiwa ameacha kula embe Bichi
“Nenda kafute kesi inayomkabili Matilda” Alisema James kisha akajitupa kochini kama Mtu aliyechoka sana
“Unasemaje?”
“Ulivyosikia ndivyo nilivyosema, hakuna sababu ya kuendelea na kesi, tuangalie namna nyingine ya kumfanya Matilda aondoke hapa Mjini” Neema akamtazama Kwa hasira James
“James Mimi natarajia kua Mama wa Mtoto wako, siwezi kuzaa Mtoto katika familia yenye migogoro namna hii, ikishindikana nitoe ujauzito ili ulee Mtoto wako na Matilda” Alisema Neema
“Sina maana hiyo Neema, Sina lengo hilo nawe huna sababu ya kufanya hivyo, tambua kiu yangu ni Mtoto lakini naona Matilda anateseka sana, Mtoto wake yupo Hospitalini”
“Kwahiyo umeanza kua na huruma si ndiyo? Basi hakuna sababu ya kujificha, jitokeze hadharani ujitangaze kua Bilionea mwenye Mtoto Mlemavu, si una shida sana ya Mtoto basi hakuna sababu ya Mimi kubeba huu mzigo wakati una Mtoto unaye muonea huruma” Alisema Neema kwa hasira zaidi, akanyanyuka ili aondoke lakini James akamshika mkono kwa lengo la kumzuia asiondoke
“Mpenzi hupaswi kua na hasira sababu wewe ni Mama mtarajiwa, natamani haya mambo yaishe kwa namna nzuri, basi nitaenda Polisi kwa ajili ya kuzungumza na Matilda ili aondoke hapa Mjini” Alisema James lakini Neema akatoa Mkono wa James akaelekea chumbani.
Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya TANO Ya PIGO TAKATIFU Msisahau COMMENTS Ziwe Nyingi
Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost RIWAYA Hapa Kijiweni
Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM
SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI
JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa
Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx
5 Comments
Sawa
kama ni kwel duuh matlida anapep yake
Aiseee huyu enema anazngua ..s wampe pesa Ile mchungaj jmn 😣😣
Moyo wangu unauma hadi joz dah!! Tukija kwenye uhalisia sure ni maisha watu wanapitia jmn
Hadithi nzri nakama ina uhalisia fulani hivi