Ilipoishia “Tulirudi kule kwenye ghorofa la Tancot House ambapo ndiyo tulilala usiku uliopita, Nilijaribu nguo zote ikapatikana moja tu ambayo ilionekana kuwa nzuri sana na yenye kunipendeza zaidi
“Wow!! Hii ndiyo yenyewe Jojo, nina uhakika hawezi kuchomoka, sasa unapaswa kuwa makini sana sababu ni lazima akuchukue kama kimada wa kulala naye Usiku, ndipo utakapo iba hayo madini, utachunguza kujuwa yalipo, baada ya kufanikisha zoezi, utafungua dirisha sababu chumba chake kipo mashariki mwa jengo hilo, utayatupa madini kwa kutumia kifaa ambacho kitakuwa kimehifadhi kisha utayachukua baada ya kushuka, kuwa makini sana vinginevyo unaweza ishia huko Hotelini, pia ni lazima ukamilishe zoezi ili uwe huru” alinieleza Sarafina. Endelea
SEHEMU YA KUMI
“Sawa” niliitikia ili kuondoa ngoma juani sababu nilishajua utakuwa ni mtihani mzito sana kufanya hivyo.
Basi tulienda kula na tuliporudi tulilala, asubuhi alinipa kadi maalum ya kuingilia Hotelini kwa ajili ya Hafla hiyo.
“Kila la kheri Jojo” Alisema Sarafina, sikuwa na maneno mengi ya kuzungumza sababu nilishapewa maelekezo yote na nikayaelewa
“Upande ambao utayatupa madini kuna bustani ya mauwa hivyo kuwa makini sana uyatupe mahali ambapo utaweza kuyaokota kirahisi, utayatupa sababu hutoweza kupita nayo mlangoni walinzi wake watakukagua”
“Ok sawa!”
Japo niliikubali kazi ile ili niwe huru ila nilikuona cha mtema kuni maana jukumu lilikuwa zito sana, niliendelea kupiganisha akili yangu, nilifikiria jambo kwa pale kwenye hoteli kuna kamera hivyo itakuwa rahisi mimi kuonekana, niliwaza nifanye nini maana kama nitaonekama nitatafutwa na kukamatwa kwa kosa ambalo litawafaidisha wengine, wakati naendelea kutafakari niliona picha ya paspot pembeni, ilikuwa ni picha ya Sarafina. Niliivuta kwa mguu bila Sarafina kushtuka kisha niliiweka kwenye mkoba wangu huku nikijuwa ndani ya akili yangu nitafanya nini ili kuwa salama.
Jioni mishale ya saa 12 Jioni, Sarafina alinieleza kuwa ndiyo muda wa kuelekea Hotelini kwa ajili ya kuiba hayo madini, nilijiangalia kwenye kioo nilijikuta nikitabasamu licha ya hatari iliyo mbele yangu, uzuri wangu, nilifanana sana na Marehemu Mama yangu.
Tulitoka, nje alinipakiza kwenye gari moja ya kifahari sana nyeusi.
“Mimi siwezi kwenda huko sababu kadi ni moja tu ambayo nimekupa wewe, ifanye kazi uwe huru Jojo, ukitugeuka basi juwa msala huu utakuwa wako peke yako” alinisistiza Sarafina
“Nimekuelewa Sarafina” Basi, nilifunga mlango kisha safari fupi sana ya kuelekea Hotelini ilianza, ilituchukua dakika nne kufika Hotelini, nilishuka kwenye gari baada ya kukaguliwa kama Mwana Malikia vile kumbe nilikuwa mwizi tu.
Mlango Mkuu wa Kuingilia nilitakiwa kuonesha ile kadi, nilifanya hivyo kisha niliruhusiwa kuelekea ndani ambako kulikuwa na hiyo Afla iliyo hudhuriwa na viongozi kadhaa na wafanya biashara wakubwa wa Tanzania. Sikuwahi kuingia sehemu nzuri na ya kifahari kama ile katika Maisha yangu, ilinifanya niwe muoga kiasi chake japo hakuna aliyeshtuka.
Hadhi niliyovishwa ilikuwa kubwa sana, mavazi niliyovaa yaliakisi ukubwa wangu na hadhi yangu, nilionekana ni mwenye Maisha mazuri, mzuri na mrembo kuliko Wanawake wote waliohudhuria kwenye Afla hiyo.
Niliketi kwenye meza ambayo haikuwa na Mtu yeyote yule huku Watu wakiwa bize na mazungumzo ya Hapa na pale, nilimuona huyo Bilionea wa Madini akiwa ameketi anazungumza. Mahali nilipochagua kuketi palikuwa na urahisi wa yeye kuniona pindi atakapogeuza shingo yake, Wanaume wengi walikuwa bize kunitazama nami nikajifanya bize na Afla hiyo ambayo ilikuwa ikiendelea.
Walikuja Wanaume kadhaa kuniuliza maswali fulani ambayo nilijuwa lengo lilikuwa ni kunihitaji kimapenzi ila niliwakatalia hata kuketi karibu na Mimi sababu kufanya hivyo kungemfanya Bilionea pindi atakaponiona asiwe na wazo la kunihitaji.
Bilionea huyo alikuwa Kijana mtanashati, kichwa changu kilikuwa na maelekezo yote kutoka kwa Sarafina na Mkuu wa Magereza juu ya kuiba hayo Madini yenye thamani kubwa sana japo nilijuwa haitokuwa rahisi kufanya hivyo, nililetewa Vinywaji na chakula nikawa ninakula ila akili na macho yangu yakiwa kwa huyo Bilionea Kijana.
Nililetewa vimemo kadhaa vya Wanaume vyenye namba, nilivisoma na kuvitupa sababu hakuna hata kimoja kilichotoka kwa Mlengwa wangu, niliendelea kusubiria kwa masaa kadhaa huku akionekana bize sana kucheka, Moyo wangu ulihitaji uhuru hivyo niliona
kazi hiyo ingenifanya niwe huru na kurudi Tabora.
Nilizuga kufanya vitu kadhaa ikiwemo kwenda chooni ilimradi anione lakini haikuwezekana hadi pale dakika za mwisho ambapo aligeuka akaniona kidogo alafu akarudisha macho kwa aliyekuwa akiongea naye, nilihisi labda hakuuona uzuri wangu, nilianza kukata tamaa kumbe alikuwa ameniona ila alikuwa akitafuta engo nzuri ya kunitazama, nikiwa nimeshakata tamaa nataka kunyanyuka. Niliona nimtazame kwa mara ya mwisho huku nikijiambia
“Geuka unitazame basi” Nilisema kwa hisia na kwa kumaanisha kabisa, ile namtazama nilikutana naye ana kwa ana tena akionekana alikuwa akinitazama kwa muda mrefu, basi nilijitingisha kidogo alafu nikatazama chakula changu, nikawa na uhakika kuwa ameniona na alikuwa akiniangalia kwa kunitamani.
Basi, Dakika chache alikuja mlinzi wake akaniambia
“Bosi anahitaji kuzungumza na wewe” Alisema, ili nisionekane mrahisi nilimwambia
“Mwambie akome sikuja hapa kwa ajili ya Mtu yeyote yule” Nilisema, yule Mlinzi aliganda kidogo kisha akasema
“Dada usipoteze bahati yako, Bosi wangu ni Bilionea Mkubwa wa Madini, amekuwa akikuangalia kwa muda mrefu sana” Alisema tena, sasa niliona nikubali maana kujizugisha wakati kilichonileta kilikuwa ni hicho niliona ni Ujinga
“Yupo wapi?” niliuliza kanakwamba nilikuwa simjui
“Yule Pale kwenye ile Meza” Alisema kisha nilipeleka macho huko, niligongana naye macho akiwa ananikodolea sana, moyoni nikasema
“Umenasa Bosi”
Basi, nilinyanyuka taratibu nikaelekea kwenye hiyo Meza, alitoa walinzi wake akaniambia
“Kuwa huru, karibu Naitwa Bilionea Vitalis Kyando” Alisema kisha alinipatia Mkono wake, nilimpa wangu tukashikana
“Naitwa….Juliana” Nilifikiria kusema jina langu halisia nikaona inaweza niletea shida baadaye, niliamuwa kumdanganya.
“Ooh Juliana! Nimefurahi kukufahamu, hakika Mungu alikuumba kwa utulivu sana, muda mrefu nimekuwa nikikutazama alafu akili yangu ilikosa utulivu, unastahili kila kilicho bora Juliana, Niambie unataka nini” Aliniuliza Swali kwa ujasiri Mkubwa sana, niliwaza vingi kwa haraka sana, nikakumbuka kauli ya Msonjo kuwa Mimi ni mzuri sana ninapaswa kuishi Dar, Nilifikiria nifanyaje na nipo kwenye mpango wa kumuibia ili niwe huru
“Asante! kukufahamu pekee ni kitu kinachonitosha” Nilisema japo nafsi ilikuwa ikinisuta na kuniita Zuzu wa Mwisho
“Juliana Usiogope kama unahitaji Biashara, Nyumba, gari zuri la kutembelea niambie tu kuwa huru labda hujajuwa unaongea na Mtu gani….Hebu nifuate” Alisema huyo Bilionea, alinyanyuka kisha nami nilinyanyuka nikajiuliza alikuwa anataka kunionesha kitu gani, Basi nilimfuata huku walinzi wake wakija kwa nyuma.
Tulipanda Lifti hadi ghorofa ya nne ambapo ndipo alipokuwa amechukua chumba.
“Kama walinzi wangu wanakufanya usiwe huru Juliana niambie sawa?” Alisema Bilionea Vitalis Kyando, niliitikia kwa ishara ya Kichwa tu hata sikusema chochote huku moyo ukianza kunienda mbio maana hao Walinzi walikuwa kama Saba tena walioshiba sasa nikawaza endapo nitagundulika naweza kuuwawa hapo kisha ndoto yangu ya kuwa huru ikazimwa.
Tulipofika karibu na Chumba chake aliwaambia walinzi wake.
“Msijali nipo sawa” Aliwaambia kisha Sisi tuliingia Chumbani kwake, angalau moyo wangu ulichanua kidogo
“Juliana, pamoja na pesa zangu na umaarufu nilio nao ila sijawahi kumuona Mwanamke mzuri kama wewe, nikikusifia sana naona nitakufuru ila Hakika Mungu alikupendelea sana” Alisema akiwa ananisogelea,, nilishajuwa alichokiwa anakihitaji kwangu na niliambiwa udhaifu wake upo kwa Wanawake wazuri weupe
“Unamaanisha nini? na huku umenileta kufanya nini?” Nilimuuliza Bilionea Kyando
“Oooh Ok!!” Alisema kama Mtu aliyesahau kitu, alielekea kwenye kabati alifungua akatoa kibegi kidogo, kisha alikuja nacho karibu yangu alikifungua akatoa madini ambayo Mkuu wa Magereza na Sarafina waliniambia, Moyo wangu ukasema
“Wow!!”
“Katika Maisha yako umewahi kushika madini Juliana….hebu yashike” Alinishikisha yakiwa kwenye mfuko maalum, kiukweli ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kushika madini tena mengi kiasi kile, Nilibakia kinywa wazi huku nikipiga hesabu nafanya nini ilia nimeweza kuyaona kirahisi hivyo.
Bilionea aliongea Kama Mtu aliyerukwa na akili kabisa ndiyo nikaamini udhaifu wa Mtu haujalishi ana nyazifa gani.
Aliyachukua madini akayarudisha kwenye kabati, kisha alirudi nilipokuwa nimesimama
“Ndiyo maana nimekwambia sema unataka nini Juliana, Mwanamke mzuri kama wewe unastahi kilicho bora, nipo tayari kukupa kilicho bora na kukutunza hata ukitaka kuishi Kama Mtoto wa Malkia” Alizidi kusema, Nilimwambia
“Nahitaji uhuru, hao walinzi wako wananiogopesha sana, sijawahi kuishi hivi kabisa sina amani” Nilisema huku nikijuwa jibu lake linanipa ishara ya kufanikiwa au kutokufanikiwa kwa mpango wangu wa kuina Madini yake
“Unataka waende wapi na kwanini wakati wapo kwa ajili ya Ulinzi wangu” Alisema kwa kukaza sauti hadi niliogopa nikahisi kama amenishtukia hivi
“Siyo lazima tubishane Mr. Bilionea, kama haiwezekani naomba niende” Nilisema kwa sauti yenye kujiamini mno
“Ok Sawa!!” alikubali niondoke, sasa vitu viwili vilinipinga na kunilaumu. Moyo ulisema Hapana, miguu ikawa tayari kuondoka pale Chumbani kwake, Ningefanyaje na tayari nimeshaweka uamuzi basi nilipiga hatua kama tatu fupi kuuelekea Mlango ghfla akasema
“Juliana!! wewe ni wa thamani huna haja ya kuondoka” Nikiwa nimesimama nilifurahi sana ndani ya nafsi yangu, alikuja mlangoni akafungua kisha akawaambia Walinzi wake
“Nendeni Chini hadi nitakapowaita”
“Lakini Bosi…”ilisikika sauti ya Mlinzi wake mmoja kisha Bilionea alimkatisha
“Mmh!! hakuna cha lakini, nitawapigia simu” Alisema kisha aliwatazama wakiondoka alafu akafunga mlango.
“Umefurahi? naamini sasa utakuwa huru kunipa uzuri wako” Alisema Bilionea huyo ambaye kwenye akili yangu nilimuita Bilionea Mwendawazimu, anaruhusu vipi Walinzi waondoke kisa Mwanamke ambaye hata hamjui, niligeuka na kurudi
Niliketi kitandani, hayo yote nilifundishwa na Sarafina sababu kazi hizo alikuwa ameshazizoea.
“Nahitaji kuoga kidogo” Nilisema
“Oooh Sawa Juliana” Alisema kama kichaa yaani Daah!! kweli udhaifu hasa kwenye mapenzi ni kitu kibaya sana,
“Nikimaliza na wewe unapaswa kwenda kuoga” Nilisema, basi aliachia tabasamu ila hakusema chochote. Nilibadili nguo nikaenda kuoga Bafuni nikamuacha pale Kitandani. Basi nilioga kwa kuzuga kama dakika kumi hivi, kisha nilitoka. Nilimkuta akiwa kitandani, alikuwa ameshabadilisha nguo zake na kuvalia pensi tu.
“Nenda kaoge” Nilisema.
“Tofauti yako na Malaika ni Majukumu tu, wao wanamsaidia Mungu na wewe upo na Mimi hapa” Alisema Bilionea nikiwa ninajifuta Maji, niliishia kutabasamu tu.
“Leo ni siku adhimu sana kwangu Juliana, nina uhakika itakuwa ni siku ya Kumbukumbu kubwa” Alisema, nilicheka tuu huku nikivaa chupi yangu, kisha nilijitupa kitandani kama Mzoga
“Ngoja nioge haraka” Alisema Bilionea Kisha aliingia Bafuni kuoga, kitendo bila kuchelewa nilivalia gauni langu kisha nilielekea kwenye Kabati ambapo alihifadhi madini, Mbinu zote nilifundishwa na Sarafina.
Nilikagua pale nilipoona aliweka lakini hayakuwepo, hapo ndipo niliposhtuka kuwa hata yeye alikuwa haniamini, nilianza kuyatafuta Fasta fasta huku nikimsikia akiwa anaoga huku akiwa anaimba.
Nilifanya Haraka mno, nilikagua kabati zima bila mafanikio, kwa jinsi ambavyo nilikuwa nimevurugua vitu pindi atakapotoka Bafuni ni lazima nitakamatwa tu, Nilifikiria nikasema ni lazima niondoke hata kama madini sikuyapata, nilichukua ile picha ya Sarafina kisha nikaitupa chini, ile nataka kutoka nililiona lile begi likiwa kwenye ubavu wa kabati, haraka nililichukua. Nikaenda kufunga mlango wa Bafu kwa nje kisha nikafungua dirisha, nilipoangalia chini niliiyona ile Bustani kisha niliyatupa yale madini yakiwa ndani ya Mfuko tu sababu sikutaka kulitumia lile begi lake.
Wakati naelekea mlangoni nilisikia akiniita nimfungulie, nilifungua mlango nikatoka ndani Mbio mbio huku nikiwa nimeziba sura yangu, nilishuka kwa mguu bila lifti, sasa ile nafika floo ya mwisho niliwaona wale walinzi wakipandisha juu, nilijificha mahali kisha nilisubiria hadi walipopita wakiwa wanapiga stori, mmoja wao akiwa anasema
“Hivi Bosi ana shida gani? hawa wanawake watakuja kumponza siku moja” Sikutaka kuendelea kuwasililiza badala yake nilikimbilia nje, mlinzi wa Hoteli aliniuliza vipi mbona Hai hai?
“Kuna kitu nimeangusha” Nilimjibu kisha nilizunguka nyuma nikachukua madini nikayatia kwenye Mkoba wangu.
“Umekipata?” aliniuliza yule Mlinzi
“Ndiyo kwaheri” Nilisema nikiwa na haraka sana maana nilijuwa tu wale walinzi wakifika kule juu kila kitu kitaharibika kama nitakuwa sijaondoka.
Kulikuwa na tax pale iliyomleta Mtu, niliitumia kuondoka, kisha nilienda kushuka kwenye kanisa la Azania Front nikamlipa pesa yake yule Dereva, sasa wakati nataka kuekea pale nilipomuacha Sarafina niliona askari, sijui askari hao walikuwa wakimitafuta mimi au walikuwa kwenye majukumu yao ya Usiku, ile Hofu nikajikuta naita Bajaji nikamwambia anipeleke Dar City Sinza.
ilikuwa ni mishale ya saa 5 Usiku, nilikuwa na hofu maana mzigo wa madini nilionao ulikuwa na thamani kubwa sana tena hata haukustahili kupanda Bajaji. Mwendo wa dakika 45 tulifika Sinza
Nilimlipa pesa kisha nilienda hapo Dar City, nilimuulizia Shonaa nikaambiwa zamu yake ni asubuh hadi mida ya Jioni hivyo yupo kwake, niliomba namba maana sikuwa na simu, ile nataka kutoka si nikakutana na Sarafina akiwa na Mkuu wa Magereza, nilijificha maana nilijuwa taarifa ya kuibiwa madini yule Bilionea iliwafikia alafu sikwenda kuwapa. niliwaza nijitoe ili niwape au nifanye nini, nikakumbuka nilichokifanya kule Hotelini niliweka picha ya Sarafina hivyo kwa vyovyote Sarafina atatafutwa ili Mimi nipatikane, wao waliponipita bila kuniona Mimi nilitoka ndani nikakimbilia kwenye Bajaji nikamwambia dereva nipeleke Mbele
“Mbele gani?” aliniuliza
“Twende tu hapo mbele haraka” Nilimsistizia yule dereva, basi aliondoa Bajaji pale akawa anaelekea mitaa ya kumekucha, nikamuomba dereva
“Naomba uipige hii namba” Nilisema
Aliichukua ikiwa kwneye karatasi akampigia Shonaa, alipokea nikaongea naye nikamwabia
“Nipo kwenye matatizo Shonaa, nielekeze Ulipo nije haraka” Nilisema, Shonaa alimuelekeza dereva wa Bajaji na uzuri mazingira hayo hayakuwa mageni ila mwanzo nilijichanganya kujuwa hiyo sehemu inaitwaje ndiyo maana sikurudi nilipopata matatizo kule Ubungo.
“Una matatizo gani Dada yangu?” aliniuliza
“Mazito hata nikikwambia huwezi kunielewa” Nilimwambia yule dereva ambaye baada ya kumjibu hivyo hakuuliza kitu kingine tena.
Tulifika alipokuwa anaishi Shonaa, nilimlipa yule Dereva wa Bajaji maana nilikuwa na pesa fulani nilizopewa na Sarafina wakati naenda kufanya kazi ya kuiba Madini.
Niligonga mlango wa Shonaa kwa kitambo sana bila kuitikiwa, akaja yule Mama aliyewahi kunidekisha choo kipindi kile
“Aah kumbe ni wewe, yumo humo ndani si umewahi kuishi hapa sasa si uingie” Alisema, yaani alikuwa Mshakunaku vibaya mno. Nilisubiria hadi alipoondoka ndipo niliposukuma mlango, kweli Mlango ulifunguka.
Taa zilikuwa zinawaka, pale sebleni hakukuwa na Mtu, nilifunga mlango kisha nilienda chumbani kwa Shonaa, niligonga napo sikuitikiwa, nilifungua mlango, nilikutana na kitu kilichonishtua sana, Shonaa alikuwa amelala kitandani damu zikiwa zimetapakaa
“Shonaa! Shonaaa!” Nilimuita, niliona akiwa bado mzima
“Ngoja nikupeleke Hospitali Shonaa umekumbana na nini Mama” Nilisema nikiwa kwenye heka heka ila Shonaa alinipa ishara ya kutulia kwanza kisha aliniambia
“Jojo aliyefanya hivi ni Sarafina, anakutafuta wewe una mzigo wa Madini. Nenda mbali sana na Jiji hili vinginevyo utauwawa” Alisema Shonaa kwa shida sana
“Siwezi kukuacha Shonaa ukiwa katika hali hii ngoja nikakuache Hospitali” Nilisema huku chozi likinibubujika
“Hapana huna muda Jojo, ondoka. Nikifa nitakufa nikiwa nakupambania, Kimbia Jojo” Alisema Shonaa, Mwanga ukamulika dirishani, nikachungulia nikaona Watu wakija uelekea wa Chumba cha Shonaa.
Haraka nilimwambia
“Naenda Shonaa nakupenda” Niliielekea ilipo swichi ya Taa ya nje, niliizima kukawa na giza kisha nikatoka haraka nikapitia mlango wa uwani nikakimbia eneo lile.
Nilikimbia sana Usiku ule huku nikiwa ninahofia kuhusu usalama wa Shonaa maana alikuwa akivuja damu nyingi sana.
Nilichukua pikipiki nikamwmabia dereva anipeleke Ubungo, nilichotaka sasa kilikuwa ni kurudi Tabora tu. Hali ilikuwa mbaya sana kwangu ndani ya Jiji la Dar, nilijiingiza kwenye janga zito sana ambalo lilihatarisha maisha yangu moja kwa moja, nilijilaumu sana ni bora hata ningekubali kumalizia kifungo changu kule Gerezani
Tulipofika Ubungo nilikata tiketi kisha nilienda kulala ndani stendi karibu na gereji ndogo iliyokuwa ikitengeneza mabasi, nilijikunyata kama kifaranga cha kuku, nilimuomba Mungu aliyenisahau anikumbuke ili niweze kuondoka salama kuelekea kwetu Tabora maana hali ilizidi kuwa mbaya.
Sikupata Usingizi, madini yalikuwa kwenye mkoba wangu, zaidi ya Bilioni 20 nilikuwa nimekaa nayo pale bila Mtu yeyote yule kujuwa kuwa nilikuwa na utajiri Mkubwa sana ambao ulkuwa na uwezo wa kubadilisha maisha ya Watu wote walio stendi kwa Usiku ule.
Baridi lilikuwa kali sana pale Ubungo lakini halikunizuia kuwa makini, gari niliyokata tiketi nilikuwa nikitazamana nayo macho. Alfajiri mapema sana nilikurupuka, pembeni kulikuwa na bomba la Maji, nilifungulia nikapata kuosha uso wangu ili kuondoa uchafu wa pale nilipokuwa nimekaa.
Macho yangu yalikuwa makali sana kuangalia huku na kule ili nisije ingia mikononi mwa Watu wanaonitafuta, Picha yangu ilikuwa imesambazwa kila kona ili nikionekana tu nikamatwe, Alfajiri hiyo nilienda kwanza kujisaidia kule chooni. Niliporudi niliona makundi ya Askari, hofu niliyonayo ilinifanya nisimame sehemu ili kuangalia Askari wale walikuwa wanafanya nini? Nilipoona wameenda mbali kidogo na nilipokuwa naenda Mimi nilisogea kwenye gari, muda huo tayari walikuwa wameruhusu Watu kuingia.
Sasa wakati naingia humo niliona picha yangu na ya Sarafina kuwa tunatafutwa atakayetuona atapata Donge nono, niliziba uso wangu nikashuka kwenye gari, nilirudi pale nilipokuwa nimekaa usiku kucha.
Hofu ilinijaa upya, niliona kabisa safari ya Tabora inaweza kufa tena, nikiwa naendelea kutafakari nilihisi kuguswa kwenye bega langu. Nilipogeuka nilikutana na Mtu ambaye alikuwa ana picha yangu, nahisi Mtu huyo alinihisi kuwa ndiye Mimi ila kutokana na giza alisema
“Samhani nilikufananisha” Alisema kisha alisonga mbele, nilitumia mkoba wangu kuficha sura yangu, nilionelea ni bora nitoweke Ubungo maana kuendelea kuwa Ubungo kungeniletea Shida kubwa sana, nilisogea geti dogo nikapita nikatokea nje kabisa, kulikuwa na kigiza fulani hivyo ile hali ilinisaidia kujificha ili nisionekane.
Polisi walisambazwa kila kona ya Jiji na maeneo ya nje ya Jiji kutusaka Mimi na Sarafina, kutokana na lile tangazo nilijuwa wazi kuwa Sarafina alikuwa hajakamatwa. Madini bado nilikuwa nayo kwenye pochi langu. Niliona ni bora nitembee kwa Mguu kuliko kupanda Usafiri maana tayari nilikuwa natafutwa Nchi nzima na atakayeniona aliahidiwa kupewa zawadi Nono.
ilikuwa ni safari ya Jojo na Madini yangu, nilitembea kama Kichaa nikiifuata barabara ya Morogoro, nilipoona Askari nilichekupa na kuzama ndani kisha baadaye najitokeza na kuendelea na safari, kulipo pambazuka nilinunua kofia nikaivaa angalau ilinisitiri kwa kiasi fulani.
Nilibakiwa na pesa kidogo sana ambayo hata isingenifikisha Morogoro ila nilikuwa na mzigo wa madini yenye thamani ya Bilioni 20 kwenye Mkoba wngu. Kila mara nilifungua na kuangalia kama madini yalikuwepo, basi nilipojisikia njaa na kuchoka nilienda sehemu nikanunua chakula ila sikula pale nilienda kukaa chini ya Mti mmoja nikapata chakula. Maisha yangu yalipoteza nuru ila kile kiasi cha madini kilinipa nguvu ya kuzidi kusonga mbele, mida ya Jioni nilifika Kibaha Maili moja miguu ikiwa haitamaniki ilikuwa ikiuma sana.
“Ooh Mungu nimechoka sasa” Nilisema nikiwa ninakaa kando ya eneo la Mnada wa nguo, nilikaa hapo hadi giza lilipoingia. Chupi ilikuwa ikiniumiza kutokana na Uchafu wa kuivaa kutwa nzima, kwasababu eneo lile lilikuwa giza basi niliondoa ile chupi pale mnadani, pia kulikuwa na ronya za nguo ambazo ziliachwa nilitafuta pensi nikavaa pia tisheti niliipata nikaavaa na wala sikujali nitaonekanaje ila nilichotaka ni kwenda mbali na Jiji la Dar.
Sikutaka kupumzika Kibaha niliendelea mbele, Watu niliopishana nao walikuwa wakiongea kuhusu Mimi kuiba Madini bila kujuwa waliokuwa wakimzungumzia walikuwa wakipishana naye.
Zile nguo nilienda kuzitupa kwenye daraja moja ambalo lilikuwa linapitisha maji mengi kisha niliendelea na safari yangu, gari za polisi zilikuwa zikipita kwa wingi kama vile kulikuwa na msafara wa Rais wa Nchi kumbe ulikuwa ndio msako wangu na kwavile nilipita barabara ya vumbi nikiwa naitazama Barabara kuu kwa Mbali niliona jinsi msako ulivyokuwa ukiendelea.
Nilipochoka nililala Kwenye kichaka fulani hadi asubuhi kisha safari iliendelea, kadiri nilivyokuwa natoka nje ya Jiji ndivyo nilivyoanza kuhisi kuwa tayari nimejikwamua kutoka kwenye msako ule mkali, Nilichofikiria sasa kilikuwa ni madini na pesa nitakayoipata.
Pesa ilikuwa imeniishia kabisa, nilipofika mbele kidogo niliona sonara ndogo. Nilikaa sehemu nikapekua yale madini nikatafuta dini dogo sana yaani kakipande fulani tu ambacho nilihisi kuwa pesa yake isingekuwa kubwa sana, niliingia humo ili niuze. Nilijitahidi sana kukwepa macho ya Mtu wa Sonara
Nilimpa lile dini, kwanza alishtuka sana maana lilikuwa ni dini lenye thamani kubwa tofauti na nilivyofikiria, alilipima na kugundua kuwa lilikuwa lenyewe siyo feki kisha aliniambia
“Dada yangu pesa sina, hili nenda kauze Kwa wale wenye Sonara kubwa kabisa” Alikuwa Kijana mmoja wa Kipemba
“Linagharimu shilingi ngapi?” Nilimuuliza maana nilikuwa sijui kuhusu Madini
“Hili siyo chini ya Milioni 45 ndiyo maana nasema sina hela ya kukupa” Alijibu yule jamaa, sasa nilifikiria niende huko anakosema nilihisi nitakamatwa nikamwambia
“Wewe nipe uliyonayo, ukiuza nitakuja kuchukua hela kwako” Nilisema kama vile mzoefu wa hiyo Biashara.
“Alivyoskia hivyo alihangaika akafungua droo akatoa milioni mbili akaniambia
“Ipo hii ila nakuhakikishia hadi kufikia jioni litakuwa limeuzika, tena nitaenda Mjini kuliuza” Alisema.
Sikumjibu nilichukua zile pesa nikazitia kwenye Mkoba bila hata kuhesabu
“Ungezihesabu kwanza Dada yangu”
“hata Usijali nakuamini” Nilisema kisha niliondoka pale, Kumbe nyuma yule Dogo alipiga simu sehemu ambapo angeuza hilo dini, sasa taarifa zangu zilikuwa zimesambazwa kwa Wauza madini nchi nzima, yule jamaa aliambiwa anikamate.
Ile anatoka nje tu Mimi ndiyo kwanza nilikuwa nitoka na Bodaboda, nilipogeuka nilimuona akihangaika kujuwa nimeelekea wapi, ni wazi alikuwa hajaniona. Nilimwambia dereva aingie njia nyingine ili asionione kabisa, kweli dereva alinipitisha njia nyingine tukaenda kutokea Barabara Kuu.
Nilimlipa kisha nilichukua Pikipiki nyingine nikamwambia anisogeze mbele kwa kutumia njia za vumbi za Shoti kati, mbele ya pesa kila kitu kiliwezekana hadi nilifika Mbele zaidi, nikapanda gari ndogo ya abiria hadi Chalinze. Hapo nilikodi Pikipiki inifikishe Morogoro.
Nilifika Morogoro mishale ya saa 10 Jioni, nilitafuta gest ya vichochoroni nikala kisha nikalala zangu bila hata hofu kuwa ninatembea na mzigo mkubwa wa Madini. Hofu yangu ilikuwa kwa polisi pekee, nikiwa hapo nilipata kuona taarifa ya Habari kuwa Sarafina na Mkuu wa Magereza walikuwa wamekatwa baada ya Sarafina kumtaja Mkuu huyo, Sasa kupitia kamera za Kule Hotelini siku ya tukio la kuiba madini sura yangu ilionekana nikawa natafutwa Kila kona huku akina Sarafina wakiwa kwenye mikono ya Polisi, kilichotakiwa kilikuwa ni Madini ya yule Bilionea.
Nilizima TV ili nisiendelee kuangalia habari hiyo, Nililala hadi Asubuhi, Mapema sana nilianza safari ya kuelekea Tabora kwa kutumia Basi. Nilifika Tabora usiku sana, nilichukua pikipiki hadi nyumbani kwetu, Nilimgongeshea mlango Mama Rafia ambaye ndiye jirani yetu kule Tabora nikamwambia
“Nifungulie tafadhali Mama Rafia” Nilisema nikiwa bado nina hofu ya kukamatwa, Mama Rafia alifungua kisha aliniuliza
“Kulikoni Jojo? taarifa zako zimeenea kila kona, Tobra nzima, imekuwaje Mwanangu” Alisema Mama Rafia,,
“Mama laiti kama ningelijuwa nisingelienda Dar, Maisha yangu yameharibika baada ya kufika huko” Nilisema
“Ni kweli umeiba Madini Mwanangu?” aliniuliza, alikuwa ni jirani pia rafiki wa Marehemu Mama yangu, nisingeliweza kumficha. Nilimwambia ukweli na nilimuonesha madini
Tuliingia ndani kwake maana alikuwa akiishi peke yake kisha alinieleza
“Msonjo amekamatwa Jana Mchana, inasemekana kuwa yeye anahusika na anajuwa ulipo”
“Hapana Mama, Msonjo sijawasiliana naye kwa zaidi ya miezi yote niliyokuwa Dar, nimepata mitihani mikubwa sana Mama” Nilisema
“Sasa Jojo, haya Madini ni mali ya Watu hivyo muda wowote unaweza kukamatwa, kuliko ukamatwe kwa kosa dogo ni bora ukamatwe kwa kosa kubwa” Alisema Mama Rafia
“Unamaanisha nini Mama”
“Yafiche kiasi alafu mengine kaa nayo ili ukikamatwa uyaoneshe! utakapotoka huko utajuwa pa kuanzia” Alisema Mama Rafia, nilimuamini yeye hivyo nilimpa kiasi cha Madini kisha mengine niliondoka nayo usiku huo na kwenda nyumbani.
Asubuhi Mapema Mlango uligongwa, Sauti ya Mama Rafia niliisikia.
“Nakuja Mama” Nilisema, kisha nilivaa vizuri maana nilikuwa nimelala. Nilipofungua mlango nilikutana na Askari wakiwa wameongozana na Mama Rafia
“Huyu hapa!! kiukweli Askari Mimi sitaki Matatizo kabisa, huyu Binti anayo hayo madini yanayotafutwa” Alisema Mama Rafia, kiukweli nilipigwa na Butwaa
“Mamaaa”
“Siyo Mama, kiukweli Jojo sitaki matatizo na Mtu ndiyo maana nimewaambia polisi, ningekaa kimya ningekuja kukamatwa na Mimi” Wale Polisi waliingia ndani wakachukua mkoba wenye Madini, Chozi lilinibubujika sana.
“Basi Mama nipe yale madini niliyokupa ili tumrudishie mwenyewe” Nilisema huku chozi likinivuja
“Madini? kuna madini uliyonipa Mimi Jojo? ndiyo maana niliyakataa mapema haya nikaamuwa kusema kwa polisi” Masikini nililia sana Aisee, Mama Rafia alinikana mbele ya Wale askari. Nilikamatwa kisha nilirudishwa Dar
Nikiwa kituo cha polisi nilikutana na Sarafina na yule Mkuu wa Magereza pia nilikutanishwa na Biliona niliyemuibia Madini. Alihakiki madini akaona hayajatimia hivyo niliteswa sana ili niseme yalipo, nilimtaja Mama Rafia ila alinikataa mbele ya Askari, Tulipelekwa mahakamani kila mmoja na kosa lake, Mimi nilikuwa na kesi ya wizi wa Madini, Sarafina alihusika na kifo cha Shonaa pia kupanga njama ya wizi wa madini, Mkuu wa Magereza alikuwa na kesi nzito zilizoihusu magereza yake, kifo cha Shonaa na Njama za kuiba Madini.
Binafsi nilihukumiwa kwenda jela Miaka Mitamo, Sarafina alienda jela miaka 25, Mkuu wa Magereza alifungwa kifungo cha Maisha Jela sababu alikutwa na kesi nyingi za mauwaji.
Kila mmoja alipelekwa Gereza lake kutumikia adhabu. Nilimpoteza Mama yangu, Nilimpoteza Shonaa, Nilipoteza thamani yangu, pia nilimpoteza Mama Rafia kisa Madini. Siku moja nilitembelewa na Msonjo nikiwa gerezani aliniambia kuwa Mama Rafia amejenga jumba la kifahari, ana Biashara nyingi anafanya tena ameahama kabisa Tabora anaishi zake Dodoma.
“Msomjo Mimi Mungu amenisahau” Lilikuwa ndiyo neno langu la Mwisho kulisema, sikuhitaji kuonana na Mtu mwingine tena. Hadi sasa unaposoma hadithi hii Mimi ninatumikia adhabu mwaka wa 8.
MWISHO
Mwisho wa HADITHI Hii Ndio Mwanzo Wa HADITHI NYINGINE…. Kukiwa na COMMENTS Nyingi Mpya Inaanza Mapema Tu
Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost RIWAYA Mpya Hapa Kijiweni
Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM
SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI
JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa
Mungu Amenisahau xx Mungu Amenisahau xx Mungu Amenisahau xx Mungu Amenisahau xx Mungu Amenisahau xx Mungu Amenisahau xx Mungu Amenisahau xx Mungu Amenisahau xx Mungu Amenisahau xx Mungu Amenisahau xx Mungu Amenisahau xx Mungu Amenisahau xx Mungu Amenisahau xx Mungu Amenisahau xx Mungu Amenisahau xx
10 Comments
Jamani, tamthiliya nzuri, natamani ingeendelea
Duh jojo Hattari kweli kweli
🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥🔥
Mh ivi mnatunga tu au mnaiba maana hii ni mfano wa AI
Heeee
Hongera sana admin kwa kweli inasisimua sana😭hadi kusoma unaogoa😢
Mwisho wa riwaya hii ndio mwanzo mzuri🌹wa riwaya nyengine
Kila lenye kheir liwe kwako ni nzur san hii riwaya☑️💯
Nimelia saaana😭😭😭😭😭
Darasa la Saba
Kuna cha kujifunza hapa wanakijiwe
Asante sana ndugu admin 👏🏻👏🏻