Katika Dirisha kubwa la usajili lililopita winga Jesus Moloko alikua na hatihati kutemwa kikosini lakini kiwango chake mahiri alichokionyesha baada ya hapo akafanikiwa kubadili mawazo ya benchi la ufundi na sasa yuko mezani amekunja Nne anaupitia mkataba mpya.
Yanga iko katika hatua za mwisho kusaini mkataba mwingine na Moloko baada ya kuimarika kwa kiwango chake ndani ya msimu huu akiwa winga aliyekuwa katika uwezo wa juu.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba uongozi wa klabu hiyo baada ya tathimini ya kiwango chake umepokea ripoti ya benchi la ufundi, winga huyo Mkongomani anatakiwa kubaki na apewe mkataba mpya haraka.
Moloko raia wa Congo msimu huu hadi sasa ameshafunga mabao matatu, akiwa ana mawili kwenye ligi na moja kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambalo timu yake ipo hatua ya makundi.
Mwanaspoti linafahamu tayari uongozi wa mchezaji huyo unapitia mkataba kabla ya kusaini dili jipya.
“Tunamuongeza mkataba mpya, nadhani bila kificho ukiwatathimini mawinga wetu utaona mtu pekee aliyedumu kwa ubora hasa msimu huu ni Moloko,” alisema mmoja wa mabosi wa juu wa Yanga.
“Tumeshampa mkataba tunasubiri majibu yake na uongozi wake, nadhani amekuwa ndiye winga aliye katika kiwango bora katika mafanikio ambayo tunakwenda kuyapata msimu huu.
“Ukiacha suala la kiwango chake ripoti zinaonyesha pia hata nidhamu yake iko juu haya yote yanatusukuma kumpa kitu ambacho kitampa nguvu ya kuendelea kubaki hapa zaidi.”