Kikosi cha Medeama ya Ghana kinatarajiwa kuja nchini Jumapili Desemba 17 kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa raundi ya nne wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam utakaopigwa Jumatano Desemba 20, kuanzia saa 10:00 jioni.
Katika mchezo huo, mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya Ghana, itamkosa beki wao wa kati, Nurudeen Abdulai (24), kutokana na majeraha ya bega baada ya kuumia kwenye mchezo wa sare ya bao 1-1 dhidi ya Yanga, jijini Kumasi kwenye Uwanja wa Baba Yara.
Beki huyo amekuwa mhimili mkubwa akiisaidia timu hiyo kufuzu hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo na kukosekana kwake kunaweza kukaathiri safu yao ya beki, ingawa kocha wa timu hiyo, Evans Adotey licha ya kueleza kusikitishwa kwake na kumpoteza Abdulai kwenye mchezo huo, ana imani na uwezo wa timu yake kupata ushindi na ana wachezaji wazuri kama kipa Felix Kyei na mshambuliaji Jonathan Sowah.
Timu zote zinakwenda kukutana zikiwa zimepania kuibuka na ushindi, huku Medeama ikitaka kuendeleza kiwango chao cha kuvutia kwenye michuano hiyo hadi sasa na Yanga SC ikihitaji kupata ushindi nyumbani ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye kundi hilo D.
Endelea kusoma zaidi habari zetu kwa kugusa hapa.