Mwaka 2018 nikiwa nimetulia zangu napekua mambo Google kama ilivyo desturi yangu kufanya hivyo huku nikiwa nimeweka Earphone zangu masikioni kusikiliza redio ambapo kipindi cha michezo kulikuwa kinaanza kwa muda huo,mara namsikia kiongozi mmoja akilalamikia wachezaji na mashabiki wao.
Alikuwa ni kiongozi wa timu ya Coastal Union na katika kuongea kwake alizungumzia wachezaji kupambana mechi mbili tu na hata hata mashabiki nao kushindwa kuongozana na timu yao pale inaposafiri. Miongoni mwa nukuu zake ilikuwa ni.
“Tangu nimeteuliwa Kuwa Kiongozi wa Coastal Union huwa nachunga sana mdomo wangu kuongea katika hadhara kuhusu mechi za Coastal union na mapungufu ninayoyaona. Tayari nimechuja maneno yangu, na naomba kuongea kama mpenzi wa Coastal union sasa.”
“Tatizo walilonalo wachezaji wa Coastal union ni la kisaikolojia na tatizo hilo pia wanalo mashabiki wa Coastal union.”
“Wachezaji wa Coast wanafikiri wakizifunga Yanga au Simba wataondoka na points(alama) kumi katika mchezo mmoja,wanasahau wakiifunga African Lyon wanaondoka na alama tatu na wakiifunga Yanga wanaondoka na alama tatu vilevile.”
“Angalia mashabiki wa Coast nao hawakushughulika kusafiri kutoka Tanga kwenda Dar siku ya mechi ya African Lyon ikicheza na Coast badala yake walishugulikia mechi ya Yanga. Wakidhani tukiifunga Yanga tutakuwa tumebeba kombe.”
“Tujiulize ndani ya nafsi zetu tumekwenda kuishangilia Coast au kuangalia Yanga?. Majibu tunayo wenyewe.”
“Sasa naongea kama katibu mkuu. Ofisi yangu itakuwa mstari wa mbele kuhamasisha safari za mashabiki ikiwezekana hata kutafuta usafiri wa bure kwa zile mechi zote za mikoa ya jirani, Tukumbuke mechi zote za ligi kuu ni muhimu. Hivyo mashabiki na wachezaji wanapaswa kuziona kama fainali na kucheza kwa ari kubwa sio kusubiri mechi za Simba na Yanga tu.”
Mwisho alihitimisha kwa kusema. “Kutoa draw na African Lyon kumeniuma sana kuliko tulivyofungwa na Yanga. Sasa mashabiki twendeni Mabatini kwa wingi siku ya jumamosi tukachukue alama zetu tatu. Go Coastal Go …”
Yalikuwa ni maneno ya uchungu wa moyoni kabisa toka kwa kiongozi huyo,aliongea kwa masikitiko sana. Japo ukweli siku zote huwa unauma lakini yalikuwa ni maneno yenye somo kubwa sana ndani yake kwa wachezaji na mashabiki. Hapa niongezee hata viongozi nao wapo hivyo.
Wachezaji wengi wa Kitanzania wapo hivyo huyo kiongozi aliyefunguka hivyo wala hakukosea wachezaji wanapaswa kutambua kila mechi ni muhimu kwa maendeleo ya timu yao. Wanapaswa kujua endapo wataipa ubingwa timu ni sehemu ya CV kubwa kwao hata kwenda nje ya nchi itawezekana tu bila kupitia Simba Sc au Yanga Sc.
Kama wadau wa soka tumekuwa tukilaum sana viongozi juu ya vilabu hivi kukosa wadhamini ila kuna wakati tunajiuliza pia ni nani ataweka pesa yake kwenye klabu mbovu?. Hakuna ambae atafanya hivyo labda awe na mapenzi tu na timu hiyo kama alivyo Bin Silum na Coastal yake,au tu GSM alivyoingia Majimaji FC kwa kuwa ni mzaliwa wa huko.
Kama wadau wa soka tumekuwa tukijiuliza pia Mbao FC na baadhi ya timu kwa nini zilikua zinapigania kutoshuka wakati zikikutana na Simba Sc au Yanga Sc zenyewe ziliweza kuongoza kila kitu?.
Nafikiri wachezaji wanapaswa kujiongeza ipasavyo katika hili,watambue thamani iliyofanya wawepo kwenye hivi vilabu na kulipwa pesa wakati kuna wachezaji hata nafasi ya Daraja la kwanza hawapati.
Wao kama wachezaji wanapaswa kujua mashabiki wao watawafata popote waendapo wakifanya kazi ya kupendeza. Lakini hata mashabiki wanapaswa kutambua kuwa hakuna shabiki ambae atatoka Dar es Salaam kuvifata vilabu hivyo zaidi ya wao ndani ya mkoa,ikiwa wanaweza kukaa na kulalamika juu ya timu yao ya mkoa basi wajue hata wao ni chanzo cha timu kuyumba.
Ni nani haikumbuki Mbeya City ya msimu wa kwanza ilipopanda?,nani hakumbuki matawi yaliyozaliwa msimu ule wa Mbeya City ama nani hakumbuki mashabiki wa Mbeya City walivyojitahidi kusafiri na timu yao?. Kila mmoja anajua uwepo wa mashabiki pia unachangamsha akili za wachezaji na kuweza kuipa thamani timu.
Vyama vya soka mikoa vina dhamana kubwa sana ya kulinda soka la mkoa husika kwa kusaidia viongozi wa timu hizo,pia wale ambao huhangaikia timu kupanda wasitengwe baada ya mafanikio hawa ndio wana ushawishi mkubwa kwa mashabiki na wadau wengine. Ikiwa wanaweza kuchangisha watu Tsh 100/= wakiwa na mechi basi hawatashindwa kutoa hamasa huku pia.
Nihitimishe kwa kuwapa ushauri wa bure tu wachezaji wanatakiwa kujua kazi zao ndio malipo yao angalau sasa. Amkeni mliolala katika kiza angali umeme umefika vijijini.
SOMA ZAIDI: Hakuna Simba Na Yanga Bila Msingi Wa Uwepo Wao
1 Comment
Pingback: Heritier Makambo Kitabu Cha Simulizi Walichokataa Wazawa