Msimu huu wa AFCON 2023 utakaofanyika nchini Ivory Coast shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika CAF likiungana na kampuni ya vifaa vya michezo ya PUMA zimekuja na mpira utakaotumika kwa ajili ya michuano hii unaofahamika kama POKOU. Bila shaka kabisa wapo ambao wamekuja na maswali mengi zaidi wakijiuliza kuhusu jina ambalo mpira huu rasmi wa michuano hii umepewa na CAF wakishirikiana na PUMA.
Mpira huu umepewa jina la Laurent Pokou ambaye ni mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ivory Coast ambaye ana rekodi kubwa kabisa ya kushinda mabao 5 katika mchezo mmoja na hii ilikua katika ushindi wa mabao 6:1 wa Ivory Coast akimfunga Ethiopia katika michuano ya AFCON ya mwaka 1970.
Streka huyu wa zamani wa Ivory Coast alizaliwa tarehe 10 ya mwezi wa nane mwaka 1947 na kufariki tarehe 13 ya mwezi wa kumi na moja mwaka 2016 huku akitumikia klabu mbalimbali za nyumbani kwao Ivory Coast na za ligi kuu ya nchini Ufaransa.
Licha ya kuitwa jina la mchezaji huyo wa zamani lakini pia umerembwa na bendera za nchi ya Ivory Coast ambazo ni nyeupe , rangi ya machungwa na rangi ya kijani na ukiwa umetegenezwa kwa kutumia teknolojia bora zaidi kwa ajili ya michuano hii mikubwa barani Afrika ngazi ya timu za taifa.
Licha ya kwamba utaanza kutumika kuanzia tarehe 13 ya mwezi wa kwanza mwaka 2024 lakini pia utatumika na timu za taifa katika mazoezi yao ya kujiandaa na mechi ambazo watakua wanazikabili mbele yao ambapo utatumika katika majiji makubwa ya nchi hiyo kama Abidjan, Bouake, Korhogo, San Pedro na Yamoussoukro.
Anafahamika kama mchezaji mwenye historia kubwa zaidi katika soka la nchi ya Ivory Coast ambapo wakati akisakata kabumbu walimpa jina la utani la L’homme d’Asmara likimaanisha Mwanaume wa Asmara kutokana na uwez mkubwa aliokua nao katika kucheza mpira na kufunga mabao. Ukiachilia mbali mpira lakini pia pokou amepewa heshima ya moja ya uwanja wa utakaotumika kwa ajili ya AFCON msimu huu ukipewa jina lake unaopatikana katika jiji la San Pedro.
Endelea kufuatilia zaidi kuhusu taarifa mbalimbali kuhusu AFCON kwa kugusa hapa.