Rais wa Barcelona, Joan Laporta amemwambia meneja Xavi kwamba klabu lazima imuuze Ansu Fati, ili kurahisisha kurejea kwa Lionel Messi katika klabu hiyo.
Sio tu kwa uwezo wake uwanjani, Laporta anafikiria ujio wa Messi kama kichocheo cha mikataba ya udhamini isiyo na kifani.
Messi, ambaye amekataa kusaini mkataba mpya na PSG, ataondoka katika klabu hiyo ya mji mkuu wa Ufaransa kama mchezaji huru msimu wa joto.
Atapata kiasi cha Euro milioni 10 akirejea Camp Nou na huu bado ni mzigo wa kifedha kwa wababe hao wa Catalan ambao wanatatizika kufuata sheria za La Liga za Financial Fair Play.
Gazeti la El Nacional limeripoti kuwa suluhisho litakuwa ni jambo la kuhuzunisha sana kwa Ansu Fati, ambaye msimu wake umekumbwa na majeraha na kupotea kwa kasi jambo ambalo limemfanya ashushwe benchi.
Kwa kuondoka kwa kijana huyo, Barcelona itaokoa euro milioni 50 na hii itaimarisha hali yao ya kifedha kwa kiasi kikubwa.
Tottenham ni miongoni mwa vilabu vinavyomtaka mhitimu huyo wa La Masia, na wako tayari kukidhi matakwa ya kiuchumi ya klabu na mchezaji huyo.