Matumaini ya Lionel Messi kurejea Barcelona kuendelea na maisha yake ya soka yamepata pigo kubwa.
Hii ilikuwa baada ya wachezaji wawili wa klabu hiyo kukataa kupunguza mishahara yao.
Express Sport inaripoti kwamba Franck Kessie na Andreas Christensen walifikiwa na Blaugrana kupunguza mishahara yao ili kumudu fowadi huyo mkongwe.
Kulingana na ripoti hiyo, wachezaji wote wawili waliojiunga na wababe hao wa Catalan kutoka AC Milan na Chelsea, mtawalia msimu uliopita wa joto, walikataa.
Klabu hiyo sasa inakabiliwa na kibarua kikubwa ikiwa itabidi kumrejesha fowadi huyo wa Paris Saint-Germain katika klabu hiyo kutokana na matatizo yao ya kifedha yanayoendelea.
Nyota huyo wa Argentina aliwaacha wababe hao wa Catalan na kuhamia Parc des Princes msimu wa joto wa 2021 baada ya mkataba wake kumalizika Camp Nou, huku klabu hiyo ikikumbwa na msukosuko wa kifedha.
Mshindi huyo wa Kombe la Dunia anaonekana kukaribia kuondoka tena PSG mkataba wake utakapomalizika msimu huu wa joto baada ya kukataa ofa ya kuongeza mkataba wake.