Kocha Mkuu wa Timu ya Young Africans S.C (Yanga), Almaarufu kama Professa, Nasreddine Nabi amefunga Safari Kuelekea Ubelgiji katika mapumziko haya ya Siku chache Kupisha Mechi za Kimataifa huku akitoa salamu za Kuwakereketa alizozielekeza jijini Lubumbashi, DR Congo huku akiweka hesabu zake sawa katika kuelekea mchezo wa mwisho wa makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika akidai kuondoka na Ushindi kwa Namna yoyote.
Kocha huyo aliyeiwezesha Yanga kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ikiwa ni kwa mara ya kwanza katika ushiriki wa timu hiyo huku ikiongoza msimamo wa Kundi D, itaifuata TP Mazembe katika mechi ya mwisho ya kundi hilo itakayopigwa Aprili 2 jijini Lubumbashi.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Jijini Dar es Salaam Februari 19, Yanga ilipata ushindi mzito wa mabao 3-1 na mchezo ujao utakuwa ni kama wa kisasi kwa Wakongo wa lubumbashi lakini tayari Kocha Nabi amesema ana mipango madhubuti kuwakabili Wakongo hao kabla ya mchezo wa marudiano.
Nabi aliweka wazi kuwa Yanga ina malengo makubwa zaidi baada ya kufuzu hatua ya Robo Fainali na sasa wanalenga kuongoza kundi hilo lenye timu za Us Monastir ya Tunisia, Real Bamako ya Mali na mabingwa hao wa zamani wa Afrika, TP Mazembe.
Mpaka sasa, Mazembe ndio inayoburuza mkia katika kundi hilo ikiwa na pointi tatu tu, huku Yanga ikiwa kileleni na alama 10 sawa na Monastir iliyopo nafasi ya pili ambayo itamaliza mechi yake na Bamako na kama Yanga itashinda ugenini, itaongoza kundi kutegemeana na matokeo ya US Monastir Nchini Tunisia.
Yanga ina malengo ya kushinda mchezo huo na kuweka rekodi ya kushinda ugenini, lakini kubwa ni kukwepa kuangukia kwa timu ngumu endapo itamaliza wa pili kwenye kundi hilo iwapo kama itashindwa kutoka na matokeo mazuri ugenini mbele ya Mazembe.
Kocha Nabi aliongeza na kusema kuwa haitakuwa rahisi lakini yeye sio kocha rahisi wa kukata tamaa, anapenda kuishi kwa malengo na anadhani kitu bora ni kujipanga na kucheza kwa hesabu sahihi.
Wakati Nabi akiweka mipango yake hiyo, huku kwingine uongozi wa timu umeamsha hamasa zaidi ikiwa imepanga kuwasafirisha mashabiki wao tayari kwa mchezo huo. Yanga imetoa basi ambapo mashabiki wanaotaka kusafiri nalo watapaswa kuchangamkia fursa huku nauli ikiwa ni Sh700,000 kwa kila mtu kwenda na kurudi.
“Fedha hizi ni nauli ya kwenda na kurudi, vibali kama viza, kadi za manjano na vipimo vya Uviko-19 na kwa siku tatu na kiingilio kitakuwa ni bure,” alisema ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe.