Kikosi cha Yanga SC leo Juni Mosi kimeondoka nchini kwenda Algeria kwa ajili ya kucheza mchezo wa marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya USM Alger.
Yanga katika mchezo wa kwanza ilifungwa mabao 2-1 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Umeshuhudiwa msafara wa wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wanaosafiri na timu hiyo wakiwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere wakiwa hawana presha yoyote wakienda kwenye mechi inayohitaji ushindi wa mabao 2 na kuendelea.
Msafara wa Yanga upo na viongozi mbalimbali kwa ajili ya kwenda kuongeza hamasa katika mechi hiyo ya marudiano.
Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF), Wallace Karia amesema anaenda kwenye mchezo huo huku akiamini kabisa wanarudi na ubingwa.
“Hili kwa sasa sio jambo la Yanga bali ni kitaifa, kwahiyo tupo pamoja kuhakikisha tunachukua ubingwa na nimewasikia wachezaji wakiwa wanazungumza wanahitaji ushindi,” amesema Karia.
Upande wa Mwenyekiti wa kamati ya Mashindano Yanga, Rogers Gumbo amesema wao kamati wamehakikisha kila kitu kipo sawa kwa upande wao.
“Tumehakikisha kwa upande wetu kila kitu kipo sawa na Ndio maana wote tunasafiri hapa kwenda Algeria, imani yetu ni ushindi,” amesema Gumbo.
Mchezo wa pili itacheza Juni 3 nchini saa 4 usiku kwa saa za Tanzania.