Ilipoishia “Aaaah Zola” ilisikika sauti upande wa Mzee Dawson, ikionesha alikuwa akijigeuza.
“Hebu fanya taratibu tuonane ana kwa ana Mzee Dawson, nahisi kuchanganikiwa sasa” Zola alikata simu bila kusikiliza sauti ya Mzee Dawson, baada ya hapo akapiga simu sehemu nyingine ndani ya kitengo cha siri cha Mzee Dawson kinachoitwa MPA, akaomba madaktari waweze kufika eneo la tukio, akawapa Ramani kamili lilipo eneo hilo. Endelea
SEHEMU YA NNE
Hakuwa na muda wa kukaa pale, akatoka taratibu hadi nje, akayaangalia vizuri mazingira yale kwa jicho na akili ya kipelelezi akajua tu kifo kile kimetokea masaa machache yaliyopita na kwa vyovyote mwenye chumba kilichokuwa kinaangaliana na mlango lilikofanyika tukio atakuwa labda amesikia au kuona chochote kile, akakumbuka kuwa mlango huo ulifungwa na funguo kuondolewa, akajiuliza haraka akiwa analitazama dirisha la Chumba jirani
“Kama funguo imetolewa maana yake kuna Mtu amefunga mlango na kumfungia Mtu ndani, Nani amefanya hivi?” Akapata akili ya kusogea chumba cha jirani, alipogonga akatoka yule Msichana ambaye alimuelekeza chumbani kwa Anastanzia, yule Mdada alipomuona Zola akaanza kujishebedua kwa kuhisi kuwa Zola alikuwa akimtaka, alionekana kuvutiwa na Mzee Zola kutokana na muonekana wa kitajiri alionao bila kujuwa kuwa alikuwa amesimama mbele ya Mtu hatari kwa upelelezi
“Nilijua tu utakuja kwangu, Anastanzia sio aina ya Mwanamke ambaye anakufaa wewe. Wazee kama nyie mnatakiwa kupetiwa vizuri ili msiwe na mawazo ya kufa kufa” Alisema huku akitabasamu mbele ya Zola, kisha Zola akamuuliza yule msichana
“Mara ya mwisho umemuona Anastanzia lini?” Mdada akaacha kujishebedua baada ya Zola kuonesha sura ya mbuzi
“Wiki sasa sijamuona ila rafiki yake si umeonana nae? Maana nimekuona ukitoka humo ndani” Zola akatoa kitambulisho cha uaskari akamuonesha yule mdada kisha akamuuliza
“Unaitwa nani?” Mdada akawa anatetemeka
“Naitwa Scolastica”
“Rafiki yake Anastanzia amekufa, naomba uniambie ni nani umemuona akiingia au kutoka mle ndani kabla yangu Mimi”
“Kulikuwa na Mkaka mmoja hivi, aliingia kisha akafunga mlango akatoka, sikumuona tena”
“Anafananaje?”
“Mrefu kiasi, mweusi ana rasta”
“Sikia, watakuja polisi kuchukua mwili wa Marehemu, asante kwa ushirikiano wako” Zola akaingia kwenye gari yake akatokomea eneo hilo, akawasiliana na Mzee Dawson ili wapate kukutana na kuzungumza, Mzee Dawson kama kawaida yake akamueleza Zola wakutane sehemu ya siri.
Alipofika Zola, Mzee Dawson aligundua ni jinsi gani Zola alikuwa katika nyakati ngumu ambayo hakupata kumuona nayo, akamimina mvinyo kwenye glasi na kumpatia, akapiga funda moja la mvinyo ukawa umeisha kwenye Glasi, kisha akaitua Glasi hiyo mezani kama Mtu aliyechoshwa na kinachoendelea.
“Dawson! Hili jambo ni zito sana, kulifahamu lilipo kundi la Mafia Gang, na kuwajua Watu hao inakuwa kazi ngumu sana. Sijui ni mafunzo ya namna gani watu hao wanapatiwa kabla ya kutekeleza jambo fulani” Alisema Zola huku akakunja midomo yake, akampa Glasi Mzee Dawson ili amuongeze mvinyo, ukamiminwa mvinyo kwenye Glasi ya Zola haraka kisha Dawson akakaa vizuri ili amjibu Zola, kwanza akajikoholesha kisha akasema
“Mauwaji yaliyofanywa na Mafia Gang huko Congo yanatisha sana, hapa bado kabisa hawajavuruga kisawasawa! John Brain kama lilivyo jina lake ni Mzungu hatari sana Zola, nahisi yupo hapa Nchini na kuna mpango wanautekeleza, umejaribu kufuatilia ni mafaili gani yaliibiwa na huyo Msichana katika kituo cha polisi” Zola alitikisa kichwa kuashiria hakufuatilia suala hilo, Dawson akapiga tena fundo la Mvinyo kisha akabeua kidogo
“Zola ninayemjua Mimi hawezi kukosa kujuwa mambo kama hayo, akili yako haipo kabisa Zola, John Brain ana akili sana na anachezea ubongo wako! Huenda ameshakujua na kukufuatilia, anachofanya ni kukuchezesha, hapa kuna mambo mawili huenda yanafanyika kwa wakati mmoja”
“Mambo gani hayo?”
“Wananunua Muda wako na muda wa Wapelelezi wengine ili watekeleze mipango yao, hata haya mauwaji yanayotokea huwenda wanakuhadaa ili usipate muda wa kutuliza akili yako, wanajuwa wewe ni hatari kiasi gani, hilo lipo wazi Zola”
“Hili suala linaninyima usingizi Dawson, nahisi nipo katika chumba chenye giza ambacho siwezi kuona kuna nini ndani yake hata kusikia sauti inayonipa ishara, nahisi kushindwa”
“Ha!ha!ha! Zola, huwezi kukata tamaa mapema hivi, umekula kiapo cha kulinda Taifa hili ikiwemo kupambana na Watu aina ya John Brain, nafikiri muda unaenda, umekuja na gari yako?”
“Ndio”
“Tuitumie sasa hivi”
“Tunaenda wapi?” Aliuliza Zola huku akimtazama kwa makini Mzee Dawson ambaye tayali alionekana kuwa ameshaanza kulewa lakini alimjuwa sawa sawa jinsi alivyo, akilewa huwa anaamuwa mambo kwa kutumia akili sana.
“Tunaenda Hospitali kuruhusu ile Maiti moja iliyosalia kwenda kuzikwa”
“Tutawapa vipi Maiti ambayo si yao, kumbuka ile ni Maiti ya Anastanzia na sio Sandra”
“Tunairudisha sura ya Bandia kama ilivyo Mwanzo, huu sio wakati wa wao kujuwa ukweli, acha waamini wanamzika Mtu wao” Waliitumia gari ya Zola hadi walipofika Hospitali, tayari maiti mbili zilikuwa zimeruhusiwa kwenda kwa wahusika ambazo ni Maiti ya Bosco na Robert.
Wakasimamia zoezi la kuveshwa sura kwa Mwili wa Anastanzia, dakika chache muonekano ulibadirika,
“Yes! Acha wamzike wanayemuamini huku sisi tukiwa bize kufuatilia” Alisema Dawson kisha alikohoa kama kawaida yake, Zola akampa kitambaa akawema mdomoni lakini alipokitoa ilionekana damu katika kitambaa hicho cheupe kuashiria kuwa mapafu ya Mzee Dawson yalikuwa katika hali mbaya
“Usijali” akasema Dawson, kisha Zola akapiga simu kwenye familia ya Mama Sandra ili waende kuuchukuwa mwili walioamini ni wa Sandra ili wakauzike.
“Naingia kazini sasa Zola, tuna muda mchache sana kuhakikisha Nchi inakuwa shwari” alisema Dawson na kumfanya Zola atabasamu maana mzigo ulikuwa ukimuelemea sana. Siku iliyofuata Mazishi ya Sandra yalifanyika, Zola alikuwa miongoni mwa waliohudhuria lakini uwepo wa Zola msibani ulikuwa na melengo makuu mawili, moja kuhakikisha familia haitambui kama anayezikwa si Sandra, jambo la pili aliamini kama Mpango ule ulisukwa basi wasukaji wangefika pale Msibani kwa ajili ya kufuatilia, lakini Pia Zola alimtilia shaka Baba yake Sandra akiamini anajuwa jambo fulani.
Akiwa ameketi alivalia miwani nyeusi na sura ya Bandia kama alivyoambiwa na Mzee Dawson kuwa Huenda Mafia Gang wameshamjuwa ndio maana walitaka kumuuwa katika jaribio la bomu, hakutambuliwa na yeyote pale lakini alionekana kuwa miongoni mwa waliokuja Msibani, Watu walikuwa wengi mno. Kifo kile kilishika mioyo ya wengi.
Naam!! Zola alikuwa bize sana kuhakikisha anazungusha macho yake kila kona, macho yake yakajikuta yametua kwa jamaa mmoja ambaye naye alikuwa bize sana kuzungusha macho yake, Zola hakufanikiwa kugundulika baada ya kubadilisha sura kisha kuvaa miwani, ingehitaji utaalam mkubwa sana kumtambua. Kilikuwa ni kipindi ambacho Msemaji wa Familia alikuwa akiwashukuru Watu waliokuja pale kwa ajili ya maziko ya Sandra ambaye alizikwa pale pale nyumbani kwao, Zola hapo ndipo akajithibitishia kuwa familia ya Sandra haikusanuka kuwa walikuwa wakizika Maiti ya Mtu mwingine, lakini hakusita kukubali uwezo wa Maadui zao ambao walifanikiwa kuuhadaa ulimwengu wa vipofu ambao macho yao hayakuweza kuona mbali zaidi ya Jicho la kipelelezi lenye mafunzo ya kijeshi ambalo Zola alikuwa nalo.
Kwa mantiki hiyo, Maadui walifanya tafiti zao kabla ya kumtumia Anastanzia kuvaa sura ya Sandra maana miili yao ilifanana sana ndio maana hawakuweza kuhisi kama kuna tatizo, akashusha pumzi zake, alijuwa ilitumika akili kubwa sana pale hadi Anastanzia akaingizwa kwenye mwanvuli ule wa Umauti, swali lililomjia akilini mwake haraka ni wapi alipo Sandra mwenyewe?. Aliporejesha macho eneo la yule jamaa aliyekuwa akimfuatilia, aliona kiti kikiwa kitupu kabisa, akaangaza huku na kule bila mafanikio yoyote ndipo akaona ni bora atoke nje ili apeleleze yule jamaa ni nani na kwanini alikuwa akichezesha yale macho ya kipelelezi, akamkubuka sawasawa jamaa huyo mwenye upara na ndevu nyingi.
Alinyanyuka kutoka kitini kama Mtu aliyemaliza tukio la mazishi, hakutaka kuonesha dalili zozote kuwa alikuwa akifuatilia chochote maana aliamini Maadui walikuwepo pale Msibani, akiwa anatoka aligongana na Mwanamke mmoja mrefu, mweupe na mwenye nywele nyingi.
“Samahani?” Alisema Mwanamke huyo ambaye alikuwa na uzuri wa kutosha, macho ya Zola yakautalii mwili wa Mwanamke huyo bila stara
“Usijali!” Akasema Zola kisha akatoka pale taratibu bila kugeuka nyuma.
Yule Mwanamke alimtazama sana Zola hadi alipozama, kisha akaketi kitini. Zola alipofika nje alimuona yule jamaa akizungumza na simu kisha akaingia kwenye gari, Zola hakuchelewa naye akaingia kwenye gari na kuanza kumfuatilia jamaa huyo ambaye alionekana kutokuwa na wasiwasi wowote ule maana hata alivyoendesha gari hilo ilionesha wazi kuwa alikuwa katika hali ya kawaida, akaingia Barabara ya tano kisha akashika barabara kuu ambayo ilikuwa ikitoka Uwanja wa ndege kuelekea eneo ambalo lilikuwa na Hoteli nyingi za nyota tano.
Bila kupoteza muda Zola alimpigia Dawson simu, akamueleza hali ilivyo kisha akasubiria jibu la Mzee huyo.
“Washa GPS ya Gari” ilisikika sauti kutoka upande wa pili, ikampa ishara Zola kuwa Mzee Dawson alikuwa na maelekezo maalum ya nini cha kufanya.
“Nakuona!” Alisema Dawson kisha alikata simu mara moja, baada ya dakika tano akampigia tena na kumwambia
“Fuata maelekezo yangu, kuwa makini hao Watu wana akili ya ziada sana wakati mwingine Watu hawaamini kama Huyo Mzungu ni Binadamu, wana akili iliyozidi…unaweza kuwa umetegwa, kabla ya kutoka Msibani hakuna ishara tata?” Alimpa wakati wa kufikria, Zola akasema
“Nilikuwa makini kuliko kawaida, hakuna aliyeniona ila wakati natoka…” Ukimya ukatawala, Mzee Dawson akamuuliza Zola
“Enhee ilikuwaje?” Zola akafikiria alipokuwa akitoka pale aliparamiana na Mwanamke mmoja mzuri sana, hakutaka kulisema hilo akiamini sio ishara ya kumueleza Mzee Dawson
“Sio ishara!”
Nini Kitaendelea? USIKOSE SEHEMU YA TANO USISAHAU PIA Kununua Kitabu Cha KOTI JEUSI Kupiga Namba+255760871896 Ufikishiwe Mpaka Ulipo
SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI
JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa
Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx Jasusi xx
7 Comments
Ukalii umepamba moto
Jasusi anajasusiwa. Noma sana
Aiseeeee hatar
✌️✌️
Thank a lot, kazi nzuri
Iko poa xnaaa
Zola!¡!!