Wakati wenzetu wakiendelea kukua katika soka haswa kimataifa , Ligi Kuu ya Tanzania imekua ikiendelea kuwa na matukio ya hovyo ambayo yamekua yakionesha namna gani timu zetu hazijiamini katika kusaka mafanikio na kuwekeza katika ujinga usiokua na tija.
Wakati mwingine unaweza kusema kuwa Bodi ya Ligi Kuu wamekua wakijipatia fedha sana kutokana na kutoza faini kwa klabu kadhaa na kubwa ni kuhusiana na Imani za kishirikina ambazo zimekua zikioneshwa waziwazi na nyingine kwa kujificha kwa baadhi ya vilabu ambavyo vinashiriki katika ligi kuu na madaraja mengine ya ligi.
Ushirikina au imani potofu zimekuwa sehemu ya historia na utamaduni wa jamii mbalimbali duniani, na Tanzania siyo tofauti. Katika muktadha wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara, kumekuwa na taarifa na matukio ambayo yanaweza kuhusishwa na imani za kishirikina na hii inaweza kuwa na athari kubwa kwa maendeleo ya soka nchini na hata kimataifa.
Kwa ujumla imani za kishirikina zinaweza kusababisha kupotoshwa kwa ushindani wa kisoka kwani timu zinaweza kuathiriwa na imani potofu kuhusu nguvu za kishirikina zinazoweza kuleta mafanikio badala ya kuweka msisitizo katika mafunzo bora, vipaji, na ufanisi wa timu.
Lakini pia mchezaji mwenye kipaji anayeamini kwamba mafanikio yanaweza kupatikana kwa njia za kishirikina anaweza kusahau umuhimu wa kujituma, kujifunza, na kufanya kazi kwa bidii. Hii inaweza kusababisha kupotea kwa vipaji vya wachezaji wenye uwezo mkubwa.
Tuseme tu ukweli,matukio ya ushirikina yanaweza kudhoofisha sifa ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara mbele ya jumuiya ya kimataifa. Wachezaji na makocha kutoka mataifa mengine wanaweza kuepuka kushiriki katika ligi ambayo inajulikana kwa matatizo ya kishirikina na mwisho wa siku kupoteza ramani ya soka la Tanzania kwa upande wa kimataifa.
Nadhani kwa maendeleo ya soka la Tanzania kufikia viwango vya kimataifa, ni muhimu kuondokana na imani za kishirikina zinazoweza kudhoofisha misingi ya maendeleo ya mchezo huu unaopendwa na watu wengi sana Tanzania. Kuna haja ya kuwekeza katika miundombinu bora, mafunzo ya kitaalamu, na kuhamasisha wachezaji kujituma ili kuleta mabadiliko yanayotakiwa katika soka la Tanzania.
SOMA ZAIDI: Simba Na Yanga Wapo Katika Kesi Kubwa Ya Dunia Sasa
1 Comment
Pingback: Guede Amebeba Mzigo Mgumu Usioonekana Kikawaida - Kijiweni