Kutokana na majeraha ya nyonga yaliyomuweka nje kwa kipindi cha miezi miwili, winga machachari wa Yanga, Mghana Bernard Morrison sasa yupo tayari kuitumikia klabu yake ya Young Africans.
Morrison aliyerejea Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Simba hajaonyesha kwa ukubwa ubora wake wa awali kutokana na majeraha ya mara kwa mara akiwa ameichezea Yanga mechi 10 tu kati ya 24 za ligi ilizocheza hadi sasa na kufunga mabao mawili na asisti tatu, huku kwenye michuano ya kimataifa ambayo ndio lengo kuu la mabosi wa Yanga kumrejesha Jangwani, amecheza mbili tu na sasa benchi la ufundi la Yanga linaamini ni muda wake wa kuisaidia timu.
Mtaalamu wa viungo na misuli wa Yanga, Mtunisia Youssef Ammar, amesema Morrison baada ya kupona majeraha alipewa programu maalumu ya mazoezi ambayo aliifanya vyema na sasa yupo tayari kutumika kwenye mechi.
Youssef alisema kwa namna Morrison alivyofanya mazoezi ya pekee yake na yale ya pamoja na timu tangu ametoka majeruhi inaonyesha yuko tayari kwa mechi na sasa kilichobaki ni kocha Nabi kuamua kuanza kumtumia kwenye mechi zijazo.
“Morrison yuko tayari kucheza hata leo, kwani amepona na sasa maamuzi yamebaki kwa kocha mkuu kumtumia tu hata akitaka mechi ya wikiendi yupo fiti,” alisema Youssef.
Kwa upande wa Nabi, alisema Morrison ametoka kwenye majeraha hivyo alihitaji muda mwingi wa kujiweka sawa ila sasa anaweza kumtumia.
“Mwanzo sikumtumia kwa kuwa alikuwa na programu maalumu ya kujiweka sawa baada ya majeraha, pia kuna watu walikuwa wameingia kwenye mfumo na ukizingatia tulikuwa tunatafuta kufuzu robo fainali, ila kwa sasa anaweza kuanza kucheza na mtamuona.” alisema Nabi.
Sambamba na Morrison, wachezaji wengine wa Yanga waliokuwa majeruhi, Chrispin Ngushi na Denis Nkane sasa wamepona na wapo tayari kwa mchezo huku kipa Aboutwalib Mshery akiendelea kuuguza jeraha lake la goti.
Yanga imeondoka nchini leo Machi 30, kwenda Lubumbashi kukamilisha ratiba ya kundi D kwenye kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe kwani tayari imefuzu robo fainali ikiungana na Monastir ya Tunisia kutoka kundi hilo huku Mazembe na Horoya zikiwa zimeaga mashindano.