Kiungo wa kati wa timu ya taifa ya Nigeria, Alex Iwobi amewaahidi mashabiki wa Super Eagles kuwa kikosi hicho, kitarejea katika ubora wake, licha ya kufungwa bao 1-0 na Guinea Bissau siku chache baada ya kumalizika kwa mchezo huo katika mchuano wa kufuzu kucheza fainali ya Afrika mwaka ujao nchini Cote D’ voire.
Iwobi ambaye anaichezea klabu ya Everton nchini Uingereza, amesema wachezaji wenzake wamekubali aibu na sasa wanaangazia michuano inayofuata.
“Sisi kama timu ni lazima tuzinduke na kile ambacho tutafanya ni kujiboresha. Kwa mashabiki nitawaomba wasife moyo waendelee kutushangilia kwa sababu tunajitolea kwa hali na mali si kwa ajili yetu binafsi bali kwa taifa kwa ujumla,” amesema Iwobi.
Kufuatia ushindi wa Guinea Bissau sasa inashikilia uongozi wa kundi A kwa alama saba, Nigeria ni ya pili kwa alama sita, Sierra Leone ya tatu kwa alama mbili na Sao Tome Principe ni ya mwisho wakiwa na alama moja.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wanasoka waliobobea walifanikiwa kufungia timu zao za taifa akiwemo Sadio Mane, Mohammed Salah na Sebastian Haller.
Sadio Mane ambaye alirejea kwenye kikosi cha Senegal baada ya kukosa kombe la dunia kufuatia jeraha, alifunga bao la pili katika ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Mozambique jijini Dakar.
Mo Salah alifunga bao la kwanza na kusaidia kupatikana kwa bao la pili katika ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Malawi jijini Cairo na kusonga kutoka nafasi ya mwisho hadi ya kwanza kwenye kundi D.
Haller ambaye alirejea uwanjani mwezi uliopita baada ya kupata matibabu ya saratani ya tezi dume, alifunga bao la pili la Ivory Coast katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Comoros mjini Bouake.