Msimu wa kujipima kwa timu ya Manchester United ulianza vibaya baada ya kupata kichapo cha mabao 3-2 dhidi ya Borussia Dortmund katika mchezo wa kirafiki uliochezwa siku ya Jumatatu.
Mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi hicho, Harry Maguire, alilalamikiwa vikali na mlinda lango wao mpya, Andre Onana, baada ya kutoa pasi mbaya iliyowawezesha wachezaji wa Dortmund kufika kwenye lango lao.
Dakika ya 47 ya mchezo huo, Onana alitoa maonyo makali kwa beki huyo kutokana na kosa lake la kutoa pasi ya hatari na kuiruhusu safu ya ushambuliaji ya Dortmund kusonga mbele.
Onana alifaulu kuokoa shuti la Sebastien Haller, lakini Karim Adeyemi alishindwa kutumia nafasi ya kufunga kwenye kona.
Baada ya mpira kutoka nje ya uwanja, mlinda lango huyo wa zamani wa Inter Milan alikimbia hadi kwa Maguire na kumkemea kwa kosa hilo.
Akizungumza baada ya mchezo, Onana alisema ana uhusiano mzuri na Maguire lakini akasisitiza kuwa lazima awe makini wakati wote anapokuwa na mpira.
“Namshawishi kufanya vizuri kwa sababu najua yeye ni mchezaji mzuri,” Onana alisema katika mahojiano na MUTV.
“Yeye ni nahodha wa timu. Yeye ni mchezaji mkubwa na mzuri na mpira, hivyo nitamshawishi kufanya vizuri. Yeye ni mtu mzuri, tuna uhusiano mzuri.”
“Anapaswa kuwa tayari kwa sababu ninapokuwa na mpira, nahitaji wachezaji wenzangu wawe tayari.
Tunapaswa kuwa tayari kwa sababu sisi ni timu moja na tunajifunza kutokana na makosa.”
Onana aliongezea, “Tunapaswa kuwa wakali na kujitathmini wenyewe.
“Ili kushinda mataji, tunapaswa kutaka mafanikio. ”
“Ni heshima kubwa kuwa hapa na ninafurahi kufanya kazi na wachezaji hawa. Harry ni mchezaji mzuri sana, hivyo tutasonga mbele.”
Inasemekana kuwa United inataka pauni milioni 40 kwa Maguire jambo ambalo limeleta changamoto kwa vilabu vinavyotaka kumsajili.
Hivi karibuni, West Ham ilifanya zabuni ya pauni milioni 20 ambayo ilikataliwa na haijatarajiwi kufanya zabuni nyingine kutokana na tofauti kubwa ya thamani kati ya vilabu hivyo viwili.
Soma zaidi: habari zetu kama hizi hapa