Ilipoishia “Fanya haraka” Akaelekezwa mahali ambapo angemwona Matilda, japo dakika mbili zisingetoshea kuzungumza naye ila alihitaji kumwona na kupata uhakika kua ana Mtoto na Bosi wake, akapelekwa chumba kimoja ambacho kilikua rasmi kwa ajili ya kuonana na Mahabusu, akasubiria hapo Matilda aletwe, sekunde chache Matilda akafika hapo akiwa ameongozana na yule Polisi
Hakumkumbuka Jack sababu alimwona kwa Mara ya kwanza pale ofisini kwa James hivyo ilikua rahisi kwake kukubali kuonana na Jack, akaketi huku akiwa anamtazama sana Jack
“Samahani na pole Matilda, Naitwa Jack” Alijitambulisha Jack
“Unanifahamu Mimi?” akauliza Matilda akionekana alikua ameteswa sana, uso ulikua na majeraha kadhaa
“Ndiyo nakufahamu japo si sana” Endelea
SEHEMU YA SITA
“Mbona Mimi sikufahamu?” akauliza Matilda
“Mimi ni mfanyakazi wa James, nimekuja nahitaji kujua baadhi ya vitu kutoka kwako” Akasema Jack
“Kwahiyo James amekutuma uje kwangu unilaghai kwa kutegemea kua nitakubali si ndiyo, sikia nikwambie kitu kimoja, Nimeamua kuishi Maisha ambayo sitaki kuitwa Msaliti na Mtoto wangu, nitasimama naye hadi mwisho na kama unafikiria utaweza basi nakwambia katu hautoweza kunishawishi kwa chochote kile, nenda kamwambie James, kama Mtoto wangu atakufa basi atabeba msalaba na kamwe sitakubali” Alisema kwa hasira sana Matilda hadi yule polisi akaona ni bora amrejeshe Mahabusu maana kusingezungumzika kabisa
“Sina nia hiyo Matilda nakuomba unisikilize” akazungumza lakini Matilda aliondolewa hapo, kisha baadaye yule polisi akamfuata Jack
“Usirudi tena, hii ilikua nafasi pekee”
“Lakini sikua na nia ya kumkasirisha kabisa, nilihitaji kumsaidia” Akasema Jack
“Hayo hayanihusu Mimi, nimetenda wema niliopaswa kukutendea, utamsaidiaje ni juu yako” Akasema Polisi huku akimtaka Jack aondoke Kiunyonge sana tofauti na alivyoingia kituoni, Jack alionekana akishusha ngazi kwa kutumia kiatu chake kirefu, Macho yake yakatua waliposimama Mchungaji na Mama Naomi, Mara moja wakasogea karibu kumpokea
“Vipi umefanikiwa kumwona?” akauliza Mchungaji
“Anaendeleaje?” akauliza Mama Naomi huku nyuso zao zikionesha shahuku kubwa ya kutaka kujua kilichotokea huko ndani
“Hataki kuzungumza na Mimi, inaonesha ana maumivu makali sana” Akasema Jack akiwa anasogea karibu na gari yake, Mchungaji na Mama Naomi wakiwa wanamfuata
“Yupo salama?” akauliza Mchungaji, Jack akatikisa kichwa kama ishara ya kua Matilda hayupo salama.
“Niambie Matilda amekuaje?” alihoji Mchungaji, yeye ndiye aliyempokea Matilda kanisani kwa mara ya kwanza. hivyo Matilda kwake ni sawa na Mtoto wa kumzaa.
“Siwezi kuzungumza nahitaji kutuliza akili kuona ninamsaidia vipi, Tutawasiliana” akasema Jack kisha akaingia kwenye gari yake na kuondoka hapo haraka sana, akawaacha Mchungaji na Mama Naomi wakiwa hawajui kilichoendelea kati ya Jack na Matilda.
“Ni bora angeeleza kiilichotokea kuliko kukaa kimya, hapana shaka amemwona Matilda, roho inaniuma sana” Alisema Mama Naomi akionekana kujawa na uchungu, chozi lilimlenga, alikua hajatulia tokea asubuhi kwa ajili ya Matilda
“Naomba urudi nyumbani giza linaanza kuingia, pesa hii itakusaidia. Mimi narudi kanisani kwa ajili ya maombi….Najua shetani yupo mahali anafanya kazi yake” Akasema Mchungaji kisha akampatia noti ya Elfu Kumi Mama Naomi
“Lakini Mchungaji natamani nilale hapa ili nijue Matilda anapitia wakati gani, naona kama tunamzika Matilda bila kusikia kilio chake” Akasema Mama Naomi akiwa ameshika noti mkononi huku chozi likianza kuvuja
“Usilie..Hakuna marefu yasiyo na Ncha, kua na imani kua Mungu atatenda na Matilda atatoka”
“Sawa Mchungaji” Alisema Mama Naomi, akaita Bajaji kwa ajili ya kurejea anapoishi maana kwa muda huo ingekua shughuli pevu kupata daladala, kwa wanaoishi Dar wanajua liingiapo giza vurugu za kugombania usafiri zinavyochukua sura tofauti.
Mchungaji alisubiria hadi Mama Naomi alipoondoka ndipo naye akaondoka kituoni.
********
Mawazo chungu mzima yalikua yakipita kwenye kichwa cha Bilionea James, alikunywa pombe ili kuondoa mawazo yaliyokua kichwani pake, moyo wake haukua na pingamizi kua Mtoto Patra alikua ni damu yake lakini Neema alikua na ujauzito ambao aliamini wazi ni wake.
Alikua na tumaini kubwa la kupata Mtoto ambaye angekuja kua Mrithi wa utajiri wake uliokithiri, hakupokea simu ya Neema wala Mama yake Neema, alizidi kuchanganikiwa, licha ya utajiri alio nao lakini alijikuta katika wakati mgumu sana kisa Mtoto, akifikiria namna Matilda na Mtoto wanavyoteseka anajikuta akikuna kichwa chake, alitamani sana kumsaidia Matilda lakini pia wazo la kua Mtoto afe lilikua likimtawala, kauli ya Matilda kua atahakikisha anamfilisi ilianza kumyima raha, akamtafuta Chilo ili apate ushauri
“Yupo sahihi sababu ana Mtoto ambaye akipimwa DNA itagundulika wazi ni wako, akikufungulia kesi unafikiria utatokea wapi Kaka? Hii serikali haiangalii una pesa kiasi gani, kwa kifupi alichosema ana uhakika nacho James” Alisema Chilo wakiwa wameketi mahali wakipeana Ushauri
“Sasa nifanye nini, Nimhudumie Mtoto kisha nimtoe Matilda?”
“Kama amekataa kurejea kwao hata kama utafanya yote bado atakugandamiza James, Kama nilivyokwambia serikali ipo macho sana kwa kesi za namna hii”
“Sasa unanishauri lipi Kaka”
“Kubali kua Patra ni Binti yako, mlee kama Binti yako, mfanye Matilda aone mpo pamoja kisha mfanye wa siri ili Neema asijue chochote hadi pale atakapojifungua”
“Ushauri wako ni mzuri sana, nimetafakari usiku kucha nawezaje kumaliza hili jambo katika namna ambayo itaniacha salama”
“Ikishindikana njia hiyo Kaka juwa kua hilo jambo ni gumu kuliko ufikiliavyo, hapana shaka Matilda ana hasira nawe kwasababu anahisi wewe umeshilikiana na Neema ili kumweka yeye ndani” Alisema Chilo
“Naamini Patra akipatiwa matibabu hilo haliwezi kua shida kwa Matilda, ikibidi nitamtibia nje ya Nchi ili Matilda aende na Mtoto huko, hadi wao watakaporejea Nchini nitakuwa nimejipanga vizuri kuhakikisha hakuna kinachoharibika”
“Tena hapo utakua umeuwa ndege wawili kwa jiwe moja Kaka, Acha Neema aamini kua Matilda amerudi kwao lakini upande wa pili unapambana kuhakikisha anatibiwa, naamini utashinda”
Haikua rahisi kwa Jack kupata Usingizi usiku huo, taswira ya Patra namna anavyoteseka Hospitalini iliendelea kujirudia katika Ufahamu wake wa akili, alijikuta akiwa katika nyakati ambayo kila alichokiwaza kilizidi kuibomoa akili yake, ikawa ngumu kuukubali ukweli kua Bosi wake James alikua ametenda unyama ule.
*****
Asubuhi mapema, Jack akaondoka katika makazi yake, alifunga safari kuelekea kwa Mama yake James. Naam! alihitaji zaidi kujua baadhi ya mambo ambayo yangemfanya apate njia ya kulianza jambo hilo ambalo aliona wazi lilimhitaji kwa kiasi kikubwa, alipahafahamu kwa Mama yake James, hata Mama yake James alikua akimfahamu sana Jack, alipomwona alimkaribisha ndani.
Jua lilikua tayari limeshaanza kuchoma na kuunguza ngozi, chai ikawa tayari, wakaketi mezani kwa ajili ya kuzungumza, Mama James alishagundua kua kuna jambo lililomleta Jack pale
“Karibu sana Jacklin” Alisema Mama yake James
“Ahsante Mama”
“Umenisusa sana Mwanangu”
“Aaah Mama unajua majukumu ni mengi nakosa hata muda wa kuja huku siku hizi”
“Wala usijali naelewa”
“Mama kuna jambo linanitatiza sana katika akili yangu, limekua ni jambo lililobadili kabisa mtazamo wangu juu ya James” Alisema Jack kisha alimtazama Mama yake James ambaye alikaa vizuri kumsikiliza huku chai ikiwa inatoa mvuke
“Jambo lipi hilo mbona unanitisha Jack”
“Mama….sijui hata nianzie wapi, naomba kujua, James ana watoto wangapi?” aliuliza Jack, Mama James akashusha pumzi baada ya kusikia swali hilo
“James hana Mtoto..”
“Una hakika Mama?”
“Jack, Mimi ndiye Mama Mzazi wa James, akiwa na jambo ni lazima anishirikishe……Hajawahi niambia chochote kile kuhusu kua na Mtoto, isipokua yupo Msichana anayetarajia kumzalia Mtoto, huyu namfahamu sababu alishawahi kumleta Hapa, zaidi ya hapo hakuna Jack…sijui ni kwanini umeuliza hilo swali”
“Mama naomba nikwambie hili jambo, pengine nitatua mzigo fulani kichwani pangu, James ana Mtoto ana miaka mitatu sasa anaitwa Patra” Alisema Jack, Mama James akashtuka kidogo
“James ana Mtoto? hilo haliwezekani Jack, hawezi kua na Mtoto alafu anifiche Mimi, angeniambia tu” akasema Mama James
“Hata Mimi nilishtuka na sikuamini kama wewe ambavyo huamini, Mama,,James kua na Mtoto siyo tatizo ila tatizo ni kwanba amemkataa huyo Mtoto kwasababu ni Mlemavu, na Hapa ninapozungumza Mtoto huyo yupo Hospitali Magomeni hali yake siyo nzuri, Mama wa Mtoto yupo polisi kwa kesi ambayo inaonekana wazi kua James ameitengeneza…”
“Jack hivi unajua unazungumza maneno mazito sana ambayo hayaingii akilini mwangu, James hajawahi niambia kua ana Mtoto. Hili jipya kulisikia.”
“Mama hiyo ndiyo hali halisi, Mtoto amefanana sana na James. Nimekuja hapa sababu sitaki Mjukuu wako azidi kuteseka, sikujua kama James hakukwambia kuhusu hili, Mama nakuomba fanya jambo katika hili vinginevyo Mtoto anaweza kufariki kule Hospitalini” Akasema Jack akiwa na uso ulio poteza nuru, alihitaji huruma ya Mama James kuingilia kati huku akiamini fika kua si rahisi kumfikia James ambaye ndiye Bosi wake
“Jack nahitaji kwanza kumwona huyo Mtoto ”
“Kama tunaweza ongozana Hospitali muda huu itakua vizuri Mama”
“Sawa!!” Mama James na Jack wakakubaliana kua waelekee Hospitali kwa ajili ya kumwona Patra.
Asubuhi hiyo, Neema akaelekea kituo cha polisi, akazungumza na yule polisi ambaye alishapewa pesa ili kumshikilia Matilda, wakazungumza kwa dakika kadhaa kisha Neema akaondoka hapo, kitendo cha kupokea simu ya polisi kua James alienda Polisi kilimfanya atengeneze mpango mwingine kwa ajili ya kutekeleza takwa lake kwa Matilda ambaye kadili muda ulivyokua ukienda alikua akiendelea kuteseka pale kituo cha polisi, yule polisi akarudi ndani ya kituo maana maongezi yalifanyika ndani ya gari ya Neema.
Masaa matatu yakapita baada ya polisi kuzungumza na Neema, Mchungaji George alikua nje ya kituo hicho huku akimpa Mama Naomi jukumu la kushinda kule Hospitali, gari ya polisi ikatoka. Mchungaji akaitazama sana gari hiyo pasipo kujua kulikua na mpango ambao Neema alikua amepanga kuufanya. Matilda alikua akihamishwa hapo kituoni muda huo huku ndani ya kituo cha polisi kukiwa na jarada la kuachwa huru kwa Matilda, nje kidogo ya kituo Neema aliingia kwenye gari baada ya kuliona gari la Polisi likitoka hapo, akalifuata kwa nyuma.
*********
“Dada, huyu ni Mama yake James” Ilikua ni sauti ya Jack, Mama Naomi alimuona Mama James kwa mara ya kwanza, akamsalimia kwa heshima sana
“Mama huyu ni kama ndugu kwa Matilda ndiye anayeshinda hapa Hospitali kuangalia hali ya Mjukuu wako” Alisema Jack, Mama James hakutaka kuyaamini maneno ya Jack hadi pale atakapomwona Patra, wakapewa ruhusa na Daktari kisha wakaingia ndani ya wodi, Mama James akamwona Patra kwa mara ya kwanza, alikua katika Mshangao Mkubwa sana, sura ya Patra ilikua imefanana sana na sura ya James, Chozi la Mama James likaanza kutiririka kila alivyozidi kumwangalia Patra, siyo tu kwasababu ni Mjukuu wake bali kilichomliza ni jinsi ambavyo Patra alikua juu ya kitanda akipigania uhai wake, Mashine pekee ndizo zilizokua zikimpa uhai Mtoto huyo
“Kwanini hukuniambia James?” aliuliza Mama yake James akiwa ameshikilia kitanda kwa uchungu mkubwa sana, Jack akasogea na kumshika Mkono Mama James akimtaka atulize hasira zake
“Mama hiyo ndiyo hali halisi, jinsi unavyoumia wewe ndivyo ambavyo Mama wa Mtoto huyu anaumia akiwa kituo cha polisi” Alisema Jack huku Mama Naomi akiwa ametulia kimya
“Jack, miaka yangu 65 katika huu uso wa Dunia, sikuwahi kuumia kama ambavyo leo naumia, hili ni Pigo Takatifu kwangu, najiuliza kwanini James hakutaka kusema juu ya ujauzito hadi Mtoto anazaliwa, Sina Mtoto mwingine zaidi ya James, pengine sina Mjukuu zaidi ya huyu aliyelala hapa, lazima nipiganie uhai wake” Alisema Mama yake James.
“Lakini Mama pamoja na yote, sitaki James agundue kua Mimi ndiye niliyekupa hizi taarifa”
“Hilo usijali Jack, kikubwa ni huyu Mtoto awe salama, atahamishwa hapa na kutibiwa kwa siri, kwakua James alimkataa huyu Mimi nitalifanya hili kwa siri sana, pia nipo tayari kuandaa wakili kwa ajili ya huyo Msichana aliye polisi, nitalimaliza hili bila kuharibu upande wowote ule” Akasema Mama yake James
Muda wote huo Mama yake Naomi alikua akilia kwa furaha baada ya mzigo huo kutuliwa, mzigo ulikua mzito upande wao maana ilikua ni ngumu sana kupata pesa za matibabu ya Mtoto.
Mama James akazungumza na uongozi wa Hospitali kwa ajili ya kumhamisha Patra kumpeleka Muhimbili kwa ajili ya Upasuaji, jambo hilo likafanyika haraka sana, Gari maalum ya wagonjwa ikaondoka na Patra na Mama Naomi huku Jack na Mama James
wakielekea Polisi kwa ajili ya kuzungumza na Matilda, hadi kufikia muda huo hakuna aliyajua kua Matilda alikua ameondolewa kituo cha polisi huku mpango huo ukisukwa na Neema.
Safari ya gari ya polisi ilikua ni nje kabisa ya Jiji la Dar-es-salaam, palikua na jumba moja lililo kando ya Msitu, Matilda akaingizwa ndani ya jumba hilo lililoonekana kutulia sana, Neema akaingia pia.
“Kua Makini nimefanya kwa upande wangu, nahitaji hicho kiasi kabla ya kupambazuka ili kama kuna kitakachotokea nisife kama Mzoga” Akasema Polisi ambaye alicheza mchezo huo wa kumhamisha Matilda na kuaandaa Jarada kua aliachiwa huru
“Ndani ya Masaa 12 kuanzia sasa kiasi kitakua ndani ya akaunti yako, ondoa shaka. Ahsante kwa hili, nikwambie tu kua kazi yako imeishia hapa lakini si mwisho wa Mimi na wewe, huu ni mwanzo mzuri” Alisema Neema kisha akatoa bahasha ambayo ilikua imetuna akampatia Polisi huyo, Polisi akachungulia akaona alichokiona ambacho kilimfanya atabasamu, kisha akaondoka hapo mara moja.
Matilda hakujua amepelekwa wapi, Nani aliye nyuma ya mchezo huo, mara akasikia mlango ukifunguliwa katika chumba ambacho alikuwepo, akamwona Neema akiingia, aliongozana na Wanaume wawili ambao walijazia vizuri, Matilda hakusema chochote baada ya kumwona Neema
“Ulihisi natania Matilda, pengine hujui wewe ni kikwazo kiasi gani katika mipango yangu, uwepo wako ni tatizo kubwa kwangu” Alisema Neema
“Mimi sijakuzuia kumzalia James, lakini siwezi kuishi mafichoni kisa wewe” Akasema Matilda, akapigwa kofi
“Hivi unajua unazungumza nini wewe Mshenzi? James ana Mtoto mmoja tu, huyu aliye tumboni na si vinginevyo, kwanini unakua king’ang’anizi, sasa utakua hapa na Dunia itakutafuta sana Matilda, hakuna atakayekuja kukusaidia hapa, na kama utaendelea kuleta ubishi basi nitamuuwa Binti yako” Alisema Neema, alionesha wazi kua hakua Mtu wa masiala kabisa
“Unasemaje….Umuuwe Mtoto wangu? laiti kama kitamkuta chochote Patra basi nitakulipiza”
“Hata haumaanishi, utatokaje hapa hilo ni suala unalopaswa kujiuliza kisha ndiyo uwaze utanizuia vipi…” Neema akatoa simu yake kisha akamwonesha video ambayo ilivuruga akili ya Matilda, video hiyo ilimwonesha Neema akiwa katika wodi ambayo Patra alikua amelazwa, ilimdhihirishia wazi Matilda kua Neema anaweza akafanya chochote kwa ajili ya kumdhuru Patra.
Tayari Mama James na Jack walikua wamefika kituoni, wakatoa maelezo kua wanahitaji kumwona Matilda, wakaambiwa kua Matilda alikua ameachiwa huru muda mchache uliopita, iliwashangaza sana sababu kama angelikua ameachiwa huru basi wangemwona
“Afande Mimi nimekaa hapo nje kwa takribani masaa matano, kama angekua ameachiwa basi ningemwona lakini sikumwona hebu angalia vizuri” Akadakia Mchungaji George
“Jarada lake hili hapa, sisi tunafanya kazi kwa maandishi, tayari ameachiwa huru. Hatukuona sababu ya kumshikilia kwani Mlalamikaji alikuja na kusema kua haitaji kuendelea na kesi” Alisema tena yule polisi
“Polisi Mimi ni Mama wa mlalamikaji, nimekuja kwa ajili ya kumwona huyo Binti tafadhali” Alisema Mama James
“Jamani nimeshawaambia kua Msichana ameachiwa, jukumu la kujua yupo wapi ni la kwenu sababu kwetu ameshatoka” Akasistiza polisi huku akionekana haitaji kuendelea kubishana nao
Taratibu watatu wakashusha ngazi hadi chini, Jack akapiga simu Hospitali ambako walikua wameenda kwa ajili ya Matibabu, wakapata taarifa kua Matilda hakwenda huko. Taharuki ikawa kubwa, hakuna aliyejua mahali ambapo Matilda alikua ameenda
“Sasa atakua ameenda wapi au ameelekea kule Hospitali ambako Mtoto amehamishwa?” akauliza Jack, akili zao zikawaza kwa pamoja kua huwenda Matilda akawa ameenda huko, mara moja Mama James na Jack wakaelekea Magomeni ilipo Hospitali ya JM.
Wakati wao wanatoka kituo cha polisi, gari nyingine nyeusi ya kifahari ikaingia hapo, akashuka James, yaani kama angewahi kidogo tu angekutana na Mama yake na Mfanyakazi wake hapo Kituoni, James alihitaji kuzungumza na Matilda, hakujua kua Matilda alikua ameondolewa hapo na Neema, akaingia na kujitambulisha, akapewa maelezo yale yale ambayo Akina Jack walipewa, haraka akatoka hapo akajaribu kuipiga simu ya Matilda lakini haikuita, akampigia simu Neema
“Neema Nahitaji kuongea nawe sasa hivi, nieleze mahali ulipo” Akasema James, akaelezwa mahali ambapo Neema alikuwepo, akawasha gari kuelekea huko.
Ilikua ni nje kabisa ya Mji, kitu ambacho kilianza kumpa Mashaka James, akasogea hadi kwenye jengo ambalo Neema alikuwa amemuelekeza James aende, Palikua ni msituni. Jengo hilo lilikua katika eneo la peke yake kabisa, James aliposhuka macho yake yakawa kwenye jengo hilo lililo kimya sana, James akasogea kama alivyoelekezwa na Neema
Alipoingia alisikia sauti ya Matilda ikiita, akashtuka sana akaenda hadi kwenye hicho chumba akamkuta Matilda akiwa amefungwa kamba
“Matilda?” akaita James kisha akamkimbilia Matilda alipokua amekaa, Chozi lilikua likimbubujika Matilda, James akamwambia Matilda
“Nataka nikutoe hapa sawa?” Akawa anafungua kamba lakini akasikia Watu wakija kwenye chumba hicho, James akashtuka, alipogeuka akamwona Neema, Masudi na wanaume wengine wawili
Nini Kitaendelea? Usikose Sehemu Ya SITA Ya PIGO TAKATIFU Msisahau COMMENTS Ziwe Nyingi
Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost RIWAYA Hapa Kijiweni
Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM
SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI
JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa
Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx Pigo Takatifu xx
9 Comments
Leo wa kwanza Mimi jamani but story is very very 🔥🔥🔥
Mambo ni motooo
Jins nlivyonashauku natamn miendelez Sasa hv
Wow nautamani uo mwisho wa neema🔥
Inavitia kuendelea kusoma hadi rahaaa,tuone ni kitakiri kwa jemsi na maltida wake
Daaaah jmn huyu Neema ana roho mbaya kiasi hiki 😭😭😭
Yaani hi dunia jamaa anapigania mimba ambayo syo yake ..wanaume tuna tabu sana..
Adimini una baya ukifa uhozi ukiozo unuki twend Kaz sanaoma simulizi kama naangalia TV yan yan dah
Namuona James akitapeliwa, Neema kuishia pabaya