Ilipoishia “Benjamin akamsogelea Malkia Zandawe na kumtuliza kwa kumshika bega, hata yule rubani wa Helkopta ya Kijeshi aliona wazi kua Binti huyo alikua akizungumza kwa hisia kali iliyomuumiza. Malkia Zandawe akafuta chozi lake kisha akamwambia ndege wake mweupe aongoze njia, akamtaka na Benjamin aingie ndani ya Helkopta hiyo pamoja na sokwe wake ampendaye.
Kitendo cha ndege kuruka kiliwafanya na Popo kuzama Msituni zaidi kwa kukimbia kwa spidi kali kisha Benjamin, rubani, Malkia Zandawe na Sokwe wakaingia ndani ya Helkopta hiyo tayari kuelekea ndani ya Black Site kuikomboa familia ya Benjamin Kingai. Dakika tano baadaye Helkopta ikawa angani ikimfuata ndege mkubwa mpelelezi aitwaye Gola. Endelea
SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA
“Bado nipo ndani ya Msitu, naandamwa kila kona Mkuu. Nipo na Msichana lakini hali ni ngumu” ilikua ni sauti ya Muuwaji akizungumza na Mtoa kazi ambaye ni Waziri Mkuu Haji Babi kwa njia ya simu. Alikua ameketi juu ya jiwe moja, Elizabeth Kimaro akiwa hajitambui yupo chini, pembeni palikua na Mkondo mdogo wa Maji uliokua umekatiza msituni, mawe kadhaa yalikua yamelizunguka eneo hilo.
“Sawa Mkuu” alisema tena baada ya kusikiliza kwa Makini simu hiyo, Waziri Mkuu akaagiza kikosi kazi cha kuhakikisha Muuwaji anatoka salama ndani ya Msiitu akiwa na Msichana Elizabeth.
Hekaheka ilikua nzito ndani ya Ikulu, Ugeni mzito wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali uliingia Ikulu kwa simu ya haraka kutoka kwa Waziri Mkuu, Haji Babi alihitaji uhakika zaidi wa Nani atakua Mrithi wa Urais endapo Rais atafia Madarakani.
“Kwanini umeniita hapa?” akauliza Mwanasheria Mkuu, walikua kwenye chumba maalum cha wageni hapo Ikulu, Mwanasheria alianza kuhisia jambo fulani baya limemfika Rais, Waziri Mkuu akakuna kidevu chake kisha akamwambia Mwanasheria Mkuu.
“Nataka ushirika baina yetu, ushirika wenye tija hapo baadaye” akasema Waziri Mkuu, tayari alishaanza kukusanya viongozi wa Serikali ili kusiwe na Mgongano endapo atatangaza kifo cha Rais, japo palikua na Makamu wa Rais lakini hakua na nguvu mbele ya Waziri Mkuu ambaye ni Mtendaji Mkuu wa shughuli zote za Serikali.
“Ushirika?”
“Ndiyo”
“Kwanini umeniita Ikulu, Rais limemfika jambo?” akauliza Mwanasheria mkuu huku akikaza macho yake madogo yenye makunyanzi kutokana na Uzee wake, Waziri Mkuu akanyanyuka na kusogea alipoketi Mwanasheria Mkuu.
“Hatuna Rais kwasasa, sheria inasemaje?” akahoji Waziri Mkuu wakati huo Mwanasheria Mkuu wa Serikali akisimama kwa mshituko
“Unamaanisha nini?”
Waziri Mkuu akamnyuka Mwanasheria Mkuu kisha akamuuliza kwa Jazba nzito “Rais asipokuwepo nini kinafuata?”
“Unataka kulihasi Taifa lako?” akahoji Mwanasheria Mkuu wa Serikali huku mawani yake ikianguka chini kutokana na purukushani, pale pale Waziri Mkuu akamnyooshea Bastola Mwanasheria Mkuu
“Unatakiwa kuamua jambo moja, kushiriki au kutoshiriki. Sihitaji maswali mengi kutoka kwako Mzee” alisema Waziri Mkuu, jasho likiwa linamtoka. Hadi kufikia hapo Mwanashria Mkuu akaingiwa na woga akajikuta akiketi. Kicheko cha juu kikamtoka Waziri Mkuu huku akiwa anahema, Halafu akarudi kuketi kitini.
“Umemuuwa Rais?” akauliza Mwanasheria kwa sauti ya unyonge ili athibitishe.
“Siyo Rais peke yake, hata wewe unaweza ukamfwata endapo utakataa kutia saini nyaraka za uthibitisho mbele ya kadamnasi” alisema Waziri Mkuu akijua fika Kua Mtu wa Mwisho kuthibitisha madaraka hayo atakua ni Mwanasheria Mkuu tena atatia saini mbele ya Kadamnasi mara baada ya kutangazwa kwa kifo cha Rais Lucas mbelwa.
“Hata hivyo nina kazi ya kuifanya kabla ya kutangaza Kifo cha Rais” alisema Waziri Mkuu Haji Babi. Hadi kufikia hapo taarifa ya kifo cha Rais Mbelwa ilianza kutoka kwa Watu wakubwa wa Serikali.
Mate ya hofu yalipita kwa Mwanasheria wa Serikali, alitupa macho yake mezani kisha akayarudisha kwa Waziri Mkuu Haji Babi.
“Utanihakikishia Usalama wangu?” akauliza, Waziri Mkuu akatabasamu kwasababu alijua amefanikiwa kumtetemesha Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
**
Ndege Gola aliwaongoza kufika Black Site akiwa Mstari wa mbele, hakuna aliyeitilia Mashaka Helkopta hiyo sababu ilikua ya jeshi pia palikua na Helkopta nyingine juu zikiranda randa juu ya Msitu kumsaka Muuwaji. Yule rubani alikua akiifahamu vyema kambi hiyo, moja kwa moja alienda kutua ndani ya Jengo la Black Site.
Wakati Helkopta inashuka kwa ajili ya kutua ikazingirwa na Walinzi wa Black Site, wakati huo Malkia Zandawe alikua amesha chomoa Bunduki kutoka kwenye begi. Moja akampa Benjamin, machoni pa Benjamin tukio kama hili lilikua likijirudia, alishawahi kupewa Bunduki na Elizabeth Mlacha
“Ulinzi wako huo Ben” akasema Malkia Zandawe nyingine akampa Sokwe wake Mkubwa, ambaye alitoa tabasamu baada ya kupewa Bunduki hiyo. Akaunguruma kidogo kisha Rubani akawaambia
“Siwezi kutua, tunahatarisha Maisha” alipayuka akionekana mwenye Hofu lakini Malkia Zandawe akamwambia huku akiwa amemnyooshea Bunduki
“Shusha Helkopta chini kama bado unahitaji kuishi” alisema kwa Msistizo mkubwa, Rubani akatii maagizo ya Zandawe, akaishusha Helkopta Chini
“Utakua ngao yangu” alisema Malkia Zandawe, kisha akashuka akiwa amemteka yule Rubani, wale Walinzi wapatao zaidi ya ishirini wakiwa ndani ya sare nyeusi kama mafundi Bomba walishapata taarifa ya moja kwa moja kua Helkopta hiyo ilibeba Watu wasio sahihi kuingia ndani ya Black Site
Panga Boi ilikua ikimaliza Mzunguko wa mwisho wakati huo Malkia Zandawe alikua amesimama mbele ya Walinzi akiwaambia
“Ole wake Mtu afanye Ujanja, mtampoteza huyu Rubani” alisema Malkia Zandawe kwa kujiamini sana huku akiikaza Bunduki kuelekea kwa Rubani aliyemkamata vizuri, sare za Rubani zilionesha wazi kua alikua ni mmoja wa Marubaji wa Helkopta za Black Site.
Hatua za taratibu zilizojaa umakini zilisikika kutoka kwa Zandawe, akawavuka walinzi waliokua mbele yake wote wakampisha, sasa macho yake akayaelekeza lango kuu la kuingilia Black Site, akalisogelea akiwa na mateka wake. Wakati walinzi wakiwa bize sana kumtazama Zandawe, nyuma yao Benjamin na Sokwe walitoka kwenye Helkopta na kutafuta uchochoro wa kuingilia, Zandawe akalifikia lango kisha akalifungua.
Akawatisha kidogo wale walinzi kisha haraka akaingia ndani na mateka wake kisha akufunga mlango Mkuu wa kuingilia Black Site, walipofika ndani Zandawe akamwacha yule Rubani kisha akamuuliza
“Ni wapi wanapohifadhiwa mateka?” akauliza kwa haraka huku kupitia kioo akiwaona walinzi walivyokua wakifanya jitihada za kutaka kuingia ndani
“Ni huku” Rubani akasema kisha akaongoza mbele kuelekea sehemu wanapohifadhiwa mateka wa Black Site, aliamini huko angeipata familia ya Benjamin Kingai, wakakimbia haraka wakati huo walinzi wakizidi kuuvunja mlango waingie ndani kumdhibiti Malkia Zandawe.
Jengo hilo lilikua la siri sana kiasi kwamba palikua na ofisi nyingine zilizo chini ya jengo, wakashuka hadi huko na kuanza kukagua chumba kimoja baada ya kingine, vyumba vingi vilikua vitupu, palikua na vyumba vingi sana huko chini, nyingi zilikua ofisi zenye kompyuta nyingi.
Wakazidi kudhurura bila mafanikio, vyumba vyote vilikua tayari vimepekuliwa na hapakua na Mtu yeyote yule, wakaziona ngazi zilizokua zikieleke juu, haraka wakazitumia wakiamini zitawafikisha mahali walipo mateka wa eneo hilo.
“Una hakika? Kumbuka sikufahamu hivyo siyo rahisi nikakuamini” alisema Zandawe baada ya kuona palikua na mzunguko mrefu bila dalili yoyote ile ya kuipata familia ya Benjamin Kingai.
“Nami nataka kua salama dhidi yako ndiyo maana nahakikisha nakusaidia ili uniache, siwezi kukuingiza chaka” akasema yule Rubani kisha akaongoza mbele zaidi, lakini huko alikokua akimpeleka Zandawe hapakuonekana kua na dalili ya kuwepo wa mateka, hisia mbaya ikaanza kumcheza Malkia Zandawe
“Sikia siwezi kwenda zaidi ya hapa, hakuna dalili ya kuwepo kwa Watu ninaowataka huku unakozidi kunipeleka” alisema Zandawe kisha alisimama, Bunduki akaielekeza kwa yule Rubani.
“Chumba namba 303, nina hakika na kumbukumbu zangu niliiyona familia moja huko siku chache zilizopita, korido ya Pili kutoka hapa” alisema yule Rubani akiwa anajianda kuzidi kusonga mbele.
“Hebu subiri, mwanzo ulisema hujui walipo. Sasa hivi unasema wapo Chumba namba 303. Una mpango gani?” akauliza Malkia Zandawe akiwa ameyasimamisha masikio yake, akihesabu pumzi zake kwa uzuri kabisa.
“Aaah unajua mwanzo niliamini hutoweza kuwapita wale Walinzi hivyo sikutaka kupoteza muda kukueleza mengi, ila kwasasa naona tumaini langu ni kusema ukweli wa yale uyatakayo” akajitetea huku akihema, Zandawe akatafakari kauli ya Rubani yule kisha akamwambia
“Ukifanya mchezo wowote ule nakumaliza huku huku, sishindwi” alisema kwa Msisitizo Mkubwa sana Malkia Zandawe, sura yake ikakazia uhalisia wa yale ayasemayo. Yule Rubani akajibaraguza kidogo kisha akasonga mbele kwa spidi huku akimwambia Zandawe kua anaijua njia ya siri ya kutoka ndani ya jengo hilo kwa usalama kabisa.
Wakazidi kusonga huku nyuma yao wale Walinzi wakisaidiana na Makomandoo walifanikiwa kuvunja Mlango, sasa wakawaandama Rubani na Zandawe popote walipo tena kwa Msako mkali sana ulioanzia kwenye chumba cha Mawasiliano ya Black Site.
Kupitia Kamera zilizotegwa kwenye korido zote walifanikiwa kuona mahali walipokua wakielekea, ikawa rahisi kwao kuwafwatilia.
**
Nje ya Jengo la Black Site Palikua na heka heka nzito ya Kumsaka Muuwaji aliyemtorosha Elizabeth ndani ya jengo la Black Site, Makomandoo walizidi kusonga Msituni wakisaidiwa na Mbwa ili kuhakikisha Mlengwa ananaswa haraka sana. Muuwaji naye alizidi kukimbia akiwa amembeba Elizabeth aliyepoteza fahamu, nguvu zilianza kumwisha hasa baada ya kudondoka wakati ule kutoka juu hadi chini ya korongo na kuumiza Bega lake.
Akafika mahali akahitaji kupumzika, vinasa mawasiliano viliacha kufanya kazi na hii ilimwonesha kua mahali alipokua akielekea ni ndani zaidi, kifupi alikua akizidi kupotea Msituni bila kujua, hata Msaada aliouomba isingelikua rahisi kumfikia tena.
Akamweka Elizabeth kando ya fukutu moja lililoshiba nyasi za kutosha, jua lilikua likipata shida sana kuangaza sehemu kubwa ya Msitu huo kutokana na miti ilivyokua imeuzonga Msitu mzima na kufanya sehemu kubwa kua Giza. Dakika kadhaa za kua hapo alianza kusikia sauti za Mbwa wakibweka, haraka akamchukua Elizabeth akasonga naye mbele kwa kasi ya Kipanga, lakini kadili alivyozidi kwenda alianza kusikia sauti kubwa ya Maji iliyoashilia kua alikua amefika mwisho wa safari yake.
NDANI YA BLACK SITE
Zandawe na Rubani walifika mbele ya chumba namba 303, kidogo ikamfanya Zandawe aingiwe na imani ya kumwamini Mtu huyo kua alikua akiijua vizuri Black Site. Macho yao yalitazama
“Una hakika?” akahoji Zandawe
“Nina hakika niliwaona huku mara ya mwisho, Mimi ndiye niliyewaleta hapa kwa Helkopta” akazidi kusema Rubani, Zandawe akausukuma mlango kwa tahadhari kubwa sana akijua fika uzembe wowote utagharinu Maisha yao, akajikuta akiwa mbele ya Rubani asiye mfahamu vizuri, ghafla akapigwa teke na kuangukia ndani ya chumba kisha Rubani akaufunga ule mlango kwa nje, kisha akaanza safari ya Mbio kurudi nyuma walipotoka.
Zandawe akajaribu kuusukuma mlango lakini aligundua ulikua umefungwa vyema, akiwa anafikiria kuuvunja kwa kutumia Bunduki alipata wazo la kuangalia ndani ya chumba hicho mlikua na Nini, akiwa ametuliza hisia zake vyema alianza kusikia sauti ikitoka nyuma ya pipa moja.
Chumba hicho kilikua kama stoo hivi, sauti aliyoisikia ilimueleza vyema kua ilikua ni sauiti ya Mtu aliyezuiwa kusema chochote mdomoni mwake, wazo la kutaka kuvunja Mlango lilimwisha Zandawe, akainyoosha Bunduki kuelekea huko, kadili alivyosogea ndivyo alivyoanza kuona kitu kikifurukuta. Akanyoosha vyema Bunduki, akamkuta Mwanamke mmoja nyuma ya Pipa akiwa amefungwa mikono, miguu pia alikua na plasta ngumu mdomoni mwake
Zandawe akaiegemeza Bunduki haraka ukutani ili amsaidie, kitu cha kwanza kufanya alimtoa plasta ngumu mdomoni ili amsikilize.
“Wewe ni Mke wa Benjamin?” akauliza Zandawe wakati huo Mwanamke yule akitaabikia kuhema vizuri, alipotulia akaitikia kwa kichwa
“Mtoto yupo wapi nimekuja kuwasaidia” alisema Malkia Zandawe
“Sijui kuhusu Mtoto, mimi ni mpenzi tu wa Benjamin. Yeye yupo wapi kwani?” alihoji, Malkia Zandawe akagundua kua Mwanamke huyo ndiye Suzan, haraka akamsaidia kumfungua kamba ili watoke. Alipomaliza akamwambia
“Benjamin yuko nje anatusubiria” kabla hata hajamaliza kusema alichokua amekikusudia, zikasikika buti mlangoni, kisha Sauti ya risasi ikasikika, damu ikamwagika ikapenya chini ya Mlango. Malkia Zandawe akaivuta bunduki yake na kuanza kujibu mashambulizi ya Risasi za mfululizo.
Alipiga risasi nyingi mlangoni ili awatishe waliokua hapo waone sasa kua aliye ndani alikua amejipanga, Malikia Zandawe hakujua nje kwenye korido palikua na Walinzi na Makomandoo wa kutosha.
Mwili wa rubani ulikua ni miongoni mwa miili iliyolala kando ya Mlango, Suzan alikua mwingi wa kugumia kila aliposikia risasi zikilia…
Nini kitaendelea?
Usikose SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA
Mpe Nguvu ADMIN Kwa ajili ya bando Kwa kumtumia Chochote aendelee kupost MSALA Hapa Kijiweni
Lipa Namba: 57900454
Jina: LIPA KIJIWENI TIPS
Mtandao: VODACOM
SOMA RIWAYA YA KOTI JEUSI KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA FUNGATE KWA KUBONYEZA HAPA
SOMA RIWAYA YA NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI
JIUNGE NIPO KIJIWENI Kwa Kubonyeza Hapa
MSALA xx MSALAxx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA xx MSALA
10 Comments
Woyooo msalaaa me WA kwanza
Duuuh
Asa huyo malikia zandawe amekaribishwa RASMI kwenye msala😁😁😁
Msala umekuwa msala kwelikweli!
Big up Admin.
Malkia ameyakanyaga ya Kandonga mtu kazi😂😂
Kwan ni mimi pekeangu cjaiona msala sehem ya 26
Sema kimeumanaaa 🤣
Good ila kuanzia sehem ya kwanza cjapat sas sjui ntazupataj kweny Hadith hii
Hii movie ni kali sana aiseeee
Huwa mizigo ya kijasusi kama hii naielewa sana..
Hivi ndio hatuipati tena, maana naona Pigo Takatifu on the air…..
Kisa cha hii adisi inasisimua na nimependa uwandishi wake na alie andaa anajua