Ilipoishia ” Hadi kufikia hapo picha ya Muuwaji ilikua ni Msichana wa chini ya Miaka 30, mweusi, mzuri na aliyevaa Baibui, Daudi alizidi kupagawa, sasa swali alilojiuliza, Msichana huyo alikua anataka nini kwa Salma, akawaza zaidi kua inawezekana akawa ndiye aliyemuuwa Bilionea Mzee Yusuf? “
Tuendelee sasa
SEHEMU YA TANO
Familia ya Marehemu Mzee Yusuf ilitaarifiwa juu ya Kifo cha Salma, Mshituko mkubwa uliikumba familia hii iliyopokea taarifa ya kifo cha mpendwa wao ambaye alitoweka Usiku wa manane. Mwili wa Salma ulipofanyiwa uchunguzi hapakukutwa na alama zozote za vidole kama ilivyo kwa Marehemu Mzee Yusuf, ilionesha kua Muuwaji alijua anachokifanya.
Pili, Marehemu aliuawa kwa ile kamba iliyobanwa kwenye shingo yake, hakukua na taarifa nyingine zaidi. Mpelelezi Mbaga akaita jopo la wapelelezi wote wa Jiji la Dar-es-salaam ili waanze uchunguzi wa kina kuhusu jambo hilo, wakagawana timu tatu za Wapelelezi
Timu moja ilitoka kituo cha polisi na iliongozwa na Daudi Mbaga, Timu ya pili ilitoka kwenye shirika la Kijasusi la Tanzania na la tatu lilikua ni shirika lisilo la kiserikali ambalo lilijikita zaidi kwenye kufanya upelelezi, wote waliivalia njuga kesi hiyo, angalau sasa Daudi Mbaga aliupunguza Mzigo kichwani kwake.
Timu ya kwanza ilijikita zaidi na wahusika wa familia, timu ya pili ilijikita zaidi na mawasiliano na timu ya Tatu ilikua ikichambua zaidi ripoti za Daktari na Ukaguzi wa maeneo ya Matukio ili kubaini kiurahisi na kwa hakika kabisa Nani Muuwaji.
Katika uchunguzi walibaini kua pesa hizo kwa hakika zilitoka kwenye akaunti ya Marehemu Mzee Yusuf, Salma alizichota pesa hizo siku ya tukio kwa kutumia kadi ya dharura ambayo alikutwa nayo akiwa amekufa.
Mara moja baada ya kutoa taarifa kwa familia ya Mzee Yusuf juu ya kifo cha Salma, mpelelezi Daudi Mbaga alirudi kwenye nyumba ya Bilionea huyo, sasa lengo lake likiwa kuzungumza na Mtoto Adela ili aeleze ule Usiku alimwona Nani. Kwa kipindi hicho chote Mtoto Adela alikua akikaa sana chumbani kwa kile kilichodaiwa ni hofu ya alichokiona, dhahili ilionesha kua Adela aliona zaidi ya Mtu mwenye koti jeusi, kwakua kilikua kipindi ambacho ndugu walikua hapo Basi waliunganisha kusubiria maziko ya Mke mdogo wa Mzee Yusuf. Mtu kwanza kumwona Daudi Mbaga alikua ni Sofia, haraka alimfuata na kumwuliza
“Mmebaini chochote?” Daudi Mbaga alishusha pumzi kisha akamweleza
“Hapana, namhitaji Adela kwanza” Sofia alishtuka sana
“Adela?”
“Ndiyo kuna maswali kadhaa nahitaji kumwuliza” alisema Agent Daudi akiwa ameweka mikono
mifukoni huku akibarizi macho yake huku na kule kijasusi zaidi
“Maswali gani hayo, Mtoto wangu hajui chochote Mpelelezi. Nani amekuongopea” alisema Sofia,
Daudi aligundua kua Sofia alifanya hivyo kumlinda tu Binti yake akiwa kama Mama. Daudi hakujibu
huku Sofia akiweweseka Daudi aliagiza kijana wake akamchukue Mtoto, Sofia alitaka kuzuia ndipo Daudi alipombadilikia ghafla na kuivaa sura ya kazi
“Acha utoto, nipo kazini. Binti yako Usiku ule alimwona Muuwaji akitoka chumbani kwa Mzee Yusuf,
Mtu pekee aliye na ushahidi wa moja kwa moja ni yeye” Sofia alitulia huku akitazama namna Binti yake Adela alivyokua amechukuliwa na Kijana wa Daudi Mbaga hadi pale waliposimama.
Mara Hamza akafika hapo baada ya kuona mazingira yasiyo ya kawaida hivyo alijua kuna tatizo.
“Kuna nini?” aliuliza
“Aaah namchukua huyu Binti nahitaji kujua mambo kadhaa kuhusu usiku ule” alijibu Daudi
“Lakini huyu ni Mtoto tu kwanini usimchukue Mtu mzima Mpelelezi?”
“Kwasababu alimwona Muuwaji”
“Unasema alimwona?”
“Ndiyo”
“Eti ni kweli Adela ulimwona Muuwaji?” aliuliza Hamza akimtazama Mtoto huyo ambaye ni Mpwa wake, Adela alikua akidondosha chozi tu kwa hofu, Daudi aliondoka na Mtoto huyo pamoja na Mama yake kuelekea kituo cha Polisi Ostabey kwa ajili ya Mahojiano Muhimu ambayo yangetoa taswira nzima ya Muuwaji. Getini walipishana na Martha na Mama yake ambao walikua wamerudi kwenye kasri hilo baada ya kupata taarifa ya kifo cha Salma Mke wa Mzee Yusuf.
“Kaka Hamza kuna nini?” Martha aliuliza, Hamza Mwanaume mkimya na mpole alisema kwa
unyonge
“Wamemchukua Adela, wanasema siku ya tukio la kifo cha Baba alimwona Muuwaji” alisema Hamza
huku akionekana kujawa na huzuni sana
“Eeeh kumbe? Masikini, naamini hakuna hatua kubwa watamwachia hivi karibuni” alisema Martha
kisha alimpiga begani Hamza katika hali ya kumpoza na machungu.
Baada ya kufika kituoni, Sofia akawa analeta vurugu akitaka kuingia chumba cha Mahojiano, kama alivyombadilikia kule nyumbani basi hata kituo cha polisi alimbadilikia hivyo hivyo, akaagiza akamatwe awekwe mahali hadi mahojiano yaishe. Kisha Mpelelezi Daudi akaingia chumba cha Mahojiano, alimkuta Adela akiwa anatetemeka huku akionekana kutaka kuanza kulia, Mpelelezi
Daudi haraka alitambua kua Binti huyo aliona na alimjua Muuwaji ndiyo Maana alikua katika hali hiyo, sasa upelelezi ulifika mbali zaidi baada ya kifo cha Mshukiwa namba moja ambaye ni Salma.
“Oooh pole Mwanangu, usilie. Nitakuuliza maswali machache tu kuhusu shule kisha nitakuruhusu uondoke na Mama yako, usiogope sawa?” alisema Daudi akiwa anaketi vizuri, mkononi alikua na juisi akampatia Adela na kumwambia anywe kidogo, alijua Mtoto huyo haitokua rahisi kwake kuzungumza kama hatotumia ujanja Adela alifuta chozi kisha akanywa kidogo juisi hiyo ya Baridi kiasi.
“Si naweza kukuuliza kidogo?” Adela akaitikia kwa kichwa.
“Una miaka mingapi?”
“Kumi na tatu”
“Oooh! Umri wako ni sawa na Binti yangu, amefanana sana na wewe” alisema Mpelelezi Daudi,
tabasamu likaanza kuonekana kwenye sura ya Adela, hapo Daudi akagundua anaelekea kuufahamu ukweli muda siyo mrefu.
“Sasa Adela, najua unampenda sana Babu yako si ndiyo”
“Ndiyo” alijibu kwa sauti ya unyonge
“Unaonaje kama haki ya kifo chake ikapatikana ili apumzike kwa amani huko aliko, naamini
anakutazama muda huu na kutaka kujua kama kweli ulikua ukimpenda. Muoneshe Babu kua
unampenda sawa?”
“Sawa” alijibu kwa hali ile ile ya Unyonge
“Hebu niambie Usiku ule uliona nini?” Adela alimeza mate kisha alishusha pumzi zote kama vile
anatua mzigo fulani kichwani pake
“Usifiche kitu sawa?”
“Sawa”
“Uliona nini?” Kwa ushawishi wa Mpelelezi Daudi, Adela alianza kufunguka
“Nilikua nasoma, lakini niliangusha glasi, sasa nikahitaji kutoka kwa ajili ya kwenda kutupa vipande vya glasi, nikatoka chumbani…” alipofika hapo alikaa kimya
“Enheee ilikuaje?” Akauliza Mpelelezi Daudi, chozi lilimbubujika Adela akalifuta
“Nilimwona Mtu aliyevalia koti jeusi akitoka chumbani kwa Babu” wakati anaelezea hivyo Adela
aliona kama vile Mama yake amemtokea na kumkataza asieleze zaidi, haraka akafupisha stori
“Niliogopa na kurudi chumbani” Mpelelezi Daudi alihisi kama Mtoto huyo alikua akimtazama Mtu mwingine, lakini ndani ya chumba hicho hapakua na Mtu mwingine zaidi yake na Mtoto huyo
“Anafananaje, uliiyona sura yake?” Adela akatingisha kichwa chake kua hakumwona Vizuri Mtu huyo hivyo sura yake haijui. Mpelelezi Daudi akaegemea kiti kwa kuchoka, alichotarajia kukisikia hakukisikia kutoka kwa Adela, Mahojiano yakaishia hapo.
Vita ya Akili na Maarifa
Usiku wa Saa tano, Mpelelezi Daudi aliyeanza kukata tamaa alikua akifikiria jambo akiwa nyumbani kwake, kila taarifa aliyoipata ilikua inamvuruga akili na wala haikuishi kumpa Maana halisi, kumfahamu Muuwaji ilikua kazi ngumu.
Vitengo vyote alivyoshirikiana navyo vilitoa taarifa zilizozidi kuleta ugumu, sasa alifikiria kuruhusu Maiti ya Salma izikwe maana Uchunguzi ulikua umeshakamilika na hakukua na shahidi yoyote ile kutoka kwenye mwili huo, hata ile pesa alifikiria kuzikabidhi kwa familia hiyo lakini akiwa katika hali hiyo ya kufikiria hakuacha kuamini kua, Salma alikua akifahamiana na Muuwaji au ndiye aliyesuka mpango wa kuuawa kwa Mzee Yusufu kisha akageukwa na mshirika wake ambaye huwenda aliomba pesa kwa Salma.
Japo dhana hiyo hakuipa nguvu sana kwa maama pesa walizikuta na hazikuchukuliwa na Muuwaji, ugumu sasa ukahamia kwenye dhana ya pili kua palikua na Wauwaji wawili waliomdhuru Mzee huyo, hapa alihitaji akili kutulia zaidi ya Maji ya Mtungi, akavuta simu na kumpigia Dokta Sekwa ambaye alikua akiikagua Maiti ya Salma kwa muda wote.
Wakati anapiga kumbe Sekwa naye alikua anampigia, simu ya Dokta Sekwa ndiyo ilikua na nguvu ikapenya na kuita. Daudi akaipokea kwa haraka sana
“Mpepelezi pole kwa kukupigia simu Usiku huu, kuna jambo la ajabu zaidi nimeligundua kwenye mwili wa Marehemu” alisema Dokta huyo, Daudi alinyoosha shingo kama nyoka mwenye hasira huku macho yakiwa yamemtoka pima kama Mjusi aliyebanwa na Mlango, aliona simu hiyo ilitaka kuibua tumaini la kesi hiyo.
“Enhee nieleze” alichangamka sasa
“Kwenye sikio la kulia ndani kabisa nimekuta karatasi nyeupe yenye maandishi ambayo siyaelewi,
karatasi ilizamishwa ndani ya Sikio la Kulia” alisema
“Karatasi sikioni? Sikia Dokta nakuja hapo sasa hivi” alisema Mpelelezi Daudi, Japo ulikua usiku lakini aliona ni vema akaenda Hospitali, mwendo wa dakika zaidi ya arobaini alifika Hospitalini hapo na kumkuta Dokta Sekwa akiwa anamsubiria, mara moja wakaelekea chumba chenye mwili wa Salma.
Akapewa hiyo karatasi ndogo sana yenye tarehe iliyosomeka 19,08,1998.
“Huu ni Mwaka, kuna mahusiano gani, nina hakika Muuwaji ametaka tutafute Maana. Hakika, si rahisi kumtambua, lakini huu Mwaka una maana gani?” alijiuliza Mpelelzi Daudi
“Haiwezi kua tarehe ya kuzaliwa ya Muuwaji?” swali la Dokta Sekwa liliibua hisia kali kwa Daudi Mbaga, akasema
“Yes, kwa mujibu wa yule Msamalia anasema Muuwaji ana umri wa chini ya Miaka 30, hivyo kama alizaliwa 1998 basi ana miaka chini ya 30” Mpelelezi Daudi alitoa meno nje kwa tabasamu, akaondoka hapo na ile karatasi ndogo sana, akafika nayo nyumbani kwake, alichofanikiwa kuhisi ni umri sahihi wa Muuwaji lakini hiyo haikutosha kutoa taswira halisi ya Nani Muuwaji. Akawa na kazi ya kuudadavua Mwaka huo wa kuzaliwa.
Lakini akili yake ikakumbuka jambo, tarehe kama hiyo aliiyona kwenye ile picha aliyoikuta kwenye meza ambayo Mzee Yusufu aliilalia baada ya kuuawa, kwanza alihitaji kuhakiki kama ni kweli, aliitafuta picha na kuipata
Alithibitisha kua picha ile ilikua na tarehe kama ile, alafu mwandiko wa kwenye karatasi ulifanana sana na ule wa kwenye picha, tena ulionekana kua ni mwandiko wa Mwanamke. Mpelelezi Daudi alijishika kichwa chake na kucheka kidogo kwa hasira maana Muuwaji aliamua tu kuwasumbua Wapelelezi, huwenda alijua wazi Mauwaji aliyoyafanya isingelikua rahisi akagundulika.
Agent Daudi aliiweka ile picha mezani ili aichambue vya kutosha akiamini huwenda Muuwaji alihitaji kutuma ujumbe fulani wenye kufungua akili za wapelelezi. Picha hiyo ilikua na sura za watu kadhaa akiwemo Mzee Yusuf, Sofia, Hamza na Mtoto mwingine wa tatu ambaye ni wa kike.
Kwenye picha hiyo alimtambua Sofia, Hamza na Mzee Yusufu. Yule mwingine hakumtambua, akaanza kuhisi huwenda huyo Mwingine ndiye Muuwaji aliyeamua kujidhihirisha ili wapelelezi wamjue, akatazama saa yake. Usiku ulizidi kwenda mbio hivyo aliona ni vema akasubiria hadi kupambazuke ndipo aelekee kwenye kasri la Mzee Yusuf. Lakini hapa akawa na fikra nyingine ya ziada kua Muuwaji anawachezea wapelelezi hivyo kama ataingia kichwa kichwa basi ataingia mtegoni, na huwenda tarehe hiyo iliwekwa kama mtego ili wazidi kupoteza muda wa kumjua Muuwaji.
Mapema sana Mpelelezi alifika nyumbani kwa Mzee Yusuf, Hamza ndiye aliyekua Mtu wa kwanza kuzungumza na Mpelelezi akiulizia mwili wa Salma ambao ulikua mikononi mwa Polisi, Mpelelezi akamvuta pembeni Hamza na kumuuliza kuhusu ile picha kabla hata hajampa jibu la ile maiti
“Tazama hii picha” alisema Mpelelezi Daudi Mbaga, alionekana kutohitaji wengine wasikie akamvuta zaidi Hamza hadi maegesho ya Magari
“Hii picha imefikaje mikononi mwako Mpelelezi?” aliuliza Hamza
“Hii picha ni miongoni mwa vitu nilivyovikuta baada ya kifo cha Baba yako, inaonesha hii picha ina mahusiano ya moja kwa moja na tukio. Niambie hii picha ilipigwa lini?” Hamza aliiangalia tena kisha akamjibu Daudi
“Kati ya 1997 au 98, hii picha ni ya familia Mpelelezi inawezaje kuingia kwenye kesi ya kifo cha
Baba?” alihoji, Daudi akaichukua picha kutoka kwa Hamza kisha akanyoosha kidole kwa Binti aliye kwenye picha hiyo
“Huyu ni Nani?” Hamza akamtazama Binti huyo kisha macho yake akayapeleka walipokaa wengi, akaonekana kumtafuta Binti huyo ambaye walipiga naye picha enzi hizo wakiwa wadogo
“Huyu ni Martha, yule Pale” alisema Hamza huku akimyooshea Kidole Martha, Binti ambaye ni zaidi ya familia kwao, ni zaidi ya ndugu kwao. Martha alikua akicheka na baadhi ya Watu aliokua akizungumza nao akiwemo Mama yake na ndugu wa Marehemu Salma. Hakuonekana kua na dalili zozote mbaya
“Una hakika?”
“Tazama vizuri sura yake, ni yule Martha. Huyo ni Binti wa rafiki yake Baba ambaye alifariki muda mrefu, tokea kipindi hicho Baba alichukua jukumu la kumfanya Martha kua Binti yake” alielezea Hamza. Macho madogo ya Mpelelezi Daudi yalihakiki ufanano wa Martha na Binti wa kwenye Picha, alithibitisha kua Binti huyo wa kwenye picha ndiye Martha. Umri wake ni chini ya Miaka 30, kwa kifupi alikua na sifa za Muuwaji lakini sura yake haikusaidiki fikra za Daudi Mbaga
Katika akili yake Daudi aliwaza kua Muuwaji yupo kwenye hiyo picha ya familia, walio hai kwenye picha hiyo ya Watu wanne ni Martha, Sofia na Hamza. Kwa sifa za Muuwaji alimtoa Hamza katika orodha hiyo, akawatazama Wanawake wawili ambao ni Sofia na Martha, akaamini katika akili yake kua Muuwaji anaweza kua mmoja kati yao.
“Martha hawezi kua Muuwaji, ni Mtu mzuri sana kwa Baba. Hata nyumba wanayoishi imejengwa na Mzee Yusuf, hiyo ni ishara kua hapakua na uadui kati yao hadi ije hiyo dhana yako. Chunguza zaidi Mpelelezi” alisema Hamza Mwanaume mpole mwenye aiba ya kipekee sana na lafudhi yake ya kiunguja, aliishi sana huko kwa Miaka mingi akisimamia Biashara za Baba yake.
“Vipi kuhusu mwili wa Salma, ndugu zake wapo hapa kumzika kwanini usiruhusu mwili wake uzikwe?” Hamza alikumbushia kuhusu Mwili, Mpelelezi Daudi akapiga simu kwa Dokta Sekwa na kutoa ruksa ya mwili wa Salma uchukuliwe kwa ajili ya Mazishi, papo hapo akawapa kazi kitengo alichokichagua kuhusika na mawasiliano, alihitaji Sofia na Martha wachunguzwe kupitia simu zao ili kubaini kwa hakika ni Nani Muuwaji kati yao.
Pia akaagiza simu ya Msamalia aliyesema alimwona Muuwaji afwatilie ili azitambue sura za Martha na Sofia, alipofwatiliwa hakupatikana tena, wakahisi huwenda ameuawa na Muuwaji baada ya kuona ametoa ushirikiano kwa Polisi, Ugumu wa kumpata Muuwaji ukazidi kuendelea huku pakihisiwa kua Muuwaji ana mtandao mkubwa wa kunasa taarifa zote za Polisi na kila hatua inayopigwa na Wapelelezi wote.
Familia ikaruhusiwa kuuchukua Mwili, wakasafiri nao hadi Mwanza kwa ajili ya Maziko, Salma alizikwa Mwanza huku kifo chake kikigubikwa na Utata Mkubwa sana, kiasi kikubwa cha pesa kikarudishwa kwenye akaunti ya Mzee Yusuf. Baada ya kikao cha familia kwa kushirikiana na Mwanasheria wa Mzee Yusuf, Hamza alipewa Usimamizi wa jumla wa mali zote kwa niaba ya Mdogo wake Sofia.
Jambo hilo lilimwacha Sofia akiwa mwenye tabasamu sana, kwa namna alivyokua na chuki za wazi kwa Salma asingeliweza kukubali Mali hizo zisimamiwe na Salma ambaye ndiye Mama yao Mdogo, kifo cha Salma kilijaza Tabasamu kwa Sofia, tabasamu lililoonekana waziwazi kabisa. Itaendelea Sehemu Ya 06
Jiunge WhatsApp Channel Ya KIJIWENI Ili Kuwa Wa Kwanza Kupata Updates Za RIWAYA Hii Kwa Kubonyeza Hapa
SOMA Uchambuzi Na Makala Mbalimbali Kwa Kubonyeza Hapa
11 Comments
Amazing story ase 💪💪💪💪💪💪💪💪💪achia hata sehemu mbili daily
Nzuri
Mtutolee sehem mbili kwa siku jaman ni nzuri 👏🔥
tunaomba uachie sehem mbil kwa sikuu
Am from Korea but hii riwaya aseee😋😋…. ina raha yake
Uakika san story inazid kolea san🤩🥰sem shida ni fupi tuma at mbil ???
Riwaya taamu
Kongole mtunzi
🤔🤔Sophia anaweza akawa muuwajii🔥
Wengine tupo kongo migodinii achia mzigo admin wangu
Hongera sanaa kazi Nzuri, nakuombea Kwa Mungu unachofanya kipate kibali kikupeleka kutoka chini kwenda juu
Pingback: KOTI JEUSI (Sehemu Ya Kumi Na Tano) KOTI JEUSI – 15 - Kijiweni